Yanga ilivyobeba Kombe la Mapinduzi
Muktasari:
- Wahenga wanasema washindani ni wengi, lakini mshindi lazima awe mmoja. Ndicho kilichotokea katika Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya timu 10 kushiriki na mwisho wa siku Yanga ikawa bingwa.
HATIMAYE safari ya siku 17 kushuhudia mechi 15 za Kombe la Mapinduzi 2026 kuanzia Desemba 28, 2025, imehitimishwa Januari 13, 2026 ilipopigwa fainali.
Wahenga wanasema washindani ni wengi, lakini mshindi lazima awe mmoja. Ndicho kilichotokea katika Kombe la Mapinduzi 2026 baada ya timu 10 kushiriki na mwisho wa siku Yanga ikawa bingwa.
Yanga imetwaa ubingwa wa mashindano hayo kwa ushindi wa penalti 5-4 dhidi ya Azam FC baada ya mechi hiyo ya fainali kuchezwa kwa muda wa dakika 120 bila ya timu hizo kufungana.
Beki wa Azam, Landry Zouzou ndiye aliyekosa penalti iliyofanya timu hiyo kupoteza baada ya kipa wa Yanga, Aboutwalib Mshery kudaka pigo hilo.
Haikuwa safari nyepesi ya siku 17 za mashindano hayo kwa mwaka huu ambapo Mwanaspoti linakupitisha yaliyojiri na kuonyesha namna gani Yanga ilistahiliu kubeba ubingwa huo.
IMEPIGWA HUKU NA KULE
Kamati ya maandalizi ya Kombe la Mapinduzi 2026 ilitangaza mwaka huu katika kuadhimisha miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar, michuano hiyo itachezwa Unguja na Pemba.
Tumeshuhudia hilo ambapo hatua ya makundi na nusu fainali, jumla ya mechi 14 zimepigwa Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja.
Fainali pekee ndio imechezwa kisiwani Pemba kwenye Uwanja wa Gombani, tukio lililokwenda sambamba na ufunguzi wa uwanja huo uliofanyiwa maboresho makubwa ikiwamo uwekaji wa paa jipya, ujenzi wa kuta, vyumba vya wachezaji, eneo la watu mashuhuri, maegesho, uwekaji wa minara ya taa, mifumo ya maji na umeme, pamoja na ujenzi wa uwanja wa mazoezi pembezoni mwa uwanja huo.
Katika ufunguzi, licha ya kufanyika kwa ukubwa sherehe, lakini mwitikio wa mashabiki ulikuwa mdogo hadi pale mechi zilizohusisha timu za Yanga na Simba zilipoanza kuchezwa.
Simba iliyokuwa Kundi B sambamba na Fufuni na Muembe Makumbi City, mechi ya kwanza ilicheza Januari 3, 2026 na kushinda 1-0 dhidi ya Muembe Makumbi, huku Yanga ikianza kutupa karata yake Januari 4, 2026 ikiichapa KVZ 2-0.
Mechi hizo zilianza kuupendezesha uwanja ulioonekana kuwa na mashabiki wengi kidogo tofauti na awali ilivyokuwa, licha ya kwamba kuna baadhi zilikuwa zikitolewa tiketi za bure.
Mechi ya fainali pale Pemba, hakukuwa na kiingilio, uwanja ulijaa kiasi cha mageti kufungwa mapema tu kuzuia wengine kuingia kwani mashabiki walijaa saa moja kabla ya filimbi ya kuanza mchezo haijapulizwa.
BINGWA MTETEZI AIBU
Mwaka jana 2205, Kombe la Mapinduzi ilichezwa kwa kushirikisha timu za taifa na Zanzibar Heroes ikawa bingwa ikiichapa Burkina Faso mabao 2-1.
Kabla ya hapo, utaratibu ulikuwa ni kushirikisha timu za klabu tangu kuanza rasmi kwa mashindano hayo mwaka 2007.
Sasa kabla ya mwaka huu, mara ya mwisho klabu iliyobeba ubingwa wa michuano hiyo ilikuwa Mlandege kutoka Unguja iliyofanya hivyo mara mbili mfululizo, 2023 na 2024 ikiivua taji Simba, mabingwa wa 2022.
Safari hii Mlandege imetia aibu, kutoka kuwa mabingwa mara mbili mfululizo hadi kuishia makundi bila pointi, ikifanikiwa kufunga bao moja pekee kupitia Aimar Hafidh ‘Haaland’ aliyesajiliwa na Azam hivi karibuni.
