Prime
Yanga hii sasa sifa, mechi 25 bila kupoteza CRDB Federation Cup
YANGA imerudi kwa kishindo katika michuano ya ndani baada ya juzi usiku kupata ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Cosmopolitan katika mechi ya hatua ya 64 Bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB na kuendeleza rekodi bora ambayo haijawahi kuwekwa na timu yoyote nchini.
Mabao mawili yaliyofungwa na nyota mpya wa Yanga, Buba Jammeh moja la dakika ya 13 na jingine dakika ya 23 yote yakitokana na pasi murua za kiungo mshambuliaji, Mudathir Yahya yameifanya Yanga kuendeleza rekodi ya kibabe katika michuano hiyo.
Kama hujui hilo lilikuwa pambano la 25 kwa Yanga ikicheza katika michuano hiyo bila kupoteza, rekodi ambayo haijawahi kuwekwa na timu yoyote tangu ilipoasisiwa mwaka 1967 kama Kombe la FAT na baadae kuja kufahamika kama ASFC na sasa CRDB.
Ndio mara ya mwisho kwa Yanga kupoteza mechi katika michuano hii ilikuwa ni Julai 25, 2021 ikiwa ni mechi ya fainali ya msimu wa 2020-2021 dhidi ya Simba iliyochezwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, mjini Kigoma na vijana hao wa Jangwani kulala kwa bao 1-0.
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa kiungo mkabaji wa Yanga, Mukoko Tonombe akilimwa kadi nyekundu sekunde chache kabla ya mapumziko kwa kumchezea vibaya, nahodha wa Simba, John Bocco 'Adebayor', bao pekee liliwekwa kimiani na kiungo mkabaji raia wa Uganda, Taddeo Lwanga 'Injinia' katika dakika ya 80 kwa kichwa akimalizia mpira wa kona iliyochongwa na Luis Miquissone.
Tangu ilipopoteza pambano hilo la Lake Tanganyika, Kigoma hadi sasa unaposoma makala haya, Yanga haijapoteza tena mchezo wowote wa michuano ya Kombe la Shirikisho ikiweka rekodi ya kucheza mechi 25 na kutwaa taji hilo mara nne mfululizo na sasa ikisaka kutetea kwa mara ya tano.
Awali, Simba ndio iliyokuwa ikishikilia rekodi ya kucheza mechi nyingi (17) mfululizo bila kupoteza kuanzia msimu ya 2019-2020, 2020-2021 na 2021-2022 ilipotolewa nusu fainali na Yanga kwa kulazwa bao 1-0 lililotokana na shuti kali la mbali la kiungo Feisal Salum 'Fei Toto', aliyepo Azam FC kwa sasa.
Mechi hiyo iliyoitibulia Simba ilipigwa Mei 28, 2022 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza na kuivusha Yanga hadi fainali na kubeba ubingwa wa kwanza kati ya iliyotwaa mfululizo hadi sasa kwa msimu huo wa 2021-2022 kwa kuichapa Coastal Union kwa penalti 4-1.
Mechi hiyo ya fainali iliyoipa Yanga taji la kwanza kati ya manne mfululizo ya michuano hiyo ilipigwa Julai 2, 2022 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ulishuhudiwa ukimaliza dakika 90 kwa sare ya 2-2 na kuongezwa dakika 30 na kila timu iliongeza bao moja na kufanya matokeo ya dakika 120 kuwa sare ya 3-3.
Yanga ikipata mabao yake kupitia kwa Feisal Salum dk57, Heritier Makambo dk82' na Denis Nkane dk113, wakati Abdul Suleiman 'Sopu' alipiga hat trick kwa kuwafungia Wagosi mabao yote matatu katia dakika za 10', 87' na 98'.
SAFARI ILIVYOANZA
Katika msimu huo ambao Yanga iliinyang'anya taji Simba kwa kuing'oa katika nusu fainali, safari ya ubingwa kwa Vijana wa Jangwani ilianza kwa kuitoa Ihefu kwa mabao 4-0 katika pambano lililopigwa Desemba 15, 2021 na kutinga 32 Bora ilipokutana na Mbao FC na kuichapa kwa bao 1-0 siku ya Januari 29, 2022.
Katika hatua ya 16 Bora, wababe hao wa soka nchini, walikutana na Biashara United na kuifunga mabao 2-1 mechi ikipigwa Februari 15, 2022 na kufuzu hatua ya robo fainali ambapo huko ilivaana na Geita Gold na kumaliza dakika 90 kwa sare ya 1-1 kabla ya kuvuka kwenda nusu fainali kwa ushindi wa penalti 7-6 mechi iliyopigwa Aprili 10, 2022.
