Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanasoka maarufu waliozomewa na mashabiki wao uwanjani

Muktasari:

  • Alexander-Arnold hivi karibuni alitangaza uamuzi wa kuachana na Liverpool bure kabisa mwishoni mwa msimu huu, ikifahamika ataenda Real Madrid, jambo ambalo mashabiki wa Anfield wameamua kulijibu kwa kumzoea beki huyo ambaye ni zao la akademia ya miamba hiyo ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
no

LONDON, ENGLAND: BEKI wa kulia, Mwingereza Trent Alexander-Arnold ameingia kwenye orodha ya wanasoka waliowahi kuzomewa na mashabiki wao wenyewe wakati alipoingia kutokea benchini kwenye mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal iliyopigwa uwanjani Anfield, Jumapili.

Alexander-Arnold hivi karibuni alitangaza uamuzi wa kuachana na Liverpool bure kabisa mwishoni mwa msimu huu, ikifahamika ataenda Real Madrid, jambo ambalo mashabiki wa Anfield wameamua kulijibu kwa kumzoea beki huyo ambaye ni zao la akademia ya miamba hiyo ambao ndio mabingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.

Hata hivyo, Alexander-Arnold si mchezaji pekee mwenye jina kubwa kwenye mchezo wa soka aliyewahi kuzomewa na mashabiki wa timu yake.


Joshua Zirkzee (Man United vs Newcastle)

Mshambuliaji wa Kidachi, Joshua Zirkzee alijikuta kwenye midomo ya mashabiki kwa maana ya kuzomewa uwajani Old Trafford baada ya dakika 32 za mchezo zilizoshuhudia Manchester Unitd ikiwa nyuma kwa mabao 2-0, Desemba 2024.

Fowadi huyo alifanyiwa mabadiliko dakika hiyo ya mchezo na kuanza kuzomewa na mashabiki, jambo ambalo lilimfanya aende moja kwa moja vyumbani baada ya kuumizwa na zomeazomea hiyo ya mashabiki wa timu yake.

Baada ya hapo, Zirkzee alirudi kwa kasi kubwa uwanjani katika mechi zilizofuata, akifunga mabao muhimu kukisaidia kikosi hicho kufika fainali ya Europa League.


Emmanuel Eboue (Arsenal vs Wigan)

Hili tukio lilimuuma sana staa wa kimataifa wa Ivory Coast, Emmanuel Eboue wakati alipokuwa akikipiga Arsenal na kisha kuzomewa na mashabiki wa timu yake.

Eboue alikumbana na kadhia hiyo wakati alipofanyiwa mabadiliko kipindi Arsenal ikiongoza 1-0 dhidi ya Wigan mwaka 2008 na wakati anatoka uwanjani badala ya kupigiwa makofi kwa mchango wake wa uwajani, alipigiwa kelele za kuzomewa na mashabiki waliokuwa uwanjani Emirates.

Hilo lilimuumiza Eboue na kusema: “Nilishangazwa sana na uamuzi ule wa mashabiki. Timu nzima tulicheza vibaya, lakini tulishinda 1-0. Wote tulicheza vibaya. Lakini, sifahamu kwa nini ni mimi tu. Unapokuwa mchezaji na mashabiki wa timu yako wanakuzomea ni mbaya sana, hali yako ya kujiamini inatoweka. Baada ya tukio lile, nilimwambia Arsene Wenger, ‘siji mazoezini kwa sababu sijisikii vizuri.’“


Harry Maguire (England vs Ivory Coast)

Beki wa kati wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Harry Maguire naye aliwahi kukumbwa na balaa hilo la kuzomewa na mashabiki wa timu anayoichezea. Na mbaya zaidi kwa Maguire, alizomewa na mashabiki wa timu yake ya taifa wakati alipokuwa akiitumikia timu hiyo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Ivory Coast mwaka 2022.

Maguire alikumbana na zomeazomea ya mashabiki wakati jina lake lilipokuwa likitajwa kwa ajili ya utambulisho wa mechi hiyo na mwanzoni mwa mchezo huo, lakini kocha alimchezesha beki huyo wa kati kwa dakika zote 90 na kuisaidia England kuibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Maguire alikumbwa na nyakati ngumu baada ya kiwango chake kushuka kabla ya sasa kuwa mchezaji muhimu kabisa kwenye kikosi cha Man United kilichotinga fainali ya Europa League.


Lionel Messi (PSG vs Bordeaux)

Masupastaa wa soka, Lionel Messi na Neymar wote walikumbana na kasheshe la kuzomewa na mashabiki wa timu waliyokuwa wakiichezea Paris Saint-Germaim katika mechi ya Ligue 1 dhidi ya Bordeaux, Machi 2022.

Wanasoka hao wawili matata kabisa ndani ya uwanja waliandamwa na mashabiki wa PSG baada ya timu hiyo kupoteza uongozi wao katika mechi muhimu ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid siku chache zilizopita.

Jambo hilo liliwakera mashabiki hao na kuamua kwenda kuwazomea wachezaji wao baada ya kwenda kuwatazama katika mechi dhidi ya Bordeaux.

Na mashabiki wa timu hiyo walifika mbali zaidi baada ya kumtaka Messi aondoke kwenye timu yao kwa kuchora maandishi kwenye uwanja wa mazoezi wa timu hiyo na kuonyesha hakuna mchezaji ambaye yupo salama mbele ya mashabiki wenye hasira ya kutaka matokeo.


