Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man United inavyopenda kusajili mastraika ‘age go’

Muktasari:

  • Inavyofahamika, kwenye soka la kisasa mchezaji akishafikisha umri wa miaka 30 tu anahesabika kama veterani, lakini Man United imekuwa na zali la kupata huduma bora kutoka kwa washambuliaji iliyowasajili wakiwa na umri mkubwa, kwamba wamekuwa moto walipotua Old Trafford wakifunga mabao ya kutosha na kuisaidia timu hiyo kubeba mataji.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER United inahusishwa na mpango wa kumsajili straika wa Aston Villa, Ollie Watkins, ikidaiwa kutaka kuendelea rekodi yake ya kusajili washambuliaji ‘age go’.

Inavyofahamika, kwenye soka la kisasa mchezaji akishafikisha umri wa miaka 30 tu anahesabika kama veterani, lakini Man United imekuwa na zali la kupata huduma bora kutoka kwa washambuliaji iliyowasajili wakiwa na umri mkubwa, kwamba wamekuwa moto walipotua Old Trafford wakifunga mabao ya kutosha na kuisaidia timu hiyo kubeba mataji.

Watkins umri wake wa sasa ni miaka 29 na anaweza kwenda kuwa suluhisho kwenye tatizo la safu ya ushambuliaji ya Man United ambayo iliwakumba msimu uliopita. Licha ya kwamba anakaribia umri wa miaka 30, ambapo atatimiza Desemba 30, hilo haliizuii Man United kupambania kunasa saini ya jumla ya mshambuliaji huyo ikiamini atakwenda kuongeza kitu Old Trafford…


Edinson Cavani, miaka 33

Mashabiki wachache sana wa Man United walionyesha kujali umri wa straika Edinson Cavani wakati anasajiliwa na timu hiyo. Kipindi hicho, Cavani alikuwa na umri wa miaka 33 wakati anatua Old Trafford kwa uhamisho wa bure akitokea PSG, ambako alifunga mabao 200 katika mechi 301. Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man United ilihitaji saini ya Cavani baada ya kutokea kuchapwa 6-1 na Tottenham uwanjani Old Trafford. Cavani alikabidhiwa jezi Namba 7, aliisaidia Man United kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu England, akifunga mabao 10 kwenye ligi na 17 katika michuano yote licha ya kwamba alikuwa akitokea benchini mara nyingi.

Cavani alianza kwa kusaini mwaka mmoja, lakini baada ya kiwango kizuri aliongezwa mwingine kabla ya vitu kutibuka baada ya ujio wa kocha Ralf Rangnick.


Cristiano Ronaldo, miaka 36

Wakati supastaa Cristiano Ronaldo alipoamua kuachana na Juventus, wala haikuonekana shida alipotangaza kurudi Man United katika msimu wa 2021/22, hakuna aliyejadili umri wake kuwa umekwenda. Katika msimu huo, Ronaldo aliishia kuwa kinara wa mabao wa Man United, akifunga mara 24 katika mechi 38. Katika msimu wake wa kwanza baada ya kurudi Old Trafford, Ronaldo alipoibuka kinara wa mabao, alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Msimu wa klabu hiyo. Ujio wa kocha Erik ten Hag ulibadili maisha ya staa huyo na kufikia hatua ya kutibuana kabla ya kwenda zake kufanya mahojiano na Piers Morgan, ambayo yalikuwa chanzo cha kumsukuma staa huyo nje ya Old Trafford na kutimkia Saudi Arabia.


Zlatan Ibrahimovic, miaka 34

Straika Zlatan Ibrahimovic alikuwa na umri wa miaka 34 wakati anatua zake Old Trafford kuungana na kocha wake wa zamani, Jose Mourinho, lakini fowadi huyo veterani alikuwa moto kwelikweli ndani ya uwanja. Alijiunga na Man United akitokea kwenye msimu ambao alikuwa hatari huko PSG, alipofunga mabao 50 katika mechi 51. Majeraha yalitibua kuongeza mkataba wa mwaka mwingine na hadi kufikia kipindi Ibrahimovic yupo fiti, tayari Man United ilikuwa imemsajili Romelu Lukaku, ambaye alikuwa anaanza kwenye kikosi na kukabidhiwa jezi Namba 9. Kutokana na hilo, Zlatan aliruhusiwa kuondoka Old Trafford, Machi akatimkia zake LA Galaxy ya Marekani. Lakini, msimu wake wa kwanza uliacha kumbukumbu nyingi tamu kwa mashabiki wa Old Trafford.


Robin van Persie, miaka 29

Kwa Man United imekuwa desturi kwa mastraika inaowanasa kwenye umri mkubwa, wanakuwa tishio sana kwenye msimu wao wa kwanza. Mdachi, Van Persie alitua Old Trafford kwenye msimu wa 2012-2013 na kuwasha moto, akiisaidia timu hiyo kunyakua taji la Ligi Kuu England ikiwa chini ya kocha Sir Alex Ferguson. Kilichowavutia mashabiki wa Man United ni kumshuhudia straika huyo akitokea Arsenal, ambako alicheza kwa misimu kibao bila ya kubeba taji, lakini alipotua tu Old Trafford, akabeba taji hilo huku akifunika pia kwenye kufunga mabao. Van Persie alifunga mabao 26 kwenye ligi na kunyakua Kiatu cha Dhahabu kwenye msimu wake huo.


Mambo yalitibuka Ferguson alipoondoka na kuja David Moyes na baadaye Louis van Gaal, ambao hawakuwa na ujuzi mzuri wa kumtumia straika huyo kutokana na rekodi zake za kuwa na majeraha ya mara kwa mara.


Teddy Sheringham, miaka 31

Straika, Teddy Sheringham hakuwa na msimu mzuri wakati anaingia Old Trafford, lakini baadaye alikuja kuwa moto kwelikweli kwenye kikosi hicho na kuwa msaada mkubwa. Sheringham alisajiliwa kuja kuziba pengo gumu sana, kumbadili Eric Cantona. Akiwa na umri wa miaka 31, straika huyo wa England alikuwa mkubwa kwa mwaka mmoja dhidi ya Cantona, ambaye alikuwa anaondoka Man United akitangaza kustafu. Alishindwa kufikisha namba ya tarakimu mbili ya mabao katika msimu wake wa kwanza na hivyo akasubiri hadi msimu uliofuatia. Baada ya hapo, Sheringham alikuwa balaa zito uwanjani, akifunga mabao muhimu kwenye timu ya Man United.