UKWELI NDIVYO ULIVYO: Utamu wa Ligi yetu unatibuliwa hapa tu

Sunday February 21 2021
ukweli pic 1

HAKUNA ubishi Ligi Kuu huwa ina utamu wake. Haijalishi ni Ligi Kuu ya nchi gani. Utamu wa Ligi Kuu uzidishwa na mbio za ubingwa.

Iangalie tu, Ligi Kuu ya England (EPL) ilivyonoga. Kwa ilipofikia sasa inazidi kuifanya ifuatiliwe zaidi na mashabiki duniani. Mashabiki wapo roho juu tu kwa sasa.

Hata kule Hispania na ligi nyingine kubwa Ulaya.

Timu zote zinawapa raha mashabiki wao, huku presha ikiwa kubwa kwa timu hizo katika vita yao ya kuwania ubingwa msimu huu, lakini ni nadra kusikia timu zikilalamika juu ya waamuzi ama kutuhumu kufanyiana hila. Timu inapoteza ama kushinda kama sio kutoka sare huku ikiridhika.

Waamuzi nao wanajitahidi kuchezesha kwa haki. Hatujawahi kusikia eti kuna shinikizo la viongozi wa FA zao kutaka timu fulani ndio ziwe bingwa.

Bingwa atapatikana kwa kile watakachovuna uwanjani kwa maandalizi yao ya kila msimu.

Advertisement

Hii ni tofauti na Ligi Kuu Bara. Kila msimu lazima usikie malalamiko dhidi ya waamuzi. Malalamiko ya timu kwa timu na malalamiko dhidi ya viongozi wa FA. Hii ni kwa vile soka letu limekuwa likiendeshwa kimaghumashi sana. Usimba na Uyanga umelitibua soka letu na kusababisha kusiwe na kuaminiana tena.

Kibaya zaidi ni kuna viongozi waliopo ndani ya FA wamekuwa wakishindwa kuficha hisia na mapenzi yao kwa timu hizo kubwa nchini. Wengine wanadiriki kusema kabisa timu yangu ikifungwa naumia sana! Hii ni aibu kubwa na wala sio uadilifu kwa kiongozi mwenye mamlaka. Ni kweli ni jambo gumu kukosekana mtu mwenye mrengo wa klabu hizo, ila uadilifu ni kuficha hisia katika kusimamia na kutenda haki.Hata ukija kwa waamuzi wanaoteuliwa na kuchezesha mechi za Ligi wana itikadi za Usimba na Uyanga. Kuna wakati hata kama wanafanya makosa ya kibinadamu, bado wanahukumiwa kwa sababu ya unazi wao kwa klabu hizo kubwa nchini.

Hii ni kwa sababu hawafichi hisia za mapenzi kwa timu hizo kubwa. Wamekuwa wakitamba vijiweni. Baadhi ni marafiki zetu wanaosema wazi kile ambacho hufanyika nyuma ya pazia. Achana na hayo, hata kwenye klabu za mikoani, nazo zimegawanyika ndani kwa ndani ya itikadi ya timu hizo kubwa.

Uongozi wa klabu unakuwa siriazi katika mechi dhidi ya timu moja wapo kati ya hizo kubwa, lakini wakapuuza wanapovaana na wengine. Wachezaji wa hizi timu wanasema kuna utofuati wa maandalizi dhidi ya Simba na Yanga na jinsi wanavyoelekezwa na viongozi wao kulingana na mrengo na itikidai zao.

Soka letu hapa litakuwapo lina ubora kama linavyosifiwa?!

Hata mashabiki nao wa timu za mikoani siasa za Simba na Yanga zimewaingia mpaka wamezitelekeza klabu za mikoani yao. Huwa wapo tayari kuona Yanga au Simba zinashinda dhidi ya timu zao za mikoani kwa hali yoyote, lakini wala hawaumii kuona timu zao zikishuka daraja.

Hapa ndipo panapoiharibu soka letu na ndiko kunakoifanya ligi yetu iwe ya ovyo hata kama wenyewe tunajisifia ni ligi bora.

