Ule utamu wa miaka 1990 umeanza kurudi Zanzibar

WALE waliokuwa wakiamini soka la Zanzibar limeporomoka kiasi kwamba isingekuwa rahisi kuwavuta mastaa wa kigeni kwenda kucheza visiwani humo, pole yao.

Wadau na mashabiki wengi wa soka visiwani humo walipata hofu baada ya kuona wawekezaji wakubwa kama kina Naushad Mohamed, Turk ‘Mr White’ na wengine baadhi yao kutangulia mbele ya haki na wengine kuachana kabisa na ishu za kufadhili mpira na kujikita kwenye mambo mengine.

Kwa miaka ya 1990 Zanzibar ilishuhudiwa wakimiminika mastaa wenye majina makubwa kutoka Tanzania Bara, mataifa ya jirani na hata barani Ulaya.

Utabisha nini wakati katika miaka hiyo Zanzibar ilimshuhudia Mordon Malitoli beki na nyota wa kimataifa kutoka Zambia, Julian Albertov kutoka Bulgaria, pamoja na waliotoka Bara, Nico Bambaga, Victor Bambo, Athanas Michael na Edibily Lunyamila, winga aliyetikisa Uganda kwenye michuano ya Kombe la Kagame 1993 na 1999?

Hata hivyo, wakati Zanzibar ikijiandaa kuadhimisha Miaka 60 ya Mapinduzi yaliyofanyika Januari 12, 1964, wadau hao hao waliokuwa wakikata tamaa, kwa sasa wameanza kushuhudia vifaa vipya vikitua kwa fujo visiwani humo na kuwapa burudani.

Klabu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) hata zile za Ligi Daraja la Kwanza kwenye visiwa hivyo wamekuwa wakishindana kwa sasa kusajili wachezaji wa kulipwa kutoka nje ya Zanzibar na wamekuwa wakiwapa burudani mashabiki kwa soka tamu na vipaji walivyo navyo.


HADI JESHINI

Tofauti na miaka ya 1990, klabu binafsi na zile za wanachama ambazo sio za vikosi za majeshi, ndizo ziliokuwa zikishindana kuleta wachezaji wakali visiwani humo.

Malindi, Mlandege, Kikwajuni, Small Simba na nyingine zilikuwa zikishindana kuleta majembe ya maana ya kutoka nje ya visiwa hivyo na kuleta burudani tamu kwa mashabiki, huku timu hizo zikitisha kwenye michuano ya kimataifa.

Lakini kwa sasa mambo yamebadilika, hata timu za taasisi za kijeshi zimekuwa zikisajili nyota wa kigeni ambao wamekuwa wakizipigania timu hizo kuonyesha kuwa Miaka 60 ya Mapinduzi yameleta baraka katika soka la visiwani.

Haishangazi leo KMKM ambao ni watetezi wa Ligi ya Zanzibar ikiwa inamtegemea Mghana Ibrahim Is’haka ambaye anauwasha kwelikweli.

Mbali na Mghana huyo, lakini kuna timu ina wachezaji wa kigeni kama Mbo Mbongu Ephraim na Djuma Mushinga Cedan wote kutoka Congo Brazzaville pamoja na Nurudeen Abiola Biliaminu, Akintunde Taiwo Wasiu wote kutoka Nigeria, wakati JKU yenyewe ina Mcameroon, Jean Jospin Angola Manti.

Sio wachezaji tu, lakini klabu za majeshi kwa sasa zimefikia hatua ya kuajiri makocha kutoka nje ya visiwa hivyo ambao hata malipo yao sio ya kitoto kwani KMKM ina Masoud Djuma, kocha wa zamani wa Simba na AS Kigali ambaye ni raia kutoka Burundi.

Msimu uliopita KVZ ilikuwa na Amri Said, kocha wa zamani wa Simba, Lipuli, Mbao aliyeifanya timu iwe tishio kabla ya mambo kugeuka mwishoni na ubingwa kurejea kwa KMKM wakati duru la kwanza kulikuwa na kila dalili maafande hao walikuwa wakienda kutwaa ubingwa.


URAIANI SASA

Kwa timu za uraiani kwa sasa mambo yamezidi kunoga, kwani zimekuwa zikishindana kuleta wachezaji wakali wa nje ya Zanzibar kama ilivyo miaka ya nyuma.

