Yanga SC, Azam FC vita nd'o imeanza

Saturday September 11 2021
AZAM PIC

ULE wakati wa lawama umewadia wakati msimu mpya wa michuano ya klabu Afrika 2021-22 itakapoanza wikiendi hii baada ya jana kuzinduliwa kwa michezo kadhaa ukiwamo wa Biashara United waliokuwa ugenini dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti.

Biashara inashiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na jana ilishinda bao 1-0.

Wawakilishi wengine wa Tanzania Azam na KMKM watashuka dimbani leo na kesho itakuwa zamu ya Yanga na Mafunzo, huku mashabiki wakiwa na kiu kubwa ya kupata burudani na kuona kama timu zao zitatoboa.

Azam itakuwa wenyeji wa Horseed ya Somalia katika michuano ya Shirikisho Afrika, ilhali Yanga kesho wataialika Rivers United iliyotua jana mchana - mechi zote zikichezwa bila mashabiki.

Yanga inacheza na Rivers United ambayo rekodi zake katika mashindano hayo ya kimataifa sio za kutisha kama zilivyo timu nyingine, lakini hicho kikiwa si kigezo cha kuichukulia poa, sawa na ilivyo kwa Azam.

Azam ina faida ya kucheza mechi zote mbili jijini Dar es Salaam - ya kwanza itakuwa Uwanja wa Azam Complex na marudiano itacheza Uwanja wa Uhuru. Kutokana na mazingira hayo ni wazi ina nafasi kubwa ya kusonga mbele.

Advertisement

Mwanaspoti linakuletea makala inayoonyesha ugumu ambao Yanga na Azam zitakutana nao katika mechi hizo.


BILA MASHABIKI

Shirikisho la Soka Afrika (Caf), limeagiza mechi hizo hazitaruhusiwa mashabiki kungia viwanjani kushuhudia mapambano hayo kama ilivyokuwa katika mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Madagascar.

Kutokana na mihemko hasa kwa mashabiki wa Yanga wanaotamani kwenda kushuhudia timu yao ikicheza mashindano ya kimataifa baada ya kukosekana kwa misimu miwili ni wazi itakuwa moja ya changamoto kwa wachezaji na mashabiki wao.

Kama mashabiki wangeruhusiwa hamu yao ilikuwa kuwaona mastaa wao wapya, vilevile wanahamu ya kuiona timu ikishinda mechi ya kwanza ya mashindano. Ni wazi kwamba uwepo wao ungetoa mchango kwa kushangilia mwanzo mwisho.

Mashabiki wa Yanga wangeshangilia maana yake wangewapa mzuka wachezaji pamoja na benchi la ufundi kufanya vizuri wakati huo wachezaji na makocha wa Rivers United wangekubana na kikwazo.

Pia, suala hilo hata wale mashabiki wa Azam FC wangepata nafasi ya kwenda kuwaona nyota wao wapya wakicheza mechi ya kwanza ya mashindano - tena katika uwanja wa nyumbani wangetoa mchango kama ule wa Yanga na kuisukuma timu yao kufanya vizuri.


YANGA KUWAKOSA WATATU

Katika mechi ya Yanga ugumu mwingine ambao itakutana nao ni kuwakosa wachezaji watatu wapya ambao walitazamiwa kuingia katika kikosi cha kwanza kutokana na aina ya maandalizi ambayo walifanya katika kipindi chote walichokuwa pamoja kambini.

Yanga itawakosa Khalid Aucho, Djuma Shabani na Fiston Mayele ambapo Djuma na Mayele wamekuwa katika timu tangu kuanza kwa maandalizi nchini Morocco na wametumika katika mechi za kirafiki.

AZAM PIC 1

Kutokana na aina ya usajili ambao Yanga imeufanya kikosi chake kingekuwa na ubora zaidi kama kingepata huduma ya nyota hao watatu ambao uwezo wao ni mkubwa pamoja na uzoefu wa kucheza mechi za mashindano hayo.

Jambo zuri ni kwamba hati zao uhamisho za kimataifa (ITC) zilishafika nchini, ingawa zilitua baada ya dirisha la Caf kufungwa na kama rufaa ya Yanga waliyokata Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) kutaka wachezaji hao waruhusiwe kucheza ikikwama, basi itawatumia ikivuka hatua ya makundi.


