Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uwanja wa Dabi sio tatizo, tukutane Unguja Machi Mosi

JICHO Pict


KAMA kawaida yetu. Wakubwa wetu wa Kariakoo lazima wagombane kwanza bila ya sababu za msingi. Ghafla umeibuka mzozo usio na maana kuelekea Dabi ya Machi Mosi ambayo itapigwa pale Unguja katika ardhi ya Mzee Abeid Amaan Karume. Inachekesha kuendelea kusoma kinachosemwa.


Tuanze na nani? Tuanze na upande wa Msimbazi. Wanadai kwamba Ally Kamwe alitoa taarifa ya Dabi kuchezwa Unguja kabla hata ya bodi ya ligi haijatoa taarifa hiyo. Hoja ni nini hapa? Haieleweki. Kwamba Simba wanahisi Yanga walikuwa na mawasiliano ya siri na bodi ya ligi na wakapanga tarehe hiyo kinyemela au? Hoja ni nini hapa? Kwamba taarifa rasmi lazima itolewe na bodi ya ligi?


Kamwe alikuwa anazungumzia mambo ya klabu yake. Kwamba wamepanga mechi ikachezwe Zanzibar. Sio jambo baya kwa sababu hakukuwa na namna ambayo Simba au bodi ya Ligi wangeweza kuzuia mechi kuchezwa Unguja. Kwanza kabisa ni kwa sababu ilikuwa ni haki ya Yanga. Wao ndio wenyeji wa pambano hilo.

Lakini pili hakuna ambacho kingebadilisha hilo kwa sababu uwanja wenyewe una vigezo. Uwanja huu huu ambao msimu uliopita ulichezewa fainali ya pambano la Shirikisho kati ya Simba na Berkane. Uwanja huu huu ambao Yanga wameutumia kwa mechi za CAF hatua ya makundi msimu huu ambao wao na watani wameambulia patupu.

JICH 01

Yanga pia wana mamlaka ya kusema wanakwenda kucheza uwanja fulani ndani ya mipaka yetu kwa sababu kanuni zinawaruhusu kuongeza viwanja vingine viwili nje ya uwanja wao wa nyumbani ambao kwa sasa ni KMC. Kama wakilipanga hilo wanaweza kujisemea hilo hadharani hata kama bado hawajawasiliana na watu wa Bodi ya Ligi ili mradi tu wanalisema hilo wakiwa ndani ya muda.

Naamini hata leo Simba wanaweza kuamua kusema pambano lijalo la marudiano la ligi dhidi ya mtani wataenda kucheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi pale Tabora au Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo pale Mbweni ili mradi tu viwanja hivyo viwe vinakidhi vigezo. Wapo ndani ya muda na wana uwezo wa kujisemea hilo bila ya kuwasiliana na Bodi ya Ligi kwa sasa. Muda ukifika watafanya hivyo kwa barua.

Hili jambo limenichekesha kwa sababu lina sura mbili. Sura ya kwanza ni kwa Yanga wenyewe. Walikuwa wajanja baada tu ya kutolewa katika kundi lake kutokana na Al Ahly kushindwa kumfunga Far Rabat pale Cairo huku wakichekwa na mtani ambaye alitolewa mapema, waliamua kupunguza 'attention' ya matokeo yao kwa kutangaza mechi yao na mtani ingechezwa Zanzibar.

Lengo ilikuwa kupunguza gumzo la wao kutolewa kikatili katika pambano la mwisho la kundi lao na kupeleka gumzo hilo katika mjadala wa pambano lao na mtani kuchezwa Zanzibar. Na wamefanikiwa katika hili kwa sababu ghafla watu wamehamia huku na kusahau kwamba Yanga walijitamba kwamba lazima wangepita katika kundi lao.

Na Yanga walijua tu kwamba watafanikiwa katika hili kama wanavyofanikiwa sasa hivi kwa sababu Simba wameanza kuchukia kucheza Unguja. Wanaamini kwamba Uwanja wa Amaan una nuksi kwao. Hawaupendi tu.

JICH 02

Dhana hii imeendelea kujengeka zaidi katika siku hivi karibuni. Simba wana woga na Uwanja wa Amaan. Waliuchukia zaidi wakati walipolazimishwa kucheza mechi yao ya marudiano ya fainali za Shirikisho na RS Berkane ya Morocco.

Yanga nao wameanza kujipa faida ya kisaikolojia kwamba uwanja wa Amaan ni wao. Ni uwanja ambao mpinzani hawezi kutoka salama kiurahisi. Wameanza kushinda mechi nyingi za michuano ya Kombe la Mapinduzi.

Lakini pia katika michuano ya CAF wamekuwa wakifanya vizuri kwenye uwanja huo. Katika pointi tisa walizotakiwa kuchukua katika kundi lao kwa mechi za nyumbani wao wamechukua pointi saba. Sio haba kwa matumizi ya uwanja wa nyumbani.

