Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Waamuzi walichambua bao la Seleman Mwalimu lililokataliwa

VAR Pict


MIONGONI mwa matukio yaliyoendelea kuwa gumzo kwa wadau na mashabiki wa soka hapa nchini baada ya Dabi ya Kariakoo iliyomalizika kwa Yanga na Simba kushindwa kufungana kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, ni uamuzi wa kukataliwa kwa bao la Seleman Mwalimu na kuotea kwa Prince Dube.


Matukio hayo yamechochea mjadala huko mitandaoni na katika vijiwe mbalimbali huku kila upande ukiwasilisha hoja zake na kufikia hadi kuuliza: “Kwani kufunga VAR ni shilingi ngapi?”


Katika dakika ya 70, Mwalimu aliunganisha kwa kichwa krosi iliyopigwa na Anicet Oura, lakini kipa wa Yanga, Djigui Diarra akakaa imara kuokoa shambulizi hilo la kwanza kabla ya Mwalimu kupiga tena kwa mguu akiwa chini na kutikisa nyavu za juu.

Wakati mashabiki wa Simba, benchi la ufundi na wachezaji wa timu hiyo wakianza kushangilia, mwamuzi msaidizi namba moja, Kassim Mpanga aliinua kibendera kuashiria mshambuliaji huyo alikuwa ameotea kabla ya kufunga.

Uamuzi huo uliibua maswali mengi kutoka kwa mashabiki, hasa baada ya kuangalia marudio ya tukio kupitia Azam TV, iliyokuwa ikionyesha mechi hiyo moaj kwa moja.

Shaffih Dauda aiponda Yanga: Wamehagaika sana Okello anahitaji muda, Simba ilistahili kushinda ...!

Ukiachana na matukio hayo, kwa kiwango kikubwa waamuzi waliifanya kazi ipasavyo hasa mwamuzi wa kati, Nassoro Mwinchui ambaye wakati anatangazwa kuchezesha mechi hiyo, mjadala ulikuwa mkubwa kama angeweza kuimudu.


MATUKIO YA KUOTEA

Baadhi ya wachambuzi walisema Mwalimu hakuwa ameotea wakati wa krosi. Wengine walienda hatua tatu au nne nyuma ya tukio hilo, wakieleza kabla ya Oura kupiga krosi, Mwalimu alishika mpira wakati akijaribu kuumiliki, jambo lililosababisha sintofahamu kuhusu chanzo cha uamuzi wa mwamuzi msaidizi.

Hata hivyo, wapo waliouliza kama tatizo lilikuwa hapo awali, kwa nini mwamuzi hakusimamisha mchezo mapema, bali akaacha shambulio liendelee hadi mpira ukamkuta tena Mwalimu akiwa tayari ndani ya eneo la hatari la Yanga?

Mwamuzi wa zamani, Samuel Hudson alisema lilikuwa tukio la haraka.

“Tukitazama kupitia televisheni tunaona marudio ya picha lakini uwanjani maamuzi hufanywa ndani ya sekunde chache. Inawezekana mwamuzi alidhani Mwalimu alikuwa ameotea. Lakini marudio ya picha yanaonyesha kinyume chake. Kama kungekuwa na VAR pengine ingesaidia,” alisema.

Pamoja na mjadala huo, Hudson alimpongeza mwamuzi wa kati, Nassoro Mwinchui kutoka Tanga, kwa kuiongoza vizuri dabi hiyo ya kwanza kwake.

“Tofauti na matarajio ya wengi, ameonyesha uwezo wa kuchezesha mechi kubwa. Makosa madogo yaliyotokea ni sehemu ya mchezo, si rahisi kumlaumu mwamuzi kwa kila kitu,” aliongeza.

Kwa upande wake, Abdallah Kambuzi ambaye aliwahi kuchezesha mechi za Ligi Kuu Bara, alizungumzia tukio lililomhusu Prince Dube, aliyedaiwa kuotea dakika ya 62.

“Kwa mtazamo wangu, Dube hakuwa ameotea. Haya ni makosa ya kibinadamu. Wakati mwingine ni vigumu kuona kila kitu kwa usahihi katika kasi ya mchezo,” alisema Kambuzi.

Mwamuzi mkongwe Soud Abdi, aliongeza mtazamo wake kwa kusema: “Bado tuna safari ndefu kufikia kiwango tunachotaka. Ni mchakato unaohitaji muda na juhudi. Kujenga ni kazi ya muda mrefu, kubomoa ni rahisi. Tumefikia hatua fulani lakini bado tunahitaji kufanya kazi zaidi ili kuboresha kiwango cha waamuzi wetu.”

Ahmed Ally akichafua Zenji: Yanga wamshukuru mno aliyekataa bao letu, ndio manyapara Simba tunayo...

ISHU YA VAR

Juni 13, 2024, aliyekuwa Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema Serikali inakusudia kuwasilisha pendekezo la kuondoa kodi kwenye vifaa vya teknolojia inayomsaidia mwamuzi kufanya marejeo ya picha (Video Assistance Referee-VAR) kuanzia mwaka mpya wa fedha 2024/2025.

Alisema pendekezo hilo litawezesha viwanja vyote hapa nchini vinavyotumika kuchezwa ligi hiyo kufungwa VAR lengo likiwa ni kuhakikisha matokeo yanayopatikana yanakuwa ya haki.

Mwigulu ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu, aliyasema hayo wakati akisoma Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka mpya wa fedha 2024-2025.

“Msimu ujao (2024-2025) wa Ligi Kuu ya Tanzania tutaanza kutumia ‘VAR’ ili kuhakikisha matokeo yanayopatikana uwanjani yanakuwa ya haki maana kuna timu zimezidi, msimu mmoja penalti 10, halafu zikifungwa zenyewe magoli yanakataliwa. Na ili tuwe na ‘VAR’ za kutosha katika viwanja vyote, naleta pendekezo la kutoa msamaha kwenye uingizaji wa mashine za ‘VAR’ na vifaa vyake kwa ufafanuzi utakaotolewa hapo baadae. Inawezekana,” alisema Mwigulu.

Julai 15, 2024, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alizindua Teknolojia ya Usaidizi wa Mwamuzi kupitia Video (VAR) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam,

Vifaa hivyo vilivyotolewa na CAF pamoja na Azam Media Limited na VAR inategemea kutumika kuanzia msimu huu wa ligi kuu Bara.

“VAR itapunguza Manung’uniko na makosa ya kibinadamu, sisi kama TFF tumeandika barua kuomba kibali cha kutumia VAR kwenye ligi yetu,” alisema Rais wa TFF, Wallace Karia kuhusu matumizi ya VAR.

Ikumbukwe, mpango wa matumizi ya VAR ulianza kufanyiwa kazi na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), liliendesha mafunzo ya kufunga vifaa vya VAR yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam yakiongozwa na Meneja wa Teknolojia ya Soka kutoka CAF, Wael Elsebaie.

VAR imekuwa ikitumika kwenye ligi na mashindano mbalimbali duniani, hata hivyo, teknolojia hiyo imekuwa ikipigiwa kelele kwamba wakati mwingine haitendi haki kwa kushindwa kutoa uamuzi sahihi.