Prime
VIDEO: Mnguto afichua ishu ya Yanga ilivyokuwa pasua kichwa

Muktasari:
- Ndani ya Bodi hiyo, yupo Steven Mnguto ambaye ni mwenyekiti aliyedumu kipindi kirefu zaidi kwenye zama hizi ambazo Tanzania imepaa zaidi kimafanikio ndani na nje ya nchi akihudumu kwa takribani miaka 10.
HUWEZI kutaka kuyazungumzia maendeleo ya Soka la Tanzania kama hutagusia mamlaka ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) ambayo kimsingi ndio husimamia ustawi wa karibu ligi zote Tanzania.
Ndani ya Bodi hiyo, yupo Steven Mnguto ambaye ni mwenyekiti aliyedumu kipindi kirefu zaidi kwenye zama hizi ambazo Tanzania imepaa zaidi kimafanikio ndani na nje ya nchi akihudumu kwa takribani miaka 10.
Mnguto anakaribia kuondoka ndani ya TPLB baada ya kumaliza muda wake wa kuwa mwenyekiti wa Coastal Union, nafasi iliyompa nguvu kikanuni kugombea nafasi ya kuiongoza bodi hiyo.
Wakati akielekea kumaliza muda wake, Mwanaspoti limefanya naye mahojiano maalum akizungumzia mambo mbalimbali kuhusu TPLB na hata maisha yake ya uongozi ndani ya Coastal Union yenye maskani yake mkoani Tanga.
Katika mahojiano hayo na Mwanaspoti, Mnguto alilitaja sakata la kuahirishwa kwa Kariakoo Dabi mwaka 2021 baada ya Yanga kugomea mabadiliko ya muda huku akifichua namna ilivyowasumbua kutoa uamuzi kwani kulikuwa na uwezekano wa timu moja kupewa pointi tatu.
Mnguto amekumbushia hilo ikiwa ni kati ya kesi ngumu ambazo TPLB imekutana nazo ikihusishwa na hii ya sasa ambayo Dabi ya Simba na Yanga iliyopangwa kuchezwa Machi 8 mwaka huu kuahirishwa huku Yanga wakienda Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kudai wapewe pointi tatu kufuatia kutokubaliana na kuahirishwa kwa mechi hiyo siku ya mchezo.
MWENENDO WA SOKA
Mnguto anaanza kueleza namna mwenendo wa soka la Tanzania jinsi mambo yanavyokwenda akionyesha kuridhishwa na hatua zinazopigwa akisema: “Mimi nadhani tunaenda vizuri kwa sababu ya uongozi bora, nikimaanisha rais wetu wa TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), Wallace Karia na wengine wote pamoja na mimi, kwa hiyo naamini kabisa kwa umoja huo ndio uliosaidia ligi yetu kuwa bora,” anasema Mnguto huku akiendelea kufafanua mambo mbalimbali.
“Lakini pia ni kwa sababu ya klabu ambazo tunaziongoza kwa jinsi zilivyoleta ushindani wa hali ya juu zaidi unaofanya soka likue zaidi.”
MIAKA 10 YA UONGOZI
“Tumepiga hatua kwa kweli, mpaka watu wengine wanaliona hilo kwa sababu unapoambiwa ligi yako ni bora kwa kuwa ya tano au ya nne, ina maana kuna watu wanaona kile ambacho unakifanya.

“Kwa maana hiyo na sisi lazima tukubali, kwa sababu hatujajisemea wenyewe ila ni ile kazi tuliyoifanya ambayo watu wengine wakaiona ndio wakasema ligi yetu ni bora, hivyo nikisema kwa uwazi ni kwamba tunapiga hatua.”
NAFASI YA WADHAMINI KATIKA LIGI
“Wadhamini kwa kweli wana nafasi kubwa, wamesaidia sana mpira wetu kwa sababu huko nyuma timu nyingine zilikuwa zimeshindwa kabisa kwenda kwenye vituo kwa sababu hawana nauli.
“Lakini wakaja Vodacom wakaleta ukombozi, wakaanza kutoa nauli mpaka ikaja na posho nayo ikaongezeka, wao ndio walifungua njia kwa wengine.
“Akaja Azam Media, NBC na wengine ambao wanafanya kazi nzuri sana, kwa hiyo ujio wa wadhamini umezipa uhai klabu hizi pale ambapo walikuwa wanashindwa kutimiza matakwa ya uendeshaji, sasa wameweza.”
MAENDELEO YA KLABU
“Kweli kuna madaraja tofauti ya timu na yanatokana na uwezo wa wadhamini na fedha za klabu, hizi za chini ni zile zinazotegemea pesa za TV (Azam) na NBC.
“Jitihada za kuwasukuma wapate wadhamini nje na hao, kusema kweli sio rahisi sana, kuna mambo mengi, kwanza ni lazima timu yako iwe inafanya vizuri ndipo utakapokimbiliwa, pia kujuana ni muhimu.

