Prime
Usiku wa deni haukawii kukucha, weka kati tupimane ubavu!
Muktasari:
- Ndio, ebu uangalie msimamo wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendelea kwa sasa, kule mkiani ndiko maskani ya Yanga ikizibeba timu nyingine tatu zilizopo kundini hapo wakiwamo vinara Al Hilal ya Sudan yenye pointi sita, MC Alger ya Algeria yenye pointi nne na Mazembe ikiwa na alama moja.
KAMA kuna kitu ambacho mashabiki na wapenzi wa Yanga wanaomba kwa leo ni kuona timu hiyo inazinduka na kupata ushindi ikiwa ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo.
Ndio, ebu uangalie msimamo wa Kundi A wa Ligi ya Mabingwa Afrika inayoendelea kwa sasa, kule mkiani ndiko maskani ya Yanga ikizibeba timu nyingine tatu zilizopo kundini hapo wakiwamo vinara Al Hilal ya Sudan yenye pointi sita, MC Alger ya Algeria yenye pointi nne na Mazembe ikiwa na alama moja.
Yanga inaburuza mkia ikiwa haina pointi hata moja wala bao lolote na leo kuanzia saa 10:00 jioni itakuwa kwenye Uwanja wa Mazembe kukabiliana na wenyeji wao hao, huku ikiwa haina namna isipokuwa kushinda.
Matokeo ya mechi mbili za awali, Yanga ilipoteza nyumbani mbele ya Al Hilal kwa mabao 2-0 kisha ikaenda kufungwa tena 2-0 na MC Alger ikiwa ugenini na kama itaendeleza gundu hilo, itakuwa na maana timu hiyo itajiweka katika nafasi finyu ya kurejea ilichokifanya msimu uliopita ilipovuka hadi robo fainali.
Mechi ya leo itakayochezeshwa na mwamuzi kutoka Benin, Djindo Louis Houngnandande, licha ya kuwa na umuhimu kwa kila timu, kutokana na Mazembe kupoteza mechi iliyopita ikiwa ugenini kwa mabao 2-1 mbele ya Al Hilal, baada ya awali kutoka suluhu nyumbani na Waalgeria, lakini Yanga inautaka zaidi mchezo huo kwa sasa ikiwa kama ndio fainali yao ya kupata dira ya msimu huu wa michuano hiyo.
Yanga Inafahamu kwamba kupoteza mchezo wa leo itawaweka kwenye wakati mgumu zaidi wa kufuzu robo fainali, kwani itasaliwa na mechi tatu ambazo italazimika kupambana izishinde zote ili kuvuna pointi tisa, kitu kinachoonekana ni kigumu kuliko kama itavuna pointi tatu mbele ya Mazembe.
Pia kushinda pekee haitatosha, kwani ni lazima pia iwaombee mabaya wapinzani wengine wa kundi hilo kuangusha pointi katika mechi baina yao.
Kwa sasa Yanga ina mechi nne za kucheza kuanzia leo zinazobeba pointi 12 ambapo mbili ugenini na nyingine nyumbani. Hesabu zao za kufuzu robo fainali zipo hapo kama ilivyo kwa TP Mazembe ndiyo maana wanawaambia wapinzani wao kwamba; “Kama kweli mnataka tushindane, basi weka mpira kati tupimane ubavu.”
ISHU IPO HAPA
Katika mechi mbili ambazo Yanga imepoteza, ilionekana kuwa na makosa mengi hasa eneo la ulinzi lililoanzia kiungo cha ukabaji hadi langoni, ikielezwa hiyo ikitokana na kukosekana kwa Khalid Aucho aliyekuwa majeruhi ambaye ndiye mfalme wa eneo hilo la kiungo cha ukabaji, licha ya uwepo wa Jonas Mkude ambaye hajacheza hata mechi moja hatua hii ya makundi.
Inaelezwa kwa sasa Aucho tayari amepona na amekuwa akifanya mazoezi na wenzake kitu ambacho kinatoa matumaini kwamba leo atakuwapo Stade de Mazembe ili kuweka utulivu wa kikosi.