Kinachoharibu zaidi ni zile hisia asilimia kubwa ya matokeo yanayopatikana uwanjani huwa yanatengenezwa na kupikwa nje ya uwanjani kwa manufaa ya baadhi ya timu.

Yapo madai ya timu kubwa licha ya kufanya usajili wa mamilioni ya shilingi, bado hushindana kununua wachezaji wa timu pinzani. Wanatuhumiwa pia kutumia hila kuwahonga marefa ili kupata matokeo uwanjani.

Mbaya zaidi tuhuma hizi zimeenda mpaka kwa viongozi wa FA nao kushiri kuhakikisha timu wanazozishabikia zinapata afueni ili kuona zinapata matokeo au kutwaa ubingwa.

Kocha Abdallah Kibadeni enzi akiifundisha Kagera Sugar aliwahi kulisema hili na kufikia kuwa tayari Takukuru waende kwake awape ushahidi. Pia rejea matukio ya kusimamishwa kwa kina Deo Munishi ‘Dida’ na wenzake wakiwa Azam enzi hizo kwa tuhuma za kuhongwa na moja ya klabu kubwa nchini ili wafanye hujuma.

Rejea mkasa wa Nsa Job alipofichua alipohongowa ili kuisaidia timu moja kubwa kupata matokeo uwanjani. Utakataa vipi wakati Ulimboka Mwakingwe alikamatwa kwa tuhuma za kupewa hela na mmoja wa viongozi wa klabu moja kubwa nchini ili kumhonga kipa kipa wa Mtibwa Sugar ili kuisaidia timu hiyo kupata matokeo ya hila?

Kwa matukio kama haya na huu ulevi wa hizi timu za urithi, kwa nini ligi yetu isiwe ya ovyo. Timu zinajisifia kuwa na vikosi vipana na nyota wenye uwezo, lakini zinajua wazi namna gani zinavyopata matokeo uwanjani kwa hila. Wapo viongozi wanaosimamia soka letu wanatuhumiwa kushiriki kwenye hila hizi za kupika matokeo uwanjani kwa kuwatumia marefa, halafu tunasema ligi yetu ni bora?

Hata kama tuhuma hizo huwa zinatolewa bila ushahidi na wakati mwingine kwa hasira na kama njia ya kuficha udhaifu wa viongozi wa timu husika, lakini kuna wakati huwa kuna ukweli kwa namna mambo yanavyoonekana.

Miezi kadhaa iliyopita nakumbuka Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete aliwahi kulisema hili juu ya viongozi wa wanaosimamia soka na hata wenye mamlaka ndani ya mikoa, kushindwa kuficha hisia zao kwa timu wanazoshabikia na kuziumiza zile ambazo hawazishabikii kwa kusahau kuwa wao ni viongozi wa wote.

Mheshimiwa Kikwete hakulisema lile kwa bahati mbaya, anajua vyema siasa za Simba na Yanga zilivyo.

Amekuwa mwanamichezo kwa muda mrefu na anajua kila kitu tangu hata hajawa Rais wa Tanzania na hata sasa akiwa amestaafu.

Kama na hili unalipinga, sikiliza malalamiko ya sasa ya Yanga dhidi ya TFF ya Wallace Karia na Wilfred Kidau halafu rejea yale yaliyokuwa yakitolewa na Simba dhidi ya TFF ya Jamal Malinzi na Celestine Mwesigwa, ndio utajua soka letu bado lina safari ndefu!

Cha ajabu malalamiko na haya mambo yanayochafua taswira ya ligi yetu hayakusikika sana enzi za utawala wa Leodeger Tenga. Jiulize kwa nini?

Hii ni kwa sababu Tenga licha ya kufahamika ana mrengo gani katika soka la Tanzania, lakini alikuwa akiiendesha TFF kwa misingi na utawala bora usiopendelea ama kuegemea kokote.

Pia hata alipokuwa akiona mambo hayaendi vizuri, ilikuwa rahisi kwake kujitokeza na kusimama kidete ili watu wapate burudani.


Imeandikwa na Badru Kimwaga

Advertisement