Prime
Kwa hili, tajiri Yanga ataimbwa maisha yote
KADRI ninavyojaribu kuipuuza habari ya Yanga kujenga uwanja ndivyo inavyoanza kuonekana huenda kweli klabu hiyo ikajenga. Mtu anayeitwa Ghalib Said Mohamed ‘GSM’ anaonekana amepania kuijengea Yanga uwanja mpya na wa kisasa. Inaonekana amepania kuacha alama kubwa.
Jana nimemuona akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kando ya kijana wake, Injinia Hersi Said ambaye ni Rais wa Yanga. Mzaha mzaha hivi hivi, Yanga huenda wakajenga uwanja wao.
Kama Hersi na Ghalib wakijenga uwanja wa kisasa Yanga wataacha alama isiyofutika. Zaidi ya kuchukua ubingwa wa Afrika, zaidi ya kuendelea kumfunga mtani, zaidi ya kila kitu.
Februari 11 mwaka huu Yanga wametimiza miaka 91 tangu kuanzishwa kwao. Zamani nilidhani ni aibu kwa timu kubwa kutokuwa na uwanja. Hapana, sio aibu. Sio kazi nyepesi sana kama ambavyo watu wengi wanafikiria.
Kuna klabu nyingi kubwa duniani hazina viwanja. Al Ahly hawana uwanja. Wao na watani zao Zamalek wanatumia Uwanja wa Taifa wa Cairo kucheza mechi zao za nyumbani.
Kule Italia klabu nyingi hazina viwanja. Juventus wamejenga majuzi tu uwanja wao wa nyumbani. Timu nyingi zinatumia viwanja vya Manispaa au vya serikali. AC Milan na Inter Milan wanatumia uwanja mmoja wa San Siro ambao hawaumiliki. Nasikia wana mpango wa kujenga uwanja wao wa pamoja. Hali ni hiyo hiyo kwa timu nyingi za Hispania. Wale wakubwa wana viwanja vyao lakini kuna wadogo ambao hawana viwanja vyao.
Rafiki zetu Kaizer Chiefs hawana uwanja. Wanahaha tu. Ni England tu ndipo ambapo klabu nyingi zina viwanja vyake. Kwingineko duniani klabu hazina ubavu wa kumiliki viwanja vikubwa vyenye uwezo wa kuchukua mashabiki 25,000 kama Yanga walivyokusudia.
Nimemsikia Hersi akisema kwamba wanataka kujenga uwanja wenye viwango vya CAF na FIFA ambao utaweza kuchezewa mechi kama za Afcon na nyinginezo.
Timu kadhaa zinamiliki viwanja kama KMC, Namungo, Singida Big Stars na Azam. Viwanja vyenye uwezo wa kuchukua mashabiki 10,000 lakini kama Yanga wakijenga uwanja ulio mkubwa mara mbili ya viwanja vya kina Azam basi watakuwa wamefanya maajabu makubwa. Watakuwa wamejitendea haki kwa namna kubwa.
Uzuri wa wenzetu, wakubwa ambao hawana viwanja huwa wanajenga viwanja vingi vizuri vya mazoezi (complex). Sisi hatuna vyote viwili. Hatuna viwanja vizuri vya mazoezi wala viwanja vya mechi. Ni miaka mingi baada ya timu hizi kuanzishwa na kuwa na mashabiki lukuki ndani na nje ya Tanzania.
Si kazi rahisi kuwa na uwanja. Na kwa hesabu za haraka haraka za uwekezaji ni kwamba uwanja haulipi. Ni makazi na heshima, lakini kwa hesabu za kiuwekezaji ni afadhali kuwa na kumbi nyingi za harusi kuliko kuwa na uwanja wa mpira. Tazama ni kiasi gani cha pesa unaweza kuingiza katika ujenzi wa uwanja na kiasi gani unaweza kupata kurudisha gharama ulizotumia.
Kama Namungo na Coastal Union wakicheza kwenye Uwanja wa Yanga wanaweza kulipa shilingi milioni moja. Ni lini kiasi kama hiki cha pesa kinaweza kurudisha uwekezaji wa mabilioni ya pesa.
Kama tajiri ameweka Sh30 bilioni katika ujenzi wa uwanja anawezaje kurudisha pesa yake? Ni afadhali angewekeza katika biashara zake. Yanga yenyewe haiwezi kurudisha pesa zake kirahisi katika biashara ya uwanja.