Alipokosekana nafasi yake aliwekwa Duke Abuya aliyeshirikiana na Mudathir Yahya walionekana kushindwa kuziba pengo hilo, kutokana na kila mmoja kupenda kupanda juu eneo la kiungo cha ushambuliaji na kuwaachia msala mabeki Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Baka na Dickson Job aliyekosa mechi iliyopita.
Mbali na Aucho, eneo la beki ya kushoto Chadrack Boka amekosekana katika mechi mbili za kwanza alikuwa akiuguza majeraha, naye amerejea na kulifanya benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha Sead Ramovic kushusha presha kwani mbadala wake Nickson Kibabage alionekana kutofanya vizuri.
Nahodha msaidizi Dickson Job aliyekuwapo katika mchezo wa kwanza dhidi ya Al Hilal na kushuhudia kichapo cha mabao 2-0, aliwakosa MC Alger na nafasi yake akaanzishwa nahodha mkuu, Bakari Mwamnyeto, lakini haikusaidia Yanga kuepukana na kipigo cha pili mfululizo ikiwa ugenini Algeria.
Sasa anarejea katika eneo hilo ni wazi yale makosa ya awali yatakuwa yamefanyiwa kazi ili kuliweka lango lao salama.
Uwepo wa Job ni kama unawatisha zaidi TP Mazembe kwani nyota wa kikosi hicho anayecheza eneo la ushambuliaji, Suleman Shaibu amemtaja beki huyo kwamba anajua kukaba akiwa mtu makini katika kunusa hatari.
Shaibu ambaye kwa sasa anachezeshwa eneo la ushambuliaji kutoka golini, amesema alimuona Job wakati timu hizo zilipokutana katika Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-23 ambapo Yanga ilishinda nyumbani 3-1 na ugenini 1-0, ikamaliza kinara wa kundi wakati TP Mazembe ikiwa mkiani.
“Jamaa anajua sana kusoma hatari za wapinzani na hata ukiangalia mchezo ule ulivyokuwa alituzuia sana,” alisema Shaibu huku kocha msaidizi wa kikosi hicho, Pamphil Mihayo akisisitiza kwamba mchezo utakuwa mgumu kwani timu zote zinahitaji ushindi kujiweka kwenye nafasi nzuri.
ENEO LA MBELE
Mbali na hilo, hata eneo la ushambuliaji limekosa ubunifu kwani timu haitengenezi nafasi nzuri za kufunga jambo lililowafanya hadi sasa kushindwa kufunga bao lolote katika dakika 180 walizocheza kulinganisha na hatua za awali walipomaliza na mabao 17 wakicheza mechi nne tena bila ya kuruhusu nyavu zao kuguswa.
Yanga ilianza mechi za mchujo kwa kuikandika Vital’O ya Burundi kwa mabao 4-0 kisha kuishindilia 6-0 na ilipotinga raundi ya pili ikafanya kweli mbele ya CBE ya Ethiopia ikiifunga bao 1-0 ikiwa ugenini kisha kushinda 6-0 ziliporudiana na kuifanya Yanga ivuke mabao 17-0 ikiwa ni rekodi ya kuvutia kwa timu hiyo.
Katika mechi ya kwanza ya makundi, Yanga ilikuwa na takwimu nzuri dhidi ya Al Hilal licha ya kupoteza mchezo kwa mabao 2-0, kwani ilimaliza dakika 90 kwa kumiliki mchezo kwa asilimia 63, ikipiga mashuti 12 huku manne yakilenga lango la wapinzani.
Pia ilipata kona 12, mashambulizi yote hayo hayakuzaa matunda wakati wenzao katika mashuti sita, mawili pekee yalilenga lango na hayohayo yakazalisha mabao, hawakuwa na kona, hali iliyokuwa tofauti dhidi ya MC Alger, kwani Yanga haikuwa na mashambulizi mengi kwani ilipiga mashuti matatu pekee, hakuna lililolenga lango la wapinzani kitu ambacho kiliikwamisha timu iliyokuwa inahitaji ushindi.
Hivyo kwa leo ni wazi Yanga itashuka uwanjani ikiwa imesharekebisha eneo hilo ili kuhakikisha inapata mabao, kibarua kikiwa kwa Clement Mzize, Kennedy Musomba na Prince Dube ambao ndio washambuliaji, licha ya kupewa tafu na viungo washambuliaji kama Clatous Chama, Pacome Zouzoua, Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya, kama sio Farid Musa au Duke Abuya.
