Ukizubaa Ligi Kuu Bara umeachwa

Muktasari:
- Gepu hilo la pointi Simba imepambana kulipunguza na kufanikiwa kwani awali zilikuwa 13 ilipokuwa na viporo vya mechi nne.
BAADA ya Simba kuilaza Singida Black Stars kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumatano wiki hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar, hivi Wekundu wa Msimbazi sasa wako nyuma ya Yanga kwa tofauti ya pointi moja.
Gepu hilo la pointi Simba imepambana kulipunguza na kufanikiwa kwani awali zilikuwa 13 ilipokuwa na viporo vya mechi nne.
Kitendo cha Simba kuichapa Singida Black Stars, timu inayoonekana kuwa ngumu kufungika kutokana na aina ya kikosi ilichonacho cha wachezaji wa kimataifa wenye rekodi nzuri, kimefanya vita ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu kuibuliwa upya na kuonekana kuwa ya moto sana.
Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu huu 2024-25 iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Juni 15 imepangwa kuchezwa mechi ya duru la pili itakayozikutanisha Yanga na Simba kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.
Huu ni mchezo wa kiporo baada ya ule wa awali uliotarajiwa kuchezwa Machi 8, 2025 kuahirishwa kiutata na Bodi hiyo kufuatia sintofahamu zilizotokea ikiwamo madai ya Simba kuzuiwa kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla ya mchezo.
Kuahirishwa kwa mchezo huo awali, kumefanya mambo mengi kuibuka ikiwamo Yanga kupeleka kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) jijini Lausanne, Uswisi kutokana na kutoridhishwa na uamuzi huo, lakini CAS iliirudisha katika mamlaka za soka za ndani huku Yanga ikiibuka kwa kusema: “Hatuchezi.”
Mpaka sasa, msimamo wa Yanga ndiyo huo kutocheza mechi hiyo ya Juni 15 na ipo tayari kwa jambo lolote litakalotokea huku kanuni za ligi zikibainisha adhabu kwa timu itakayoshindwa kufika uwanjani kwa mechi moja itakatwa pointi 15 na faini.
Kwa namna msimamo ulivyo, ni wazi mchezo wa Juni 15 kama utafanyika kulingana na ratiba inavyoonyesha, basi unaweza kuamua timu ipi inakwenda kubeba ubingwa msimu huu. Hiyo inatokana na ratiba ya mechi zilizobaki kwa Yanga na Simba kuonekana kutokuwa ngumu sana kwao kulingana na rekodi zilivyo.
Akizungumzia mchezo huo wa Juni 15 ambao umekuwa na pande mbili za wanaocheza na hawachezi, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania, Steven Mnguto, alisema: “Tumeshapanga tarehe, basi tusubiri.”

UBINGWA
Yanga inapambana kutetea ubingwa iliouchukua kwa misimu mitatu mfululizo, inasaka rekodi ya Simba ya misimu ya karibuni ilipochukua taji hilo mara nne mfululizo kuanzia 2017-2018, 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021. Baada ya hapo ndipo Yanga ikachukua utawala
Kitendo cha Yanga kuendelea na msimamo wake wa kutocheza Juni 15, huku ratiba ikiendelea kama ilivyo, maana yake Simba itapewa pointi tatu na mabao matatu, huku Yanga ikikabiliwa na adhabu ya kupokwa pointi 15 ambazo moja kwa moja itafanya kupoteza nafasi ya kubeba ubingwa kwani itakuwa nazo 58 na Simba 75 zikibaki mechi mbili. Yanga ikishinda mechi hizo mbili zitakazobaki, itamaliza na pointi 64 kwenye nafasi ya pili.
Kama mchezo huo utafanyika, basi matokeo yatatoa picha ya timu itakayokwenda kubeba ubingwa. Ikiwa sare, Yanga itakuwa na pointi 74 na Simba 73. Mbio zitabaki kwenye mechi mbili ambapo moja nyumbani na nyingine ugenini.
Simba itakwenda ugenini kukabiliana na KenGold kisha kumalizia nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, timu hizo zote zimeshuka daraja na rekodi zinaonyesha duru la kwanza Simba ilishinda zote. Iliichapa KenGold 2-0, ikaikanda Kagera 5-2.
Yanga itaifuata Tanzania Prisons na kumalizia nyumbani dhidi ya Dodoma Jiji. Duru la kwanza, Yanga iliichapa Tanzania Prisons 4-0, pia ushindi kama huo dhidi ya Dodoma Jiji.