“Kwa hiyo timu nyingine zinahangaika, zipo za Jeshi na Halmashauri, zinapata nguvu kupitia maeneo hayo, hizo zimebaki kidogo sana, nikisema za watu binafsi ni za wanachama.
“Hapo tunazungumzia Coastal Union, Simba, Yanga, Tabora United na KenGold, zinazobakia ni za mashirika na watu wanaojiweza kama Azam FC, taratibu nadhani tutasogea kwa sababu nikiitolea mfano timu yangu Wagosi wa Kaya, haivutii sana wawekezaji, tumefanya juhudi pia na wengine wakijipambanua watafanikisha tu.”
MSAADA WA BODI KWA TIMU CHIPUKIZI
“Ukisema utegemee Bodi ndio iweze kusaidia kutoka pointi A kwenda B, si sawa, nasema kwamba klabu pia itakuwa haijui wajibu wake, kwanza hatuna pesa hiyo.
“Lakini Bodi tunachoweza kusaidia ni kujaribu kuwavutia wafanyabiashara waone umuhimu wa kuzidhamini hizi timu, lakini juhudi zinatakiwa kutoka kwenye klabu zenyewe.
“Ndio maana tunawaambia wawe na vitengo vya masoko ili waweze kuzitangaza timu zao, ndipo unapovuta wadhamini kwa sababu atataka kujua unampa nini cha ziada, lazima ajue atakuwa anatangazwa kwa jinsi gani ili atoe pesa.”
KUHUSU BODI YA LIGI KUJITEGEMEA
Wadau wengi wana kiu ya kuona TPLB ijitegemee wakiona kama inavyoendeshwa sasa ipo chini ya uamuzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ambapo Mnguto amekubaliana nao huku akitofautiana nao kwa maeneo kadhaa akisema: “Wako sahihi wanaodhani kuwa Bodi ya Ligi inatakiwa ijitegemee, hii bado iko kwenye mwamvuli wa TFF kwani hatuwezi kusaini hata mkataba wenyewe.
“Lakini rais wangu anaiona hiyo hali ya hii Bodi kujitegemea, ndio maana mara nyingi ananiagiza kuangalia uwezekano wa kulifanya hili litimie.
“Tunalichukua hilo kwa uangalifu mkubwa, kwa sababu tukiangalia uzoefu wa nchi nyingine kama Kenya, walijaribu kuwa hivyo matokeo yake kukawa na bodi mbili zinazoendesha ligi, hicho ndio tunachokiogopa, kwa sababu tumechelewa kidogo lakini kunalipa sasa, tunaendesha vizuri.
“Ingawaje nakubaliana na rais wangu kuwa, kweli hii Bodi inatakiwa iwe inajitegemea lakini lazima tuwe na utulivu na uvumilivu mkubwa katika kufanya uamuzi huo.”
USIMAMIZI WA VIWANJA
“Hili ni takwa linakuja kwenye leseni za klabu, mojawapo ni hili la viwanja, mpira ili uchezwe ni lazima kuwe na viwanja vizuri, sio mchezaji timu yake ina kiwanja kizuri halafu unampaleka sehemu mbovu.
“Kwanza unamuharibia, pia kiwanja ambacho sio kizuri kinaweza kuleta hatari ya majeraha, hili tumelisisitiza kutokana na matakwa ya leseni za klabu ambayo hayo yanatoka huko juu FIFA na CAF, kazi yetu ni kusimamia na kuhakikisha inatekelezwa.

“Kuna watu mwanzoni walikuwa hawaelewi umuhimu wa kuwa na viwanja vizuri, lakini tuliposimamia jambo hili vizuri na tukahakikisha kwamba ligi yetu haichezwi kwenye viwanja vibovu, vile vibovu tunavifungia na hapo watu wote wametii.”
KAMATI YA USIMAMIZI WA LIGI
“Hiki ni chombo kingine ambacho kimesaidia, kuifanya ligi yetu iwe bora na kazi yake kubwa hasa ni kuangalia matokeo yote ambayo yanafanyika viwanjani.
“Kuhakikisha kwamba kila mtu anafuata zile sheria 17 za mpira na taratibu zote, kwa hiyo bila kamati hii sijui tungeendaje, hii ni kamati ambayo nimeiteua, tunakaa kila baada ya mchezo kujadili ripoti zote kwa sababu ndio jicho letu la kwanza.

