Wosia wa Madega kwa wanayanga

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa mwanaye, Abdul Madega baba yake ambaye aliitumikia Yanga kati ya 2006 hadi 2010, alijisikia vibaya jana asubuhi na akamwambia ampeleke Hospital ya Wilaya ya Chalinze iliyopo Msoga, lakini bahati mbaya alifariki wakati akipatiwa matibabu ya shinikizo la damu.

Imani Mahugila Madega, mwenyekiti wa zamani wa Yanga, alifariki dunia jana, nyumbani kwake Chalinze mkoani Pwani.


Kwa mujibu wa mwanaye, Abdul Madega baba yake ambaye aliitumikia Yanga kati ya 2006 hadi 2010, alijisikia vibaya jana asubuhi na akamwambia ampeleke Hospital ya Wilaya ya Chalinze iliyopo Msoga, lakini bahati mbaya alifariki wakati akipatiwa matibabu ya shinikizo la damu.


Hata hivyo wakati leo saa 10 jioni akitarajiwa kuzikwa nyumbani kwake Chalinze, kifo chake kimekuja takriban mwaka miezi 12 tangu alipofanya mahojiano makubwa ya mwisho na gazeti hili, ambapo alizungumzia mambo mbalimbali.  
Mwanaspoti linakuletea sehemu ya mahojiano hayo na kiongozi huyo wa zamani wa Wananchi na huu ni wosia wake kwa wanachama na mashabiki wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

NENO KWA WANACHAMA
Madega anasema, katika vitu ambavyo vinamkwaza ni tabia ya mashabiki kuwa na ubaguzi kwa viongozi kwamba kama mtu hana pesa hata akipigania maslahi yao wanakuwa hawamuungi mkono na kuwageukia matajiri hata kama wanajali maslahi yao binafsi.


“Tatizo katiba yetu haisemi kiongozi bora anatakiwa kuwa na shilingi ngapi, na niliweza kuondoa hali hiyo kwa kuwa mimi kwanza nilikuwa najiamini na pia naipenda Yanga. Ilipelekea nikatoa neno kuwa ‘tajiri baki na mali zako ila tuachie timu yetu’. Nilikuwa najiamini, uongozi na pesa ni vitu viwili tofauti,”  anasisitiza.


Anasema kwenye uongozi wake alikuwa hapendi kuwa na idadi kubwa ya watu, jambo lililofanya amwajiri Lawrence Mwalusako kuwa katibu wa klabu. Mwalusako kwa sasa pia ni marehemu.


“Maana sikuona sababu ya watu kukaa klabuni bila kufanya kazi. Sipendi uvivu, nilitamani mashabiki wa Yanga wawajibike kutoa michango inapotokea. Ingekuwa ngumu kama wanashinda klabuni pia kumuajiri katibu nilikuwa na kazi zangu za uwakili, hivyo nisingeweza kupatikana muda wote kazini,† anasema.


Anaongeza kuwa: “Nilikuwa sina pesa za kuwapa sijui mabaunsa. Ndio maana nilikuwa sipendi kuendekeza hayo mambo, watu wachape kazi inapotokea klabu inahitaji mchango wanatoa.”


USHIRKIANO NA SIMBA
Madega anasema yeye ni muumini mkubwa wa ukweli na uwazi na ndio maana alikuwa akishirikiana vilivyo na viongozi wa Simba na wanakaa meza moja na kuyajenga.


“Mimi na watu wa Simba wala hatuna shida hata kidogo kwa kuwa hatuna uadui. Utani maana yake wanafanya marafiki na siyo maadui. Niliwahi kusaini mkataba wa Kilimanjaro ambao Simba ndio waliniita tukakaa na kufanikisha na ulikuwa udhamini mkubwa na mzuri uliotusaidia wote,”  anasema.


Alipokuwa Dar es Salaam maskani yake kubwa ilikuwa ni Break Point, Kijitonyama, ambayo ni ya watu wa Simba na ni kijiwe kikubwa cha tawi la Friends of Simba.


“Nakumbuka jiko lilikuwa la Magori (Crescentius), aliyekuwa kama patna ni Harrison Mutembei alikuwa mweka hazina wa Simba. Daud Machumu mwenye eneo hilo naye alikuwa Simba, na ndiyo ilikuwa sehemu sahihi na niliwahi kupata matatizo nikionekana na watu wa Simba, lengo langu nilikuwa najaribu kuondoa dhana ya uadui kwenye michezo,” anasema.


“Mimi niliwauliza Rais wetu Kikwete ni Yanga, lakini mbona alimpa uwaziri Juma Kapuya (wa Simba) na hakuna shida? Hawakuwa na la kunijibu na nilichokipenda kwa sasa cha wazi wazi Haji Manara kutoka Simba kwenda Yanga.”  