MAANDALIZI YALIVYO

Licha ya kuwa na maandalizi ya kuugaunga, Yanga ina nafasi nzuri ya kupata matokeo mazuri nyumbani kama itashuka uwanjani na kiu ya kutaka kushinda mchezo huo dhidi ya Wanigeria, huku Azam FC kwa maandalizi ya Dar es Salaam na yale ya Zambia kuna kila dalili za kuwashinda Wasomali.

Mechi mbalimbali walizocheza kila moja kwa wakati wake zinaweza kuwa msaada kwa timu hizo mbili dhidi ya wapinzani wao, huku pia uwepo wa nyota kadhaa wenye uzoefu wa michuano ya Caf utawabeba hata kama watacheza mechi za leo na kesho bila mashabiki kuwepo viwanjani.


RIVERS KITAMBO

Ugumu mwingine ambao Yanga huenda ikakutana nao katika mchezo huo ni wapinzani wao Rivers United

walioanza maandalizi ya mechi kitambo pamoja na kucheza michezo ya kirafiki.

Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mchezo huo kwao Nigeria, Rivers United ilianzishwa mashindano ili kujiweka fiti kiufundi kwa kucheza mechi za kirafiki kujiandaa.

Kitendo cha kuanza maandalizi muda mrefu kabla ya mechi maana yake timu hiyo ilitaka kuimarisha kikosi ili kuwa cha ushindani katika mchezo dhidi ya Yanga inayotakiwa kuwa makini dhidi ya wapizani wao.


YANGA MPYA

Kikosi cha Yanga kina maingizo ya wachezaji wapya ambao wengi wao huenda wakapewa nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza ambacho kitakuwa kipya tofauti na kile cha msimu uliopita.

Kutokana na kukosa muda wa kutosha wa kufanya maandalizi huku kukiwa na wachezaji wengi ambao ni wapya ni wazi mastaa hao wa Yanga wanahitaji muda wa kutosha ili kuzoeana na wale ambao walimaliza msimu uliopita.

Upya huo wa kikosi kama wachezaji watashindwa kucheza kwa kuelewana na wale ambao walikuwapo katika kikosi msimu uliopita, maana yake watashindwa kufanya vizuri na kuwapa urahisi Rivers United kupata matokeo mazuri.

Katika mechi hiyo upya huo wa kikosi cha Yanga hautakiwi kuonekana licha ya changamoto mbalimbali inazokutana nazo. Hii ina maana kuwa inatakiwa kucheza kitimu ili kupata matokeo mazuri, lakini tofauti na hivyo lolote linaweza kutokea.


DUBE NJE AZAM FC

Ukiachana na changamoto ambazo Yanga inakutana nazo pamoja na ile ya wote ambao hawatapata nafasi ya kuingiza mashabiki uwanjani, Azam inapitia mitihani mingine.

Azam itamkosa straika wake bora wa msimu uliopita, Prince Dube katika mechi hiyo baada ya kupata majeraha yatakayomuweka nje ya uwanja kwa zaidi ya wiki sita.

Kukosekana kwa Dube ambaye alikuwa katika ubora msimu uliopita licha ya majeraha yaliyomkabali, ni wazi Azam inakosa mchezaji muhimu ambaye uwepo wake uwanjani na aina ya wapinzani inaokutana nao alikuwa na uwezo wa kufunga bao zaidi ya moja.


MABADILIKO AZAM

Kikosi cha Azam msimu huu kimefanya mabadiliko ikiwamo kusajili wachezaji wapya wa kigeni na wazawa ambao kinaamini wataongeza makali ya kikosi na kuachana wale ambao walishindwa kufanya vizuri msimu uliopita. Miongoni mwa timu ambazo zimesajili wachezaji waliokuwa na rekodi nzuri katika timu walizotoka ni Azam na kama wataonyesha ubora huo itakuwa na kikosi imara zaidi msimu huu.

Kutokana na muda waliotumia kufanya maandalizi wakiwa Dar es Salaam na Zambia, ni wazi mabadiliko na maingizo ya wachezaji wapya hayataonekana kama upungufu katika mechi hiyo.

Kama maingizo hayo yatashindwa kuwa na maelewano na wachezaji waliokuwapo msimu uliopita watashindwa kucheza kwa maelewano katika mechi hiyo na huenda wakashindwa kufanya vizuri, japo haitegemewi kuwa hivyo.


