Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yohana: Kwa tizi, Dube ni msumbufu balaa

Muktasari:

  • Kama hufahamu Dube ni mchezaji mwenye akili kubwa, alijitafutia kocha wa maana kimyakimya akawa anamsimamia kila kitu kuhusu mazoezi ya kutunza mwili ambaye Mwanaspoti linamtoa mafichoni mwalimu huyo aliyefunguka mambo kadhaa kuhusu mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe.

WENGI wanajiuliza mshambuliaji wa Yanga, Prince Dube, amewezaje kuendelea kuwa bora licha ya kukaa nje ya uwanja kwa takriban miezi sita bila kucheza wakati akipambana kuachana na Azam FC.

Kama hufahamu Dube ni mchezaji mwenye akili kubwa, alijitafutia kocha wa maana kimyakimya akawa anamsimamia kila kitu kuhusu mazoezi ya kutunza mwili ambaye Mwanaspoti linamtoa mafichoni mwalimu huyo aliyefunguka mambo kadhaa kuhusu mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe.

Yohana Ulanda, ndiye mwalimu wa mazoezi binafsi wa Dube na kaeleza mambo mbalimbali ya taaluma yake hiyo ambayo mastaa wengi wa soka wameshtuka na kujipa ratiba ya kujiweka sawa kabla ya mazoezi ya timu zao kama ambavyo wanafanya wachezaji wakubwa wa Ulaya.


AKUTANA NA DUBE

Yohana anaeleza kwamba, alikutana na mwana mfalme huyo wakati anapiga kazi katika gym moja iliyopo Kigamboni, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

"Mara ya kwanza nakutana na Dube ilikuwa Kigamboni kwenye gym moja ambayo nilikuwa nafanyia kazi. Alikuja hapo  nakumbuka ilikuwa Novemba au Desemba, mwaka jana. Alikuja pale nadhani ni ule wakati ambao alikuwa nje ya timu yake (Azam) alikuwa hachezi mpira. Kwa hiyo akataka awe anajipa mazoezi ya kuutunza mwili wake," anasema Yohana.

"Watu wengi wakati huo walikuwa wanaona kama Dube alikuwa amekaa tu, hapana. Jamaa ana akili nyingi, alijua ambacho kingemtokea kama asingekuwa anafanya mazoezi. Anapenda sana mazoezi kuna muda alikuwa ananisumbua hata kama sina ratiba naye, lakini anakuomba ukampe mazoezi.

"Siku ambayo alikuja kwenye gym pale alikuja kama mteja wa kawaida wa kukimbia kwenye mashine. Akanifuata, akaniambia ameniona nawafundisha watu na kama naweza kumpa mazoezi, nikamwambia inawezekana, tukandaa programu na kuanza baada ya siku chache. Akaniambia malengo yake kipi anataka."

Hata hivyo, wakati Dube anatua kwa Yohana, alimweleza juu ya kuandamwa mara kwa mara na majeraha kutokana na shughuli yake uwanjani.

"Alinieleza kuwa kitu kikubwa anachokichukia ni kuambiwa ana pancha nyingi (majeraha). Kwa hiyo akataka apewe ratiba ya mazoezi makali ikiwezekana mara mbili ya yale anayoyafanya ili awe fiti aonyeshe ubora wake," anasema.

"Nadhani mmemuona. Sasa siwezi kusema hawezi kuwa majeruhi, lakini amekuwa na mabadiliko makubwa na yuko fiti ndio maana mnaona anafanya vizuri akiwa na Yanga. Mengine niliyoacha ni ya ufundi ambayo hayo yatawahusisha makocha wake wa klabu."

MISOSI, USUMBUFU

Wakati mkufunzi huyo akiyasema hayo, lakini kumbe Dube kumbe ana kitu kingine ambacho kipo nyuma ya pazia na ndicho kinachmfanya hivi sasa atese uwanjani.

