Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zidane Sereri... Straika anayetembelea nyota ya Samatta Azam FC

Zidane Pict

Muktasari:

  • Baada ya kujiunga na kikosi hicho, Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza naye na kueleza bayana safari yake ya soka hadi alipofikia, pamoja na malengo aliyojiwekea, ikiwemo pia kufanya vizuri ili kufika mbali katika karia yake.

MOJA ya vipaji vya soka inavyojivunia Tanzania ni cha kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Zidane Sereri kilichomfanya ajiunge na matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea kwa 'Walima Zabibu', Dodoma Jiji FC.

Baada ya kujiunga na kikosi hicho, Mwanaspoti limepata nafasi ya kuzungumza naye na kueleza bayana safari yake ya soka hadi alipofikia, pamoja na malengo aliyojiwekea, ikiwemo pia kufanya vizuri ili kufika mbali katika karia yake.


KUFUATA NYAYO ZA SAMATTA

Zidane anasema mojawapo ya mshambuliaji anayemkubali na kutaka kufuata nyayo zake ni Mbwana Samatta anayekipiga klabu ya PAOK ya Ugiriki, huku akiweka wazi kiwango na mafanikio yake yanamfanya kuongeza juhudi zaidi akiwa uwanjani.

"Samatta kwangu ndio kioo katika karia yangu ya soka, nafurahia aina ya uchezaji wake na kwa hakika kila nikipata nafasi ya kucheza nahakikisha napambana ili kufikia mafanikio yake, ni ngumu ingawa ananipa motisha ya kutimiza malengo hayo."

ZD 01

CHIMBUKO LA ZIDANE

Anasema sababu kubwa ya kuitwa jina hilo ni Baba yake, Ally Sereri kumpenda nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Zinedine Zidane kutokana na kipaji kikubwa alichokuwa nacho ambacho kiliteka hisia za mashabiki wengi duniani.

"Baba yangu alikuwa shabiki wa Zidane, sasa wakati nazaliwa alimwambia mama yangu nipewe jina hilo, baadhi ya watu wanajua ni la utani ila ni la uhalisia, najivunia heshima niliyopewa na naahidi kupambana ili kuonyesha kiwango kizuri."


SAFARI YA SOKA

Zidane anasema safari yake ya soka ilianzia wilayani Songea katika timu ya Kondoa Rangers kisha Ajax na baada ya hapo ndipo akachukuliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dodoma, Mohamed Adeni aliyempeleka kikosi cha vijana.

"Baada ya kwenda timu ya vijana ya Dodoma Jiji, Adeni akawa ananilea kama mwanaye, kwa kipindi hicho nashukuru nilipata malezi mazuri katika akademi ya Makole niliyoitumikia kwa miaka miwili na nusu kisha kupandishwa timu ya wakubwa."


KOCHA ASIYEMSAHAU

Anasema wakati wote akiwa katika kituo hicho cha Makole, moja ya makocha ambao hatokuja kuwasahau kwenye maisha yake ni Omary Omary maarufu 'Omaroo', kutokana na mchango wake.

"Atabakia katika kumbukumbu ya maisha yangu. Yeye ndiye aliyenifanya kufika hapa nilipo leo kwa sababu ya malezi bora aliyonipa kwa wakati wote niliokuwa chini yake, namshukuru kwa ukarimu wake na atabaki kuwa mtu muhimu sana kwangu," anasema.

ZD 05

KUMBE ANGEKUWA DAKTARI!

Zidane anasema moja ya malengo yake makubwa yalikuwa kufanya kazi ya udaktari kwa sababu alikuwa anapenda tangu utotoni, japo baada ya kujihusisha na soka aliamua kubaki huko kutokana na ukaribu na watu wengi aliokuwa nao.

"Nafikiri bahati ya kucheza soka ilianzia kwa baba yangu kwa sababu tangu aliponipa hilo jina, nadhani ikawa rahisi pia kwangu kutembelea upepo huo, hata watu walionizunguka kipindi hicho walikuwa wa soka, hivyo ikanirahisishia kuupenda."


KUJIKITA KWENYE BIASHARA

Anasema mbali na kucheza soka ila miongoni mwa malengo yake mengine ni kufungua biashara mbalimbali ambazo zitamuingizia kipato.

"Mchezo wa soka ni wa muda mfupi sasa kama mchezaji ni lazima niangalie mambo mengine nitakayoyafanya yatakayoniingizia kipato tofauti na kazi ninayofanya, kwa sasa siwezi kueleza ni biashara gani ila muda ukifika kila kitu kitakuwa wazi."

ZD 02

MALENGO YA KUCHEZA NJE

Nyota huyo anasema moja ya malengo yake ni kuhakikisha anaendelea kupambana ili kuonyesha kiwango bora kitakachomsaidia kuonekana na kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi, huku akiweka wazi Azam ni sehemu salama ya kufanikisha jambo hilo.

