WANAPENYAJE? Vita ya mwisho kusaka tiketi Afcon 2025

Muktasari:
- Hadi sasa timu 19, tayari zimeshafuzu kucheza michuano hii na timu tano ndio zinasubiriwa kukamilisha idadi ya 24.
Kesho na keshokutwa itakuwa ni mwisho wa kuzisaka timu 24 zitakazoshiriki mfainali za mataifa ya Africa (AFCON), zitakayofanyika kuanzia Desemba 21 mwakani hadi Januari 18, 2026.
Hadi sasa timu 19, tayari zimeshafuzu kucheza michuano hii na timu tano ndio zinasubiriwa kukamilisha idadi ya 24.
Hapa tumekuletea hesabu za vidole za mataifa mbalimbali ambayo yanagombania nafasi hizo tano zilizobaki katika mechi za mwisho za makundi.

KUNDI D
Timu iliyofuzu katika kundi hili hadi sasa ni Nigeria pekee ambayo ina pointi 11.
Leo itakuwa ni zamu ya timu nyingine tatu ambazo zinawania nafasi moja ya kuungana na miamba hiyo ambazo ni Libya, Rwanda na Benin.
Rwanda iliyo nafasi ya pili kwa pointi zao saba, inahitaji ushindi tu katika mchezo wao dhidi ya Nigeria ili kufuzu, sawa na ilivyo kwa Libya na Benin ambazo mbali ya kushinda zitatakiwa kuiombea Rwanda ipate sare ama ifungwe.
Ikiwa Rwanda itashinda itakuwa na pointi 10 ambazo Libya na Benin mmoja wao akimfunga mwenzake hawatoweza kuzifikia.
Hata hivyo, Rwanda inaonekana kuwa na wakati mwenye dimba la Godswill Akpabio International huko Uyo.
Nigeria ilipata bahati ya kufuzu mapema katika kundi hili baada ya kupewa ushindi wa mezani kutokana na kuahirishwa kwa mchezo wao dhidi ya Libya baada ya kile kilichodaiwa kuwa ni hujuma za makusudi walizofanyiwa na wenyeji wao na kujikuta wakikwama kwenye uwanja wa ndege wa Libya kwa zaidi ya saa 10, hali iliyosababisha wakatae kucheza.

KUNDI C
Katika kundi C, Misri tayari imeshafuzu kwa alama zake 13 baada kushinda mechi nne kati ya tano ilizocheza hadi sasa.
Bado inatafutwa timu moja itakayoungana na Misri na mechi zao za kuamua zitapigwa kesho ambapo Botswana na Mauritania ndio zitakuwa zinaipambania huku Cape Verde tayari ikiwa imeshaondolewa kwa sababu hata ikishinda mechi ya mwisho na kufikisha pointi saba haitoweza kuishusha Botswana kwani katika mechi zao mbili zilizowakutanisha ilipoteza zote.
Botswana ambayo itacheza dhidi ya Misri, inahitaji kushinda ama kutoa sare tu ili kufuzu wakati Maurtania yenye pointi nne inahitaji ushindi kwa namna yoyote na kuiombea Botswana ipoteze.

KUNDI F
Moja kati ya mambo yaliyoshangaza watu wengi katika kundi hili ni matokeo ya Ghana ambayo tayari imeshatupwa nje ya kinyang'anyiro cha kufuzu ikiwa mkiani mwa kundi kwa pointi zake tatu.
Angola tayari imeshafuzu baada ya kufikisha alama 13, na timu zinazowania nafasi ya pili ni Sudan na Niger zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu mtawalia. Sudan ina pointi saba huku Niger ikiwa na pointi nne.
Niger inahitaji ushindi ili kufikisha pointi saba na Sudan inahitaji walau sare tu itakayoifanya ifikishe pointi nane.
Sudan itacheza dhidi ya Angola ambapo kwa sababu za kiusalama mchezo wao utapigwa kwenye dimba la Benina Martyrs, Benghazi, Libya.
Mchezo huu unatarajiwa kuwa na ushindani zaidi kwa sababu Angola haijawahi kupoteza mchezo wowote katika kundi hili hadi sasa na tayari imeshafuzu huku hata ikipoteza haitoshushwa.
Kwa upande wa Niger licha ya Ghana kuonekana kama moja ya timu mbovu zaidi kwenye kundi hili la kufuzu, bado inaonekana kuwa mechi ngumu kwao kwani itacheza katika ardhi ya Ghana.
Licha ya ukweli kwamba ushindi hautawapeleka popote, lakini wanaweza kuhitaji kukataa unyonge kwani wakifungwa watazidi kupoteza imani kwa mashabiki wao.

KUNDI I
Baada ya Mali kufuzu wiki iliyopita, nafasi moja iliyobakia inagombaniwa na Msumbiji iliyo katika nafasi ya pili kwa pointi nane na Guinea-Bissau ambayo inashikilia nafasi tatu kwa pointi tano.
Utamu wa kundi hili ni kwamba Msumbiji na Guinea ya Bissau zitaamua nani aungane na Mali zenyewe zitakapokutana kesho.
Msumbiji inahitaji kutoa sare ama kushinda ili kufuzu wakati Guinea italazimika kushinda.
Ikiwa Guinea-Bissau itashinda itafikisha pointi nane na kitakachoamua nani aende ni mabao ya kufunga na kufungwa baina ya timu hizi mbili.
Mchezo wa kwanza uliowakutanisha ulimalizika kwa Msumbiji kushinda mabao 2-1, hivyo Guinea Bissau itahitaji kushinda mabao 2-0 na ikipata ushindi ushindi chini ya hapo itakuwa imeipa nafasi Msumbiji ya kwenda Morocco.

KUNDI H
Baada ya Tanzania na Guinea kushinda mechi zao zilizopita, mechi ya mwisho itakayozikutanisha ndio itaamua nani afuzu.
Tayari DR Congo imeshafuzu huku Ethiopia ikiwa imeondolewa kabisa katika kinyang'nyiro baada ya kupoteza mchezo wao uliopita dhidi ya Tanzania.
Mchezo wa Guinea na Tanzania ambao utapigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Guinea itakuwa inahitaji angalau sare ili kupenya wakati Tanzania ni lazima ishinde.
Tanzania ambayo ina alama saba ikishinda itafikisha alama 10, wakati Guinea ikishinda itafikisha 12 kutoka tisa ambazo inazo kwa sasa.
ZILIZOFUZU
Morocco, Burkina Faso, Cameroon, Algeria, DR Congo, Misri, Angola, Equatorial Guinea, Ivory Coast (Mabingwa watetezi), Uganda, Afrika Kusini, Gabon, Tunisia, Nigeria, Zambia, Mali, Zimbabwe na Comoros.