Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bao moja mfukoni, Simba walikuwa ni watamu zaidi

HISIA Pict


TUANZIE wapi? Nadhani tuanzie namna Yanga ilivyokamatwa juzi usiku pale Unguja. Ndiyo, Kocha Pedro Concalves amekuwa na milima na mabonde tangu awasili. Mashabiki wa Yanga walikuwa na imani tu timu yao imekuwa bora kwa muda mrefu kuliko Simba lakini hawakujua nini cha kutazamia.


Kabla ya kucheza na JKT Tanzania na kushinda mabao matano walicheza na Namungo katika pambano ambalo walishinda kwa mbinde. Mashabiki wakaanza kuhisi kuna hatari inakuja mbele yao. Walipocheza na JKT wakatakata kiasi cha kumtisha mtani.

HISI 01

Unguja halikuonekana kuwa eneo salama kwa Simba lakini kitu cha kushangaza ni Simba walionekana kuwa salama zaidi uwanjani. Walicheza kwa swaga. Walicheza kwa kujiachia. Muda mwingi wa mechi walionekana kutafuta kitu kuliko Yanga. Hii siyo kawaida kwa timu hizi mbili. Kwa mechi sita zilizopita Yanga ndio wanaonekana kutafuta kitu.

Concalves kwa kucheza na viungo wanne wanaofanana, Duke Abuya, Mudathir Yahaya, Damaro Camara na Maxi Nzingeli aliyekuwa anashinda katikati ilikuwa kama vile anacheza na 'handbrake'. Wazungu huwa wanasema hivyo kwa kocha ambaye anaangalia zaidi namna ya kujihami kuliko kupeleka mashambulizi mbele. Ni tofauti na zamani, Yanga ingewapanga Aziz Ki, Maxi Nzingeli, Pacome Zouzoua na Prince Dube kwa pamoja.

Mbele aliachwa mshambuliaji anayeitwa Depu atumie uwezo wake binafsi mbele ya walinzi wawili wa kati wa Simba, Ismael Toure na Rushine de Reuck. Prince Dube alikuwa anatokea pembeni lakini muda mwingi alijikuta mbali na Depu. Matokeo yake ungeweza kumpelekea gazeti kipa wa Simba, Djibrila Kasali akasome katika kipindi cha kwanza.

HISI 02

Depu alikuwa amefunga katika mechi tano mfululizo kabla ya juzi na katika pambano hili usingeweza kumlaumu. Alikuwa hapati huduma kwa muda mwingi na alikuwa ametengwa mbali na wenzake. Wakati mwingine alipigiwa hata mipira mirefu na Djigui Diarra ili apambane na kina Rushine lakini haikuwezekana.

Simba walionekana kuwa moto hasa katika maeneo ya pembeni. Libasse Gueye alimpa wakati mgumu Mohamed Hussein Tshabalala. Anicet Oura naye akampa wakati mgumu Israel Mwenda. Tatizo lao kubwa na la msingi lilikuwa mipira yao ya mwisho. Baada ya chenga na kila kitu hawakuweza kutengeza nafasi. Hawakuweza pia kufunga mabao. Hawakuweza kumaliza mechi kama ambavyo Yanga wamefanya katika mechi sita zilizopita dhidi yao.

Katikati ya uwanja Inno Loemba alionekana kuwapa Simba uhai huku akicheza sambamba na kaka yake, Clatous Chotta Chama. Hata hivyo ni wazi miguu imeanza kumsaliti Clatous. Alikuwa anapoteza mipira ovyo. Alikuwa anazidiwa kasi na Damaro. Hakuonekana kuwa na nguvu au ubora wa kuamua mechi kama alivyokuwa anafanya miaka michache iliyopita kabla hajaenda Yanga.

HISI 03

Kipindi cha pili kikatuletea gumzo la mechi. Kwanza kabisa ilianzia kwa mpira aliopasiwa Prince Dube na kuvunja mtego wa kuotea wakati akitazamana na Kasali. Filimbi ikapigwa huku sisi ambao tulikuwa tunatazama mpira katika televisheni tukiona wazi Dube alikuwa hajaotea. Kwa fomu ambayo Dube alikuwa nayo asingeweza kumkosa Kasali.

