WIKI YA MWANANCHI: Yanga mziki mnene, Mayele ni yule yule

Saturday August 06 2022
Yanga PIC
By Khatimu Naheka

TUKIO kubwa kesho Jumamosi ni lile la Wiki ya Mwananchi inayofikia kilele cha wiki yake. Hii inakuwa ni msimu wa nne Yanga kuiadhimisha. Hii ni kama sikukuu kwa klabu hiyo na inaiadhimisha ikiwa na kila aina ya furaha na kuanza kuangalia mapya kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na mashindano mengine itakayoshiriki.

Siku hiyo hapana shaka itakuwa ya kipekee kutokana na Yanga kwa mara ya kwanza tangu ianze kuiadhimisha itaingia ikiwa bingwa mtetezi wa mataji matatu ambayo iliyachukua msimu uliopita.

Kama haitoshi sio tu mataji matatu, pia haikupoteza mchezo wowote msimu uliopita katika mashindano yote ikimaliza ligi bila kupoteza, Ngao ya Jamii haikufungwa pia Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) nalo haikupoteza hadi inachukua taji.


KIKOSI CHAO

Yanga baada ya kuchukua mataji matatu ilithibitisha kuwa ina kikosi imara lakini kama haitoshi kuelekea msimu mpya bado ina kikosi kilekile kilichoipa mafanikio na zaidi.

Advertisement

Kwenye kikosi chake cha kwanza cha msimu uliopita hakuna staa muhimu sana ambaye aliondoka, wote wamewabakiza na wataanza nao msimu mpya. Hii itaifanya Yanga kuwa na ubora wake mkubwa ambao timu zote ziliushindwa.

Ubora wa mastaa hao ulidhihirika hata katika Tuzo za Wachezaji Bora wa msimu ambapo Yanga ndiyo iliondoka na tuzo nyingi kuliko timu yoyote huku bado wengine wakikosa lakini wakiwa na sababu za utambuzi katika ubora.


MASTAA WATANO WAPYA

Gumzo kubwa katika utambulisho wa wachezaji wa Yanga katika kilele cha Wiki ya Mwananchi itakuwa ni mastaa wake wapya watano ambao wamewasajiliwa msimu huu.

Yanga imewasajili beki Joyce Lomalisa (DR Congo), kiungo Gael Bigirimana (Burundi), kiungo mshambuliaji Bernard Morrison (Ghana) washambuliaji Lazorous Kambole (Zambia) na Stephane Aziz KI (Burkinafaso).

Wachezaji hawa kila mmoja atakuwa na kishindo chake kutokana na sababu mbalimbali lakini watatu ndio watakuwa gumzo zaidi ambao ni Bigirimana aliyesajiliwa akitokea Ulaya akiwahi pia kuitumikia Newcastle United ya England.

Mwingine ni Morrison ambaye amerejea nyumbani, utakumbuka Morrison kabla ya kuelekea Simba, alikuwa Yanga. Yanga ndio iliyomleta nchini akifanya kazi iliyoheshimika akiwafunga pia Wekundu hao.

Staa mwingine mkubwa ambaye ndiye anaweza kuwa jina kubwa ni Aziz Ki ambaye usajili wake umetingisha zaidi nchi akitokea ASEC Mimosas ya Ivory Coast huku Yanga ikifanikiwa kuzipiga bao klabu nyingi kubwa ambazo zilikuwa zikivizia saini ya mshambuliaji huyo.


MAYELE NI YULE YULE

Licha ya Yanga kumleta Aziz Ki akiaminika ndiye mchezaji bora aliyevuma zaidi lakini bado Mbukinabe huyo anatakiwa kufanya kazi ya ziada kupunguza nguvu ya kukubalika ya Mshambuliaji, Fiston Mayele ambaye ametumia msimu mmoja tu kuitingisha nchi kisawasawa kupitia mabao yake 16 aliyoyafunga msimu uliopita.

Mayele katika ubora huo, amefanikiwa kuwateka wengi kutokana na staili yake ya kushangilia mabao.

Staili hiyo imewabamba wengi na kuwafanya hata baadhi ya viongozi kuitumia katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika pale Dodoma.


BENCHI LA UJAZO

Yanga iko vilevile katika benchi lake la ufundi. Labda kama itaamua kuwaongeza watu wengine bora lakini usisahau yuko Kocha Mkuu Nasreddine Nabi, raia wa Tunisia ambaye ameitingisha ligi ya msimu uliopita kutokana na mbinu zake dhidi ya timu pinzani na kupata mafanikio makubwa kwa kuchukua mataji hayo huku pia akibeba Tuzo ya Kocha Bora.

Advertisement