Pia timu hiyo imeruhusu mabao sita ikiwa na wastani wa kufungwa mawili kila mechi ambapo matokeo yake yalikuwa hivi; Singida Black Stars 3-1 Mlandege, URA 1-0 Mlandege na Azam 2-0 Mlandege.
Ukiachana na Mlandege, hakuna timu nyingine katika mash indano hayo mwaka huu iliyoshindwa kupata angalau pointi moja.
IBENGE AONYESHA TOFAUTI
Kitendo cha Kocha wa Azam, Florent Ibenge kuwaamini vijana kutokea akademi ya klabu hiyo na kuonyesha ushindani hadi fainali, imempa kocha huyo muda mzuri wa kukiona kikosi chake ni namna gani kinaimarika.
Wakati makocha wengine wakishusha mziki kamili ikiwamo Yanga katika mechi ya fainali ilipowasafirisha Ibrahim Bacca, Dickson Job, Bakari Mwamnyeto na Mohamed Hussein waliotoka kuitumikia Taifa Stars katika AFCON 2025, Ibenge alikomaa na kikosi chenye mchanganyiko wa vijana na wakongwe.
Mwanzo wa mashindano hadi mwisho, Ibenge aliwakosa nyota watano waliokwenda kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 ambao ni Feisal Salum, Idd Seleman, Pascal Msindo, Zuberi Foba na Lusajo Mwaikenda, ndipo akawaamini vijana saba aliosafiri nao kwa ajili ya kushiriki Kombe la Mapinduzi.
Vijana hao ni Twalib Nuru, Feisal Othman, Antony Remy, Alobogast Kyobya, Ilese Caleb, Abdallah Hassan na Ngita Kamanya.
Twalibu amecheza mechi zote tano ambapo moja pekee alitokea benchi akicheza kwa dakika 45, zilizobaki amezima mwanzo mwisho, huku fainali akipewa tuzo ya mchezaji aliyeonyesha mchezo wa kiungwana.
Kijana huyo ameonyesha uwezo mkubwa eneo la ulinzi akishirikiana vyema na Lameck Lawi ambaye aliifunga Simba na kuipeleka Azam fainali katika ushindi wa 1-0.
Akizungumzia kiwango cha Twalibu, Ibenge alisema: “Ana ubora mzuri, akiendelea hivi muda si mrefu nitamuona akicheza timu ya taifa kwani ana ubora huo wa kuitumikia Tanzania.
“Kwa sasa anatakiwa kuongeza juhudi na ndio maana nampa nafasi kuonyesha uwezo na kupata uzoefu zaidi. Nampongeza kwa kuonyesha juhudi kubwa ya kupambana, anahitaji kucheza mechi zaidi ili kuongeza ubora wake na uzoefu kwani bado kijana mdogo.”
Kijana mwingine aliyeng’ara ni Alobogast Kyobya, bao lake dhidi ya URA liliihakikishia Azam kufuzu nusu fainali ikiongoza kundi A iliposhinda 2-1.
Haikuishia hapo, mwisho wa mashi ndano Kyobya ametangazwa kuwa Mchezaji Bora Chipukizi.
Pia kuna Ngita, mshambuliaji aliyetoa pasi ya mwisho lilipofungwa bao na Kyobya na kuifanya Azam kuichapa URA 2-1 na kumaliza kinara wa kundi A.
Vijana hao wa Ibenge wamecheza dhidi ya Singida Black Stars na kutoka 1-1, kisha wakaichapa Simba Bo 1-0, wakaja kupoteza fainali mbele ya Yanga kwa penalti 5-4 baada ya dakika 120 kumaliza 0-0.
Hata hivyo, mecho ya fainali, Azam ililazimika kucheza pungufu ya mchezaji mmoja kwa takribani dakika 48 baada ya Cheikna Diakite kuonyeshwa kadi nyekundu dakika ya 72, lakini vijana hao walikomaa.
PEDRO AIJENGA YANGA IMARA
Katika Kombe la Mapinduzi 2026, kikosi cha Yanga kinachoongozwa na kocha Pedro Goncalves kimeweka rekodi ya kucheza mechi zote bila ya kuruhusu bao, hali iliyomfanya kipa wa timu hiyo, Aboutwalib Mshery kuondoka na clean sheet nne. Mbili hatua ya makundi, nyingine nusu fainali na fainali.
