Vigogo watoboa, Simba, Yanga zinakwama hapa tu

NI zaidi ya miaka 80 klabu za Simba na Yanga zinasherehekea kuzaliwa, umri ambao hauendani na maisha halisi ambayo klabu hizo zinaishi kwa sasa. Timu hizo zinajiita vigogo katika soka, lakini hazina miundombinu ya kueleweka inayoendana na umri Yanga ikiwa imeanzishwa 1935 na Simba 1936.
Simba ina maskani yake Mtaa wa Msimbazi, huku Yanga ikiwa ile mitaa ya Twiga na Jangwani  na zote ni Kariakoo, isipokuwa ukizitazama timu hizo zinatia huruma na mashaka japokuwa zinaongoza kwa kuwa na mashabiki wengi nchini.
Mwanaspoti linakuletea ripoti maalumu ya vigogo hao na ukongwe walionao, lakini hata viwanja tu vimewashinda na kujikuta wakiona kwa jirani yao Azam FC wenye muda mfupi katika soka.
Angalau Simba imepunguza matumizi makubwa ya pesa baada ya kukamilisha uwanja wa mazoezi na kujikuta ikiepuka kutoa kati ya Sh500,000 hadi 700,000 kwa siku kwa ajili ya mazoezi. Lakini, Yanga bado wanajikongoja licha ya kujaza kifusi Jangwani, lakini haiwezi kupatumia kutokana na kutokamilika mpaka sasa huku timu ikitumia Uwanja wa Avic - Kigamboni ambao sio mali yake.


ISMAIL ADEN RAGE
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage anasema Simba na Yanga tatizo kubwa wanawaza uwanjani tu kushinda, lakini mambo ya viwanja hawana habari nayo.
“Hizi timu na mashabiki wengi waliokuwa nao ni shida sana, maana wao wanahitaji zaidi matokeo ya uwanjani. Mbali na hilo jambo lingine hawawezi kukuelewa, kiongozi ili ufanikiwe unatakiwa kutumia nguvu za ziada sana," anasema Rage.
Rage anasema viongozi waliotangulia walijitahidi kuhakikisha timu zinakuwa na mashabiki ambao ndio mtaji mkubwa kwa sasa hadi kampuni na watu wenye pesa wanaamua kuwekeza, hivyo ni jukumu lao sasa kuwavusha licha ya kuchelewa.
“Mpira sasa hivi umebadilika, umekuwa biashara maana hata mashabiki wao wameanza kujielewa. Mbali na matokeo ya uwanjani wanahitaji pia maendeleo ya nje, viongozi wa sasa wana changamoto kubwa ambayo wanatakiwa kukabiliana nayo baada ya mashabiki kuanza kuwa na uelewa tofauti,” anasema.
“Naamini Simba na Yanga kwa namna ambavyo wamebadilika kwa sasa muda si mrefu wataweza kumiliki viwanja maana utandawazi umesaidia sana. Lakini wakati wa nyuma unaanza kumwambia mtu habari za uwanja halafu timu haishindi, kukuelewa ngumu ila sasa hivi wako tofauti."


HASSAN DALALI
Mwasisi wa tamasha la Simba Day ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti Dalali anasema kilichozikwamisha timu hizo kuwa na viwanja ni kukosekana kwa uchumi thabiti muda mrefu.
Anasema klabu asilimia kubwa zilikuwa zinaendeshwa na mapato ya milangoni sambamba na ada za wanachama.
“Mimi wakati naingia (madarakani) nilikuta ada ya uanachama ilikuwa Sh50 nilikomaa kuwashawishi wanachama ikawa hadi 1,000 ambayo ipo hadi sasa. Halikuwa jambo dogo hiyo pesa kuendesha klabu ni ngumu,” anasema Dalali.
“Nikapambana na kadi za uanachama kutoka Sh500 hadi Sh10,000. Kwa staili hiyo ni ngumu kujenga uwanja, mnabakia hivyo hivyo. Hata suala la uwanja wa Bunju nilikuwa nawaambia viongozi wakati huo mimi ni mwenyekiti wa matawi. Nikaona isiwe tabu acha nigombee uenyekiti nikalisimamie mwenyewe.”
Anasema alipopata nafasi hiyo alianza kwenda uwanja wa Machava uliopo Kigamboni na alipokwenda Wizara ya Ardhi  wakamwambia ana watu na ndipo alipoelekezwa kwenda Bunju, haikuwa kazi ndogo lakini aliamua kukomaa.
"Maendeleo ya Simba kwa sasa mpaka inatumia uwanja wa mazoezi mimi ndiye niliutafuta. Nashukuru sana hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alivyokwenda juzi alinitaja, nilifurahi. Mimi naijua mipaka yote lakini sikushirikishwa. Nawapongeza wanachama kwa kuchangia hata mimi mbali na kuutafuta nimechangia pia harakati za ujenzi," anasema Dalali.


