WAMETISHA! Waliocheza mechi nyingi WPL

WAMETISHA! Waliocheza mechi nyingi WPL

Muktasari:

  • IKIWA Ligi Kuu ya Wanawake Bara iko karibu kurejea wiki chache zijazo baada ya kumalizika kwa maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, kuna baadhi ya wachezaji wamemwaga jasho jingi

IKIWA Ligi Kuu ya Wanawake Bara iko karibu kurejea wiki chache zijazo baada ya kumalizika kwa maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli, kuna baadhi ya wachezaji wamemwaga jasho jingi.

Wachezaji hao ndio wanaongoza kwa kucheza dakika nyingi zaidi kwenye ligi hiyo zikiwa ni 1350 ambazo ni sawa na michezo 15.

Kinadada hao wamemwaga jasho la kutosha uwanjani, ingawa kuna baadhi yao jasho lao limekuwa halina faida na wengine limekuwa na faida.

Hawa hapa wachezaji wanane ambao wamecheza dakika nyingi zaidi kwenye ligi hiyo na mchango wao kwenye timu.


Amina Bilal - Yanga Princess

Huyu ni mmoja kati ya viungo mahiri wa Yanga Princess na timu ya taifa ya Tanzania. Ndiye mchezaji pekee anayeongoza kwa kucheza dakika nyingi kwenye kikosi hicho na vilevile kwenye upande wa mabao amefunga matano ambayo yanamuweka nafasi ya tatu nyuma ya Aisha Masaka mwenye mabao 20 na Philomena Daniel mabao sita.

Mbali ya Shelda Boniphace kutoka Yanga kwenda Simba Queens, huyu pia aliwahi kutoka Simba kwenda Yanga.

Mchango wake umeifanya timu yake kushika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 15 na kukusanya alama 38 wakiwa nyuma ya Simba inayoongoza kwa alama 39.


Anastazia Katunzi - JKT Queens

Ni kitasa wa JKT Queens. Mrembo huyu awapo kwenye timu yake hucheza namba tano, lakini hubadilishiwa majukumu awapo timu ya taifa kwa kuchezeshwa namba sita.

Mbali ya uwezo mkubwa wa kuzuia na kulinda safu yake ya ulinzi, pia ana uwezo mzuri wa kufunga.

Msimu huu ameingia kambani mara sita akiiwezesha timu yake kushika nafasi ya tatu kwa kuwa na alama 36.


Elieth Edward - Fountain Gate Princess

Mchezaji wa zamani wa Marsh Queens ambaye mbali ya kukiwasha ndani ya uwanja kama beki wa kati akiwa na Fountain Gate Princess, pia huyu ni mama wa mtoto mmoja. Ni mmoja kati ya wa-chezaji wakongwe kwenye ligi ya wanawake. Timu yake inashika nafasi ya nane ikiwa na alama 19 ilizokusanya katika mechi 15 ambazo zote ali-kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.


Adija Petro - TSC Queens

Baada ya kusajiliwa na TSC katikati ya m-simu uliopita na kuonyesha kiwango bora kwa kumaliza akiwa na mabao saba, msimu huu amezidi kuwa lulu na hata kumshawishi kocha wa timu ya taifa ya Wanawake, Bakari Shime amuite kwenye kikosi chake kilichokuwa kinajiandaa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia na Michuano ya Mataifa ya Afrika (Afcon).

Hadi sasa ameingia kambani mara 13 na timu yake inashika nafasi tisa.

Abeda Said - E.S Unyanyembe

Mbali ya kucheza kama beki pia anaimudu kiungo. Amecheza mechi nyingi, lakini hazina faida kwani licha ya kuipandisha timu daraja wana asilimia 70 kushuka nayo msimu huu kwa sababu haifanyi vizuri kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu ikishika mkia ikiwa haijapata walau hata alama moja katika mechi 15 ilizocheza.


Jamila Mnunduka - Baobab Queens

Ni staa mwingine ambaye faili lake lipo kwa Shime akitegemea kumtumia zaidi kwenye timu ya taifa.

Kabla ya kutua Baobab alikuwa akiitumikia Panama ambayo ilishushwa daraja msimu uliopita.

Jamila ameonyesha kiwango bora msimu huu ambapo amefunga mabao 13 katika mechi 15 ambapo hajakosa hata moja kuichezea timu hiyo.

Kiwango chake kimekuwa na msaada kwenye timu kwani inashika nafasi ya saba kwa kuwa na alama 23.


Halima Mcheni - Baobab Queens

Ni kiungo mnyumbulifu ambaye kabla ya kutua Baobab alikuwa akiichezea Ruvuma Queens. Halima ametengeneza muunganiko mzuri kati yake na Jamila ambaye ndiye mfungaji kinara wa timu hiyo. Pasi za upendo zenye kujaa marashi huwa zinatoka kwake.


Amina Ramadhani - kigoma Sisterz

Licha ya kuwa si miongoni mwa wachezaji walioitwa timu ya taifa kwa mara ya mwisho, lakini bado fundi huyu wa kucheka na nyavu amekuwa na kiwango bora msimu huu. Katika msimamo wa wafungaji bora anashika nafasi ya tano na mabao 14 na kabla ya kutua Ruvuma alipita Simba na Kigoma Sisterz. Hadi sasa ameiwezesha Ruvuma kushika nafasi ya tano ikiwa na pointi 24.