NAFASI YA TATU
Licha ya kwamba timu zinazowania nafasi hiyo kuwa na uhakika wa kucheza Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, lakini kuna heshima inasakwa.
Kwa sasa Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 57, huku Singida Black Stars ni ya nne na pointi 53. Zimebaki mechi mbili kwa kila moja.
Azam inahitaji ushindi katika mechi moja kati ya mbili zilizobaki ili kujihakikishia nafasi ya tatu kwani ikifikisha pointi 60, haziwezi kufikiwa na Singida Black Stars.
Katika msako wa pointi hizo tatu, Azam inaweza kumaliza kazi mechi ijayo dhidi ya Tabora United. Licha ya kwamba duru la kwanza Azam ilipoteza ugenini kwa mabao 2-0, lakini nyumbani ina rekodi nzuri, imewahi kushinda 4-0 mara ya mwisho. Baada ya hapo, Azam itakwenda ugenini kumalizana na Fountain Gate.
Singida Black Stars mechi mbili zilizobaki itakuwa ugenini dhidi ya Dodoma Jiji kisha nyumbani ikiikaribisha Tanzania Prisons.

PLAY OFFS
Kwa ujumla hadi sasa, ukiacha vita ya kuwania ubingwa, pia kuna timu zinapambana zisiangukie mtego wa kucheza mechi za mtoano kuwania kubaki kwenye ligi kwa msimu ujao baada ya Kagera Sugar na KenGold kushuka daraja mapema.
Timu ambazo zinapambana zisiangukie mechi za mtoano (play offs) zipo tisa kuanzia inayoshika nafasi ya sita hadi 14 kwenye msimamo. JKT Tanzania iliyopo nafasi ya sita ikiwa na pointi 35, iwapo itapoteza mechi mbili ilizo bakiza, huku Pamba Jiji na Tanzania Prisons zenye pointi 30 katika nafasi ya 12 na 13 zikishinda mechi zake mbili zinaweza kuwashusha wanajeshi hao.
Dodoma Jiji iliyo katika nafasi ya saba kwa pointi 34, Mashujaa nafasi ya nane kwa pointi 33, Coastal Union nafasi ya tisa kwa pointi 31 sawa na Namungo, huku Pamba Jiji na Tanzania Prisons zikiwa zimevuna pointi 30 kila moja wakati Fountain Gate ya 14 kwa pointi 29, ndiyo timu zilizopo kwenye mtego huo.
Kwa namna msimamo ulivyo, JKT Tanzania inahitaji pointi moja tu kuwa salama ambapo mechi mbili zote itacheza ugenini dhidi ya Pamba Jiji na Mashujaa ambazo nazo zote zipo kwenye kuukwepa mtego wa play offs.
Dodoma Jiji, Mashujaa na KMC, nazo zinahitaji kushinda mechi mojamoja kati ya mbili zilizobaki ili kufikisha pointi kuanzia 36 ili kuwa salama.
Timu ambayo ipo kwenye hatari zaidi ya kubaki kwenye playoffs ni Fountain Gate ambayo inahitaji kushinda mechi zote mbili dhidi ya Coastal Union (ugenini) na Azam (nyumbani) ili kufikisha pointi 35, kisha kuziombea Pamba Jiji, Namungo na Coastal zisishinde mechi yoyote ili yenyewe itoke huko chini.
Mbaya zaidi, Namungo mechi mbili zilizobaki zote itacheza nyumbani dhidi ya timu zilizoshuka daraja, Kagera Sugar na KenGold ambazo unaweza kusema hazina zinachotafuta.
Pamba Jiji nayo mechi mbili zote itacheza nyumbani dhidi ya JKT Tanzania na KMC, licha ya kwamba zote kila moja inatafuta jambo lake, lakini Pamba Jiji nyumbani mechi tano za mwisho haikuwa na matokeo mabaya zaidi, imeshinda mbili sawa na sare, ikipoteza moja.
Kumbuka pia Coastal itaikaribisha Fountain Gate mechi inayofuata, hivyo moto utawaka si kitoto, kisha Coastal kumalizana na Tabora United, mechi zote zitachezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kocha Mkuu wa Tanzania Prisons, Aman Josiah alisema vita ni kubwa japo hadi sasa wana uhakika wa kucheza play offs, lakini hesabu zao ni kuondoa presha hiyo ili kumaliza salama ligi.
“Hatutaki kusubiri ishu ya play offs, tunataka tumalize mapema ligi tujiandae na msimu ujao, tunaenda kujipanga kwa mechi zijazo tukianza na Yanga nyumbani kisha Singida Black Stars ugenini tukitafuta pointi sita,” alisema Josiah.
Kocha Msaidizi wa Pamba Jiji, Mathias Wandiba alisema mechi zilizobaki dhidi ya JKT Tanzania na KMC ni kufa au kupona akieleza kuwa wanaenda kusuka kikosi kwa muda huu ligi imesimama ili kuwa bora.
“Hatutaki hata sare kwenye mechi hizo na bahati nzuri tutakuwa nyumbani Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kuhakikisha hatuachi mtu, pointi sita ni muhimu sana kwetu ili kubaki salama Ligi Kuu,” alisema Wandiba, huku kocha wa Coastal Union, Joseph Lazaro akisema dakika 180 zilizobaki ni za utulivu na ushindi.
“Hatuko salama sana japokuwa vita si kwetu tu, timu nyingi presha ni kubwa hivyo tunaenda kutumia mapumziko haya kusahihisha makosa hasa eneo la ushambuliaji ili kushinda michezo iliyobaki,” alisema Lazaro.
Kwa sasa ligi imesimama, ukiondoa mechi ya kiporo Yanga dhidi ya Simba iliyopangwa kuchezwa Juni 15, ligi itaendelea rasmi Juni 18 mwaka huu kwa kuchezwa raundi ya 29, kisha Juni 22 ni raundi ya 30 kuhitimisha msimu wa ligi.

