Prime
Hawa ndo wapiga kura Mkutano Mkuu wa TFF

BADO tunaendelea kuwaletea mfululizo wa makala maalumu kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), uliopangwa kufanyika Agosti 16 jijini Tanga ukihusisha nafasi saba, ikiwamo Urais na Wajumbe (6) wa Kamati ya Utendaji ya shirikisho hilo.
Mchakato wa uchaguzi huo unaofanyika kila baada ya miaka minne, ulianza Juni 16 kwa wadau mbalimbali kuchukua na kurudisha fomu, zoezi lililofikia tamati Juni 20 kabla ya kutangazwa orodha ya waliojitokeza, ambapo jumla ya wagombea 25 walifahamika wakiwamo sita wa nafasi ya Urais.
Wagombea hao waliojitokeza katika nafasi hizo ni Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia, Ally Mayay, Dk Mshindo Msolla, Richard Shija, Ally Thabit Mbingo na Mustapha Salum Himba, huku 19 wakijitokea kuomba ridhaa ya kuwania nafasi sita za Kamati ya Utendaji ya TFF.
Wagombea wote waliojitokeza walikuwa wasikilizia mapingamizi kutoka kwa wadau kabla ya kupenya na kwenda kwenye usajili na wakitoka hapo salama, wataingia katika kampeni kabla ya kusubiri upigaji kura utakaofanyika Agosti 16 katika Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa shirikisho hilo.
Leo katika muendelezo wa makala za uchaguzi tunaangalia wapiga kura wa uchaguzi huo ambao ndio walioshikilia hatma ya wagombea waliojitokeza na hasa wale watakaopenya hadi kuingia kwenye hatua ya kupigiwa kura Agosti 16 ni kina nani? Endelea nayo...
WAPIGA KURA
Kumekuwa na mkanganyiko wa idadi halisi ya Wajumbe Wapiga Kura wa Uchaguzi Mkuu wa TFF, wapo wanaoamini ni 76, wengine wakidhani wajumbe 47 wenye dhamana ya kuwaidhinisha wagombea katika mchakato wa awali (endorsements) ndio wahusika.
Hata hivyo ukweli ni kwamba kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uchaguzi huo wa TFF, wajumbe wenye dhamana ya kuchinja na kupitisha wagombea kuwa viongozi wa shirikisho hilo kupitia Uchaguzi Mkuu ni 83 ambao wanachagua Rais na Wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji.
WENYEVITI/ RAIS 16 WA KLABU
Klabu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara zinahusika kutoa wajumbe wapiga kura wa Uchaguzi wa TFF kwa mujibu wa mabadiliko ya Kanuni za Uchaguzi wa TFF ya mwaka 2021.
Wenyeviti au Marais wa klabu hizo 16 za Ligi Kuu wote wanatambulika kama wajumbe halali wa uchaguzi huo wa TFF, ikiwa na maana kwa mfano kwa sasa kuna klabu za Yanga, Simba, Azam, Singida Black Stars, Tabora United, JKT Tanzania, Mashujaa, Coastal Union, Namungo, KMC, Pamba Jiji, Dodoma Jiji sambamba na zilizopanda msimu huu zina baraka zote za kuwapigia kura wagombea katika uchaguzi huo, ikiwa na maana zinabeba wapiga kura 16 wa kwanza.
WAJUMBE 52 WA VYAMA 26
Mbali na Wenyeviti na Marais wa Klabu za Ligi Kuu wanaopiga kura katika Uchaguzi wa TFF, pia kuna wajumbe 52 kutoka Vyama vya Soka vya Mikoa 26 inayotambuliwa kisoka.
Kwa mujibu wa kanuni na taratibu ni kwamba kila mkoa unawakilishwa na wajumbe wawili tofauti na wale wa Klabu za Ligi Kuu ambao wanawakilishwa na mjumbe mmoja mmoja tu.
Kwa wanaopiga kura kupitia vyama vya soka wanawakilishwa na wajumbe wawili, Mwenyekiti na Mjumbe wa Mkutano Mkuu, ndio waliobeba dhamana ya kuamua safu ya uongozi wa TFF kila baada ya miaka minne ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu.
Wawakilishi hawa wamekuwa wakipatikana kupitia chaguzi ambazo zinamalizikia zikifanyika kutoka kila mkoa kabla ya mkutano mkuu wa TFF wa uchaguzi.
WAJUMBE VYAMA SHIRIKISHI
Kundi la mwisho la wapiga kura wa Uchaguzi Mkuu wa TFF ni Wajumbe 15 kutoka vyama vitano shirikisho vya TFF ambao hutoa Mwenyekiti, Katibu Mkuu na Mjumbe wa Mkutano Mkuu.
Vyama hivyo ni vile vya Chama cha Wachezaji Tanzania (SPUTANZA), Chama cha Madaktari wa Michezo (TMSA), Chama cha Makocha (TAFCA), Chama cha Marefa (FRAT) na Chama cha Soka la Wanawake (TWFA).
Kwa kuwa kila chama kinatoa wajumbe watatu wa kushiriki kupiga kura, maana yake ni kwamba kupitia vyama hivyo vitano vyenyewe vinakuwa na wapiga kura 15 katika Uchaguzi Mkuu wa TFF.
Hivyo basi ukijumuisha wapiga kura hao kutoka katika kila kundi utapata jumla ya watu 83 na sio 76 kama ilivyokuwa ikielezwa awali na wala sio wale 47 waidhinishaji wanaofanya endorsement kwa wagombea mara wanapochukua fomu za kuwania nafasi katika uchaguzi huo kwa mujibu w Ibara ya 10(3-4) ya Kanuni za Uchaguzi Mkuu wa TFF ya Mwaka 2021.
Wajumbe hao 47 wa kupitisha endorsement kwa wagombea wapo ndani ya wajumbe 83 wanaopiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa TFF na kanuni inawabana ni lazima wasipungue watano kwa kila mgombea na mjumbe mmoja hawezi kuidhinisha zaidi ya mtu moja.
Kesho tutaangalia kanda zipi zenye nguvu na zilizoshikilia hatma ya wagombea wa Uchaguzi Mkuu wa TFF.