LLOYD NCHUNGA
Aliyekuwa mwenyekiti wa zamani wa Yanga, Lloyd Nchunga anasema kikubwa kinachokwamisha timu hizo ni utashi kutoka kwa wanachama ambao ndio wenye klabu hizo.
"Hizi klabu mbili zina mambo ya mazoea tu kuwa sisi tuko hivi. Ukileta jambo jipya wanakushangaa hasa wanachama. Mara nyingi viongozi wanakuja na mawazo chanya sema historia iliyopo inafanya mambo yakwame," anasema Nchunga.
Anasema hata katika ilani ya uchaguzi wakati anaingia madarakani suala la mfumo wa mabadiliko lilikuwepo, lakini hakuna aliyekuwa akitaka mabadiliko hayo.
"Ukisema mabadiliko mwingine anaona unaelekea kumpotezea ugali au umaarufu. Ni kazi kubwa, lakini mambo yanayofanyika sasa hivi ndio yaleyale katika ilani yangu, sema muda huu tunaweza kwenda kwa kuwa wanachama wamekuwa na utashi, hivyo kufanikisha jambo inakuwa vyepesi," anasema.


TITO OSORO
Mjumbe wa kamati ya utendaji ya Yanga miaka iliyopita, Tito Osoro anasema: “Shida ya kwanza wakati hizi timu zimeanzishwa zimekamatwa na Serikali na tayari ina viwanja na wao wakajisahau kuwa viwanja sio vyao ni vya Serikali na ndio maana wenzetu Ulaya kabla hujaanzisha timu unatakiwa kuwa na uwanja wa mazoezi.
“Lakini kwetu timu inaanzishwa, uwanja inafanya mazoezi shule za msingi. Sasa hawa Simba na Yanga walipokuwa wakitumia Uwanja wa Uhuru waliona ni kama wao ulipojengwa Taifa ndio basi kabisa.”
Osoro anasema, England uwanja wa timu ya Taifa hakuna klabu ambayo inautumia kwani kila timu ina uwanja wake.
“Wakati timu hizi zinaanza maeneo yalikuwepo mengi sana, sema maono hayakuwepo, mfano Yanga kweli klabu inaenda kuwekwa pale kwenye mto sehemu hatarishi halafu wanakomaa kujenga hapohapo wakati watu wanaondolewa haiwezekani,” anasema.
“Walikuwa sio wa kukosa sehemu nzuri tambalale. Kwa umri walionao walitakiwa kuwa na viwanja katikati ya mji kabisa, Simba angeweza kuwa Posta, Yanga akawa Kariakoo hata Magomeni, lakini kujisahau kumewafanya sasa hivi wanaenda Kigamboni na Bunju,” anasema Osoro.
Anasema kwa namna ambavyo timu hizo zinajipapatua kwa sasa na umbali wa viwanja husika ni ngumu kuwapata baadhi ya mashabiki wao mfano wanaotoka Mbagala kwenda Bunju au wanaotoka Mbezi kwenda Kigamboni wataamua kuangalia kwenye runinga.
“Ukijenga uwanja inatakiwa watu wanaoingia gharama zile zirudi maana walikuwepo muda mrefu, ila siasa ndizo zimetufanya Simba na Yanga kufikia hali hii tuliyo nayo licha ya miaka zaidi ya 80,” anasema.