VIPIGO VIKUBWA
Ukiangalia katika timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara msimu huu, Dodoma Jiji, Fountain Gate na Kagera Sugar, zinaongoza kwa kupokea vipigo vikubwa hadi sasa zikiwa zimebaki raundi mbili kuhitimisha msimu wa ligi hiyo.
Mbali na timu hizo, nyingine zilizopokea vipigo vikubwa msimu huu ni KMC, Pamba Jiji, Tanzania Prisons, KenGold, Mashujaa na JKT Tanzania.
Dodoma Jiji inayoshika nafasi ya saba kwenye msimamo ikikusanya pointi 34, katika mechi 28 ilizocheza imepoteza tatu kwa vipigo vikubwa huku ikiruhusu mabao mengi zaidi kupitia vichapo hivyo ambayo ni 15. Ilianza kwa kufungwa 4-0 na Yanga, kisha Simba 6-0 na Azam 5-0.
Fountain Gate inafuatia kwa kupoteza mechi tatu kwa vipigo vikubwa ikiruhusu mabao 13, ikifungwa na Yanga mara mbili 4-0 na 5-0, pia ikafungwa 4-0 na Simba.
Wakati timu hizo mbili zikiruhusu idadi hiyo kubwa ya mabao kwa vipigo vikubwa, Kagera Sugar ambayo pia imepokea vipigo vitatu vikubwa, angalau imetikisa nyavu za wapinzani wake.
Kagera Sugar iliyoshuka daraja, imepoteza mechi tatu kwa vipigo vikubwa ikiruhusu mabao 13 huku yenyewe ikifunga manne. Ilifungwa 5-2 na Simba, 4-2 dhidi ya Azam na 4-0 kwa Yanga.
KMC pia imepokea vipigo vikubwa viwili ikifungwa 4-0 na Azam, kisha ikachapwa 6-1 na Yanga, huku Pamba Jiji nayo ikifungwa 4-0 na Yanga na ikapokea kichapo cha mabao 5-1 mbele ya Simba. Tanzania Prisons imefungwa 4-0 na Yanga, kisha kipigo kama hicho ikikipata kwa Azam.
KenGold ambayo nayo imeshuka daraja, imeshuhudiwa mechi moja pekee ikipokea kichapo kizito kutoka kwa Yanga cha mabao 6-1, wakati Mashujaa ikichapwa 5-0 na Yanga, huku Tabora United ikiipiga JKT Tanzania mabao 4-2.