Halafu likaja bao la Suleiman Mwalimu ambalo lilikataliwa. Bakari Nondo Mwamnyeto alijisahau kuondoka na Mwalimu akavunja mtego wa kuotea. Shuti lake la kwanza likamgonga Djigui Diarra. Shuti lake la pili akapeleka mpira katika nyavu. Mwamuzi wa pembeni akadai Mwalimu alikuwa ameotea. Haikuwa kweli. Tuna tatizo la msingi kwa waamuzi wa pembeni.

Mara zote hawasimami katika mstari mmoja na mchezaji wa mwisho. Hawana kasi ya mwili wala akili. Wanachofanya ni hiki ambacho kinatokea sasa hivi. Huwa 'wanabeti'. Wanaweka tu 'offside' kama mchezaji mmoja amebakia na golikipa. Wanajaribu kujiweka katika mstari salama ni bora walaumiwe kwa kukataa bao la halali kuliko kukubali bao ambalo baadae itaonekana mfungaji alikuwa ameotea.

HISI 04

Kwa sasa waamuzi wa pembeni hawajishughulishi kuwa makini. Wanahofia lawama huku wakibeba lawama. Ndicho ambacho kimetokea juzi. Tulihitaji bao la halali ambalo lisingekuwa na makandokando ya 'offside' ili waamuzi wetu wapeleke mpira katikati. Mwalimu alidhulumiwa bao lake kama ambavyo Dube naye angeweza kufunga lakini akadhulumiwa nafasi yake.

Kitu gani cha kuondoka nacho? Kuna mambo mawili hapa. Bila ya kujijua sana lakini Yanga wanaendelea kupoteza ubora wao waliokuwa nao wakati ule wa kina Khalid Aucho, Aziz Ki, Fiston Mayele, Pacome Zouzoua na Clement Mzize. Wengine bado wapo lakini siamini kama wameletewa wabadala wa kuendelea kuitawala Simba.

Kama tatizo sio wageni waliokuja basi huenda tatizo likawa kwa makocha waliokuja baadae. Kuanzia kwa Roman Folz hadi kwa huyu Pedro. 'Flow' ya Yanga imepotea. Ule utawala wa lazima umepotea. Mwendelezo wa ubora pia umepotea. Ni kama ambavyo mechi za Namungo, JKT Tanzania na Simba zilivyochezwa na tofauti huku wachezaji wakiwa wale wale na kocha akiwa yule yule.

HISI 05

Kwamba Pacome hakuwepo sidhani kama ni tatizo. Pacome na Aucho walikosekana katika pambano gumu dhidi ya Mamelodi Sundowns, lakini bado Yanga nusura watinge nusu fainali kama sio mwamuzi kumdhulumu bao Aziz Ki. Kuna wakati Yanga walikuwa na utajiri huo wa wachezaji. Kukosekana kwa mchezaji mmoja au wawili mahiri hakukuwa tatizo lao. Bado wangekufunga na bado wangecheza kwa swaga.

Kwa Simba? Ukweli ni kwamba dirisha la Januari limewanufaisha. Wameleta wachezaji ambao wana ubora kuliko kina Joshua Mutale. Kitu cha msingi ni kwa wachezaji wenyewe kutengeneza maelewano ya kucheza mpira rahisi pale mbele. Wengi nahisi wanataka kujitengenezea ufalme wao wenyewe kuliko kuitengenezea timu ufalme. Yanga wakiwa katika ufalme wao walikuwa wanacheza mpira rahisi.

Nini kinafuata?  Tukutane katika raundi ya pili. Hapa katikati kuna mitego kadhaa lakini wakubwa wetu hawa watavuka. Nadra sana kwa Simba na Yanga kukwama kwa watoto kama ambavyo Yanga alikwama kwa Mbeya City au Simba alikwama kwa Dodoma. Sehemu pekee wanayoweza kujikwaa mazima ni kwa Azam tu. Vinginevyo wakubwa wanaweza kujikuta wakiamua ligi wenyewe kwa wenyewe katika raundi ya pili.