Granit Xhaka (Arsenal vs Crystal Palace)

Kiungo, Granit Xhaka aliingia kwenye anga za kuzomewa na mashabiki wa Arsenal mwaka 2019 licha ya kwamba alikuwa nahodha wa timu hiyo kipindi ilipokuwa chini ya kocha Unai Emery.

Kiungo huyo wa Uswisi alionekana kukasirika baada ya kutolewa katika mechi ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Crystal Palace kitu ambacho kilijibiwa na mashabiki wa timu yake uwanjani hapo kwa kutoa kelele za kumzomea.

Xhaka alifanya tukio la kuwajibu mashabiki, kitu ambacho kilimfanya avuliwe unahodha baada ya tukio hilo.

Hata hivyo, aliendelea kuitumikia timu hiyo kwa miaka minne zaidi kabla ya kuondoka kwenye Ujerumani, ambako aliandika rekodi ya kuipa ubingwa Bayer Leverkusen bila ya kupoteza mechi msimu uliopita.


Wayne Rooney (England vs Malta)

Supastaa, Wayne Rooney anakumbukwa kama shujaa wa England, lakini bado alijikuta kwenye balaa la kuzomewa na mashabiki wa timu hiyo katika nyakati za mwisho za maisha yake ya soka la kimataifa.

Baada ya England kufanya vibaya kwenye Euro 2016, supastaa Rooney alitumika kwenye eneo la kiungo katika mechi za timu hiyo na kujikuta kwenye hali ya kuzomewa na mashabiki wa kikosi cha Three Lions katika mechi dhidi ya Malta.

Siku tatu baadaye, kocha wa kipindi cha mpito wa England, Gareth Southgate aliwekwa kando kwenye kikosi kilichoanza dhidi ya Slovenia na hilo lilikuwa mwanzo wa mwisho wa Rooney kwenye soka la kimataifa.


Jorginho (Chelsea vs Malmo)

Kiungo, Jorginho baadaye alifanikiwa kubadili maisha yake kwenye kikosi cha Chelsea, lakini Mtaliano huyo alikuwa kwenye wakati mgumu mwanzoni mwa maisha yake ya mwanzo uwanjani Stamford Bridge, wakati alipokumbana na balaa la kuzomewa na mashabiki wa timu yake.

Kiungo huyo anayekipiga Arsenal kwa sasa na mwenye mpango wa kuachana na klabu hiyo ya Emirates mwishoni mwa msimu ujao, alikumbana na balaa la kuzomewa kwenye mechi ya Europa League wakati alipotolewa uwanjani kumpisha Ross Barkley dhidi ya Malmo.

Katika mechi hiyo, Jorginho alicheza kwa kiwango cha hovyo sana na kuwatibua mashabiki.


Gareth Bale (Real Madrid)

Winga Gareth Bale, aliyewahi kuwa mchezaji ghali duniani alikumbana na kasheshe hilo la kuzomewa na mashabiki wakati alipokuwa akiichezea Real Madrid.

Mashabiki wa Los Blancos walikuwa hawamwelewi kabisa staa huyo wa zamani wa kimataifa wa Wales na kitu ambacho walikuwa wakikifanya ni kumzomea staa huyo.

Bale alionyesha kuwa ni jeuri kabisa baada ya kuwajibu mashabiki wa Madrid baada ya kuwaambia kwa mtiririko vitu anavyovipenda ni Wales, gofu kisha ndio inafuata Madrid, kitu kilichowatibua zaidi mashabiki wa kikosi hicho cha Bernabeu.


Rio Ferdinand (Man United vs Chelsea)

Baada ya miaka mitatu ya kuwa kwenye kikosi cha Manchester United, beki wa kati Rio Ferdinand aliaminika kama kipaji matata kabisa ambacho kisingetokea siku yoyote kikapingwa na mashabiki wa timu yake.

Kwa namna ambavyo alikuwa akichukua timu yake ya Man United kuachwa nyuma na Arsenal ya Arsene Wenger na Chelsea ya Jose Mourinho, Rio aliingia kwenye mzozo wa mashabiki baada ya kugomea kusaini mkataba mpya wa kuendelea kubaki Old Trafford.

Kutokana na hilo na baada ya kudaiwa kwamba Chelsea ingeweza kunasa saini yake, Ferdinand alijikuta kwenye wakati mgumu wa kuzomewa na mashabiki wa Man United katika majira ya kiangazi 2005.

Baadaye aliamua kusaini mkataba mpya na kubaki Man United, ambako kwa sasa anahesabika kama gwiji.


Ashley Cole (England vs Kazakhstan)

Hakuwa akikubalika sana kwa mashabiki licha ya kuwa mmoja wa mabeki wa kushoto mahiri kabisa waliowahi kutokea kwenye mchezo wa soka.

Ashley Cole alionyesha kiwango bora kwenye timu zote alizocheza, lakini aliingia kwenye kasheshe la kuzomewa na mashabiki wa timu yake ya taifa ya England baada ya kufanya kosa katika mechi dhidi ya Kazakhstan kwenye mechi ya kufuzu fainali ya Kombe la Dunia 2010.

Lakini, uhusiano wake na mwimbaji wa pop, Cheryl Cole ulimfanya kuwa maarufu na kupamba kurasa za mbele za magazeti ya udaku huko England huku akipondwa na mashabiki wa Arsenal baada ya kuwaacha na kuhamia Chelsea, wakimtuhumu tamaa ya pesa ilimponza.