Prime
Sasa ni Kamati ya Uchaguzi kuonyesha weledi, uhuru

Muktasari:
- Habari hizo hazikuwa na chanzo zaidi ya kupachikwa jina la ‘habari za kuaminika’, lakini zikionekana kuwa na lengo la kuitisha serikali isiingilie sakata hilo lililosababishwa na Simba kutishia kugomea mechi dhidi ya mtani wake wa jadi ile ya Machi 8 baada ya kuzuiwa kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufanya mazoezi ya mwisho.
HIVI karibuni wakati sakata la mechi ya Simba na Yanga likianza kupamba moto, kulivumishwa habari kuwa Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa), litatuma wawakilishi wake kuja kuchunguza mambo kadhaa yanayoendelea katika soka na hasa uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), utakaofanyika mwezi ujao.
Habari hizo hazikuwa na chanzo zaidi ya kupachikwa jina la ‘habari za kuaminika’, lakini zikionekana kuwa na lengo la kuitisha serikali isiingilie sakata hilo lililosababishwa na Simba kutishia kugomea mechi dhidi ya mtani wake wa jadi ile ya Machi 8 baada ya kuzuiwa kuingia Uwanja wa Benjamin Mkapa kufanya mazoezi ya mwisho.
Kadri mgogoro huo ulivyokuwa unakua ndivyo ilivyoonekana kuwepo kwa uwezekano wa vyombo vya nje, na hasa serikali, kuingilia kati kuumaliza. Ni jambo la kushukuru kwamba Rais Samia Suluhu Hassan alilimaliza kwa njia ambayo haikumaanisha serikali imeingilia kati.
Fifa imezuia mamlaka za nje kuingilia katika masuala ya uendeshaji mpira, ikiamini kuwa ina uwezo wa kujenga vyombo vyake vya ndani kwa ajili ya kutatua matatizo yoyote yale yanayojitokeza ndani ya mchezo huo maarufu duniani.
Ndio maana katiba yake mwongozo inaunda vyombo huru kama Kamati ya Uchaguzi, Kamati ya Nidhamu, Kamati ya Maadili, Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro (DRC) na kamati nyingine muhimu.
Hizo nilizozitaja ni kamati zenye uhuru kamili na zina uwezo wa kujadili suala linalomhusu mwanafamilia yeyote wa mpira, bila ya kujali nafasi yake kwenye uongozi wa mpira wa miguu. Ndio maana hata rais wa zamani wa Fifa, Sepp Blatter alishughulikiwa na moja ya kamati hizo.
Uhuru huo hujenga imani na hali ya kuaminika kwa wanafamilia wa mchezo huo, lakini unapochezewa ndipo mamlaka za nchi hujikuta zinaingilia kujaribu kukomesha kiburi kinachojengwa na watu wa mpira kuwa serikali hairuhusiwi kuingilia kati na hivyo kujifanyia mambo bila ya kujali yale ya msingi kama usawa, haki na mengine muhimu.
Kwa hiyo, kamati hizo zinatakiwa zifanye kazi kwa kuweka mbele haki, kutopendelea, kutoonea huku suala la uadilifu na weledi likichukua nafasi kubwa. Bila ya kufanya hivyo, wanafamilia hutafuta mlango mwingine na hapo ndipo migogoro huanza.
Katika uchaguzi mkuu wa TFF, wagombea wanasubiri Kamati ya Uchaguzi ikutane na kuchuja wagombea baada ya wote kurudisha fomu wiki iliyopita.
Lakini limejitokeza suala la mgombea mmoja, Wallace Karia anayetetea kiti cha urais kudaiwa kuwekewa pingamizi na mwanachama mmoja tu - Klabu ya Yanga ya Dar es salaam.
Wanachama wengine 46 wanadaiwa walikubaliana na ‘azimio’ lililofikiwa mjini Moshi la kumpitisha agombee tena urais na hivyo kuipa nguvu kanuni inayozuia mwanachama mmoja kudhamini zaidi ya mgombea mmoja. Wanachama wote hao, ambao ni mikoa 26, vyama shiriki vitano na klabu 15 za Ligi Kuu walimuidhinisha na hivyo wagombea watano waliojitokeza kuwania urais kukosa udhamini unaotakiwa.