Malindi na Mlandege wanarejesha enzi zao za kushindana kuleta mastaa ambapo kwa sasa, mabingwa hao wa zamani wa Zanzibar vikosini mwao kuna wachezaji kadhaa wa kigeni.

Malindi ina straika Mnigeria, Patrick Jude Chisom, huku Mlandege juzi kati tu imeshusha straika raia wa Jamaica ambaye ameonyesha makali kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 kwa kuanza kwa kufunga bao kwenye sare ya 1-1 dhidi ya Chipukizi.

Mjamaica huyo ambaye amezichezea klabu mbalimbali za nchini kwao pamoja na Marekani ambako pia ana uraia pamoja na Hispania amesajiliwa kwenye dirisha dogo na uongozi umetamba ni moja ya silaha ya kurejesha makali ya watetezi hao wa Kombe la Mapinduzi iliyotwaa msimu uliopita.


KITU CHA KUFANYA

Kutokana na kasi hiyo ya kushushwa kwa mastaa wa kutoka nje ya Zanzibar, mashabiki na wadau wamekuwa na matumaini makubwa muda sio mrefu lile soka tamu na la ushindani kwa timu za visiwa hivyo itarejea, lakini ikielezwa ni lazima kifanywe kitu mambo yawe bam’bam.

Baadhi ya wadau na wapenzi wa soka visiwani wanasema Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ambalo juzi kati limeingia makubaliano na Kampuni ya Zanzibar Digital Limited ili kulifanya liende na wakati, inapaswa kulegeza masharti kwa wafadhili na wadhamini ili wajitokeze kwa wingi na kuinua soka.

Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) udhamini iliyonayo kwa sasa hautoshi kuzifanya timu nyingi kumudu gharama za kuwalipa wachezaji na makocha wa kigeni kama klabu za Tanzania Bara zinavyofanya kwa vile wenzao wana udhamini mnono kutoka Azam Media na Benki ya NBC mbali na wale binafsi wa klabu kutoka kampuni ya Bia na yale ya kubeti ambayo hayaruhusiwi visiwani humo.

Wametolea mfano ongezeko la zawadi za michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 imechochea ushindani sio kwa klabu shiriki tu, lakini hata kwa wachezaji kutokana na kuwepo kwa zawadi za wachezaji bora na wale wenye nidhamu kwa kila mechi tangu hatua ya makundi.

‘Wachezaji wamekuwa na mzuka wa kupambana kwa kujua kuna zawadi kila baada ya mechi kuna ile ya Nyota wa Mchezo anayepewa Sh500,000 na ile ya Mchezaji Mwenye Nidhamu anayebeba Sh200,000, mbali na zawadi za ubingwa zilizoongeshwa kutoka Sh50 milioni za ubingwa hadi 100 milioni na 70 milioni za mshindi wa pili badala ya Sh30 milioni ni chachu michezoni,” alisema mmoja wa viongozi wa klabu ya KVZ.

Kiongozi huyo alisema hata kwenye Ligi Kuu kukiwa na wadhamini wengi watakaokuwa wakimwaga fedha zinawarahisishia kazi klabu kusajili wachezaji wanaowataka wenye ubora na uwezo wa kuzibeba mbali na kuifanya Ligi iwe na ushindani na kutoa wawakilishi watakaoibeba nchi mechi za kimataifa.


DK MWINYI ATAJWA

Wadau wamesema kasi na ufanisi wa Serikali ya Awamu ya Nane iluiyo chini ya Dk Hussein Ali Mwinyi katika kuwekeza kwenye sekta mbalimbali ikiwamo michezo ni jambo lililofungua njia ya kuanza kurejesha makali katika soka la visiwani hivyo.

Ukarabati uliofanywa na serikali hiyo kwenye viwanja mbalimbali vya soka vikiwamo vya Gombani Pemba na Amaan Unguja uliobadilisha muonekano wa viwanja hivyo imeelezwa ni moja ya matunda ya kasi na kazi nzuri ya serikali ya Dk Mwinyi.

Wadau wamesema kama kuna viwanja vizuri, bila ya kuwa na klabu za ushindani inawezekana ikawa haina maana, ndio maana wanaomba udhamini na uwekezaji kwenye soka la Zanzibar liongezwe ili soka hilo lilirudi kwenye ubora wake kama ilivyokuwa miaka ya 1970 hadi 1990.