Prime
Kwa Simba asanteni, Yanga kuna hii moja!
SIMBA walihitimisha mechi yao ya mwisho ugenini Jumamosi usiku saa moja kwa saa za Tanzania. Walikuwa katika ardhi ya Jonas Savimbi na waliambulua sare ya ajabu ugenini. Shomari Kapombe alipewa kadi nyekundu mapema na bado Simba walisawazisha licha ya kutanguliwa.
Wanachoweza kusema kwa sasa ni Alhamdulillah. Ndugu zetu Waislamu huwa wanashukuru kwa kila kitu. Kwa kila wanachokipata. Safari ya Simba imeishia hapo. Wenyewe hawaamini walichokiona katika michuano hii. Mpaka sasa wana pointi mbili tu baada ya mechi tano.
Kulikuwa na nyakati ambazo waliongoza kundi lenye Al Ahly na AS Vita kwa pointi 13. Nyakati zimekwenda wapi? Wakati ule wakiwa kamili. Wakiwa na Clatous Chotta Chama katika ubora wake. Jose Luis Miquissone, Meddie Kagere, John Bocco, Chris Mugalu, Hassan Dilunga na wengineo. Leo imebakia historia tu. Ndani ya mechi tano wamekusanya pointi mbili na hakuna wanachoweza kufanya kutoka mkiani.
Kitu cha kushangaza ni kwamba hawakuwa katika kundi gumu. Na hata mechi yao ya mwisho ugenini haikuwa ngumu. Kosa la kipa wao mpya, Djibrilla Kasalli liliwagharimu bao la wenyeji Petro De Luanda.
Aliutokea mpira ambao hakujua kama angeweza kuupata au hapana. Kipa ukitoka inabidi uuguse mpira. Kama hauna uhakika ni bora ubakie zako langoni. Kasalli alichemsha.
Baadaye Shomari akapewa kadi nyekundu. Baadae Simba ikaendelea kucheza vizuri tu kama vile Shomari alikuwepo uwanjani. Wachezaji wapya wa Simba wameongeza kitu. Tofauti na rafiki zangu kina Joshua Mutale. Bado nasisitiza kwamba Chama ambaye anacheza asilimia 40 ya ubora wake ni bora kuliko Mutale anayecheza asilimia 95 ya uwezo wake. Ni ukweli mchungu, lakini lazima uzungumzwe hadharani.
Simba wanaweza kusema Alhamdulillah kwa walichokipata Luanda. Hakuna baya. Wanayo timu ya kuanzia katika kujipanga upya msimu ujao. Wanaweza kuitumia mechi ya mwisho dhidi ya Stade Mallen katika kuchunguza wachezaji ambao wanaweza kuwapata kwa ajili ya dirisha kubwa la uhamisho.
Baadaye saa nne usiku ikachezwa mechi ya Yanga dhidi ya Far Rabat kule Morocco. Hii ilikuwa mechi muhimu zaidi kuliko mechi ya Simba. Tayari tulishajua hatima ya Simba tangu siku saba zilizopita wakati walipowaruhusu Esparance Du Tunis kurudisha mabao mawili Uwanja wa Taifa. Tayari Simba walikuwa wamekatwa kichwa Temeke. Mechi ya msingi juzi ilikuwa Rabat.
Yanga walihitajika kutoka sare tu kisha kushinda mechi ya mwisho kule Unguja. Haikuwa hivyo. Na haikuwa bahati mbaya kwamba haikuwa hivyo kwa sababu kila kitu kilikwenda upande wa Far Rabat.
Walikuwa bora uwanjani kuanzia dakika ya kwanza mpaka ya mwisho. Na waliondoka na bao lao moja ingawa walitaka kushinda mengi. Mabao mawili yangeweza kuwahakikishia kupita.
Yanga walicheza vibaya katika maeneo mengi ya uwanja kasoro eneo la ulinzi tu ambapo Bakari Nondo Mwamunyeto aliwaongoza vema wenzake kukabiliana na mashambulizi ya Far Rabat. Nondo ni kama amezaliwa upya. Nahodha na kamanda hasa katika safu ya ulinzi. Bila ya bao lao pekee, Far Rabat wangeweza kucheza na Yanga wiki mbili wasizione nyavu za Djigui Diarra.
Tatizo la Yanga lilikuwa kuanzia kiungo kwenda mbele. Na mchezaji aliyekuwa ovyo hasa alikuwa ni Pacome Zouzoua. Inashangaza. Ni mara chache kwa Pacome kuwa ovyo kama alivyokuwa juzi. Alipoteza mipira mingi na hakuonekana kuwa makini na mechi. Kuna hisia kwamba Pacome ndiye Yanga na Yanga ni Pacome. Sijui kwanini hakujitambua katika hilo katika mechi ambayo Yanga walimuhitaji kama roho.