Ni Ally Mayay pekee ndiye aliyepata angalau mdhamini mmoja wakati sheria inataka mgombea awe na wadhamini watano. Kwa maneno mengine ni kwamba Karia ameshapigiwa kura na zaidi ya nusu ya wajumbe wa mkutano wa uchaguzi.
Ni kwa jinsi hiyo, pingamizi la Yanga limehusu matumizi mabaya ya madaraka kwamba hali akijua kuwa wadhamini wanaotakiwa ni watano na kwamba kuchukua wadhamini wengi kunakosesha wanafamilia wengine kuingia kwenye mpira, na Karia alichukua zaidi ya wadhamini watano ambao isingekuwa rahisi kuwapata kama asingekuwa rais wa TFF.
Yanga pia inadaiwa inadai Karia alianza mapema kukusanya wadhamini kabla ya tangazo la Kamati ya Uchaguzi kuhusu mchakato. Ilikuwa ni ajabu kwamba mwanafamilia aliyechukua fomu mapema zaidi, aliambiwa udhamini ushaisha.
Klabu hiyo pia idaiwa kwamba inapinga Karia kugombea muhula wa tatu tofauti na sera ya nchi ya mwaka 1995 inayotaka wagombea wa nafasi hiyo kwenye vyama ambavyo mihula ni miaka minne, wagombee vipindi viwili.
Tayari suala hilo la muhula wa tatu limeshawasilishwa na wadau wengine Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na inaonekana wadau wengi zaidi wanasubiri Kamati ya Uchaguzi ifanye mchujo, ambao kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi, atabaki Karia pekee, kabla ya kuchukua hatua ama za kwenda Kamati ya Rufaa au serikalini na wengine Fifa au Mahakama ya Kimataifa ya Michezo.
Hatustahili kwenda kote huko kama mambo yamenyooka. Huu ni wakati wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuonyesha uhuru, weledi na uadilifu kwa kufanya uamuzi utakaoiepusha nchi kuingia kwenye mgogoro usio wa lazima.
Huko nyuma tuliogopa serikali kuingilia kati kwa sababu wanasiasa wengine walikuwa na maslahi yao binafsi, lakini sasa tunaogopa serikali kuingilia kati kwa vyombo vya haki vya TFF kukosa weledi na uadilifu.
Ni muhimu sana kwa kamati kuwa na msimamo thabiti uliojiegemeza kwenye sheria, iwe kwa kumpitisha Karia au kumzuia kutokana na pingamizi lililowekwa au mazingira ya kisheria yanayokinzana na sheria za nchi.
Pia ni muhimu kwa hoja hizo zinazoegemea kanuni iliyosababisha wagombea wengine wote kukosa udhamini wa kutosha, likazingatiwa kwa kuwa ni sumu kwenye mpira wa miguu.
Ni muhimu hata Kamati ya Maadili ikaliona hilo mapema kwa kuwa linahusu tuhuma za matumizi mabaya ya madaraka.
Vyombo hivyo muhimu kwa ustawi wa mpira wa miguu havina budi kuzingatia kuwa mchezo huo ni kwa wadau wote na si watu wachache waliopewa dhamana ya kuingia mkutano mkuu kwa ajili ya kuwakilisha wengine.
Watu hao hawakutakiwa hata kufikiria kufanya lolote ambalo linaweza kuzuia walio nje ya muundo wa uongozi wa TFF hawatakiwi na hawana haki ya kugombea muda wa uchaguzi unapofika. Katiba imeweka muda wa uchaguzi kila baada ya miaka minne kwa lengo la kuweka ushindani ambao husukuma maendeleo mbele. Huu ni wakati wa Kamati ya Uchaguzi kuwa na weledi na uadilifu.
Mwandishi wa safu hii ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF na mchambuzi wa masuala ya soka. Maoni: 0659-626 656