Wilder amchana Joshua ‘wazichape’
Muktasari:
- Unajua ilikuwaje? Joshua alikuwa ameketi karibu na ulingo (ringside) akishuhudia moja ya mapambano ya kukata na shoka katika uzito wa juu ambalo lilifanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa The O2 Arena jijini London na Wilder alimshinda bondia mkongwe Derek Chisora.
LONDON,ENGLAND: BONDIA mashuhuri Deontay Wilder siku chache zilizopita alikutana uso kwa uso na mpinzani wake wa muda mrefu Anthony Joshua na kutumia nafasi hiyo kumtaka wapande ulingoni ‘haraka iwezekanavyo’ wazichape kama kweli anaweza.
Unajua ilikuwaje? Joshua alikuwa ameketi karibu na ulingo (ringside) akishuhudia moja ya mapambano ya kukata na shoka katika uzito wa juu ambalo lilifanyika wiki iliyopita katika ukumbi wa The O2 Arena jijini London na Wilder alimshinda bondia mkongwe Derek Chisora.
Ushindi huo ulikuwa muhimu sana kwa Wilder, maarufu kama ‘Bronze Bomber’, kwani ulimrudisha kwenye mstari wa ushindi baada ya kipindi kigumu. Pia umeondoa kabisa uvumi wa kustaafu na kuonyesha wazi bado ana nia ya kupambana na majina makubwa duniani.
Kwa muda mrefu, pambano kati ya Wilder na Joshua limekuwa likitajwa mara nyingi lakini halijawahi kutimia licha ya kuwa karibu kufanyika mara kadhaa. Hii imeongeza mvutano mkubwa kati yao.
Baada ya pambano, Wilder alipokuwa akielekea vyumbani kubadilishia nguo, alimwona Joshua akiwa anamsubiri. Wawili hao walisalimiana kwa kupeana tano (kugonganisha mikono yao) ishara ya heshima lakini mara moja Wilder alimtolea uvivu na kumwambia kwa kujiamini: “Tufanye hili pambano.”€
Joshua alimwangalia tu bila kusema neno lolote, hali iliyozua ukimya mzito kwa sekunde chache huku kamera zikiwamulika mafahari hao. Wilder aliendelea kuondoka huku Joshua akiendelea kumtazama akitoka uwanjani.
Katika tukio jingine tofauti, wawili hao walikutana tena kwenye korido lakini safari hii kila mtu alikuwa na hamsini zake, jambo lililoonyesha wazi bado kuna mvutano mkubwa kati yao.
Kwa sasa, inaonekana pambano kati yao linaweza kuwa karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote. Wote wawili wana nguvu kubwa ya kibiashara na wanaweza kuvutia mashabiki wengi duniani, hivyo pambano lao lingekuwa na thamani kubwa sana.
Joshua anatarajiwa kurejea ulingoni Julai, 2026 baada ya kuwa nje tangu Desemba, 2025 kutokana na ajali ya gari iliyochelewesha mipango yake ya mwaka 2026. Katika pambano lake la mwisho alimshinda Jake Paul kwa kumpiga ‘KO’.
Kwa upande mwingine, Wilder amesema sasa yuko fiti kabisa na tayari kupigana mahali popote duniani. Amesisitiza: “Ama ukubali au nyamaza. Niko tayari sasa Wilder aliyepo vizuri ni hatari zaidi.”
Wachambuzi wa ndondi wanaamini pambano hili linaweza kufanyika mwaka 2026, hata mwezi Septemba, ikiwa mipango itakamilika. Pia kuna mazungumzo ya pambano kati ya Joshua na Tyson Fury, jambo linaloweza kuathiri ratiba.
Kwa jumla, hali inaonyesha mashabiki wa ndondi wanaweza kushuhudia pambano kubwa sana kati ya Wilder na Joshua ambalo limekuwa likisubiriwa kwa miaka mingi.
KURUDI KWA JOSHUA
Safari ya kurejea kwa Joshua imekuwa ndefu, ngumu na yenye changamoto nyingi za kujifunza. Kila hatua imehitaji nidhamu, uvumilivu na uwezo wa kuhimili presha, hasa baada ya ajali mbaya ya gari iliyotokea Desemba 2025 huko Lagos, Nigeria. Ajali hiyo ilisababisha vifo vya watu wawili muhimu katika maisha yake, Sina Ghami, kocha wake wa utimamu wa mwili na Latif ‘Latz’ Ayodele, mwalimu wake binafsi wa mazoezi.
Kupoteza marafiki hao na washirika wake wa karibu kulimvua Joshua sehemu ya hisia na kumuacha akihisi huzuni kubwa. Hawakuwa tu sehemu ya timu yake ya ndondi bali pia walikuwa marafiki wa karibu, waliokuwa wakimsaidia kukuza kipaji chake na kumtia moyo kila siku.
Hali hii ilimlazimu Joshua kuchukua muda wa kutafakari na kujiweka kando na mchezo wa ndondi kwa muda.
Kurejea kwenye ndondi hakukuwa rahisi. Joshua alilazimika kupitia mchakato wa matibabu ya kimwili na kiakili ili kupona kwa ukamilifu. Alijifunza kukabiliana na maumivu ya kupoteza wapendwa wake na kuimarisha akili yake, siyo tu ili aweze kushinda tena ulingoni bali pia ili kuheshimu alichopitia.
REKODI ZA JOSHUA
Joshua amejijengea jina kubwa duniani kutokana na rekodi yake ya kuvutia katika ndondi za kulipwa. Tangu aingie katika ulimwengu huo, ameonyesha kiwango cha juu cha nidhamu, nguvu na ushindani uliomfanya kuwa mmoja wa mabondia bora wa kizazi chake.