"Dube wakati akiwa nje alikuwa anazingatia mambo mengi. Kuna wakati alikuwa ananiomba nimuelekeze aina ya vyakula ambavyo anatakiwa kula ili autunze mwili wake na ukimwambia anafuata. Akiwa anakula anakutumia picha kabisa uone. "Kingine ni msumbufu wa kufikia malengo, kama kuna ratiba hamjaikamilisha atakusumbua mpaka ikae sawa ili akamilishe kile anachokitaka kuhusu mazoezi," anasema Yohana.

Kama ulikuwa unamchukulia poa mchezaji huyo kuwa tu wa matawi ya juu, basi sahau na hapa Yohana anaweka wazi: "Dube anaweza kuwa tofauti na wachezaji wengine mastaa. Ana nidhamu kubwa kwa wadogo hata wakubwa, sio rahisi kupita bila kukusalimia kama mkikutana naye atakupa salamu na kuendelea na mambo yake. Siyo aina ya wachezaji wanaojisikia, hata wateja wangu wengine wanajikuta wanamfurahia juu ya nidhamu yake. Lakini kingine anaheshimu muda, mkikubaliana mnaanza mazoezi saa 12, basi dakika kumi kabla utamkuta yuko hapo anakusubiri."


KILICHOONGEZEKA KWA DUBE

Kwa Yohana, kuna kitu anakiona kimeongezeka kwa mchezaji huyo sawa na mashabiki wanavyoona namna anavyofanya uwanjani, akitupia na kuwatesa mabeki wa timu pinzani kwa namna atakavyo.

"Kwenye ratiba kubwa ya mazoezi yangu na Dube huwa anataka sana kujiimarisha kwenye pumzi. Tutafanya mazoezi yote lakini zoezi la pumzi analitaka sana niliwahi kuweka video moja ya mazoezi yake hayo, nilimkimbiza sana," anasema.

"Ninapokuwa namfundisha mchezaji, lazima nimfuatilie kwenye klabu anayocheza kipi kipo sawa, kipi kinapungua na anahitaji tufanyie kazi kipi ili awe kwenye ubora mkubwa. Kwa Dube tangu awe kwangu kwanza, ameongezeka kuwa fiti siyo Dube yule ambaye unaweza kumsukuma na akaanguka, na ana kasi.

"Mwili wake umekuwa na nguvu sana. Unaona namna anavyopambana na mabeki, lakini bado kasi yake iko juu na nguvu iko sawasawa kwa pande zote za mwili. Bahati nzuri nafasi yake inamtaka kufunga na ameanza na moto mzuri wa kufunga kwa mitindo tofauti. Lakini hata zile mechi ambazo hajafunga huwa nampa nguvu kwa kumwambia amshukuru Mungu na aendelee na mapambano.

"Ratiba yetu ya mazoezi inategemea na ya timu yake. Unajua haya ni mazoezi ya ziada, kwa hiyo kama anakuwa ana muda wa kupumzika ananiambia mwalimu wiki hii nina siku hizi tunaweza kuendelea, lakini kuna wakati anabanwa, anakwenda labda mazoezini asubuhi akirudi anapumzika na jioni wanarudi tena kuna wakati tuliwahi kufikisha mpaka wiki mbili mpaka tatu hatukufanya mazoezi yoyote kutokana na ratiba ya timu yake na yetu ni mara moja tu kwa siku na huwa haizidi saa mbili.

"Anapokuwa na mechi huwa kuna ujumbe mfupi namtumia. Namtakia kila la heri na kumwambia kaka nenda kafanye vizuri nijivunie kufanya kazi na wewe. Dube ni mchezaji mwenye imani sana, atanijibu Mungu akipenda. Labda nisema hili akiwa hapa mazoezini kabla na hata akimaliza utamuona anamuomba Mungu, akitaka kuanza na anamshukuru akimaliza ni kama mnavyomuona akiwa kwenye mechi."

