Ufahamu mchezo wa mbio za vitanda

Muktasari:
- Achana na mchezo wa mbio za ngumi, mchezo mwingine wa kuburudisha ni wa mbio za kwenye kitanda ambao asili yake ni Uingereza.
KAMA unadhani umetazama michezo yote na huujui mchezo wa mbio za kitanda, basi soma hapa. Duniani kuna michezo mingi na baadhi imekuwa na umaarufu mkubwa kama mpira wa miguu, lakini mingine haijapata umaarufu ingawa ni burudani kuitazama ikichezwa.
Achana na mchezo wa mbio za ngumi, mchezo mwingine wa kuburudisha ni wa mbio za kwenye kitanda ambao asili yake ni Uingereza.
ASILI YAKE
Mashindano ya mbio za vitanda yalianza 1966 katika mji wa Knaresborough, Uingereza, chini ya shirika la Knaresborough Round Table ambalo lilikuwa likijumuisha vijana waliokuwa wakifanya kazi za jamii.
Lengo la kuanzisha mashindano hayo ilikuwa ni kuchangisha fedha kwa ajili ya shughuli za kijamii, kudumisha mshikamano na kutoa buruani. Tangu wakati huo tukio hilo limekuwa likifanyika kila mwaka, likijumuisha mashi-ndano ya kusukuma vitanda kwa umbali wa maili 2.4 ikiwa ni pamoja na kuvuka mto Nidd.
Katika miaka ya 1980 na 1990, mchezo huo ulianza kuchezwa katika maeneo mengine, hasa katika miji mbalimbali huko Marekani, Australia, Ujerumani na hata baadhi ya vyuo vikuu Afrika na Asia.
Katika mji wa Louisville, Kentucky, mashindano hayo ni sehemu ya sherehe za Kentucky Derby Festival, ambapo timu zaidi ya 30 hushiriki kila mwaka. Pia vyuo vikuu kama Lehigh University na University of Texas at Arlington huandaa mashindano hayo kama sehemu ya kuimarisha mshikamano wa wanafunzi.

MASHARTI
Kila timu huwa na wachezaji sita - watano husukuma au kuvuta kitanda na mmoja hukaa juu ya kitanda kama abiria.
Kitanda ni lazima kiwe na magurudumu manne au zaidi na pia kinatakiwa kusukumwa kwa mikono, hairuhusiwi kuwa na injini au nguvu za umeme. Ukubwa na uzito wa kitanda huwa na mipaka maalumu kulingana na mashindano na mara nyingi kitanda hupambwa kwa ubunifu, lakini mapambo hayapaswi kuathiri usalama.
Mchezaji anayelala katika kitanda anatakiwa kuvaa helmeti kwa ajili ya usalama wake ikitokea akadondoka. Timu zote haziruhusiwi kusukumana au kuharibu vitanda vya timu nyingine na waandaaji hufanya ukaguzi wa vitanda kabla ya mashindano ili kuhakikisha vinafaa.
Vilevile njia ya mashindano huwa na urefu uliowekwa (mfano: kilomita 2 au zaidi), ambapo timu hupangwa kuanza kwa ratiba au muda tofauti (kama ni mashindano ya muda). Baadhi ya mashindano hujumuisha vizuizi vya asili kama kupanda mlima au kuvuka maji (kwa mfano kuna mashindano ya Knaresborough Bed Race). Kunywa pombe kabla au wakati wa mashindano ni marufuku.

VIGEZO
1. Umri wa Washiriki
Kiwango cha chini cha umri hutegemea na mashindano, lakini kwa kawaida wasukuma kitanda lazima wawe na umri wa miaka 16 au zaidi, lakini abiria anaweza kuwa mtoto, ingawa lazima awe na ulinzi na vifaa vya usalama. Kwa mashindano ya shule huwekwa madaraja maalumu kwa wanafunzi.
2. Usalama
Abiria lazima avae helmeti (kofia ngumu ya kinga) na timu zote zinatakiwa kuhakikisha kitanda hakina ncha kali au vitu hatari, kina breki au udhibiti wa kasi katika maeneo hatari na hakuna kusukumana, kugongana au kutumia lugha chafu dhidi ya timu nyingine.
3. Malipo ya Usajili
Timu nyingi hutakiwa kulipa ada ndogo ya usajili ambayo husaidia kugharamia ulinzi, vibali vya barabarani, gharama za tukio na kuchangisha fedha kwa hisani.

4. Utii wa sheria za mashindano
Timu lazima zisome na zikubali sheria rasmi kabla ya kushiriki na ukiukaji wa sheria (kama vile kubadilisha abiria katikati ya mashindano au kutumia vitanda visivyokubalika) kunaweza kusababisha onyo, faini au kufutwa kabisa kwenye mashindano.
ZAWADI
Katika mashindano hayo timu ya kwanza kumaliza mbio ndio huhesabika kuwa bingwa, lakini mara nyingi washiriki wa mchezo huingia kwa sababu ya kurudisha kwa jamii, hivyo lengo huwa sio kupata pesa badala yake kusaidia kukusanywa pesa ambazo zitakwenda kusaidia watu wenye uhitaji.
Kwa mashindano yanayofanyika Uingereza, mara nyingi washindi hupata vyeti na vikombe ili kutambua ushindi. Kwa upande wa Marekani mashindano hayo yanadaiwa kuwekewa zawadi ya pesa hususan yale ya shuleni ambapo huwa Dola 300 kwa mshindi wa kwanza, wa pili Dola 200 na wa tatu Dola 100.