Katika maisha yake ya ndondi, Joshua ameshinda mapambano 26 kwa njia ya KO kati ya 29 aliyoshinda kwa jumla huku akipoteza manne kati ya mapambano aliyocheza, jambo linaloonyesha uwezo wake mkubwa wa kumaliza pambano mapema. Ushindi wake umejengwa katika mambo matatu nguvu, mbinu na utulivu ulingoni.
Ameshinda mataji makubwa ya dunia yakiwemo IBF, WBA na WBO na kuwa bingwa wa uzito wa juu mara mbili mafasi ambayo sio rahisi kuyapata.
Moja ya mafanikio yake makubwa ni kushinda medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya mwaka 2012, tukio lililomfungulia milango ya umaarufu na kumweka kwenye ramani ya dunia kabla hata hajaanza kulipwa.
Licha ya kukumbana na vipigo kutoka kwa mabondia kama Andy Ruiz Jr., Joshua aliweza kurejea na kulipiza kisasi, jambo linaloonyesha uimara wake wa kiakili na uwezo wa kujifunza kutokana na makosa.
WILDER ATAWEZA?
Swali kubwa linalozungumzwa kwa sasa ni kama Wilder ataweza kuhimili presha na ubora wa Joshua iwapo pambano lao litafanyika.
Hii ni kutokana na tofauti kubwa ya mitindo yao ya kupigana ambayo inaweza kuamua matokeo ya pambano hilo.
Wilder anajulikana kwa nguvu za ajabu za mkono wa kulia, ambayo imekuwa silaha yake kuu kwa miaka mingi. Ana uwezo wa kumaliza pambano kwa sekunde chache hata kama alikuwa nyuma kwa pointi kabla ya hapo.
Mabondia hawa, hawajawahi kupigana, licha ya mazungumzo ya muda mrefu yaliyowahi kufanyika kati ya timu zao. Sababu kubwa zilikuwa ni tofauti ya mkwanja na makubaliano ya mikataba ambayo hayakufikiwa.
Kuna kipindi kati ya 2018 na 2020 na pambano hilo lilikuwa karibu kutimia lakini likashindikana dakika za mwisho hali iliyowaacha mashabiki wengi wakiwa na maswali mengi.
Iwapo pambano litafanyika sasa, litakuwa ni vita ya mafahari wawili na matokeo yake yanaweza kuwa ya kushangaza kwa yeyote.
REKODI ZA WILDER
Wilder ana rekodi inayotisha katika uzito wa juu, hasa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kumaliza mapambano kwa KO. Takwimu zinaonyesha kuwa asilimia kubwa ya ushindi wake umetokana na KO, amecheza jumla ya mapambano 50, ameshinda 45 huku 43 yakiwa kwa KO, amepoteza manne na kutoa sare moja.
Aliwahi kushikilia taji la WBC kwa muda mrefu, akilitetea mara kadhaa dhidi ya wapinzani tofauti na kuonyesha ubora wake katika uzani huo.
Mapambano yake na Tyson Fury yalikuwa miongoni mwa mapambano makubwa zaidi katika historia ya hivi karibuni ya ndondi, yakionyesha ushindani wa hali ya juu.
Wilder anajulikana kwa kujiamini kupita kiasi, jambo ambalo limekuwa likimsaidia pia wakati mwingine likimgharimu katika baadhi ya mapambano.
Kwa jumla, ni bondia hatari ambaye anaweza kubadilisha matokeo ya pambano kwa pigo moja.
MKWANJA MEZANI
Pambano kati ya Wilder na Joshua linatarajiwa kuwa moja ya mapambano yenye mapato makubwa zaidi katika historia ya ndondi za kisasa, kutokana na ukubwa wa majina yao na mvuto wao kwa mashabiki duniani kote.
Takwimu kutoka vyanzo vya tasnia ya ndondi zinaonyesha pambano hilo linaweza kuingiza zaidi ya Dola 200 milioni kutokana na mauzo ya tiketi, haki za matangazo na mfumo wa Pay-Per-View (PPV), ambao umekuwa chanzo kikubwa cha mapato katika mapambano makubwa.
Soko la Uingereza, ambako Joshua ana mashabiki wengi, lina uwezo mkubwa wa kuuza tiketi kwa bei ya juu huku Marekani ikiwa ngome ya Wilder na chanzo kingine kikubwa cha mapato ya PPV.
Kwa makadirio, kila bondia anaweza kupata kati ya Dola 50 milioni hadi 100 milioni kulingana na makubaliano ya mkataba pamoja na bonasi na gawio la mauzo ya PPV.
Kampuni kubwa za matangazo na wadhamini wa kimataifa zinatarajiwa kuwekeza fedha nyingi ili kuhusishwa na pambano hilo, jambo linaloongeza thamani yake kibiashara.
Haki za kurusha matangazo katika nchi mbalimbali zitachangia mamilioni ya dola huku majukwaa ya kidijitali yakitarajiwa kunufaika zaidi.
Ukumbi utakaochaguliwa unaweza kuwa uwanja mkubwa wa wazi kama vile, Wembley wenye uwezo wa kubeba mashabiki zaidi ya 80,000, hali itakayoongeza mapato ya tiketi kwa kiwango kikubwa.
Bidhaa za kumbukumbu kama fulana, kofia na vifaa vingine vitauzwa kwa wingi, vikichangia mapato ya ziada.
Pia kutakuwa na mapambano ya utangulizi (undercard) yatakayovutia mashabiki zaidi na kuongeza thamani ya tukio zima.
Kwa ujumla, pambano hili linaelezwa kama ‘mgodi wa fedha’ ambao unaweza kuvunja rekodi nyingi za mapato katika ndondi.