Yohana anafichua kwamba Dube humueleza mipango mingi ya kutaka kufanya mambo makubwa ndani ya Yanga, na mkufunzi huyo anasema: "Nikiwa naye mazoezini kuna muda unamuona anawaza halafu anakwambia 'kaka kuna kitu kikubwa nataka kuifanyia hii timu'. Huwa namwambia mbona unakifanya, anasema 'hapana hivi ninavyovifanya ni vitu vya kawaida ila kuna makubwa nitayafanya hapa Yanga'.

"Kauli hizi nikiangalia na juhudi zake mazoezini huwa naona kabisa Yanga imepata mchezaji bora ambaye kama ataendelea hivi atawafanyia mambo makubwa wakiwa naye."

ANAUMIA AKICHEKA

Unavyomuona Dube akiwa uwanjani na hata nje ya uwanja mara nyingi ni mchezaji asiyeweza kuficha tabasamu, na mkufunzi wake wa mazoezi anasema huwa anaumia mazoezini, lakini anacheka.

"Mnavyomuona Dube anapenda kutabasamu, basi hata mazoezini huwa inatokea. Sina maana kwamba muda wote anatabasamu, hapana. Kuna wakati anaweza akawa anaumia na mazoezi makali, lakini anakuomba huku anatabasamu anakwambia 'kocha hii inauma' na mimi namwambia akazane hapo anapoumia ndio anaingiza kitu na anapambana kweli."

Lakini kama ulikuwa hujui, basi elewa kwamba pia Dube anakielewa Kiswahili.

"Dube anajua Kiswahili fasaha na usije ukamsema ukajua hajui. Lakini pia anazungumza Kiingereza, akija hapa mara nyingi anaongea Kiswahili tunaelewana vizuri. Nakumbuka mara ya kwanza alipokuja nikawa naongea naye kwa Kiingereza akaniambia kaka nataka kujifunza Kiswahili zaidi naomba ukitaka kuongea na mimi tutumie Kiswahili."

MASHABIKI WA YANGA

Yohana anaeleza kuwa video ambazo huwa anaziweka kwenye mitandao ya kijamii akimfua Dube huwa anajikuta anacheka kutokana na ujumbe wanaotuma mashabiki wa Yanga.

"Kuna wakati napokea simu za mashabiki na hata ujumbe mfupi wakizungumzia tunachofanya na Dube. Wapo wanaopongeza kazi yangu, wengine wanampongeza Dube, lakini wengine wanachekesha. Kuna mmoja amewahi kusema ole wangu Dube avunjike hata kidole sisi tutapambana na wewe, basi najikuta nacheka tu. Ndiyo mashabiki wetu hao," anasema Yohana.

"Kuna mashabiki wengine wanakupigia simu wanataka kuja kufanya mazoezi, lakini wanauliza Dube anafanya wakati gani ili nao waje muda huo wakijua watamkuta. Sasa huwezi kuwapa muda huo kwa kuwa hutakiwi kuwakutanisha mashabiki na wachezaji ili kumpa muda mzuri mwanafunzi wako azingatie mazoezi yake."


WENGINE ANAOWAFUNDISHA

Yohana ni mkufunzi wa mastaa kibao wa soka na miongoni mwao ni hawa.

"Siyo Dube tu nafanya naye kazi, nina wachezaji wengi mfano Juma Mahadh ni mwanafunzi wangu, Moses Phiri wakati akiwa Simba alikuwa mwanafunzi wangu, Pascal Msindo wa Azam FC, Tepsie (Evance wa Azam). Wapo wengine ambao hawataki mazoezi yao yawe wazi kwa jamii. Hili nalo ni muhimu kuliheshimu na hata wewe siwezi kukuambia, kwa hiyo nina wachezaji wengi," anasema mkufunzi huyo.

