Yanga yashtua Afrika! rekodi zageuka gumzo

Yanga yashtua Afrika! rekodi zageuka gumzo

YANGA imeendelea kuboresha rekodi yake ya kucheza mechi mfululizo za Ligi Kuu Bara bila kupoteza, ikifikisha 41, baada ya Jumanne wiki hii kuifumua Mtibwa Sugar kwa mabao 3-0 katika pambano lililopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.

Mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mechi katika ligi hiyo ilikuwa ni Aprili 25, mwaka jana ilipolala kwa bao 1-0, lililowekwa kimiani kwa mshuti wa mbali wa straika wa Azam FC, Prince Dube na baada ya hapo, timu hiyo chini ya Nasreddine Nabi imepata matokeo ya ushindi na sare tu.

Kabla ya Yanga kuweka rekodi hiyo mpya nchini, timu ya Azam ndio iliyokuwa ikiishikilia ya kucheza mechi 38 bila kupoteza, rekodi iliyodumu kwa muda wa miaka saba na miezi na siku 26 ambayo ni sawa na siku 2856 kabla ya vijana wa Jangwani kuivunja msimu huu.

Azam iliandika rekodi hiyo kwa kuunganisha mechi za misimu mitatu tofauti yaani 2012-2013, 2013-2014 na 2014-2015 kama ilivyofanya Yanga iliyounganisha 2020-2021, 2021-2022 na 2022-2023.

Azam iliweka rekodi hiyo baada ya kutoka kufungwa na Yanga bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Februari 23, 2012 na baada ya hapo ikacheza mechi nane zilizofuata za kumalizia msimu huo wa 2012-2013 bila kupoteza na kuunganisha mechi 26 za msimu wa 2013-2014.

Katika msimu huo ndio Azam ilibeba taji lake la kwanza na la pekee la Ligi Kuu Bara kisha kucheza mechi nyingine nne za msimu wa 2014-2015 bila kupoteza.

Hata hivyo, mechi yao ya nyumbani ya Okt 25, 2014 dhidi ya maafande wa JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania) mambo yalitibuka baada ya kuchapwa bao 1-0 na kuifanyia Azam ikwamie kwenye idadi ya mechi 38 ikicheza bila kupoteza, rekodi iliyodumu karibu miaka nane kabla ya Yanga kuifikia na kisha kuipita msimu huu wa 2022-2023.

Yanga ilifikia rekodi ya Azam msimu huu baada ya kuifunga Polisi Tanzania kwa mabao 2-1, baada ya msimu uliopita kufikisha mechi 37, zikiwamo saba za msimu wa 2020-2021 na 30 ilizocheza msimu uliopita ilipobeba ubingwa bila kupoteza kama ilivyofanya Azam.

Kisha ikaivunja ilipoifumua Coastal Union mabao 2-0 kabla ya kufikia mechi ya 40 ilipotoka sare ya 2-2 na Azam na Jumanne wiki hii ilipoishinda Mtibwa, imefikisha jumla ya mechi 41 katika ligi bila kupoteza hadi sasa.


REKODI ZA KIBABE

Japo Azam ilidumu na rekodi yake kwa miaka nane, lakini rekodi ya Yanga imeifanya ijipe ugumu yenyewe na hata kwa timu nyingine, kuweza kuja kuirudia tena siku za baadaye kwa idadi hiyo ya mechi na ushindani mkubwa ulioongezeka katika ligi nchini.

Utamu wa rekodi ya Yanga ni kupata ushindi wa mechi nyingi za ugenini kulinganisha na ilivyokuwa kwa Azam, kwani kumbukumbu zinaonyesha Azam katika mechi zake 38 ilicheza 18 ugenini na kushinda 11 na kutoka sare saba ikifunga mabao 25 na kufungwa saba na kuvuna jumla ya pointi 40, ilihali kwa nyumbani ilicheza michezo 20 na kushinda 15, ikipata sare tano na kufunga mabao 47, huku ikiruhusu 14 na kukusanya jumla ya pointi 50.

Kwa ujumla Azam katika mechi zake 38, ilishinda 26 na kutoka sare 12, ikifunga mabao 72 na kuruhusu nyavu zao kuguswa mara 21 na kuvuna jumla ya pointi 90

Kwa upande wa Yanga katika mechi hizo 41, imecheza 22 ugenini na kushinda 15, ikitoka sare saba, ikifunga mabao 30 na kuruhusu nane, huku ikikusanya jumla ya pointi 52, wakati kwa nyumbani imecheza mechi 19, ikishinda 15, ikidroo nne tu na kufunga mabao 39, huku ikifungwa saba na kujibeba jumla ya pointi 49.

Kupitia mechi 41 ilizocheza imeshinda mechi 30, ikitoka sare michezo 11 na kufunga mabao 69, imeruhusu mabao 15 tu na kujikusanyia jumla ya pointi 101, kuonyesha wababe hao wa Jangwani wana balaa sio mchezo, japo idadi ya mabao kwa mechi ilizocheza imeonyesha udhaifu mkubwa, licha ya uimara wa ukuta wao kuruhusu mabao machache kuliko Azam.


MUDA MCHACHE ZAIDI

Ukirejea rekodi ya Azam utabaini ilitokana na kipigo kutoka kwa Yanga, iliyowachapa bao 1-0 katika mechi iliyopigwa Februari 23, 2012 na kukaza buti na kuzitimiza mechi hizo 38 kabla ya maafande wa JKT kuwatibulia Oktoba 25, 2014 ikiwa na maana wababe hao walitumia miaka miwili na miezi miwili na siku mbili sawa na siku 975 bila kuonja machungu ya kipigo.

Lakini ukirejea kwa Yanga, imetumia muda mfupi zaidi kuifikia na kuivunja rekodi hiyo ya Azam na kuiboresha zaidi ikitumia jumla ya siku 506 tu ambazo ni sawa na mwaka mmoja na miezi minne na siku 19 kufikisha idadi ya mechi zote 41.

Kama umesahau ni kwamba ni Azam hao hao ndio walioipa akili Yanga kukaza kwenye mechi hizo kama wao walivyoamshwa walipolala mbele ya Vijana wa Jangwani.

Yanga ilipoteza mechi ya mwisho mbele ya Azam Aprili 25, 2021 kwa bao la Prince Dube akimtungua kipa Faruk Shikhalo ambaye kwa sasa yupo Mtibwa Sugar na baada ya hapo wababe hao wamekuwa wakitoa vipigo ama kuambulia sare na kuweka historia hadi sasa.


SASA HADI LINI?

Kilichosalia kwa sasa ni mashabiki kusubiri kuona rekodi hii ya Yanga ya kucheza mechi mfululizo bila kupoteza itadumu hadi lini kabla ya kuja kutibuliwa na pia kutaka kuona itadumu kwa miaka mingapi baada ya ile ya Azam ya mechi 38 kudumu kwa miaka kama nane.

Je, ni maafande watakaowatibulia kama ilivyowatokea Azam kwa JKT Ruvu, ikizingatiwa msimu huu kuna timu tatu tu za maafande ambao ni Polisi Tanzania iliyokubali kipigo kwenye ufunguzi wa msimu huu. Pia ipo Tanzania Prisons na Ruvu Shooting ambao ndio itakayotangulia kucheza na watetezi hao wa Ligi Kuu. kabla maafande wenzao wa Prisons kufuata baadae.

Ngoja tuone.