Wamotoo! Makipa wa benchi wakali Ligi Kuu

Muktasari:

KILA kikosi Ligi Kuu Bara kina makipa imara ambao wana uwezo kuhakikisha timu zinafanya vizuri kwenye kila mchezo wa michuano hiyo na mingine itakayohusisha vikosi vyao.

KILA kikosi Ligi Kuu Bara kina makipa imara ambao wana uwezo kuhakikisha timu zinafanya vizuri kwenye kila mchezo wa michuano hiyo na mingine itakayohusisha vikosi vyao.

Timu nyingi kwenye Ligi Kuu zina makipa namba moja na mbili wenye uwezo mkubwa na yote hiyo ni kuhakikisha tu kunakuwa na ushindi muda wote ambao iwapo kipa namba moja atakosekana, basi yule wa pili anachukua mikoba yake. Mwanaspoti linakuletea timu zenye makipa wanaosugua benchi, lakini bado wana uwezo mkubwa wa kucheza kikosi cha kwanza na bado kusiwe na tatizo lolote.


SIMBA

Katika kikosi cha Simba kipa namba moja ni Aishi Manula, lakini msimu huu amesajiliwa Jeremiah Kisubi akitokea Tanzania Prisons. Kipa huyo msimu uliopita alikuwa katika kiwango bora hali ambayo iliwalazimu mabosi wa Simba wamvute mitaa ya Msimbazi msimu huu.

Wakati Kisubi akijiunga kwenye timu hiyo, yupo pia Beno Kakolanya ambaye naye ni wa moto kwelikweli akiwa kama chaguo la pili nyuma ya Aishi Manula. Chaguo la tatu kwenye kikosi cha Simba ni Ally Salim ambaye naye yupo vizuri akiwa kipa kijana anayehitaji muda zaidi wa kukua na kujifunza mbele ya makipa wenye uzoefu.


BIASHARA UNITED

Ujio wa kipa James Ssetuba katika kikosi cha Biashara United umeongeza ushindani kwa kipa Daniel Mgore. Ssetuba amechukua namba na kuwa kipa tegemeo katika kikosi cha kwanza.

Mgore ni kipa mzuri na aliwahi kuitwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kwa vipindi tofauti, lakini kwa sasa hana uhakika wa namba kwenye kikosi cha Biashara United.

Ssetuba amekuwa katika kiwango kizuri kwenye Ligi Kuu hadi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika akihakikisha timu inafanya vizuri kwa kutoruhusu mabao - akiwapanga vizuri pia mabeki wake.


KMC

Kwenye kikosi cha KMC nako moto unazidi kuwaka kwani kwenye benchi la makipa ukiondoa uwapo wa mkongwe Juma Kaseja, wapo pia Sudy Dondola na Farouk Shikhalo ambaye msimu uliopita aliidakia Yanga.

Shikhalo akiwa Yanga alikuwa akipokezana kijiti na Metacha Mnata, lakini KMC kakutana na Kaseja ambaye amejihakikishia nafasi kwenye kikosi hicho.

Naye Dondola kwenye kikosi hicho aliwafanya Denis Richard na Rahim Sheikh wasiwe na namba wakaamua kutimkia kwa mkopo Dodoma Jiji.


AZAM FC

Kipa namba moja katika kikosi cha Azam ni Mathias Kigonya. Awali, kulikuwa na Benedict Haule na David Kissu lakini wametolewa kwa mkopo baada ya kushindwa kumpa changamoto Kigonya.

Kuondoka kwao kumempa nafasi Wilbol Maseke aliyepandishwa toka timu ya vijana na kuwa namba mbili kutokana na uwezo wake. Kipa huyo pia amekuwa akiitwa mara kwa mara katika kikosi cha Taifa Stars.


YANGA

Hata kama kipa namba moja Diara Djigui atakosekana kikosini, benchi la ufundi Yanga litakuwa na amani kubwa kutokana na uwepo wa wengine.

Kwenye benchi yupo Erick Johola ambaye ana uzoefu wa soka la kulipwa nje ya nchi wakati huohuo pia yupo Ramadhan Kabwili. Hivi karibuni Kabwili amekuwa akiitwa timu ya Taifa na kocha Kim Poulsen.


DODOMA JIJI

Kipa Rahim Sheikh baada ya kuona mambo si mazuri KMC msimu uliopita, mwanzoni mwa msimu huu alienda zake Dodoma Jiji kwa mkopo. Ni kipa mwenye uwezo mkubwa, lakini kucheza na wakongwe kama Kaseja na Dondola kulimnyima nafasi hali iliyomfanya atumike zaidi kwenye timu za vijana.

Hata hivyo, kwenda Dodoma Jiji anamekutana na Hussein Masalanga ambaye anasimama langoni kikosini.


NAMUNGO FC

Msimu uliopita kwenye kikosi hicho kulikuwa na vita ya namba kati ya Razack Barola na Jonathan Nahimana. Barola baada ya kuona mambo si mambo licha ya uwezo wake mkubwa, aliamua kuondoka na kujiunga Kagera Sugar msimu huu.

Msimu huu, David Kissu amejiunga na Namungo kwa mkopo akitokea Azam. Ubora wake unaendelea kuifanya Namungo kuendelea kuwa katika mikono salama hata akikosekana Nahimana.


MTIBWA SUGAR

Chipukizi Abuutwalib Msheri amejihakikishia namba kwenye kikosi cha kwanza cha Mtibwa Sugar tangu msimu uliopita, lakini hata akikosekana Mtibwa ipo salama kwa sababu yupo mkongwe Shaban Kado. Kado amekuwa akipishana golini muda mwingine na Msheri pindi panapokuwa na ulazima wa kufanya hivyo.


MAKOCHA WANASEMAJE

Kocha wa msaidizi wa Twiga Stars, Edna Lema anasema ni vyema kila timu kuwa na makipa wenye viwango vizuri hata kama hawalingani ubora.

“Kikubwa ni kwamba akikosekana mmojawapo, basi mwingine akiingia naye atakuwa na wakati mzuri.”

Kocha wa Friends Rangers, Heri Mzozo alisema: “Ni kitu kizuri na inaonyesha (makipa Ligi Kuu) wote wana uwezo ambao haupishani sana. Timu zenye hela lazima ziwe hivyo, lakini natamani ligi ingekuwa na mechi nyingi ili wote wacheze. Kwa mechi zilizopo ni ngumu wote kucheza hasa wale wa Simba.”