Washtueni kina Mwakinyo ngumi zinalipa

Muktasari:
- Licha ya kupata utajiri mkubwa kwa mabondia katika mataifa mengine, hapa nchini hakuna mabondia waliofikia viwango vya juu kiasi kwamba ngumi ziliwafanya waishi kitajiri na hivyo mabondia kama Hassan Mwakinyo na wenzake wanapaswa kukaza.
NEW YORK, MAREKANI: MBALI ya maumivu, mchezo wa ngumi umekuwa ukiwanufaisha kiuchumia mabondia wengi duniani, kwani baada ya kustaafu huishi maisha ya kitajiri kutokana na pesa nyingi walizolipwa walipocheza mapambano mbalimbali.
Licha ya kupata utajiri mkubwa kwa mabondia katika mataifa mengine, hapa nchini hakuna mabondia waliofikia viwango vya juu kiasi kwamba ngumi ziliwafanya waishi kitajiri na hivyo mabondia kama Hassan Mwakinyo na wenzake wanapaswa kukaza.
Kwa waliofanikiwam baadhi yao wamekuwa wakitumia pesa hizo kuwekeza na kuzidi kujitengenezea utajiri zaidi kila uchao.
Hii hapa orodha ya mabondia 10 ambao hadi sasa wanaongoza kwa utajiri kutokana na pesa walizokunja kupitia mapambano na wengine wametajirika zaidi baada ya kufungua kampuni zinazowaingizia vipato vya maana tu. Baadhi ya mabondia hao wamestaafu na wengine wanaendelea kupigana.

10. Tyson Fury (Dola 50 milioni)
Unaweza kumuita ‘The Gypsy King’ alipata malipo ya juu zaidi katika mchezo huu baada ya kushinda pambano lake dhidi ya Dillian Whyte lililopigwa Aprili, mwaka huu, ambapo amekusanya Dola 33 milioni.
Malipo mengine makubwa yalitokana na mapambano dhidi ya Wladimir Klitschko pamoja na mfululizo wa mapambano dhidi ya Deontay Wilder.
Licha ya kudai kwamba anataka kustaafu, ripoti taarifa zinaeleza anaweza kurudi ulingoni kupigana mapambano yasiyo ya ubingwa. Mbabe huyo ana utajiri unaofikia Dola 50 milioni.

9. Anthony Joshua (Dola 83 milioni)
Mwamba huyo alijipatia karibu Dola 80 milioni baada ya kushinda medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki ya London 2012.
Kwa sasa ndiye bondia aliyeweka rekodi ya pambano lake kutazamwa na watu wengi zaidi waliolipia moja kwa moja nchini Uingereza.
Malipo makubwa zaidi kwa Joshua maarufu AJ aliyapata 2019 wakati wa pambano lake la marudiano dhidi ya Andy Ruiz Jr, ambapo Mwingereza huyo aliripotiwa kupata Dola 85 milioni.
Hata hivyo, staa huyo anaweza akatoka katika nafasi hiyo na kwenda juu zaidi iwapo atapigana tena hivi karibuni ambapo pambano linatarajiwa kuwa kati yake na Daniel Dubois. Kwa ujumla utajiri wake unafikia Dola 83 milioni kwa mujibu wa Fobres.

8. Wladimir Klitschko (Dola 90 milioni)
Bondia huyo ambaye aliwahi kutawala miaka ya 2000 aliwahi kutawala katika uzito mzito wa juu duniani kwa muda mrefu ambapo tangu alipopigwa na Lamon Brewster 2004, Klitschko hakuambulia tena kichapo kwa miaka 11 hadi alipokutana na Tyson Fury 2015.
Pambano hilo lilimfanya apate pesa nyingi ambazo hakuwahi kupata awali na aliuongeza utajiri wake baada ya kwenda kupigana na Anthony Joshua, ambapo kwa ujumla mapambano hayo mawili yalimwingizia zaidi ya Dola 70 milioni.

7. Sugar Ray Leonard (Dola 120 milioni)
Akitambulika kama mmoja wa ‘Wafalme Wanne’ kwenye ngumi, Sugar Ray alishinda mataji ya dunia katika uzito wa aina zote na akashinda medali ya dhahabu kwenye michezo ya Olimpiki ya Montreal 1976.
Mmarekani huyo alikunja pesa nyingi kupitia mapambano dhidi ya Marvin Hagler, Donny Lalonde na Thomas Hearns. Lakini, malipo makubwa zaidi aliyapata alipopigana na Roberto Duran ambapo alikunja Dola 15 milioni.
Kwa sasa ni mmoja kati ya mabondia ambao wamewekeza katika biashara na anazidi kuuendeleza utajiri wake huko. Kwa ujumla anakadiriwa kuwa na utajiri unaofikia Dola 120 milioni.