Wanauita uwanja huu Guantanamo Bay wakiufananisha na gereza maarufu lililomo nchini Cuba ambalo linamilikiwa na Wamarekani. Kwamba mfungwa ana nafasi ya mwisho ya kutoroka katika gereza hilo.

Zanzibar inaonekana kuwa ngome ya Yanga na wenyewe wanaonekana kuimarisha dhana hii kiasi kwamba wameitumia pia kuhamisha mjadala wa kushindwa kufuzu hatua ya robo fainali na kuupeleka mjadala katika dabi.

JICH 03

Zamani dhana hii haikuwapo. Simba wamewahi kuichapa Yanga mara mbili pale Unguja mwanzoni mwa miaka ya 1990. Yanga wamewahi kufungwa kwa matuta na Simba katika mechi muhimu pale Unguja. Damian Kimti pia amewahi kuizamisha Yanga pale Unguja. Hata hivyo, nyakati zimekwenda kasi na sasa inaonekana kama vile Simba hawana amani na Uwanja wa Amaan.

Binafsi naamini kwamba timu bora huwa inashinda uwanjani. Kuna imani zisizo na msingi ambazo zilikuwa zinatanda katika mechi hizi, lakini zilikuja kufa kifo cha mende. Kwa mfano Simba wanaamini kwamba siku yao bora kucheza na Yanga huwa ni Jumapili. Hata hivyo, walifungwa 1-5 katika siku kama hii ikiwa ni kipigo kikubwa zaidi kutoka kwa mtani tangu kupinduka kwa milenia.

Yanga wanaamini kwamba siku yao bora kucheza na Simba ni Jumamosi. Ni mara ngapi Simba amemfunga Yanga Jumamosi? Mara kadhaa. Simba anaweza kwenda Unguja na akashinda mechi.

Akijiweka katika mazingira ya ulalamishi mapema anaweza kupoteza mechi nje ya uwanja kabla hajagusa katika nyasi za Amaan. Ni jambo lile lile la 'hatuchezi' ambalo lilitawala mechi yao ya mwisho. Binafsi naamini timu bora inashinda uwanjani.

Jambo la pili ambalo nalisikia ni kwamba Uwanja wa Amaan unawanyima fursa mashabiki wengi wa soka kutazama pambano hilo. Nimemsikia hata rafiki yangu, Haji Manara akijaribu kulijadili mahali suala hilo.

Limezua utata kweli kweli kuhusu haki za mashabiki katika kutazama mechi yenyewe. Hili nalo limenishangaza kidogo. Na linafungua mjadala kuhusu idadi ya mashabiki katika mechi hii.

JICH 04

Katika miaka ya hivi karibuni wasemaji wamekuwa wakihaha kweli kweli kuhakikisha mashabiki wanajitokeza uwanjani.

Zamani pambano la Simba na Yanga lilikuwa linajiuza lenyewe. Siku hizi inaonekana kama vile mashabiki wanalazimishwa kwenda uwanjani. Kumbe hata mpira ukiuweka kwenye Uwanja wa Taifa bado suala la mashabiki kwenda uwanjani ni gumu.

Na tukigeukia Uwanja wa Amaan, Manara analalamika kwamba inakuwa ngumu kwa shabiki wa Nzega kwenda Zanzibar na pia idadi ya mashabiki uwanjani ni chache. Nadhani inabidi tubadilike katika suala la mauzo ya tiketi.

Tiketi inabidi iuzwe mtandaoni ili shabiki wa Nzega ajinunulie tiketi yake na ajipange kwenda Zanzibar mapema. Uzuri wa tiketi za mitandaoni ni kwamba zinauzwa bila ya kujali eneo ambalo shabiki yupo. Ubaya wa tiketi za papo kwa papo ni kwamba wanufaika wengi wanakuwa wakazi wa eneo husika.

Lakini pia lazima tujikumbushe kwamba katika mchakato wa mauzo ya tiketi ya sasa ni uvivu wa wenyeji tu ndio ambao unasababisha watu walio mbali na uwanja wa mechi kama hii waweze kupata tiketi. Mfano, kama wakazi wa Dar es salaam wangekuwa wanaamua kwenda kwa wingi uwanjani sidhani hata kama watu wa Pwani tu wangeweza kupata tiketi.

Mfano, Wazanzibari wenyewe tu wakiamua kuujaza Uwanja wa Amaan sioni nafasi hata kwa mashabiki wa upande wa Bara kupata tiketi. Ni uvivu tu ndio unasadia watu wa mikoani wapate tiketi kutoka Nzega na kuhudhuria pambano la Simba na Yanga pale Temeke.