Yanga v Tanzania Prisons... Kwani nyie mnatakaje?

Muktasari:
- Ikiwa tayari baadhi ya timu zimekamilisha duru la kwanza kwa kushuka uwanjani mara 15 kila moja, Tanzania Prisons leo ndio inahitimisha, ilihali Yanga itakuwa michezo 13 na kusaliwa na viporo viwili dhidi ya Dodoma Jiji na Fountain Gate.
NI siku nyingine tena mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga SC inashuka dimbani kukabiliana na Tanzania Prisons katika mwendelezo wa ligi hiyo inayokaribia kufika ukingoni mwa duru la kwanza.
Ikiwa tayari baadhi ya timu zimekamilisha duru la kwanza kwa kushuka uwanjani mara 15 kila moja, Tanzania Prisons leo ndio inahitimisha, ilihali Yanga itakuwa michezo 13 na kusaliwa na viporo viwili dhidi ya Dodoma Jiji na Fountain Gate.
Katika mchezo wa leo utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam kuanzia saa 10:00 jioni, Yanga inaingia ikiwa imetoka kufanya yao uwanjani hapo mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa.
Huu utakuwa mchezo wa pili kwa watetezi hao kwenye uwanja huo, baada ya ule wa Mashujaa iliyowanyoa mabao 3-2, huku Prince Dube akipiga hat trick na kuweka rekodi ya kuwa nyota wa kwanza kufanya hivyo msimu huu, lakini utakuwa mchezo wa kwanza wa Prisons kukutana na Yanga msimu huu, huku ikiwa haipo vizuri uwanjani.

YANGA IMEANZA KUJIPATA
Baada ya kuichapa Mashujaa, ni kama Yanga imeonekana kuanza kujipata kwani katika mchezo huo ilicheza soka la kuvutia.
Zile pasi za gusa, achia twende kwao zilionekana katika mchezo huo ambao ulikuwa na kikosi chenye mabadiliko makubwa kufuatia kukosekana kwa baadhi ya wachezaji akiwemo kipa namba moja, Djigui Diarra ambaye ni majeruhi, huku pia Maxi Nzengeli na Clatous Chama nao wakikosekana kutokana na majeraha.
Tulimshuhudia Kibwana Shomari akicheza mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya kukaa nje kwa muda mrefu na alionyesha kiwango kizuri huku akifanikiwa kutoa asisti ya bao la tatu.
Tofauti na Yanga iliyocheza mechi nne zilizopita, zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Ligi Kuu dhidi ya Namungo ikiwa chini ya Kocha Sead Ramovic, timu ikionekana kucheza kinyonge na kupoteza hovyo mipira, dhidi ya Mashujaa mambo yalibadilika ikionekana wachezaji wamechangamka hali iliyochangia ushindi huo uliowarudisha kwenye morali kubwa.

Katika mchezo wa leo, tunaweza kushuhudia hilo likiendelea kutokea kwani hesabu za Yanga ni kuhakikisha mechi hizi tatu zilizosalia inashinda zote ili kufikisha pointi 39 zitakazowaweka sehemu nzuri zaidi ya sasa.
Ikiwa hivi sasa Yanga ina pointi 30 katika nafasi ya tatu, inafahamu ushindi kwenye mechi ya leo kwa tofauti ya mabao matatu utawapandisha juu ya Azam iliyo na pointi 33 licha ya kwamba zitalingana pointi.

PRISONS WANYONGE
Ukiachana na rekodi ya mechi zao tano za mwisho katika ligi ikiwa imeshinda moja pekee kama ilivyo upande wa sare huku ikipoteza tatu, kwa ujumla Prisons ni wanyonge mbele ya Yanga.
Rekodi zinaonyesha kwamba, timu hizo tangu msimu wa 2012-2013 hadi sasa zikiwa zimekutana mara 24 kwenye ligi, Yanga haijawahi kupoteza mechi yoyote mbele ya Prisons baada ya kushinda 16 na sare nane.
Katika mechi tano za mwisho baina yao, Yanga imeshinda nne mfululizo wakati sare ni moja. Matokeo yakiwa hivi; Yanga 4-1 Prisons, Prisons 1-2 Yanga, Prisons 0-2 Yanga, Yanga 1-0 Prisons na Yanga 0-0 Prisons.
Rekodi hizo zinadhihirisha kwamba Prisons ina kazi kubwa ya kufanya kwenda kuikabili Yanga ili kujitoa kwenye nafasi mbaya kwenye msimamo kitu ambacho kinaonekana si rahisi ingawa katika soka lolote linawezekana.