Pedro aliunda safu yake ya ulinzi imara ikiongozwa na Mshery huku mabeki wakiwa Israel Mwenda aliyecheza mechi moja na kumuachia Kibwana Shomari, Chadrack Boka ambaye naye alikichafua zote, fainali akafanyiwa mabadiliko na kuingia Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Frank Assinki aliyezima hatua ya makundi hadi nusu fainali, akapigwa benchi fainali akicheza Ibrahim Bacca, wakati Dickson Job akicheza fainali, alikosekana mechi zote za makundi na nusu fainali, nafasi hiyo alicheza Aziz Andabwile, Nizar Othman ‘Ninju’ na Moussa Balla Conte.
Kwa namna Yanga ilivyocheza tangu mwanzo wa michuano hiyo ikishinda mechi zote za awali kisha kutwaa ubingwa wa penalti, wababe hao walistahili kabisa ikifikisha taji la tatu tangu 2007, kwani ilionyesha ilikuja Zenji kusaka taji la pili msimu huu baada ya Ngao ya Jamii aliyoipata mapema kwa kuifunga Simbva kwa bao 1-0 Septemba 15 mwaka jana.
KADI NYEKUNDU NNE
Waamuzi watatu, Mohamed Simba, Rashid Farhan na Nassir Salum Siyah ‘Msomali’ wametoa adhabu ya kadi nyekundu kwa nyakati tofauti kwa wachezaji wanne ambao ni David Kameta ‘Duchu’ (Simba), Morice Chukwu (Singida Black Stars), Mohamed Damaro (Yanga) na Cheikna Diakite (Azam).
Duchu alikuwa mchezaji wa kwanza katika michuano hiyo kuonyeshwa kadi nyekundu ambapo tukio hilo lilitokea hatua ya nusu fainali, Simba ikifungwa 1-0 na Azam, Januari 8, 2026.
Duchu kwanza alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 58 kwa kumuangusha Cheikna Diakite, kisha dakika ya 90+2 akaonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyoambatana na nyekundu kwa kosa la kusukumana na mwamuzi Mohamed Simba akipinga uamuzi wake.
Baada ya hapo, ikawa zamu ya Damaro na Chukwu walioonyeshwa kadi nyekundu kutokana na kuvuragana wenyewe wakati Yanga ikiifunga Singida Black Stars bao 1-0, mechi ya nusu fainali iliyochezwa Januari 9, 2026.
Damaro alionyeshwa kadi hiyo baada ya kumchezea rafu Chukwu ambaye naye aliadhibiwa kwa kadi hiyo kutokana na kuonekana akirudisha mashambulizi.
Tukio hilo lilitokea dakika ya 85, ambapo katika kuwania mpira wa juu, Damaro alionekana kumpiga kiwiko Chukwu ambaye baada ya kuanguka, akaamka haraka na kwenda kumsukuma mwenzake. Mwamuzi Rashid Farahan akaanza kumuonyesha kadi ya njano Damaro ambayo ilikuwa ya pili baada ya kwanza kuonyeshwa dakika ya 33, hivyo ikafuatia nyekundu, huku Chukwu akionyeshwa nyekundu moja kwa moja.
Wa mwisho ni Diakite katika fainali ambayo Azam ilifungwa kwa penalti 5-4 na Yanga, Januari 13, 2026 baada ya dakika 120 kumalizika bila kufungana.
Mwamuzi Msomali alimtoa Diakite dakika ya 73, kufuatia kumuonyesha kadi ya pili ya njano kwa kumchezea vibaya Kibwana Shomari. Kabla ya hapo, dakika ya 55 alionyeshwa kadi ya njano kwa kumchezea vibaya Dickson Job.
UIMARA WA MANULA, METACHA
Katika mechi 15, zimeshuhudiwa penalti mbili zikipatikana ndani ya muda wa kawaida, lakini wapigaji hawakuwa na bahati kwani makipa walikaa imara na kuokoa michomo hiyo.
Alianza Metacha Mnata wa Singida Black Stars kuokoa penalti ya Yussuf Suleiman Haji ‘Jusa’ wa Mlandege, Desemba 28, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Unguja. Hiyo ilikuwa mechi ya ufunguzi iliyomalizika kwa Singida kushinda 3-1.
Aishi Manula wa Azam, naye akapangua penalti katika fainali dhidi ya Yanga iliyopigwa na Pacome Zouzoua dakika ya 115, baada ya beki wa Azam, Twalibu Nuru katika harakati za kuokoa, akaushika mpira. Hata hivyo, Manula katika kumsaka mshindi wakati wa mikwaju ya penalti baada ya mechi hiyo iliyochezwa Januari 13, 2026 kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba kumalizika kwa 0-0, alifungwa zote tano huku Aboutwalib Mshery akiokoa moja. Yanga ikashinda 5-4.