Usipime! Makocha wamekata mawingu kisa Ligi Kuu Bara

Wednesday November 17 2021
USIPIME PIC
By Charity James

USIICHUKULIE poa Ligi Kuu Bara. Ni ligi yenye mvuto wa aina yake kwa mashabiki, wachezaji hadi makocha, ambao wanamiminika kusaka dili.

Msimu huu, Ligi Kuu Bara ina timu 16, lakini unaambiwa kati ya hizo, zaidi ya nusu (tisa) zinanolewa na makocha wa kigeni kutoka nchi 11 tofauti ukichanganya na makocha wawili wasaidizi.

Mwanaspoti linakuchambulia makocha hao waliopanda ndege na kusafiri maili za kutosha angani kutoka kwenye mataifa yao kuja kufanya kazi kwenye ligi hii.

.

PABLO FRANCO (HISPANIA)

Pablo alitambulishwa Simba Novemba 6, na kusaini mkataba wa miaka miwili akichukua nafasi ya Mfaransa Didier Gomes aliyeachana na klabu hiyo Oktoba 26 baada ya kuondoshwa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Advertisement

Klabu ya kwanza kwa Pablo kufundisha kama kocha mkuu ilikuwa ni Santa Eugenia ya (Hispania), baada ya hapo aliifundisha timu ya CD Illescas. Msimu wa 2013-14 alijiunga na CD Puertollano ya (Hispania), mwaka 2015 alitua Getafe CF ya Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’ na klabu yake ya mwisho ni Saburtalo Tbilisi ya nchini Georgia.

Klabuni Simba hadi sasa hajapata nafasi ya kukaa benchi kuiongoza katika mechi ya kimashindano, ukiachana na mechi ya mazoezini akiwa hana kikosi chake kamili kwenye Uwanja wa Boko Veterans ambako walibanwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya timu ya kituo cha soka cha Cambiasso.


THIERRY HITIMANA (RWANDA)

Alitua nchini na kuanza kuinoa Biashara United baadaye Namungo ambao waliachana naye na baadaye kurudi kwao Rwanda, kisha akarejea tena Tanzania kwaajili ya kujiunga na Mtibwa Sugar kabla ya kusaini mkataba na Simba waliomnyakua na kumtumia kama kocha mkuu kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo Gomes kukosa vigezo.

Simba walitolewa katika hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na uongozi uliamua kuachana na Gomes na kubaki na Hitimana akiwa kaimu kocha mkuu na baadaye msaidizi baada ya Pablo kutua.

Hitimana akiwa kama msaidizi ameiongoza Simba kwenye mechi tatu akianza na Polisi kwa ushindi wa bao (1-0), suluhu (0-0) na Coastal Union na kushinda bao (1-0) dhidi ya Namungo.


NASREDDINE NABI (TUNISIA/ Ubelgiji)

Ujio wa kocha Nabi, mwenye uraia pacha wa Tunisia na Ubelgiji, ndani ya Yanga umeonyesha mabadiliko mengi kuanzia uchezaji, mifumo na nidhamu kwa wachezaji. Hana muda mrefu ndani ya kikosi lakini ameweza kufanya mabadiliko makubwa yaliyoleta chachu ya ushindani na kuisaidia timu kumaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara msimu uliopita ikipata nafasi ya kushiliki mashindano ya Ligi ya Mabingwa.

Nabi mwenye umri wa miaka 56 amejiunga Yanga akitokea Al-Merrikh SC ya Sudan na amepita katika timu kama Al-Ahly SC, Al-Hilal Club, Ismaily SC na sasa anainoa Yanga.

Hadi sasa akiwa Yanga ameshinda mechi 5 za ligi akianza na Kagera Sugar (1-0), Geita Gold (1-0), KMC (2-0), Azam (2-0) na Ruvu Shooting (3-1) na amefanya hayo akisaidiana na Cedrick Kaze raia wa Burundi.


CEDRICK KAZE (BURUNDI)

Ni msaidizi wa Nabi. Si mgeni kwenye Ligi Kuu Bara kwani tayari alishainoa Yanga alipokuchukua mikoba ya Zlatko Krmpotic ambaye alifutwa kazi Oktoba 3 na uongozi wa Yanga kwa kile ilichoeleza kuwa hakuendana na falsafa za timu hiyo.

Machi 7 Yanga iliachana na kocha Cedric Kaze aliyesaini mkataba wa miaka miwili ya kuitumikia Oktoba 16, 2020 pamoja na msaidizi wake Nizar Halfan, kocha wa makipa Vladimir Niyonkuru na ofisa usalama wa klabu, Mussa Mahundi.