"Azam ni timu nzuri ambayo naamini kwangu itanipa nafasi zaidi ya kuonekana, hapa naweza kusema nipo sehemu salama na hakika najivunia, jambo kubwa ni kuendelea kuonyesha kiwango bora kwa sababu ushindani ni mkubwa tofauti na nilipotoka."


DILI LA AZAM LAMSHTUA

Zidane anasema wakati anasikia Azam FC inamhitaji alipatwa na mshtuko wa furaha kwa sababu mojawapo pia ya malengo yake yalikuwa ni kupata nafasi ya kucheza timu kubwa hapa nchini, hivyo anaamini itampa fursa ya kuendelea kuonekana zaidi.

"Hakuna mchezaji asiyetamani kucheza Azam, ni timu iliyokamilika katika kila idara, nimejisikia furaha kupata nafasi hii muhimu maishani mwangu, kilichobaki kwangu ni kuipambania ili ifanye vizuri kwenye mashindano mbalimbali tunayoshiriki."

ZD 04

JAMBO AMBALO HATOLISAHAU

Anasema wakati anaichezea timu ya vijana ya Dodoma Jiji alipitia changamoto ambayo hatokaa akaisahau, kwani kwa kipindi hicho alikuwa hajaanza kulipwa kiasi chochote cha fedha, huku familia yake ikiwa inapitia wakati mgumu katika maisha.

"Ilikuwa inaniuma sana kwa sababu wakati huo familia yangu ilikuwa haina chochote, sikukata tamaa kwa sababu niliamini ipo siku Mwenyezi Mungu atanifungulia milango ya baraka, nashukuru wakati sahihi ulipofika kila kitu kilienda vizuri."


AIOTA TUZO YA MFUNGAJI BORA

Moja ya malengo ya nyota huyo katika Ligi Kuu Bara ni kuibuka mchezaji au mfungaji bora, huku akiweka wazi haitokuwa rahisi ingawa atahakikisha anaendelea kupambana, akiamini hakuna jambo linaloshindikana ikiwa mtu ataweka nia ya dhati.

"Hakuna jambo jepesi maishani ila nikifikiria nilipotoka na hapa nilipo leo inanifanya kuamini kila kitu kinawezekana chini ya ardhi, nitapambana kadri ya uwezo wangu na namuomba Mwenyezi Mungu anisaidie kutimiza malengo hayo," anasema.


MECHI BORA KWAKE

Sereri anasema mojawapo ya mechi ambayo hatokaa akaisahau katika maisha yake ni wakati alipofunga bao la kwanza la Ligi Kuu Bara kipindi akiichezea Dodoma Jiji dhidi ya Mbeya City msimu wa 2022-2023.

"Ilikuwa siku nzuri maishani mwangu na ya kihistoria iliyojawa na furaha tele moyoni mwangu, kwa hakika itabaki kuwa mechi muhimu na yenye kumbukumbu nzuri, kwani ndiyo bao langu la kwanza la Ligi Kuu Bara," anasema.

ZD 02 (1)

HUMWAMBII KITU KUHUSU PILAU

Anasema chakula anachokipenda ni pilau nyama kwa sababu mama yake alikuwa anapenda kumpikia.

"Nikikumbuka maisha tuliyopitia ndiyo maana mambo mengi siwezi kuyasahau kwa sababu hata huku kupenda pilau ni kutokana na mama yangu alikuwa anapenda ananipikia, kila safari ya maisha yangu imejaa matukio nisiyoyasahau."


JOB HATARI

Licha ya kupambana na mabeki wa timu mbalimbali hapa nchini, ila Zidane anasema beki anayemsumbua kila wanapokutana ni Dickson Job wa Yanga kutokana na aina ya uchezaji wake, huku akiweka wazi ni mtu anayejua kusoma hatari za wapinzani.

"Ni beki mzuri anayejua kusoma hatari za washambuliaji kwa sababu ana akili sana, kwangu ndiye anayenisumbua kila tunapokutana."


ANAPENDA USHAURI

Sio kila mtu anapenda kushauriwa au kukosolewa pale anapokosea ila kwa Zidane ni tofauti kabisa kwani nyota huyo hupenda kufanyiwa hivyo ikitokea kakosea, akiamini ni njia mojawapo ya kumkuza kiakili na kumfanya azidi kuonyesha ubora wake.

"Ninapokosea huwa napenda sana nikiambiwa ukweli kwa sababu naamini ni njia ya kunifundisha, huwa sikasiriki hata siku moja bali inaniongezea morali ya kuzidi kupambana ili nifanye kitu kilicho bora kitakachowafurahisha mashabiki zangu."