“Hawa ndio wanaoweza kumpa alama refa kama amechezesha vizuri au vibaya, bila kusahau hali ya kila kitu uwanjani mpaka mashabiki na tabia za wachezaji, pointi zake zikiwa chini tunamuondoa au kutoa mafunzo ya kutosha ili arudi kwenye ubora wake kwa sababu mwamuzi ni mtu muhimu ndio maana haguswi na anatakiwa achezeshe kwa haki ingawaje ni ngumu.”
MABORESHO WAAMUZI
“Hili ni eneo ambalo linafanyiwa kazi, kuanzia TFF mpaka sisi na wahusika wote, ujue makosa yanatokea kwa haraka sana japokuwa wengine wana makosa ila tunajitahidi kutoa semina na wakati mwingine tunaita wakufunzi kutoka CAF.

“Hilo ndilo tunaloweza kulifanya, pamoja na yote hayo lakini minong’ono bado ipo, wakati mwingine tunaenda mbali zaidi kwa kuyaangalia matendo yake kwa sababu ya kuwepo kwa televisheni, hatujalala tunaangalia.
RUSHWA
“Mambo ya rushwa kusema ukweli huwa ni magumu na taasisi ya kupambana na rushwa iko kazini na huku kwenye mpira wetu hawajapaacha.
“Kati ya hao watoaji na wapokeaji walivyobaini tunafuatilia wakapunguza nyendo zao, lakini binadamu ni wajanja sana japo hawawezi kuuzidi mkono wa serikali ambao ni mrefu.
“Ule mkono ukisharefuka nadhani watapatikana na tukishampata mmoja huyo atakuwa mfano kwa wengine, bahati mbaya sana hakuna aliyewahi kupatikana ila ni hisia tu na tunawalaumu sana marefa na ni dhambi mpaka uwe na uhakika.
POSHO ZA WAAMUZI
“Sijajua kama kuna baadhi ya waamuzi wanasafiri kwa ndege na wengine kwa basi, ila sisi gharama zetu ni za basi na inapohitajika sana ndio tunampandisha ndege awahi kwa haraka.
“Mara zote huwa wanaenda kwa basi, ila waandishi macho yenu yanafika mbali zaidi tutafurahi kama tukishirikiana katika suala hili la rushwa kwa kutupa hizo taarifa.
“Hii itatufanya tujue aliyepanda ndege amewezaje kulipia kwa sababu kwenda Mwanza nauli yake inafika hadi laki sita, mtu kama huyo anatupa pa kuanzia.
KESI NGUMU ZAIDI
“Ziko nyingi, mojawapo ilikuwa 2021, pale Yanga ilipogoma kwa sababu ya muda kusogezwa, ilitusumbua zaidi ya hii ya sasa, ilikuwa inaenda kutoa alama tatu kama tusingetoa uamuzi haraka, ndio maana tukaahirisha mchezo.
“Nikubali kuwa tunaongoza timu ambazo ziko na umaarufu mkubwa hiyo hakuna anayeweza kukataa, ndio maana tunasumbuka kukaa vikao.
“Piga picha umeishusha Yanga au Simba, hivyo imekuwa tatizo kubwa kurekebisha mambo kwa sababu linaweza kuhatarisha amani, presha ni kubwa ila maneno ndio mengi.
“Tuko kwenye hatua ya uamuzi tunataka kuelemisha umma kuhusu kile kilichotokea, hizi ni timu kubwa ambazo hata Serikali zinaziangalia, hivyo ni lazima kutumia hekima na busara.
“Ushindani unaupata kutokana na hizi timu kwa sababu hatujashindwa kabisa na kama ikitokea hivyo tutaziingiza na Serikali, kwa sababu mpira ni mchezo mkubwa.
“Tutakapotoa uamuzi wa bodi hapo ndio itajulikana kama sisi tumekosea au tumepatia tutawakaribisha wananchi waongee wanavyoweza, kama waendeshaji wakuu tuna uwezo wa kutoa aumuzi,” anasema Mnguto.
Katika sakata hilo lililotokea Jumamosi ya Mei 08, 2021, mchezo huo wa Kariakoo Dabi wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-21 ambao ulipangwa kuwakutanisha Simba dhidi ya Yanga, uliahirishwa baada ya Yanga kugomea mabadiliko ya muda.
Awali, mchezo huo ulipangwa kupigwa saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na baadaye kusogezwa hadi saa 1:00 usiku kitendo ambacho Yanga walikigomea, wakapeleka timu muda wa awali, kisha wakaondoka baada ya kukaa kwa muda.
Simba nao wakaenda uwanjani muda mpya uliopangwa, hata hivyo mechi haikuchezwa kufuatia tangazo la kuahirishwa kwake, ikapangiwa tarehe nyingine na Yanga ikashinda 1-0.
ITAENDELEA KESHO