Baadaye Septemba 20 Yanga wamemrudisha tena Kaze akiwa kocha msaidizi ameiongoza Yanga sambamba na Nabi wakishinda michezo yote mitano ya ligi.


GEORGE LWANDAMINA (ZAMBIA)

Ni mkongwe kwenye ufundishaji ana umri wa miaka 57. Alianza kuzinoa timu mbalimbali kuanzia msimu wa 1984–1985 alipokuwa kocha wa Mutondo Stars, kisha akapita Mufulira Blackpool, Mufulira Wanderers, Green Buffaloes, Kabwe Warriors, timu ya taifa ya Zambia (kocha wa mpito), 2011–2014, Red Arrows, Zesco United na Yanga 2018–2020.

Msimu huu, ameiongoza Azam katika mechi tano za Ligi Kuu hadi sasa vs Coastal Union (1-1), walifungwa na Poilisi Tanzania (2-1), Namungo (1-0), walifungwa na Yanga (2-0) na walipata ushindi wa bao (1-0) dhidi ya Geita Gold.


PATRICK ODHIAMBO (KENYA)

Ni mgeni kwenye ligi ya Tanzania ndiye aliyeipeleka Biashara Kombe la Shirikisho Afrika japo alikuta michezo imebaki michache akipokea kijiti kutoka kwa Francis Baraza ambaye alitimkia Kagera Sugar.

Ubora wake tunatarajia kuuona msimu ujao ambao ataanza na timu yake mwenyewe baada ya asilimia kubwa ya wachgezaji kuachwa dirisha kubwa la usajili. Uongozi umempa mamlaka ya kusajili mwenyewe.

Wamecheza michezo mitano hadi sasa walianza na suluhu na Simba (0-0), walifungwa na Ruvu Shooting (1-0), walishinda (3-0) dhidi ya Prisons, walitoka 0-0 na Mbeya City na sare ya 1-1 na Mbeya Kwanza.


FRANCIS BARAZA (KENYA)

Jina lake lilikua zaidi alipokuwa na Biashara. Aliondoka na kujiunga na Kagera Sugar ambayo ilikuwa hatarini kushuka daraja.

Aliikuta timu hiyo ikiwa kwenye hali mbaya baada ya kuamua kumtimua Meck Mexime, aliipambania timu na kuinusuru kushuka daraja.

Msimu huu ameanza vibaya baada ya timu yake kucheza mechi tano kwa kufungwa na Yanga (1-0), sare 1-1 na Namungo, 0-0 na Mbeya City, wameshinda mbili 1-0 vs Mtibwa Sugar (1-0) na 1-0 vs KMC.


HERERIMANA HARUNA (BURUNDI)

Sio mgeni kwenye soka la Tanzania kwani kabla hajajiunga na Mbeya Kwanza alianza kuzinoa Lipuli na KMC alijiunga na timu iyo baada ya Amri Said kutimuliwa na uongozi wa timu hiyo kutokana na matokeo mabaya.

Ameiongoza timu ya Mbeya Kwanza kwenye michezo mitano sasa akianza na Mtibwa Sugar alishinda bao (1-0), alitoka sare na Mbeya City (2-2), alitoka suluhu na Dodoma jiji (0-0) alitoka sare (1-1) na Biashara na sare nyingine dhidi ya Polisi Tanzania (2-2).


MATHIUS LULE (UGANDA)

Desemba 2 Mbeya City ilimtangaza rasmi Mathias Lule kutoka Uganda kuwa kocha mkuu. Kocha huyo wenye leseni A ameiongoza City na kuisaidia kukwepa janga la kushuka daraja.

Ameiongoza timu ya Mbeya City kwenye mechi tano hadi sasa akianza na ushindi wa bao (1-0) vsTanzania Prisons, (2-2) vs Mbeya Kwanza, (0-0) vs Kagera Sugar, (1-1) vs Geita Gold na (0-0) vs Biashara.


MELIS MEDO (MAREKANI)

Timu yake ya kwanza kuinoa Tanzania ilikuwa ni Gwambina haikuwa na matokeo mazuri kwani aliishusha daraja na baadaye kibarua chake kuota nyasi baada ya hapo ndio alijiunga na Coastal Union.

Ni msimu wake wa kwanza kuinoa Coastal Union hajaanza vizuri baada ya sare ya bao (1-1) vs Azam, alifungwa bao 1-0 na Ruvu Shooting, kutoka suluhu tatu KMC, Simba na Prisons.


JOSEPH OMOG (CAMEROON)

Kocha wa Mtibwa. Omog, ni mzoefu wa ligi, alianza kufundisha soka la Tanzania kwa mafanikio akiiongoza Azam FC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu 2013/14 bila kupoteza mechi baadaye aliitumikia Simba na kuipa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam 2017.

Advertisement