HAMIS KILOMONI
Hamis Kilomoni aliyekuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Klabu ya Simba, anasema tatizo kubwa viongozi wanaoziongoza timu hizo wanakosa mawazo ya mafanikio ili kuzifanya zipige hatua kubwa ya maendeleo kulingana na umri wao.
"Wakati wetu tulikimbilia kuwa na makazi sehemu ya kuishi na tulifanikisha, ila kiongozi akiamua hiki kifanyike kinafanyika tu wale wafuasi wanasikiliza kauli za viongozi wao," anasema Kilomoni.
Anasema viongozi wa sasa wana maono tofauti na ndio maana wameweza kuwashawishi mashabiki kwa ajili ya ujenzi wa viwanja vya timu zao.
"Hata uwanja wa Bunju katika uongozi wetu ndio tuliuomba, sasa waliokuja baadaye walitakiwa kuendeleza tulichokianza, lakini mambo ya kutazama matumbo yao ni shida sana," anasema.
"Mashabiki wa Simba na Yanga wanawasikiliza sana viongozi. Wale wafuasi wao wanafuata kama kiongozi hasemi wala kufikiria hilo. Ni ngumu mfuasi kuanzisha hoja, ila viongozi wa sasa nawapongeza jitihada zao zinaonekana."
Kilomoni anasema waliacha alama kubwa kuanzia nyumba hadi uwanja na baada ya kuondoka madarakani ni ngumu kuchukua pesa za nyumbani kwenda kujenga klabu licha ya michango midogo midogo kuchangia.


HERSI SAID
Mwenyekiti wa sasa wa klabu ya Yanga, Hersi Said wakati anaingia madarakani kipaumbele chake kikubwa katika mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji suala la uwanja alilipa nafasi kubwa.
Hersi anasema ataanza kutengeneza sehemu ya kuchezea katika eneo la Jangwani ambapo kifusi kilijazwa ili kupunguza  gharama kwa timu ya wanawake ya Yanga Princess. Wakati Jangwani pakiwekwa sawa pia Kigamboni ramani na michoro kwa ajili ya uwanja mkubwa imeshaanza kuandaliwa.


SALIM ABDALLAH ‘TRY AGAIN’
Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Simba, Sali Abdallah 'Try Again' anasema uwanja ni mojawapo wa kipaumbele chao kikubwa na ndio maana waliamua kuanza na sehemu ya mazoezi wakiwa wanakusanya nguvu.
“Mohamed Dewji Mo tayari alionyesha mwanga kwa kuanza kuchangia juu ya ujenzi na hata mashabiki pia wameichangia klabu yao na tayari mambo yanaendelea huko Bunju japo tulichelewa," anasema Try Again.


MDAU
Akizungumzia suala la maendeleo ya klabu hizo, mmoja wa wadau ambaye jina lake hakutaka litajwe anasema: “Timu zimekaa kisiasa sana, dunia ya sasa inahitaji watu wenye weledi kufanya kazi na ndio maana watu kama kina Senzo (Mazingis) wameshindwa na kuamua kuondoka."
Mdau huyo aliyewahi kuwa kiongozi wa Yanga anasema kabla ya kuleta wataalamu wakubwa viongozi wanapaswa kuondokana na  mazingira ya kisiasa na kujikita katika mpira.
“Hata upelekwe na taaluma fulani ukifika pale (kwa viongozi na ukiwa na wazo zuri) kutokana na mambo yaliyomo ndani linakufa. Hata sehemu za kitaaluma wanaweka watu wao ambao wanafanya kwa maelekezo. Ndani ya hizo timu kuna mambo mengi sana kufanya kazi kwa mazoea anapokuja kiongozi, anakuja na plan yake na watu wake," anasema.
“Mshindo Msola alivyokuja walianzisha 'application' ikawa inaingiza pesa, ila wakaja watu wakaiua ili isiingizie pesa klabu na wao wapate nafasi, lakini ikafa na juzi wameanzisha nyingine sasa unajiuliza mambo mengi majibu haupati ndio maana timu hizi haziendelei.


MATHEW AKRAMA
Mwamuzi mstaafu wa soka, Mathew Akrama anasema siasa na watu kujali matumbo ndivyo vimezifikisha zilipo timu hizo na kwa miaka 80 aibu ni kubwa kutokuwa na viwanja kiasi cha kuzidiwa na Azam FC ambayo wenye timu wana maono mazuri.
"Naona kuchelewa kuingia katika mfumo mpya wa kiuendeshaji ndio kumechangia yote hayo, lakini sasa hivi watafanikisha hilo. Huko nyuma haya mambo ya makomandoo milangoni yametuchelewesha sana," anasema.
"Halafu walaji na wapiga dili walikuwa wengi, lakini sasa hivi maono ni makubwa. (Timu) zinazinduka yaani hizo timu hazina tofauti na vitimu vidogo ila ubabaishaji mwingi. Unakuta timu watu wengi na wote wanatazama mapato ya milangoni hakuwezi kuwepo maendeleo.”