Mwingine alikuwa dogo Alan Okello. Maji yalizidi unga na hakuonekana kufanya lolote uwanjani. Hakuweza kukaa na mpira. Hakuweza kupiga pasi sahihi. Hakuweza kufanya jambo lolote la maana uwanjani. Kama yeye na Pacome hawakuweza kufanya mambo ya msingi katika eneo la mwisho nani angeweza kufanya?
Kabla ya mechi hizi za Simba na Yanga mashabiki wengi mchana tulikuwa tunafuatilia mechi ya Manchester United na Tottenham iliyochezwa Old Trafford. Kuna mchezaji mmoja mwehu wa Spurs, Cristian Romero alikuwa amepewa kadi nyekundu ya kijinga kwa kumchezea rafu mbaya Casemiro wa United.
Ilikuwa ni kadi yake ya tisa katika maisha yake ya soka. Romero anafanana na mchezaji anaitwa Camara Damaro. Huyu Damaro ameendelea kutuonyesha juzi namna ambavyo asivyo na umakini katika mipira ya nusu kwa nusu. Alichukua kadi yake ya njano mapema tu na imekuwa kawaida yake. Sijui kwanini hawezi kuuzuia mwili wake wakati anapopambania mpira wa nusu kwa nusu na adui. Lazima atafika katika mwili wa adui.
Alimlazimisha kocha Pedro Concalves kufanya mabadiliko wakati wa mapumziko. Vinginevyo yeye akiwamo, na hata wakati ameondoka uwanjani, Far Rabat walikuwa bora uwanjani. Ilikuwa ni timu tofauti kabisa na ile ambayo ilifungwa Unguja mwaka jana. Mechi ile walifungwa kihalali na hii wameshinda kihalali.
Nini kinafuata? Yanga wanahitaji mabao mengi katika pambano la mwisho dhidi ya JS Kayblie na wote tunaweza kuitikia kwa kusema ‘”In shaa Allah”. Na sio tu kwamba wanahitaji mabao mengi lakini wanahitaji pia Far Rabat afungwe pale Cairo katika pambano lao la mwisho dhidi ya Al Ahly. Yote haya mawili yanawezekana na wote tuseme ‘In shaa Allah’.
Yanga wanaweza kuifunga JS Kabylie Unguja. Wale Waarabu hawana timu ya maana na hawana kitu cha kupambania mpaka sasa. Wanakuja kukamilisha ratiba tu. Lakini kitu cha msingi ni kwamba Al Ahly wana sababu nyingi za kuifunga Far Rabat. Kwanza kabisa timu za Afrika Kaskazini zina upinzani mkubwa baina yao. Timu za Misri, Algeria, Morocco na Tunisia huwa hazipendani. Hazina urafiki.
Mechi yao ya mwisho iliyochezwa Rabat ndio ilikuwa chanzo kikubwa cha Far Rabat kucheza bila ya mashabiki kwa sababu za vurugu ambazo Al Ahly walifanyiwa na mashabiki wa Far Rabat. Kwao ni mechi fulani hivi ya kisasi ambayo sioni kama Far Rabat watasalimika ndani na nje ya uwanja. Maisha yao yatakuwa magumu Cairo.
Jambo jingine ni kwamba hili litakuwa pambano la kuwania nafasi ya kwanza katika kundi. Al Ahly atahitaji kucheza na timu yoyote ambayo itashika nafasi ya pili katika kundi jingine. Hawezi kukubali kufungwa nyumbani wakati akihitajj kuongoza kundi lenyewe. Akifungwa nyumbani atashika nafasi ya pili. Akitoka sare au kushinda ataongoza kundi.
Jambo jingine ni kwamba Waarabu wanafanyiana roho mbaya kwa sababu wanajuana kuna hatari ya kukutana mbele ya safari. Kwa Al Ahly ni bora mbele ya safari akutane na Yanga kuliko Far Rabat. Inapopatikana nafasi ya kumpunguza Mwarabu mwenzako ni jambo bora kuliko kukutana naye mbele ya safari. Yote haya kwa Yanga tunasema ‘In Shaa Allah’.
Yanawezekana lakini ni mambo ya kumuachia Mungu zaidi. Tusubiri mpaka wikiendi ijayo kujua nini kinaweza kutokea na nini hakiwezi kutokea. Kwa Simba tunaweza kusema Alhamdulillah lakini kwa Yanga tunasubiri yajayo na tunaweza tu kusema In Shaa Allah.