Bado mapato ya mechi na matangazo mengine ya uwanjani yatakwenda zaidi katika kuiendesha timu yenyewe. Na hasa katika nyakati hizi ambazo Yanga na klabu nyingine kubwa zimetanua goli katika gharama za uendeshaji wa timu. Wachezaji wananunuliwa kwa pesa kubwa na wanalipwa mishahara mikubwa. Hauwezi kuona moja kwa moja faida ambayo Yanga wataipata.
Kule Ulaya kwa klabu ambazo zinamiliki viwanja au zimejenga viwanja katika miaka ya karibuni kama Arsenal, Atletico Madrid, Everton na Tottenham Hotspurs zimefanya hivyo kwa kuchukua mikopo ambayo wakati mwingine inawaumiza.
Wakati ule Arsene Wenger alikuwa analalamika kwamba Arsenal ilikuwa haina ubavu wa kushindana na Manchester United kifedha kwa sababu ilikuwa na deni kubwa la kurudisha benki baada ya kukopa pesa kujenga uwanja.
Sio kazi rahisi kujenga uwanja. Kama Ghalib akijenga uwanja ataacha alama isiyofutika. Kuna wale ambao wanaamini kwamba huenda Ghalib atanufaika kwa kuweka matangazo katika uwanja.
Hawajiulizi ni namna gani angeweza kutumia pesa za ujenzi wa uwanja kuendeleza biashara zake nyingine. Inahitaji moyo na kujitoa tu. Hakuna faida ya moja kwa moja hata kama uwanja utaitwa GSM Stadium.
Ghalib ataacha alama. Atakuwa amefanya kitu ambacho kimeshindikana kwa miaka 91. Kuna wakati Yanga walikuwa na uwanja wao wa Kaunda, lakini ulikuwa kama uwanja wa mazoezi tu na kucheza mechi za kirafiki ambazo hazikuwa na uzito. Ghalib atakuwa amefanya kitu kizito kilichozishinda timu nyingi za soka duniani.
Labda maumivu ambayo anaweza kuyapunguza ni namna ya kuufanya uwanja kuwa wa kibiashara zaidi. Uwanja uwe na biashara nyingi ambazo zitakuwa zinaendelea kila siku hata kama hakuna mechi.
Majukwaa pia yanaweza kupewa majina ya makampuni makubwa kwa mikataba maalumu. Wengine wenye pesa kina Manchester United wao majukwaa yao yanepewa majina ya watu wakubwa waliofanya mambo makubwa. Kina Sir Alex Ferguson na Bobby Charlton.
Tusubiri na kuona Yanga wakikamilisha mradi huu. Kitu ambacho nina uhakika nacho ni kwamba kule kwa mtani hawataweza kukubali kuona Yanga wakitamba na uwanja mpya. Na wao watafanya juu chini ya kuhakikisha wanajenga uwanja wao.
Watani wana tabia ya kushindana katika mambo mengi ya maendeleo. Hata hivyo, itakuwa kazi ngumu kwa mtani kwa sababu mambo yao mengi hayaeleweki katika siku za hivi karibuni.
Ghalib atakuwa ametisha kama akiwaachia Yanga uwanja. Kuna watu ambao wanapita katika hizi timu na wanasahaulika kwa urahisi kwa sababu hawaachi alama nzito.
Kama ni kutwaa ubingwa au kumfunga mtani kuna watu wengi wamefanya hayo mambo na wamesahaulika kwa sababu sio vitu ambavyo vinaacha sana alama katika historia ya klabu. Watu wanasahau kiurahisi.
Hadi leo hatujui nani alikuwa Mwenyekiti wa Simba wakati wakiifunga Yanga mabao 6-0 mwaka 1977. Kama Mwenyekiti huyo angekuwa amejenga uwanja wa Simba pengine angekumbukwa daima kama ambavyo huwa tunamkumbuka marehemu Abeid Aman Karume kwa kujenga majengo ya Simba na Yanga.
Ghalib awaachie tu Yanga uwanja. Ndizo alama ambazo huwa hazifutiki na ndio maendeleo ya ukweli ambayo mashabiki wanayaheshimu zaidi na wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuyaona yanapatikana katika timu zao. Imechosha kuona dharau zinakuwa kubwa wakati ‘watoto’ wa juzi kama Azam, KMC, Namungo na Singida Big Stars wakiwa na viwanja hata kama ni vidogo.