DHARAU KWA WAGENI

Kutokana na aina ya wapinzani wake Azam kutokuwa na rekodi za maana kwenye mashindano hayo inaweza kudharau na ikishindwa kucheza katika ubora mwisho wa siku itapoteza mchezo.

Kuna msemo wa Kiswahili usemao ‘msituni hakuna nyoka mdogo’, hivyohivyo kwa Azam haitakiwi kudharau wapinzani wao kwani inatakiwa kuwafunga kadri itakavyopata nafasi.

Azam ikipata ushindi mnono katika mechi ya kwanza itajirahisishia kazi katika mechi ya marudiano, lakini kuweka rekodi mbalimbali kama kuwa timu ya kwanza kupata ushindi mkubwa na huenda ikatoa mchezaji atakayewania tuzo ya mfungaji bora.

Kama ikiingia na akili ya kudharau wapinzani wao inaweza kushangazwa kwa kupata matokeo mabaya, jambo ambalo litaongeza ugumu wa mchezo wa marudiano utakaochezwa hapahapa nchini.


MECHI NYUMBANI

Ukifuatilia wapinzani wa Azam sio timu ya kutisha kutokana na rekodi zake, lakini mechi zote mbili kupigwa nchini kuna faida ya kuwa na uhakika wa kushinda na hasara yake ni kujiamini kupita kiasi.

Azam ikijiamini kuwa hakuna lolote linaloweza kutokea kutokana na kucheza mechi zote mbili nyumbani, Horseed inaonekana haina la kupoteza inaweza kushangaza.

Wanalambalamba wanatakiwa kucheza mechi ya kwanza kama wapo nyumbani kweli na hata ile ya marudiano itakayopigwa Uwanja wa Uhuru inatakiwa kuwa hivyo.


HATUA INAYOFUATA

Changamoto nyingine ya Azam huenda ikawa inaingia katika mechi ikiwa na akili kuwa tayari imesonga hatua inayofuata ambayo itakutana na matajiri wa Misri, Pyramids.

Azam inatakiwa kucheza huku benchi la ufundi na wachezaji wakiwafikiria wapinzani wake hao ili kufanikiwa kwanza kuwatoa na baada ya hapo kuanza mipango mingine.

Ni wazi kutokana na ubora wa Pyramids huenda Azam ikawa inacheza mechi hiyo huku akili zao zikiwafikiria Wamisri hao, jambo ambalo si sahihi na huenda ikashindwa kufanya vizuri.


WASIKIE WADAU

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula anasema kutokana na mazingira na changamoto za Yanga ambazo imekutana nazo wakati wa maandalizi ni wazi itakwenda kucheza mechi dhidi ya Rivers kwa ugumu.

Mwaisabula anasema Rivers United ilianza maandalizi ya mchezo dhidi ya Yanga mapema na inaonekana ilipata muda wa kutosha kuwafuatilia wapinzani wao ilhali kuna mambo mengi ya kiufundi itakuja kuyaonyesha nchini.

“Ukiangalia Yanga hawakupata muda mzuri kule Morocco na hata waliporejea hapa kuna wachezaji hawakuwepo kutokana na majukumu ya timu zao za taifa. Hawajafanya mazoezi ya pamoja kwa muda wa kutosha,” anasema Mwaisabula na kuongeza kuwa Yanga ina kazi kubwa ya kufanya.

“Kwa Azam wao kutokana na aina ya wapinzani ambao wanakutana nao - tena mechi zote mbili wanacheza hapa nyumbani, wamepata muda wa maandalizi na wamefanya usajili mzuri, naona watashinda bila shida.”

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Mohammed ‘Adolf’ Rishard anasema kutokana na aina ya maandalizi ambayo Azam imefanya na wapinzani wake itapata matokeo mazuri katika mechi zote mbili.

“Yanga wana mitihani - kwanza mashabiki wao wanategemea makubwa msimu huu kutoka kwao kutokana na usajili pamoja na kushindwa kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali kwa muda mrefu,” anasema Rishard.

“Maandalizi binafsi ni kitu muhimu kabla ya kucheza mechi au mashindano yoyoye, lakini mbali ya changamoto hizo wachezaji, makocha na viongozi wanatakiwa kila mmoja kutimiza majukumu ili kupata matokeo mazuri katika mechi ya kwanza kwani wanaanzia nyumbani.”

Advertisement