YANGA WABABE
Wakati hali ikiwa hivyo, upande mwingine Yanga ndiyo inayoongoza kwa kugawa dozi nzito kwa wapinzani ikifanya hivyo mara tisa ikizifunga Fountain Gate (4-0 na 5-0), KMC (6-1), Pamba Jiji (4-0), Kagera Sugar (4-0), Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), KenGold (6-1) na Mashujaa (5-0).
Simba na Azam, zimetoa vipigo vikubwa mara nne kila moja. Simba imezifunga Fountain Gate (4-0), Pamba Jiji (5-1), Kagera Sugar (5-2) na Dodoma Jiji (6-0). Kwa upande wa Azam, imezifunga KMC (4-0), Kagera Sugar (4-2), Tanzania Prisons (4-0) na Dodoma Jiji (5-0).
SIMBA NYUMBANI, YANGA UGENINI
Ukiangalia msimamo wa ligi kwa matokeo ya nyumbani pekee hadi sasa, Simba inaongoza kwa kukusanya pointi nyingi ambazo ni 35 ikifuatiwa na Yanga (33), kisha Azam (32), huku Singida Black Stars na Dodoma Jiji zina 28 kila moja.
Yanga inaweza kuipiku Simba kwani imebakiwa na mechi mbili nyumbani ikishinda zote itakusanya pointi 39 ambazo Simba haiwezi kuzifikia kwani ina mechi moja tu nyumbani. Ikishinda itakuwa na 38. Yanga nyumbani imebakiza dhidi ya Simba na Dodoma Jiji, huku Simba nyumbani ikiwa ni dhidi ya Kagera Sugar.
Kwa upande wa ugenini, Yanga ndiyo wakali wao hadi sasa ikikusanya pointi 40, inafuatia Simba yenye 37, Azam na Singida Black Stars kila moja inazo 25.
KenGold imekusanya pointi mbili pekee, ikiwa ndiyo timu yenye matokeo mabaya zaidi ugenini kufuatia kutoshinda mechi yoyote. Timu nyingine ambazo hazijaonja ladha ya ushindi ugenini msimu huu ni Coastal Union, Dodoma Jiji na Kagera Sugar.
Hapa Simba inaweza kulingana na Yanga kama itachanga vizuri karata zake kwani imebakiza mechi mbili ugenini dhidi ya Yanga na KenGold, ikishinda zote itakusanya pointi 43 na kama Yanga nayo ikishinda moja iliyobaki dhidi ya Tanzania Prisons.
Upande wa mabao, Simba nyumbani imefunga 38, Yanga 36, hizo ndiyo timu zilizofunga sana upande huo. Kwa ugenini Yanga imefunga mabao 35, Simba 25, hapa inaonyesha namna Yanga ilivyokuwa na makali zaidi viwanja vya ugenini kulinganisha na timu yoyote ikiipiga gepu Simba la mabao 10.

UFUNGAJI BORA
Katika mechi zilizobaki, kuna vita ya kuwani ufungaji bora, tuzo ambayo mtetezi wake ni Stephane Aziz KI aliyekuwa akiitumikia Yanga kabla ya kuondoka hivi karibuni na kutua Wydad ya Morocco. Aziz KI aliyefunga mabao 21 msimu uliopita na kuwa kinara wa ligi, ameondoka akiwa na mabao tisa, akiachwa sita na kinara wa sasa Jean Charles Ahoua wa Simba aliyefunga 15.
Kwa sasa vita iliyobaki ni kuwania tuzo hiyo ikiwahusisha wachezaji saba waliofunga mabao kuanzia kumi na kuendelea. Ukimuweka kando Ahoua ambaye ni kinara, wanafuatia washambuliaji wa Yanga, Clement Mzize na Prince Dube ambao kila mmoja amefunga 13.
Chini yao ni washambuliaji wa Simba, Steven Mukwala na Leonel Ateba kila mmoja akifunga mabao 12, kisha Jonathan Sowah wa Singida Black Stars aliyefunga 11 akifuatiwa na mshambuliaji mwenzake wa Singida Black Stars Elvis Rupia (10).

ASISTI
Hapa mkali wao ni Feisal Salum wa Azam mwenye asisti 13, akiwaacha mbali kidogo washindani wake kwani anayefuatia ni Maxi Nzengeli na Pacome Zouzoua wanaocheza Yanga, kila mmoja anazo tisa. Ahoua na Dube wanazo nane kila mmoja.
Msimu uliopita, Kipre Junior aliyekuwa Azam, aliibuka kinara wa asisti akiwa nazo tisa, akifuatiwa na Aziz KI (8), huku Lusajo Mwaikenda (Azam), Feisal Salum (Azam), Kouassi Yao (Yanga) na Clement Mzize (Yanga) wakimaliza na saba.

CLEAN SHEET
Moussa Camara wa Simba anahitaji kucheza mechi mbili tu kati ya tatu bila ya kuruhusu bao ili kuweka ufalme wake kufuatia sasa kuwa kinara wa clean sheet akifikisha 17. Anachuana vikali na Djigui Diarra wa Yanga mwenye 15. Patrick Munthari wa Mashujaa ana clean sheet 11, wakati Mohamed Mustafa (Azam) na Yona Amosi (Pamba Jiji) wanafuatia wakiwa nazo 10.
Msimu uliopita, Ley Matampi aliyekuwa Coastal Union alimaliza na clean sheet 15 akiwa kinara akifuatiwa na Diarra (14).