Prime
Yanga kuikimbia Mkapa... Haya Ni Maajabu
KWA miaka na mikaka ardhi ya kijiji changamani cha michezo, ndio imekuwa ngome kuu ya klabu kongwe ya Yanga.
Ardhi ya kijiji changamani ni pale panapopatikana viwanja viwili vya kihistoria, Uhuru na Mkapa.
Eneo hili wakati wa mkoloni lilikuwa Uwanja wa Ndege, kabla ya kuhamia Kipawa mwaka 1954.
Uwanja wa ndege ulipohama ndipo pakajengwa Uwanja wa Michezo.
Baada ya Uhuru mwaka 1961 serikali ikataka kujenga Kijiji cha Michezo katika ardhi ile.
Kwa Kiingereza kijiji hicho kiliitwa Sports Complex Village, kwa Kiswahili ni kijiji changamani cha michezo.
Japo mradi wa kijiji haukuwahi kukamilika, lakini jina lilishatolewa na likawa...hadi sasa unapolisoma hapa.
Baadaye ukajengwa uwanja mwingine hapo hapo...ndio huo wa Benjamin Mkapa kwa sasa.
Hapa ndipo mahali ambapo Yanga imekuwa ikicheza kwa muda mwingi wa maisha ya klabu hiyo.
Hapa ndipo mahali ambapo Yanga imeandika historia nyingi katika zile ilizonazo.
Hapa ndipo Yanga ilipopageuza machinjio yake kwa mechi za kimataifa, tangu ianze kushiriki.
MWANZO 1969
Yanga ndio klabu ya kwanza ya Tanzania kuitumia ardhi ya kijiji changamani kwa mechi za kimataifa.
Ilikuwa mwaka 1969 iliposhiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) kwa mara ya kwanza baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi mwaka 1968.
Yanga ilitwaa ubingwa huu baada ya kufanikiwa kumaliza Ligi kwa mara ya kwanza, kwani tangu ligi inaanza mwaka 1965, Yanga ilikuwa inasusa katikati ya msimu na kujitoa.
Kwa hiyo ilipomaliza ligi kwa mara ya kwanza 1968 na kutwaa ubingwa, ikapata tiketi ya kushiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.
Wakati huo uwanja uliotumika kwa mechi za kimataifa ulikuwa Uwanja wa Taifa ambao sasa ni Uhuru.
Lakini mabingwa wa kabla ya hapo hawakuugusa uwanja huo kimataifa.
Sunderland (sasa Simba) walitwaa ubingwa 1965 na 1966, lakini hawakushiriki mashindano ya kimataifa kwa sababu zilizokuwa nje ya uwezo wao.
Cosmopolitan waliokuwa mabingwa wa mwaka 1967 ndio wangekuwa wa kwanza kushiriki, lakini walishindwa kwenda Somalia walikopangiwa kutokana na hali mbaya ya ukata.
Kwa hiyo Yanga walipotwaa ubingwa wa Ligi 1968, wakashiriki Afrika 1969....wakawa wa kwanza.
Hapo ndipo walipoitambulisha kimataifa ardhi ya kijiji changamani.
Walicheza mechi tatu na kufunga mabao 10 juu ya ardhi hiyo, katika safari iliyoishia robo fainali.
Raundi ya awali
Yanga 4-1 Fitarikandro (Madagascar)
Raundi ya kwanza
Yanga 5-0 Saint-George (Ethiopia)
Robo fainali Yanga 1-1 Asante Kotoko
Safari ya Yanga iliishia robo fainali baada ya kutolewa kwa kurusha shilingi na Asante Kotoko ya Ghana.
Baada ya sare ya 1-1 katika mechi zote mbili, mechi ikaingia hatua ya kuamuliwa kwa kurusha shilingi kwa sababu wakati huo hakukuwa na sheria ya mikwaju ya penalti.
Hata mwaka uliofuata wa 1970 iliwakilisha tena nchi na kukutana na Asante Kotoko na ikaishia robo fainali, ila safari hii sio kwa kurushwa shilingi, bali ilipoteza kwa jumla ya mabao 3-1 ilianza na sare ya 1-1 kisha kupigwa 2-0, ila ikaendelea kutumia viwanja vya eneo hilo la changamani.
