Vinara wa kutupia nyavu za ugenini VPL

Thursday January 14 2021
simba bocco pic
By Oliver Albert

STRAIKA John Bocco wa Simba na Adam Adam wa JKT Tanzania ndio vinara wa kutupia mabao nyavuni katika viwanja vya ugenini huku Prince Dube wa Azam, Meddie Kagere na Clatous Chama wa Simba wakitisha zaidi nyumbani.

Bocco ndiye kinara wa mabao kwenye Ligi Kuu Bara hadi sasa akiwa amefunga manane akifuatiwa kwa karibu na Adam na Kagere wenye mabao saba kila mmoja wakati Dube, Meshack Abraham (Gwambina) na Chama wamefunga mabao sita kila mmoja huku Fully Maganga (Ruvu Shooting ) na Rashid Seif Karihe wa Dodoma Jiji wakiwa wamefunga matano kila mmoja.

Kati ya mabao manane aliyofunga Bocco, matano amefunga ugenini huku matatu pekee akifunga kwenye uwanja wa nyumbani wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

VINARA ADAM

Bocco alifunga bao moja dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya Septemba 6, mwaka jana, Simba iliposhinda mabao 2-1 huku lingine likifungwa na Mzamiru Yassin.

Pia alifunga hat trick alipoiongoza timu yake kuichapa Coastal Union mabao 7-0 katika mchezo uliofanyika Novemba 11,2020 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, huku pia akifunga bao moja na kuipa pointi tatu muhimu timu yake iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Mbeya City Desemba 13, mwaka jana kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.

Advertisement

Bocco ametupia mabao matatu tu kwenye uwanja wa nyumbani dhidi ya Mwadui alipofunga mabao mawili na kuiongoza timu yake kushinda mabao 5-0 katika mchezo uliofanyika Oktoba 31, 2020. Pia alifunga bao moja kwa mkwaju wa penalti pale Simba ilipoifunga Kagera Sugar mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Novemba 11 kwenye Uwanja wa Uhuru.

Kwa upande wa Adam, kati ya mabao saba aliyofunga hadi sasa, sita amefunga ugenini huku moja pekee akifunga kwenye uwanja wa nyumbani wa Jamhuri, Dodoma.

Mabao ya ugenini aliyofunga ni dhidi ya Kagera Sugar, Septemba 7, mwaka jana, alipoingoza timu yake kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, dhidi ya Mwadui alipofunga hat trick, JKT ilipoifunga Mwadui mabao 6-1 Oktoba 25, 2020 Kwenya Uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga na dhidi ya Namungo alipofunga mabao mawili na kuikoa timu yake kulala ugenini kwenye Uwanja wa Majaliwa uliopo Ruangwa mkoani Lindi Novemba 11.

Alifunga bao moja tu nyumbani JKT Tanzania ilipocheza na Biashara United Desemba 12 na kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Hawa wametisha nyumbani

Wachezaji hao ndio waliotisha zaidi kwa kuzifumania nyavu nyumbani huku Dube akitia fora kwa kufunga mabao matano nyumbani na moja tu ugenini kabla ya kuumia mkono na kupelekwa Afrika Kusini kutibiwa, ingawa kwa sasa ameshaanza mazoezi mepesi na timu yake.

Dube, raia wa Zimbabwe alifunga mabao mawili katika mechi dhidi ya Coastal Union iliyofanyika Septemba 11, mwaka jana kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi na Azam kushinda mabao 2-0, pia alifunga mabao mawili alipoiongoza timu yake kuichapa mabao 4-0 Kagera Sugar Oktoba 4, 2020 na alifunga bao moja Oktoba 15, mwaka jana walipoifunga Mwadui mabao 3-0. Mshambuliaji huyo amefunga bao moja tu ugenini mpaka sasa katika mchezo dhidi ya Prisons uliofanyika Septemba 26, mwaka na kuibuka shujaa baada ya kufunga dakika za mwisho.

Kwa upande wa Kagere amefunga mabao matano nyumbani na mawili ugenini huku mabao ya nyumbani akifunga katika mchezo dhidi ya Biashara United, Septemba 20, mwaka jana, Simba iliposhinda 4-0 huku akifunga moja. Pia alifunga bao moja katika mechi dhidi ya Gwambina iliyofanyika Septemba 26 na akafunga tena moja kwa penalti iliyozua utata katika mchezo dhidi ya KMC uliofanyika Desemba 16, mwaka jana, kwenye Uwanja wa Mkapa huku pia akifunga mabao mawili Simba ilipoichakaza Ihefu mabao 4-0 katika mchezo uliofanyika Desemba 30.

Mnyarwanda huyo amefunga mabao mawili tu ugenini katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji uliofanyika Oktoba 4 kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambao Simba ilishinda 4-0 huku akitupia nyavuni mabao mawili.

Upande wa Chama amefunga mabao manne nyumbani katika mechi dhidi ya Biashara United iliyofanyika Septemba 20, mwaka jana, ambayo Simba ilishinda mabao 4-0. Pia alifunga mawili dhidi ya Polisi Tanzania na kuisaidia timu yake kushinda mabao 2-0 katika mchezo uliofanyika Desemba 9 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mzambia huyo amefunga mabao mawili tu ugenini katika mchezo ambao Simba ilishinda 7-0 dhidi ya Coastal United uliofanyika Oktoba 21 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kwa uponde wa Meshack Abraham wa Gwambina ameonekana kokote anatupia zaidi kwani amefunga mabao matatu nyumbani na matatu ugenini.

Ligi Kuu Bara kwa sasa imesimama huku Yanga ikiwa kileleni na pointi 44 ikifuatiwa na Simba yenye pointi 35 ilhali Azam FC ni ya tatu na pointi 32.

Advertisement