Waliokosa wadhamini wapewe nafasi, kura zitaamua

Oscar Oscar akizungumza na wandishi wa habari baada ya kurudisha fomu ya kugombea nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).Picha na Michael Matemanga

Muktasari:

KINACHOENDELEA kwenye michezo hivi sasa hasa kwa hapa nchini mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 7, jijini Tanga.

KINACHOENDELEA kwenye michezo hivi sasa hasa kwa hapa nchini mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) utakaofanyika Agosti 7, jijini Tanga.

Walijitokeza wengi uchukuwa fomu ingawa wengine waliishia njiani kwa kushindwa kurudisha fomu hapo ikiwa na maana kwamba walijiengua wenyewe.

Mbali na hilo ilidaiwa kwamba baadhi yao hawakurudisha fomu ni baada ya kukosa wadhamini kama kanuni ya uchaguzi inavyoeleza kwamba mgombea ni lazima awe na wadhamini kuanzia watano.

Mchujo kwa wagombea uliendelea hadi juzi ambapo jana yalitangazwa majina ya wagombea watatu tu waliopita katika mchujo wa awali ambapo kama ilivyotarajiwa Wallace Karia anayetetea kiti chake cha Urais alipenya, pamoja na Evans Mgeusa na mwanamke pekee, Hawa Mniga.

Kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo kushindwa kufikisha idadi wa wadhamini watano, walijitosa kutaka kugombea kama kina Ally Mayay, Rahim Kangezi ‘Zamunda’, mwandishi wa habari na mchambuzi wa soka, Oscar Oscar, Ally Saleh wamechujwa.

Lakini wakati yote hayo yanaendelea tangu mchakato huo uanze kwa kutangazwa tarehe ya kuanza kuchukuwa fomu, ni juu ya kipengele hicho cha wadhamini ambacho ndicho kinalalamikiwa hadi hivi sasa na wadau wa soka.

Katiba ya TFF ilibadilishwa muda kidogo ikiwamo na mabadiliko ya kanuni ya uchaguzi kwa baadhi ya vipengele, mabadiliko hayo yalizungumzwa lakini huenda wengine hawakuyapa umakini ama hawakuyazingatia madhara yake ya baadaye.

Walio wengi waliyachukulia ni mabadiliko ya kawaida pengine waliamini kupata udhamini ni jambo dogo ambalo lisingeweza kuwaathiri, hivyo wamekumbuka shuka wakati tayari kumekucha kabisa, siku zimekwisha labda busara tu itumike sasa kubadilisha kanuni hiyo ya uchaguzi kipengele cha udhamini.

Malumbano na malalamiko ni mengi ingawa TFF yenyewe imetoa ufafanuzi juu ya mabadiliko hayo na hata serikali nayo imeelezea kuwa hakutakuwepo na mabadiliko yoyote kwenye uchaguzi huo na kanuni zitakazotumika ni hizo hizo zilizowekwa na kupitishwa.

Ndio maana nimesema labda itumike busara juu ya kipengele hicho na kuwapitisha wagombea ila kila mmoja akaamuliwe kwenye sanduku la kura kwa yule ambaye kura hazitatosha atatulia na kuridhika kuliko inavyokuwa sasa wanaoneka kuonewa na kutotendewa haki.

Wanasema mtoto akililia wembe mpe ukimkata ndiyo atajua madhara ya wembe huo, hivyo hata hao wengine wasichujwe, kura ndiyo zitaamua siku ya mwisho na hii itasaidia kuepusha kuwepo na malumbano pamoja na chuki zisizokuwa na msingi.

Ikumbukwe kwamba kuna maisha baada ya uchaguzi huo, kuna urafiki baada ya uchaguzi hivyo huu mchakato usiwagawe watu na kuwa watu wa makundi ambayo yatasababisha mipasuko na kutengenezeana fitina za ajabu ajabu.

Kila mmoja akijipime kwa ubavu wake pale Tanga, maana wapiga kura ndiyo walioshika makali na sio wagombea, mgombea siku hiyo akipata kura moja amshukuru Mungu kupata hata hiyo aliyojipigia mwenyewe lakini hatamlaumu mtu maana wajumbe watakuwa wameamua kufanya yao.

Wagombea wasinyimwe haki kwa kukosa wadhamini kama wana sifa nyingine waache wapitishwe ili wakapambane mbele ya safari maana sera zao ndizo zitakazowapa kura ingawa siku hizi sera haziangaliwi sana, bali kupendwa ndiyo kila kitu.

Wajumbe wakikukubali hata uwe na sera mbovu unapitishwa mengine itafahamika baadaye ila huku tayari wamefanya yao, sasa mgombea jiandae na sera zako za maana huku ukiwa na wadhamini wa kutosha lakini wajumbe wakikukataa andika tu maumivu.

Jambo moja la kukumbusha kuwa tujitahidi kuwa watu wa kufuatilia mambo mapema kuliko kusubiri dakika za lala salama, hili jambo lingefuatiliwa mapema na wadau ama wanachama huenda kipengele hicho kingekuwa kimerekebishwa na wagombea wanaolalamika sasa wasingetoa malalamiko yao.

Tufuatilie mambo yanayotuhusu kwa karibu, tusipuuze na kusubiri maji yamwagike, maana kwa kufanya hivi kunasababisha kutengenezeana chuki zisizo na sababu za msingi.