Ndipo katika nusu fainali bao la kombora la mbali la Fei Toto likaizamisha Simba na kuitemesha taji na kwenda kuvaana na Coastal katika fainali kali iliyopigwa jijini Arusha na Yanga kubeba taji kwa msimu huo ambao pia ilimaliza pia kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa rekodi ya bila ya kupoteza.
MOTO WA 2022-2023
Katika msimu huu, Yanga ilianza michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho kwa kupangwa kukutana na Kurugenzi FC ya Kagera katika hatua ya 64 Bora na kupata ushindi wa kishindo wa mabao 8-0, mchezo ukipigwa Desemba 10, 2022 jijini Dar es Salaam.
Yanga iliendeleza kugawa dozi nene katika michuano hiyo hatua ya 32 Bora baada ya kuifumua Rhino Rangers ya Tabora kwa mabao 7-0, mechi ikipigwa Januari 29, 2023 na kufuzu hatua ya 16 Bora ambapo ilipangwa kuvaana na Tanzania Prisons ya Mbeya,
Katika mchezo huo wa 16 Bora uliopigwa Machi 3, 2023, Yanga ilishinda kwa mabao 4-1 na kukata tiketi ya robo fainali ambapo ilipangwa kukutana na Geita Gold mchezo uliopigwa Aprili 8, 2023 na kushinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Fiston Mayele.
Yanga ilikutana na Singida Big Stars (sasa Fountain Gate) katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Mei 21, 2023 mjini Singida na kushinda kwa bao 1-0 na kufuzu kwenda fainali ambapo ilikutana na Azam FC, mechi ikipigwa Juni 12, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga.
Bao pekee lililoizamisha Azam liliwekwa kimiani kwa kichwa na Mzambia, Kennedy Musonda katika dakika ya 13 akimalizia mpira wa krosi ya beki Djuma Shaban ambaye awali alipiga kona fupi kwa Tuisila Kisinda na kunyunyiza mpira uliotendewa haki na mshambuliaji huyo aliyekuwa ametua kikosini katika dirisha dogo la msimu huo.
Bao hilo lilidumu na kuifanya Yanga kutetea taji kwa msimu wa pili mfululizo ikifikisha jumla ya mechi 12 bila kupoteza katika michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho.
UBABE WA 2023-2024
Yanga iliuanza msimu huu kibabe kwa kugawa dozi katika safari ya kutetea taji ikianza hatua ya 64 Bora kwa kuifumua Hausing ya Njombe kwa mabao 5-1 katika mechi iliyopigwa Januari 30, 2024 na kutinga hatua ya 32 Bora,
Katika hatua hiyo ya 32 Bora, watetezi hao walikutana na maafande wa Polisi Tanzania siku ya Februari 20, 2024 na kuwafumua kwa mabao 5-0 na kuvuka salama kwenda 16 Bora na huko wakakutana na Dodoma Jiji siku ya Aprili 10, 2024 kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma na kushinda kwa mabao 2-0.
Hatua ya robo fainali, Yanga ilikutana na Tabora United katika mchezo uliopigwa Mei Mosi, 2024 na kushinda kwa mabao 3-0 na kuvuka kwenda nusu fainali ambapo ilikutana na Ihefu (sasa Singida BS) kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
Mechi hii ilikuwa dume kwelikweli, kwani ilishuhudiwa zikipigwa dakika 120 na Yanga kushinda bao 1-0 lililopatikana katika dakika za nyongeza baada ya dakika 90 kumalizika kwa suluhu na kufuzu kwenda fainali kukutana na Azam FC.
Mchezo huu wa fainali ulipelekwa mjini Unguja kwenye Uwanja wa New Amaan Complex na Yanga kuibwaga Azam kwa penalti 6-5 baada ya dakika 120 kushindwa kutoa mshindi kwani timu hizo hazikufungana. Mechi hiyo iliyowapa Yanga ubingwa wa tatu mfululizo wa michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho ilipigwa Juni 2, 2024, ikifikisha jumla ya michezo 18 bila kupoteza.
MSIMU ULIOPITA
Katika msimu huo wa 2024-2025, Yanga ilianza kutetea taji kwa kupangwa kuumana na Copco FC ya Mwanza inayoshiriki First League na watetezi hao waliibuka na ushindi wa mabao 5-0.
Ushindi huo ulipatikana katika pambano hilo la hatua ya 64 Bora lililopigwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, siku ya Jan 25 mwaka 2025 ambapo Shekhan Ibrahim alifungua pazia kwa kufunga bao katika dakika ya 35'.