Ukiangalia msimamo wa ligi ulivyo, Prisons inashika nafasi ya pili kutoka chini ikiwa na pointi 11 baada ya kushinda mechi mbili, sare tano na kupoteza saba ikiwa imefunga mabao sita pekee na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 13.
Kazi kubwa kwa Prisons ni kuhakikisha inawazuia kwanza Yanga wasifunge bao ambayo hadi sasa imefunga 19 na kuruhusu sita pekee ikionekana kuwa vizuri kwenye kulinda na kushambulia pia.
Prince Dube aliyetoka kupiga hat trick, anaonekana kuwa na uchu wa kuendelea kufunga baada ya kufikisha mabao matatu na kuwa kinara wa ufungaji kikosini hapo sawa na Pacome Zouzoua na Maxi Nzengeli ambaye kwa sasa anauguza majeraha.
Prisons yenye mabao sita, hakuna aliyefunga zaidi ya bao moja hivyo haina mchezaji ambaye inamtegemea katika kucheka na nyavu kitu ambacho kwenye timu ya ushindani hakionyeshi picha nzuri.
Mabao hayo sita yamefungwa na Nurdin Chona, Ezekia Mwashilindi, Vedastus Mwihambi, Oscar Mwajanga, Jumanne Elifadhili na Meshack Abraham.
Hata hivyo, unyonge huo wa Prisons usichukuliwe kwamba Yanga itakuwa na mchezo mwepesi kwani inafahamika wapinzani wao wamekuwa wakicheza soka la nguvu licha ya kwamba haina matokeo mazuri.
Prisons itakuwa na mabadiliko ya benchi la ufundi huku taarifa zikibainisha kwamba kocha wao mkuu, Mbwana Makata na msaidizi wake, Renatus Shija wamewekwa pembeni na kikosi hicho kimekabidhiwa kwa Shaban Mtupa aliyeanza kuisimamia tangu Desemba 18, 2024 katika maandalizi ya mchezo huu.
“Najua mechi ijayo ni dhidi ya Yanga ugenini, nimeona vijana wana ari na morali, tutaenda kupambana na kufanyia kazi sehemu yenye upungufu hasa dirisha dogo ili kufanya vizuri.
“Tumeandamwa sana na majeruhi kikosini, lakini tutaboresha, nina uzoefu na timu na lolote linawezekana, tupeane sapoti na muda,” alisema Mtupa.
KAULI ZA MAKOCHA
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema: “Tuna mchezo mgumu mbele yetu, tunachukua tahadhari dhidi ya timu ambayo inajilinda zaidi huku tukijaribu kuvunja mstari wao wa mwisho.
“Tumecheza siku mbili zilizopita, tunacheza tena, si kitu rahisi, tunapaswa kufanya vizuri kwa sababu tunazihitaji pointi tatu.
“Siangalii yaliyopita hata kama hawajawahi kushinda dhidi yetu, kila siku tunapoingia uwanjani unakuwa ni mchezo mpya, tunaweka nguvu kwa asilimia zote kusaka ushindi, tunawaheshimu wapinzani wetu.
“Katika mazoezi ya mwisho tutaangalia mchezaji gani yupo fiti na yupi ana shida lakini tunaiandaa timu ya kufanya vizuri.”
Kaimu Kocha Mkuu wa Prisons, Shaban Mtupa, alisema: “Kama mnavyojua nimeingia siku chache zilizopita kwenye timu kama kaimu kocha mkuu, lakini vitu vikubwa nimeviangalia uwanja wa mazoezi ni kurudisha morali ya wachezaji ambayo unaona kabisa ilikuwa chini. Kitu kingine nilichokifanya ni kuamsha hali ya kujiamini kwa vijana wangu.

“Kama mnavyojua mchezo wa kesho ni muhimu sana kwetu, hatujapata matokeo mazuri huko nyuma, Yanga ni timu nzuri, tunacheza na timu nzuri yenye wachezaji wenye uwezo wa kubadili matokeo muda wowote, siku tatu za mazoezi tumelifanyia kazi hilo kuona katika madhaifu yao tuyatumie vizuri.
“Tunacheza na timu ambayo tunatakiwa kuwa makini muda wote kwani tukipoteza umakini hata kwa sekunde mbili tutaathirika, vijana wakiamka na afya njema na kufuata maelekezo tuliyowapa kwenye uwanja wa mazoezi naamini tutapata matokeo mazuri.”