Tangu hapo ardhi ya kijiji changamani ikawa ngome kuu ya Yanga...wageni wakiumia vibaya sana...iwe Uwanja wa Taifa wa zamani ambao sasa ni Uhuru au uwanja mpya wa taifa ambao sasa ni Mkapa!
Lakini walipoamua kuhamisha mechi kutoka ardhi ya kijiji changamani na kuzipeleka sehemu nyingine hawakuwa na matokeo mazuri sana na siku zote namba haziongopi! Hapo chini ni mechi za Yanga kimataifa zilizohamishwa kutoka viwanja vya eneo la Changamani.
2001 - CCM Kirumba Mwanza
Yanga 3-3 Mamelodi Sundowns
2007 - CCM Kirumba Mwanza
Yanga 0-0 Esperance de Tunis
2021 - CCM Kirumba Mwanza
Yanga 1-2 Pyramids
Hizi ni baadhi tu ya mechi muhimu ambazo Yanga walizitoa nje ya ardhi ya kijiji changamani kama sehemu ya mikakati yao ya kuusaka ushindi muhimu.
Kuna nyakati Yanga ilicheza nje ya ardhi hii na kushinda, kama 2022 na 2023 Chamazi na 2024 Zanzibar.
Lakini hii ilitokana na ardhi ya kijiji changamani kutopatikana...hakukuwa na namna.
Ila pale ardhi ya kijiji changamani inapopatikana na Yanga kuamua kwa kibri tu kwenda kucheza mbali, waliishia kusonya baada ya dakika 90.
Huu ndio wasiwasi wa Mzee wa Pumzi ya Moto kwa kinachofanyika sasa.
Ardhi ya kijiji changamani inapatikana, ila Yanga wameamua tu kwa kibri kuikimbia...wasije wakaishia kusonya baadaye.
Kwa mujibu wa baadhi ya wachambuzi wanaoegemea upande wa Yanga, sababu ya kukimbilia Zanzibar ni ukubwa wa eneo la kuchezea.
Kwamba wachezaji wa Yanga kwa sasa wamezoea kucheza KMC Complex, uwanja ambao una eneo dogo la kuchezea, tofauti na Mkapa.
Hivyo wanaenda Zanzibar kufuata faida hiyo kwa sababu eneo lake la kuchezea ni dogo kama la KMC Complex.
Lakini hata hivyo, kitu ambacho wamekisahau ni kwamba Uwanja wa New Amaan Complex una vipimo sawa na Uwanja wa Mkapa.
Urefu mita 105
Upana mita 68
Na hiki ndicho kipimo cha Azam Complex pia.
Yawezekana kuna sababu nyuma ya uamuzi huu wa Yanga, lakini sio hii inayosikika hasa kutoka kwa wachambuzi wa Yanga.
Yanga wapo kundi gumu sana, lenye timu bora na imara. Unahitajika mkakati mzuri kuhakikisha wanapata matokeo kutoka hili kundi.
Al Ahly
FAR Rabat, JS Kabylie, Yanga
Hili so kundi la kubeza hata kidogo, japo kwenye mpira chochote kinawezekana.
Kucheza Benjamini Mkapa mbele ya mashabiki zaidi ya 40 wanaokuunga mkono ni faida kubwa kuliko New Amaan Complex, uwanja unachukua watu elfu 15 tu.
Vichwa vya wachezaji wa Yanga, na mashabiki wao pia, vimejenga picha kubwa kwamba kwa Mkapa ndio machinjio.
Wanapokuwa pale huwa na hisia za kipekee kabisa wakiamini wapo sehemu sahihi ya kichinjia.
Unapowahamisha, unawatengenezea mazingira mengine na kuondoa ile hisia...unapunguza kitu fulani na kujikaba mwenyewe.
Yanga wasije kushangaa hilo kundi likaisha kama msimamo ulivyo sasa.
Kukimbia ardhi ya kijiji changamani ni maajabu!