Prince Dube alifunga bao la pili katika dakika ya 57 kabla ya Maxi Nzengeli kufunga kwa penalti dakika ya 68 huku Dube Abuya na Mudathir Yahya wakifunga mengine mawili ya mwisho na kuivusha Yanga kwenda hatua ya 32 Bora.
Katika hatua ya 32 Bora, Yanga ilipangwa kuvaana na Coastal Union, mchezo uliopigwa pia kwenye Uwanja wa KMC Complex siku ya Machi 12 na watetezi hao kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 yaliyofungwa na Maxi Nzengeli aliyetupia mawili dk2 na 15, kisha Mfungaji Bora wa michuano hiyo kwa msimu uliopita, Clement Mzize alifunga la tatu dk21 muda mchache baada ya Miraj Abdallah kuifungia bao Coastal dk18.
Yanga ikavuka salama hadi hatua ya 16 Bora na kama kawaida, watetezi wakatoka na ushindi kwenye Uwanja wa KMC Complex dhidi ya Songea United iliyopo Ligi ya Championship.
Yanga ilipata ushindi wa mabao 2-0 na kuifanya ifikishe mechi ya 21 mfululizo katika Kombe la Shirikisho bila kupoteza kwa mabao ya Duke Abuya dakika ya 22 na jingine la Jonathan Ikangalombo 'Ikanda Speed' aliyefunga dakika ya 54.
Katika robo fainali, Yanga ilipangwa na Stand United iliyopo Ligi ya Championship na iliyotinga play-off ya mwisho ya kuwania kupanda Ligi Kuu kuzifuata Mtibwa Sugar na Mbeya City zilizotangulia mapema.
Katika mechi hiyo, Yanga ilifanya kweli kwa kuifumua Chama la Wana kwa mabao 8-1, yaliyofungwa na Stephane Aziz KI aliyetupia manne dakika za 16, 51, 60 na 64, Clatous Chama dk 32 na 41, Nickson Kibabage dk 20 na Kennedy Musonda dk 86, huku la kufutia machozi la Stand likifungwa na Msenda Senga dk 49.
Katika nusu fainali, Yanga ilikutana na JKT Tanzania na kuichapa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga kupitia mabao na Prince Dube dk 41 na Mudathir Yahya aliyefunga sekunde chache kabla ya filimbi ya mwisho na kuipeleka timu hiyo fainali.
Kisha ikahitimisha mechi ya 24 kwa kushinda fainali ya michuano ya msimu huo kwa ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Singida Black Stars iliyokuwa imetoka kuitoa kwa kishindo, Simba katika nusu fainali kwa mabao 3-1.
Mechi hiyo ilienda kupigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar ikiwa ni fainali ya pili mfululizo wa Kombe la Shirikisho kupigwa huko, baada ya ile ya 2023-2024 dhidi ya Azam na kupata ushindi kwa penalti 6-5.
Mabao ya ushindi wa mechi hiyo iliyopigwa Juni 29, 2025 yaliwekwa kimiani na Duke Abuya dk40 na Clement Mzize aliyemaliza kazi dakika ya 50 na kuipa Yanga ubingwa wa nne mfululizo wa michuano hiyo kabla ya juzi kuongeza idadi ya mechi kwa ushindi wa 2-0 dhidi ya Cosmopolitan.
1,669 Siku ambazo Yanga imefikisha bila kupoteza mechi katika Kombe la Shirikisho tangu Julai 25, 2021
25 Idadi ya mechi ambazo Yanga imecheza mfululizo katika Kombe la Shirikisho bila kupoteza.
9 Ndio idadi ya mataji ya michuano hiyo ambao Yanga imebeba tangu ilipoasisiwa mwaka 1967.
2015 Mwaka uliorejeshwa michuano ya FA ikibadilishwa jina kuwa Shirikisho (ASFC)
05 Mataji iliyotwaa Yanga ikiwa kinara pia tangu michuano hii iliporudishwa mwaka 2015.
2002 Mwaka ambao JKT Ruvu ilibeba taji la michuano ya mwisho ya Kombe la FA.
MABINGWA WA SHIRIKISHO
1967-: Yanga
1974-: Yanga
1985-: Majimaji
1995-: Simba
1996-: Sigara
1997-: Tanzania Stars
1998-: Tanzania Stars
1999-: Yanga
2000-: Mtibwa Sugar
2001-: Yanga
2002-: JKT Ruvu
2003-2015-: haikufanyika
2015-2016-: Yanga
2016-2017-: Simba
2017-2018-: Mtibwa Sugar
2018-2019-: Azam FC
2019-2020-: Simba
2020-2021-: Simba
2021-2022-: Yanga
2022-2023-: Yanga
2023-2024-: Yanga
2024-2025-: Yanga
2025-2026-: "??"