6. Lennox Lewis (Dola 140 milioni)
Lewis ndiye bondia wa ria wa Uingereza mwenye utajiri mkubwa zaidi katika orodha, ambapo kwa mujibu wa Celebrity Net Worth unafikia Dola 140 milioni.
Mapambano makubwa yaliyompa pesa zaidi ni dhidi ya Evander Holyfield, Shannon Briggs na Frank Bruno.
Lakini pambano lake dhidi ya Mike Tyson ndilo ambalo lililompa pesa nyingi zaidi kiasi kinachokadiriwa kuwa Dola 112 milioni.
Tofauti na mabondia wengi, Lewis alistaafu akiwa bado bingwa wa uzito wa juu na hakuwahi tena kurudi ulingoni.

5. Oscar De La Hoya (Dola 200 milioni)
Licha ya kupigana katika baadhi ya mapambano makubwa zaidi katika maisha yake ya ngumi kama dhidi ya Felix Trinidad na Bernard Hopkins, mwanamasumbwi De La Hoya hakuwahi kupata pesa nyingi kama alizopata baada ya kupigana na Mayweather ambapo alikunja Dola 52 milioni.
Kwa sasa bingwa huyo wa zamani aliyewahi kushinda mikanda sita ya uzito wa juu anaendelea kuingizia kupato kupitia kampuni yake ya usimamizi wa mabondia na uandaaji wa mapambano ya Golden Boy Promotions. Awali alikuwa akimsimamia Canelo Alvarez na sasa anafanya kazi na Virgil Ortiz Jr, Jaime Munguia, Gilberto Ramirez na Ryan Garcia. Utajiri wake unadaiwa kufikia Dola 200 milioni.

4. Manny Pacquiao (Dola 220 milioni)
Kama ilivyo kwa mabondia wengine waliopo katika orodha hii, Pacquiao pia alipata malipo yake makubwa zaidi alipokuwa akipambana na Mayweather ambapo pambano hilo liliingiza kiasi cha Dola 600 milioni, huku likiweka rekodi ya kuwa pambano lililotazamwa zaidi na kulipwa katika ulimwengu wa ngumi.
Utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola 222 milioni na anatajwa katika jarida la Fobres kama mmoja kati ya wanamichezo waliolipwa zaidi katika miaka 10 iliyopita.
Kwa sasa anajihusisha na siasa ambapo alihudumu kama seneta wa Bunge la Ufilipino hadi kufikia 2022.

3. Saul ‘Canelo’ Alvarez (Dola 275 milioni)
Canelo bado anacheza ndondi hadi sasa na pambano lililowahi kumpa pesa nyingi ni dhidi ya Floyd Mayweather ambapo watu milioni 2.2 walinunua na kulitazama moja kwa moja kupitia mitandao ya kijamii.
Alijipatia kiasi cha Dola 5 milioni wakati Myweather akipata Dola 41 milioni.
Bondia huyo kutoka Mexico pia alipata pesa kupitia pambano dhidi ya Chavez na Golovkin. Tangu apigwe na Dmitry Bivol, mashabiki wengi wa ngumi wamekuwa wakitamani kuona pambano la marudiano ambalo linaweza kumpa mkwanja mrefu zaidi.
Mbali ya pesa za ulingoni staa huyo anapata pesa nyingi kupitia mikataba ya udhamini na kampuni mbalimbali pamoja na miradi binafsi. Utajiri wake unakadiriwa kufikia Dola 275 milioni.

2. George Foreman (Dola 300 milioni)
Bondia huyo mkongwe hadi alipostaafu alipigana mapambano 81 na anashika nafasi ya pili kwa utajiri wake unaokadiriwa kufikia Dola 300 milioni, ambapo mbali ya mkwanja wa maana alioupata katika ngumi pia amekunja pesa kupitia uwekezaji wake katika biashara mbalimbali.
Mapambano yake yaliyomfanya awe tajiri zaidi kabla ya kustaafu mchezo huo ni dhidi ya Joe Frazier, Evander Holyfield na Muhammad Ali.

1. Floyd Mayweather (Dola 400 milioni)
Majina ya utani anaitwa Money, Pretty Boy au TBE (The Best Ever) kwa sababu ya utajiri alionao. Mayweather aliwawezesha mabonda wengi aliopigana nao kupata pesa nyingi ambazo hawakuwahi kuzipata awali. Mr Money yupo katika rekodi ya mabondia wanne ambao waliingiza pesa nyingi kwa mapambano kutazamwa kwa njia ya mashabiki kulipiwa moja kwa moja mitandaoni. Mapambano yaliyowahi kumpa pesa nyingi zaidi ni dhidi ya Manny Pacquiao (Dola 250 milioni), Connor McGregor (Dola 275 milioni) na Logan Paul (Pauni 10 milioni).