Prime
Ni Februari nyingine Ronaldo hoi, Neymar yuko chali
KILA ifikapo Februari 5, huwa Cristiano Ronaldo anazaliwa. Neymar huwa anazaliwa. Carlos Tevez huwa anazaliwa. Na wapo mastaa wengi wa soka ambao wanazaliwa tarehe hiyo. Na juzi ilikuwa Februari 5.
Mastaa wakubwa ambao bado wamezaliwa tarehe hiyo na bado wanavuja jasho uwanjani ni Ronaldo na Neymar. Ronaldo amefika akiwa hoi. Miguu imekuwa mizito. Akili inataka lakini mwili hautaki tena. Amefikisha umri wa miaka 41. Tusubiri kuona ataamua nini baada ya Kombe la Dunia kumalizika pale Canada, Mexico na Marekani.
Kinachomsumbua Ronaldo ni kutwaa Kombe la Dunia tu. Hawezi kusema hivyo hadharani na majuzi aliwahi kutoa kauli ambayo ipo katika hisia zangu. Alizungumza ukweli kwamba kutotwaa Kombe la Dunia hakumfanyi mchezaji asiwe miongoni mwa wachezaji bora wa muda wote.
Kwamba unaweza kutwaa Kombe la Dunia kwa mechi saba tu na haiondoi maisha ya soka yalikuwa vipi. Hapo Ronaldo alizungumza ukweli, lakini ndani ya moyo anajua kwamba hasimu wake, Lionel Messi ametwaa Kombe la Dunia na amewekwa katika kiganja kimoja na kina Pele, Diego Maradona, Franz Beckenbauer na wengineo.
Moyoni Ronaldo amelipania Kombe la Dunia ambalo anajua ana askari wanaoweza kumsaidia kufanya hivyo kule Ureno. Kina Bernado Silva, Rafael Leao, Vitinha, Bruno Fernandes, Ruben Neves na wengineo. Ni kama tu Messi alivyosadaiwa na vijana wake.
Sioni Ronaldo akiendelea kucheza soka baada ya Kombe la Dunia. Kwa sasa yupo hoi. Pale Al-Nasr huwa anafunga, lakini binafsi naona pia huwa anawakaba. Timu inacheza vizuri zaidi wakati yeye akiwa nje ya uwanja kwa sababu wanajikuta watu 11 wenye nguvu ya kutosha wakicheza uwanjani.
Uzuri wa Ronaldo ni kwamba hata akiacha mpira leo akiwa na umri wa miaka 41 bado atakuwa ameacha alama kubwa katika mchezo wenyewe. Sidhani kama akikosa hili Kombe la Dunia basi jina lake litafutika katika historia. Hapana. Ataishia kunyanyaswa tu kwa maneno ya kejeli ya hapa na pale na wafuasi wa Messi.
Cristiano ametwaa mataji mengine. Ametwaa tuzo nyingi binafsi na hapana shaka zilifika nyakati tuzo ya mwanasoka bora wa dunia ilikuwa inamilikiwa na watu wawili tu. Yeye na hasimu wake, Messi. Basi. Wengine waliishia kwenda ukumbini tu kushuhudia Messi na Ronaldo wakitwaa.
Mtu ambaye jina lake lipo matatani na amefika Februari hii akiwa hoi ni Neymar. Ametimiza miaka 34 huku wengi tukishindwa kutafakari kwamba pindi akiachana na soka tutamuweka wapi katika kundi la wachezaji bora wa muda wote.
Ni kweli kwamba Neymar ametwaa mataji mengi ya ligi za Ulaya ikiwemo La Liga na Ligi Kuu Ufaransa. Ametwaa pia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hata hivyo, kipaji cha Neymar hakikufika mwisho ambako tulitarajia. Mambo mawili ambayo Neymar hajajitendea haki wala hajawatendea haki Wabrazili wenzake.
Kwanza kabisa Neymar hajawahi kutwaa Kombe la Dunia. Ni tofauti na mastaa wa Brazil wanaoimbwa. Kuanzia kwa kina Pele, Garincha, Tostao, Romario, Bebeto, Ronaldo de Lima, Rivaldo, Ronaldinho, Kaka na wengineo, Neymar hajawahi kutwaa Kombe la Dunia.
Brazil inaheshimu sana wachezaji wake waliowahi kuwepo katika vikosi vilivyotwaa Kombe la Dunia. Neymar hayupo katika orodha hii licha ya ukweli kwamba alikuwa na kipaji maridhawa. Namuona akiwa amepania kwenda Canada, Marekani na Mexico kwa ajili ya kujaribu bahati yake kwa mara ya mwisho.
Katika mechi za mwisho za mwisho za timu yake ya Santos, Neymar aliwaokoa kushuka daraja kisha akaenda kufanyiwa operesheni mapema kwa ajili ya kujiandaa na Kombe la Dunia. Kocha Caro Ancelotti anaweza kumbeba katika kikosi chake.
Uzuri wa Neymar ni kwamba ana watu ambao wanaweza kumsaidia kazi. Kina Vinicius Junior, Rafinha, Gabriel Martinelli na wengineo wengi. Labda anaweza kuambulia Kombe la Dunia Julai, mwaka huu na akajikuta ameangukia kundi la kina De Lima.
Kitu kingine ambacho Neymar amejiangusha mwenyewe ni hili hapa la kutowahi kutwaa tuzo ya mwanasoka bora wa dunia. Sidhani kama ataweza kurekebisha tena kwa sasa na kwa namna hali ilivyo. Labda afanye maajabu makubwa katika Kombe la Dunia.
Wanasoka wengi wakubwa wa Brazil ndani ya miaka 20 iliyopita wametwaa tuzo hii. Wakiwemo Ronaldinho, De Lima na Kaka. Neymar alitumwa kwenda Ulaya 2013 kwa ajili ya kuwapa Wabrazili Kombe la Dunia na kuendelea kushikilia tuzo ya mwanasoka bora wa dunia, lakini haya yameshindikana mpaka sasa.
Uhamisho wake kutoka Barcelona kwenda PSG haukueleweka vyema, lakini baada ya hapo majeraha ya mara kwa mara yalikwamisha kipaji chake. Nyuma yake kulikuwa na starehe nyingi kama ambavyo tunawafahamu wachezaji wa Kibrazili.
Nafasi yake ya kutwaa tuzo hii inategemea na namna ambavyo michuano yenyewe itakwenda. Akienda Kombe la Dunia bado simuoni kama atakuwa tegemeo kikosini kuliko kina Vinicius na Rafinha. Lakini hapo kumbuka kwamba katika ngazi ya klabu alikuwa anachezea timu ya Brazil ambayo ilikuwa inakwepa kushuka daraja.
Neymar amefikisha miaka 34 juzi akiwa hoi. Kitu kikubwa na cha msingi kwake ni kwamba amefikisha umri huo akiwa na fedha nyingi. Ukifikiria fedha alizovuna PSG na kisha kwa Waarabu pale Saudi Arabia kichwa kinaweza kukuuma. Tatizo kubwa katika maisha ya mwanasoka ni kwamba huwa hakumbukwi kwa fedha. Anakumbukwa kwa mafanikio yake uwanjani.