WIKI YA MWANANCHI: Yanga imepania kimataifa

Saturday August 06 2022
U1

Klabu ya Yanga imekabidhiwa taji lake la 28 Ligi Kuu kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City.

By Oliver Albert

HHAKUNA watu wanaojiamini kwa sasa na wenye vaibu kama mashabiki wa Yanga na yote ni kutokana na mafanikio ya timu hiyo msimu uliopita baada ya kutwaa vikombe vitatu, Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Ngao ya Jamii.

Usajili bora uliofanywa na klabu hiyo msimu uliopita ulizaa matunda na hata msimu ujao wanaweza kuendeleza mafanikio hayo kutokana na wachezaji waliowasajili hivi karibuni.

Timu hiyo itatambulisha wachezaji wake katika kilele cha Wiki ya Wananchi itakayofanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga ndio timu iliyochukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara nyingi zaidi ikiwa imebeba mara 28 lakini bado kwa upande wa kimataifa haijatisha kwani haijawahi kuvuka zaidi ya robo fainali ya Ligi Mabingwa Afrika hatua ambayo ilifika mara mbili mfululizo 1969 na 1970.

Usajili uliofanywa na klabu hiyo kwa ajili ya mashindano ya msimu ujao, kidogo unatoa mwanga kuwa uongozi wa timu hiyo umepania kufanya maajabu kwenye michuano ya kimataifa na kuvunja rekodi iliyowekwa na Simba kwenye mashindano hayo kwa miaka mitatu ya karibuni.

Yanga imewaongeza kikosini wachezaji Lazarous Kambole kutoka Kaizer Chiefs Bernard Morrison (Simba), Stephane Aziz Ki (ASEC Mimosas), Joyce Lomalisa (G.D. Sagrada Esperanca) na Gael Bigirimana (Glentoran FC) ambao wanatakiwa kuunganisha nguvu na wenzao ili kuipa timu hiyo mafanikio kimataifa msimu ujao na kuendelea kuwatambia watani wao wa jadi Simba.

Advertisement


LIGI YA MABINGWA AFRIKA

Yanga ndio timu ya kwanza Tanzania kutinga robo fainali ya Klabu Bingwa Afrika (sasa Ligi ya Mabingwa Afrika) na ilifanya hivyo mwaka 1969.

Timu ilianza hatua ya awali kwa kuichapa Fitarinkandro ya Madagasca kwa jumla ya mabao 4-3, ikishinda mabao 4-1 nyumbani na kulala kwa mabao 2-0 ugenini.

Raundi ya kwanza iliifumua ST George ya Ethiopia mabao 5-0 iliyoyapata kwenye mchezo wa marudiano uliofanyika jijini Dar es Salaam baada ya kutoka suluhu ugenini hivyo kufuzu robo fainali.

Yanga ilikutana na Asante Kotoko ya Ghana kwenye mchezo wa robo fainali, ambapo mchezo wa ugenini timu hizo zilitoka sare ya 1-1 kama ilivyokuwa mchezo wa pili uliofanyika Dar.

Baada ya matokeo hayo ikaamriwa mechi ya kuamua nani aende nusu fainali ifanyike kwenye uwanja huru na ndipo mchezo mwingine ukapigwa nchini Ethiopia.

Hata hivyo, Yanga ilishindwa kutinga nusu fainali baada ya kufanyiwa hila na nahodha wa Asante Kotoko ambaye aliokota shilingi na kuanza kushangilia.

Ilikuwa hivi baada ya mchezo huo kumalizika kwa sare kipindi hicho kulikuwa hakuna mikwaju ya penalti hivyo mshindi kuamuriwa kwa mwamuzi kurusha shilingi.

Baada ya manahodha wote wawili wa Yanga na Asante Kotoko kuitwa, mwamuzi alirusha shilingi juu lakini wakati ikitua chini, nahodha wa Kotoko aliikota haraka haraka na kuanza kushangilia na kuungana na wenzake hivyo mwamuzi hakuwa na la kufanya zaidi ya kuwapa ushindi Waghana hao.

Yanga ilipambana tena na kurejea kwa nguvu mwaka uliofuata (1970) na kufika tena robo fainali ya michuano hiyo.

Ilianza raundi ya kwanza kwa kucheza na US Fonctionnaries ya Madagasca ambayo waliichapa jumla ya mabao 6-4, baada ya kuanza vizuri nyumbani kwa ushindi wa mabao 4-0 na kupoteza ugenini kwa kufungwa mabao 4-2.

Yanga liingia raundi ya pili na kupambana na Nakuru All Stars ya Kenya na kuichapa mabao 3-2, wakipoteza ugenini kwa bao 1-0 na kushinda nyumbani mabao 3-1 hivyo kutinga robo fainali.

Timu hiyo ilikutana tena na Asante Kotoko kwenye robo fainali na kukubali kipigo cha jumla ya mabao 3-1, baada ya kutoka sare nyumbani kwa bao 1-1 na kuchapwa ugenini mabao 2-0 hivyo kutupwa nje ya mashindano hayo.

Yanga ikakaa muda mrefu bila kufanya vizuri kwenye mashindano hayo lakini ikarejea kwa nguvu mwaka 1998 na kutinga hatua ya makundi.

Ilipata nafasi hiyo baada ya kuifunga Rayon Sport ya Rwanda kwa jumla ya mabao 3-3 ikifaidika na bao la ugenini baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 nchini Rwanda huku pia ikitoka sare ya bao 1-1 Dar es Salaam.

Raundi ya pili Yanga ilicheza na Ethiopian Coffee SC na kuichapa jumla ya mabao 8-3 na kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Hata hivyo, kwenye makundi Yanga haikutisha kwani ilishika nafasi ya mwisho katika kundi lao lililokuwa na timu za Asec Mimosas ya Ivory Coast, Manning Rangers ya Afika Kusini na Raja Casablanca ya Morocco.


KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

Baada ya mwaka 1998 Yanga kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika haikutikisa tena miaka iliyofuata na kutolewa raundi ya awali kila iliposhiriki.

Hata hivyo, baada ya miaka 18 kupita timu hiyo ilitinga tena hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikitokea Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga ilitinga hatua hiyo baada ya kupenya kwenye hatua ya mwisho ya mchujo kwa kuitoa timu ya Sagrada Esperanca ya Angola kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.

Hata hivyo, kwenye hatua ya makundi haikufanya vizuri na kushika mkia kwenye kundi lake ikiwa na pointi nne nyuma ya TP Mazembe ya Congo iliyokuwa kinara kwa pointi 13, Mo Bejaia ya Algeria iliyomaliza ya pili kwa pointi nane sawa na Medeama ya Ghana.

Mwaka 2018 iliingia tena hatua ya makundi ya mashindano hayo ambapo ilimaliza ikiwa ya mwisho nyuma ya timu za USM Alger, Rayon Sports na Gor Mahia ikivuna pointi nne. Ilitinga hatua hiyo baada ya kuitupa nje Welayta Dicha ya Ethiopia kwa ushindi wa jumla wa mabao 2-1.


KOMBE LA WASHINDI

Yanga pia iliwahi kufika robo fainali ya Kombe la Washindi kabla ya mashindano hayo kuunganishwa na yale ya Caf na sasa kujulikana kama Kombe la Shirikisho Afrika.


KOMBE LA KAGAME

Yanga imewahi kuchukua ubingwa wa Kombe la Kagame mara tano mwaka 1975, 1993, 1999, 2011 na 2012 huku ikichukua ubingwa wa kombe la Tusker mara mbili mwaka 2007 na 2009.


Advertisement