Kocha Ramovic kwa kipindi cha zaidi ya siku 25 alizokaa na timu hiyo tangu atambulishwe Novemba 25 mwaka huu, ni wazi ana jukumu kubwa la kufanya kurekebisha hali hiyo lakini pia marekebisho hayo yanapaswa kuwa ya haraka kwani muda hausubiri.
TP Mazembe kitakwimu katika mechi mbili za kwanza angalau imeonyesha ina uwezo wa kushambulia na kufunga kwani ina bao moja ililopata wakati ikifungwa 2-1 na Al Hilal ugenini, lakini nyumbani ilitoka 0-0 dhidi ya MC Alger.
MARA YA TANO
Katika mchezo wa leo, Yanga na TP Mazembe itakuwa ni mara ya tano kukutana kwao kwenye michuano ya Caf kwani tayari zimekutana mara nne zote zikiwa ni za makundi ya Kombe la Shirikisho tofauti na safari hii zinapokuana kwa mechi za Ligi ya Mabingwa.
Mwaka 2016 ilikuwa ni mara ya kwanza kukutana kwao ambapo TP Mazembe iliibuka kidedea mechi zote mbili ikianzia ugenini kushinda 1-0, kisha nyumbani ikaichapa tena Yanga 3-1 kabla ya Yanga kujibu mapigo msimu wa 2022-23 kwa kushinda nje ndani kama ilivyokuwa kwa Wakongomani hao.
Yanga ilianzia nyumbani na kushinda kwa mabao 3-1, kisha zilipenda kurudiana ikaibuka pia na ushindi wa bao 1-0 na leo itakuwa ni vita ya kutafuta mbabe baina yao, lakini kuvuna pointi tatu muhimu.
Utayari wa Yanga katika mchezo wa leo unamfanya mkuu wa msafara ambaye ni Mjumbe Kamati ya Utendaji na Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya klabu hiyo, Rodgers Gumbo kusema kila kitu kwa maana ya kuhakikisha timu inashinda kimefanyika.
“Tupo tayari kwa mchezo wa Jumamosi, kila kitu kinachohitajika kwa ajili ya kusaka ushindi katika mchezo huu kimefanyika ikiwamo hamasa kwa wachezaji,” alisema.
Ukiweka katika mzani, TP Mazembe inaonekana ni daraja la juu zaidi ya Yanga upande wa mashindano ya Caf kwani timu hiyo ina mataji 11 ambayo Ligi ya Mabingwa (5), Kombe la Shirikisho (2), Super Cup (3) na moja African Cup Winner’s ambapo michuano hiyo sasa haipo. Pia Mazembe ilishika nafasi ya pili katika michuano ya Klabu Bingwa Dunia mwaka 2010.
Yanga mafanikio yao makubwa zaidi katika michuano ya Caf tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1935 ni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023 ambapo ilipoteza kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger.
WATANI KWA MKAPA
Wakati Yanga ikiwa na kibarua hicho leo, watani wao wa jadi Simba wenyewe watashuka uwanjani kesho Jumapili katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika, dhidi ya vibonde wa Kundi A, CS Sfaxien ya Tunisia ambayo kama ilivyo kwa Yanga katika Ligi ya Mabingwa, imepoteza mechi zote mbili za awali.
Simba itakuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda katika mechi ya kwanza dhidi ya Bravos do Maquis ya Angola, kisha kupasuka wiki iliyopita ikiwa ugenini kwa mabao 2-1 kutoka kwa vinara wa kundi, CS Constantine, hivyo kesho itakuwa na kazi ya kuendelea ilipoishia.
Rekodi za Simba ikiwa Kwa Mkapa zinaipa nafasi kubwa ya kuzidi kuididimiza Sfaxien iliyopoteza nyumbani kwa bao 1-0 mbele ya CS Constantine kisha ikicheza ugenini dhidi ya Bravos ilikandikwa mabao 3-2.
Hivyo timu zote zinakutana zikizitaka zaidi pointi tatu kwa nia ya kujiweka pazuri kundi kabla ya kurudiana wiki ijayo na kujitengenezea mazingira mazuri.