Pamoja na ushirikiano waliokuwa wanaufanya katika kujenga maendeleo ya soka, anasema Simba iliwasaliti baada ya kukubaliana wasishiriki michuano ya Kombe la Kagame, jambo ambalo aliingia kwenye mgogoro na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Cecafa, Nicholaus Musonye.


“Tulikubaliana tugome baada ya Musonye kuonekana kutaka kuchukua mapato mengi lakini wenzetu Simba wakasaliti waliamua kupeleka timu walitukwaza sana kusema ukweli ilikuwa 2010 kama sijasahau,” anakumbuka.

KAMATI ZA UFUNDI ZIPO
Akizungumzia kile kinachoaminika kwamba ni kamati zinazofanya mambo nje ya uwanja ili kufanikisha ushindi, Madega anasema:


“Ni kweli hizo kamati zipo, lakini mie siziamini sana kwa kuwa mambo yanabadilika lakini ndio mambo ambayo tumeyakuta katika timu na yanaleta utulivu mkubwa, na kuna watu wanaamini hata kama una benchi zuri na wachezaji wazuri lakini kamati ya ufundi muhimu.


“Nakumbuka ilinitokea kulikuwa na mechi moja hivi usajili wetu ulikuwa unaonekana dhaifu. Azam walikuwa bora na Simba pia, lakini mechi ya kwanza ya Simba na Azam Simba alipigwa.


“Mchezo uliofuata Yanga na Azam wale wazee (wa kamati ya ufundi) wakati mechi inakaribia nilidhani watanipigia kuchukua hela ya kazi lakini haikuwa hivyo. Wakanijibu walishaona tumechukua hela Azam, na eti waliichungulia mechi wakaona Azam itashinda, basi tukawaacha, tukaandaa timu bila kuroga na tukashinda 3-0.”

HATAMSAHAU MANJI
Anasema wakati huo kulikuwepo na sintofahamu wakati wa udhamini wa Yusuf Manji.


“Niliondoka kwa sababu nilihitaji unyoofu. Kuna baadhi ya mashabiki walikuwa wakipewa pesa tu wanayumbishwa, jambo ambalo halikuwa zuri sana. Niliweka mipaka uongozi na udhamini, siyo mdhamini aanze kuipangia klabu hiyo siyo sawa. Nikaona ya nini, hilo linajidhihirisha baadaye akawa mdhamini na mwenyekiti pia,”  anasema.

KINARA WA MABADILIKO
Akiwa Mwenyekiti wa Yanga alianzisha wazo la kutaka mabadiliko na anajivunia kuona lilipata mwamko wa kwenda kutimiza kile alichokuwa amekipanga miaka mingi nyuma na sasa timu hiyo inaendeshwa kwa mfumo wa hisa.


“Kwanza kabisa hata siku Yanga wanaingia makubaliano na LaLiga kwa ajili ya mabadiliko walinialika na nilikwenda. Niliona nimepewa heshima ya kipekee ya kuenzi kitu ambacho nilikiwekea misingi imara ambayo inakwenda kuwa kwenye matendo,”  anasema Madega.


“Sio hilo tu hata baada ya mchakato kuanza waliniweka kwenye kamati ya mabadiliko. Naamini tutafika mbali sana kwa kuwa tuna nia ya dhati ya kufanikisha hilo.”


Vilevile Madega alifanikisha timu hiyo kulinda nembo ya klabu akisema: “Pia nilifanikiwa kutengeneza sheria za kulinda nembo ya Yanga, thamani ya klabu ndio maana katika mabadiliko yanayoendelea kwa sasa wapo hatua ya kujua thamani ya mali za klabu kabla ya kuingia kwenye mfumo huo.

MAISHA YA UPWEKE
Hata hivyo, katika siku zake za mwisho akiwa kijijini, Madega aliliambia Mwanaspoti kuwa amekuwa na jina kubwa tofauti na alivyokuwa anachukuliwa mjini, jambo linalomfanya kuwa mwangalifu ili kulinda heshima isiingie tope.


“Siwezi kujiachia kunywa ama kufanya vitu vya hovyo hovyo kwa sababu nina heshima kubwa katika kijiji hiki. Kiukweli inanishangaza sana ninavyokubalika,† anasema.


Anasema pamoja na furaha yake ya kurejea Chalinze ni kukosa marafiki ambao alikuwa analazimika kuwapata anapokuja Dar es Salaam kwa shughuli au kutembea.


“Tatizo kubwa la huku (kijijini) wengi wao wameniweka daraja la juu sana kiasi kwamba wanaogopa kunizoea, japokuwa wapo baadhi ninabadilisha nao mawazo ya hapa na pale. Ila najihisi upweke marafiki zangu wa zamani nakutana nao nikienda Dar es Salaam.”  


Jana jioni Yanga ilitoa taarifa kwa wanachama kuelezea jinsi ilivyoguswa na msiba huo, ikimtaja kuwa mmoja wa viongozi wake maarufu walioifanyia mambo makubwa.