Yohana anasema ukiachilia kufundisha watu mbalimbali pia hata timu ya wanawake wa Yanga Princess wapo baadhi ya wachezaji anawapigisha tizi.

"Wachezaji wachache walinifuata, lakini mwisho wakaongezeka na kuwa wengi. Wengine walikuwepo msimu jana, lakini wapo ninaoendelea kuwafundisha, hivyo sio wanaume tu niko pande zote."

KUPIMA AFYA

Mkufunzi huyo amepangilia vyema ratiba kwa ajili ya watu wake ili kuhakikisha kwamba wanapata kile wanachokitaka.

"Mteja wangu yeyote kabla ya kuanza programu lazima kuna vitu nitaongea naye kwa kumuuliza ili nifahamu na kitu cha msingi ni juu ya kupata taarifa kamili ya afya ikiwezekana hata kwa kupima na baada ya hapo mnaanza kazi," anasema.

"Tunafanya hivi kwa sasabu kuna matatizo mengine hayaruhusu mtu aliye nayo kufanya baadhi ya vitu, kundi lake la damu, kama ana matatizo ya presha ya kupanda au kushuka, ana mshono maana hao wana mazoezi yao ambayo siyo kila kitu kinaweza kufanyika kwao.

Hata hivyo, kwa wachezaji kuna tofauti kidogo.

"Hii ratiba ya mazoezi ni binafsi kwa mchezaji. Sina sababu wala mchezaji hana sababu ya kuomba kibali cha kuja kufanya mazoezi na mimi. Ila upo wakati anaweza kuja kuniambia kocha amemwambia anataka aimarishe kitu fulani, sasa kama kipo katika eneo ambalo naweza kulifanyia kazi kwa taaluma yangu tunalifanyia kazi. Kwa hiyo sina sababu ya kuomba kibali kutoka kwa klabu au makocha wake," anasema.


ALIVYOANZA KAZI

Yohana anasema ukufunzi wa mazoezi aliianza miaka 10 iliyopita. "Nina miaka 10 kwenye hii kazi kuanzia mwaka 2013. Unapofanya kitu ambacho unapenda unatakiwa kukipambania. Kazi yetu wakati mwingine unaifanya hata saa 24 tukiwa humu ndani. Kuna nyakati unakosa hata muda wa kupumzika ili uwe unapatikana."

"Kwanza kutangulia kuipenda kazi na baada ya hapo unaamua kufuata utaratibu kwa kuisomea ili uifanye kama taaluma zaidi. Baada ya hapo nikaenda kuisomea. kuna kozi yake maalumu, wapo baadhi ya walimu wanakuja hapa Tanzania na kufundisha wanatoka nje ya nchi," anasema.

"Taaluma hii yetu inategemea unataka uwe mwalimu wa mazoezi ya aina gani. Kama unataka kuwa mwalimu wa mazoezi ya kuimarisha mwili hapo utasoma kozi fupi na zingine zipo za miaka kadhaa. Ukisema usome kwa muda mrefu huwezi kupata watu watakaokusubiri uje uwafundishe, ndio maana wengi tunasoma hizi za muda mfupi ambazo utasoma kwa wiki mbili au wiki moja na nusu.

"Mimi nimejikita kwenye mazoezi ya physic, aerobic, Yoga, riadha, kunyanyua vitu vizito, lakini tunajikuta muda mwingi tunafanya kazi na wale wateja ambao wanataka kupunguza uzito wa mwili na wawe fiti. Wateja wetu sana ni wale ambao wanataka kupungua unene, naweza kusema hao ni kama asilimia 60 ya wateja wangu. Wanawake ndiyo wengi sana kuliko wanaume."

Ukitaka kupiga tizi kwa Yohana, basi zingatia hili. "Malipo inategemea nakufundisha kipi, kama ni gym au namfuata (mtu) huko alipo. Kila eneo lina malipo yake kutegemea na umbali ulivyo, lakini kama unakuja hapa gym ni Sh 200,000."