Prime
Simba inavyopunguza utamu wa Dabi

Muktasari:
- Katika mchezo huo namba 184 ulioahirishwa mara mbili Machi 8 na Juni 15, ulipigwa juzi jioni na kama kawaida, Yanga iliendeleza ubabe mbele ya watani wao Simba kwa kuifunga kwa mabao 2-0 na kuwa ni mara tano mfululizo, huku pia wakilitawala pambano hilo mwanzo mwisho.
MECHI iliyokuwa ikisubiriwa kuamua bingwa wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024-2025, hatimaye imepigwa juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Katika mchezo huo namba 184 ulioahirishwa mara mbili Machi 8 na Juni 15, ulipigwa juzi jioni na kama kawaida, Yanga iliendeleza ubabe mbele ya watani wao Simba kwa kuifunga kwa mabao 2-0 na kuwa ni mara tano mfululizo, huku pia wakilitawala pambano hilo mwanzo mwisho.
Hicho kilikuwa ni kipigo cha pili kwa Simba katika Ligi Kuu msimu huu kwani cha kwanza ilipigiwa pia na Yanga katika Dabi ya Oktoba 19 mwaka jana, miezi michache ilipotoka kufumuliwa 1-o katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii.
Kabla ya hapo ilishapasuka tena 5-1 Novemba 5 mwaka juzi na ziliporudiana Aprili 20 mwaka jana ikalala 2-1.
Mara ya mwisho kwa Simba kushinda mechi ya Dabi ilikuwa Aprili 16, mwaka juzi katika mechi ya kufungia msimu baina ya timu hiyo ilipoishindilia Yanga mabao 2-0 na Henock Inonga na Kibu Denis, baada ya hapo imekuwa ikigaragazwa kila inaposhuka uwanjani na kuwakata stimu Wanamsimbazi.

Matokeo hayo yamewafanya wapenzi wa soka kuanza kutilia mashaka kama Dabi ya Kariakoo itaendelea kuwa na hadhi ileile ikiwa timu moja itakuwa ikishinda tu, huku upande mwingine ukipoteza tofauti na awali ilivyokuwa na kipindi Simba ikitawala ligi kwa kuchukua ubingwa mara nne, Yanga haikuwa ikifungwa mfululizo, licha ya kwamba haikuwa vizuri kiuchumi kulinganisha na sasa.
Nawaelewa walio na wasiwasi wa kuporomoka kwa hadhi ya Dabi ya Kariakoo na kuonekana ni mechi ya kawaida ikiwa upande mmoja utashinda mfululizo kwa muda mrefu hasa kibiashara sababu bado timu itabaki kwenye mioyo ya watu lakini biashara nyingi zitakuwa ngumu kufanywa na watu ambao hawana furaha ikiwemo mahudhurio kwenye mechi husika.
Simba na Yanga zina tofauti sana namna zinaichukulia Dabi kulingana na nyakati kutokana na falsafa za timu.
Simba wanaathiriwa sana na falsafa yao ya kucheza mpira na kushinda mechi, hii imewafanya kuwa na taswira ileile ya kiuchezaji bila kujali hali ya timu yao au mtani yukoje tofauti na watani zao ambao wao wanachokijua ni ushindi tu bila kujali timu imechezaje.

Huu utamaduni umewafanya kunyumbulika wanapoiendea Dabi kulingana na wakati huo timu yao ikoje ndiyo maana hata kipindi wanatembeza bakuli bado walikuwa wanaweza kuingia na kuzuia wakapata matokeo ya sare ama ushindi na wanarudi kwa chinja mpaka nyumbani.
Tukitazama ndani ya uwanja kuna faida zaidi kwa Yanga kuliko Simba kutokana na vikosi vilivyopo, kwanza ni faida ya umri wa kikosi kukaa pamoja, pili ni daraja la wachezaji kwa maana mchezaji mmoja mmoja ukilinganisha na umri wa kikosi cha Simba kukaa pamoja na madaraja ya wachezaji.
Inawezekana takwimu za baadhi ya wachezaji wa Simba ukizitazama zinaweza kukufanya uilinganishe na Yanga ila ukiitazama timu kijumla ndio unapogundua kuna tofauti kati yao kwa timu inayojengwa, kwa Simba inatia moyo kuona takwimu za baadhi ya wachezaji kwa msimu wao wa kwanza.

Kwa vigezo vilivyopo, Simba inatoa kipa bora, pia inatoa mfungaji bora, achilia mbali washambuliaji wao wawili wenye mabao 13, unaweza kuona wengi wao wamejiinua.
Kufika hapa wailipo, Yanga iliwachukua miaka minne wakiitazama Simba ikitwaa ubingwa na kung’ara kimataifa, hata Simba nao wako katika mchakato wa kuwa na timu bora, msingi ukiwa ni msimu huu tofauti yao ni Simba haingii kwenye mechi kama timu ya pili dhidi ya mpinzani aliye na timu bora, matokeo yake Dabi inataka kupoteza heshima na kuwa mechi ya kawaida.
Matarajio ya wengi ni kutaka kuona Dabi inarejesha heshima ile ile iliyozoeleka kwa msimu ujao kwa kutupatia mshindi tofauti kama sio sare na hili litatokea ikiwa kila mmoja atabaki kwenye nafasi yake kiuhalisia kuiendea mechi husika.
Kuendelea kuchapika kwa Simba kila inapokutana na watani wao, inaweza kupunguza kabisa mvuto na kuifanya mechi hiyo kuchukuliwa ya kawaida, wakati ukweli dabi ni mechi ya kipekee na yenye daraja la aina yake kuanzia kwa mashabiki hadi wachezaji.
Hivyo, kazi kwa watani hata dabi ni dabi!