Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujio mpya wa Mr Money ngumi za kulipwa duniani

Muktasari:

  • Mayweather ambaye amepigana mapambano 50 akishinda yote na kati ya hayo 27 akiwachapa wapinzani wake kwa knockout, wiki mbili zilizopita alikubaliana na mkongwe mwingine wa ngumi za kulipwa, Mike ‘Iron’ Tyson, kuzichapa katika pambano lisilo la ubingwa litakalopigwa Aprili 25, 2026 jijini Kinshasa, DR Congo, huku pia kukiwa na lile la mpinzani wake wa muda wote, Manny Pacquiao ‘Pac Man’, litakalofanyika Septemba 19, 2026.

OHIO, MAREKANI: FLOYD Mayweather Jr maarufu kama Mr Money, ameamua sasa kufanya kweli katika ulingo wa ngumi za kulipwa duniani, akifanya mazoezi ya ‘kufa mtu’ nyumbani kwake huko Las Vegas, Nevada, Marekani, akijiandaa kwa mapambano mawili ambayo tayari keshatangaza kwamba atazichapa mwaka huu.

Mayweather ambaye amepigana mapambano 50 akishinda yote na kati ya hayo 27 akiwachapa wapinzani wake kwa knockout, wiki mbili zilizopita alikubaliana na mkongwe mwingine wa ngumi za kulipwa, Mike ‘Iron’ Tyson, kuzichapa katika pambano lisilo la ubingwa litakalopigwa Aprili 25, 2026 jijini Kinshasa, DR Congo, huku pia kukiwa na lile la mpinzani wake wa muda wote, Manny Pacquiao ‘Pac Man’, litakalofanyika Septemba 19, 2026.

Pambano la Mayweather na Tyson linafanyika Afrika katika kile kilichobatizwa ‘Part Two ya Ngumi za Karne’, likilenga kuadhimisha kile kilichofanywa na Muhammad Ali na George Foreman waliozichapa DR Congo Oktoba 30, 1974 katika pambano maarufu lililofahamika kama ‘Rumble in the Jungle’ linalotajwa kuwa bora kuliko mapambano ya ngumi yaliyowahi kufanyika.

Lakini, wakati unasikilizia wakongwe Mayweather na Tyson kuzichapa katika ardhi ya Afrika, Mr Money amekubaliana fasta na bingwa wa dunia wa kickboxing, Mike Zambidis, wapimane ubavu Juni 27 mjini Athens, Ugiriki katika Uwanja wa OAKA Arena kusaka nani bora kati yao baada ya ubishi ulioanzia mitandaoni.

Kwa miaka mingi Zambidis, bingwa wa kickboxing mara 18, amekuwa akitamba kwamba Mayweather hamuwezi ulingoni katika ngumi, na kila mara amekuwa akimuomba wazichape, lakini awali hakuwa akimjibu kabla ya kukubaliana na hoja yake hivi karibuni.

Pia anatarajiwa kurudiana na mpinzani wake mkubwa wa muda mrefu, Pacquiao, katika tukio kubwa jijini Las Vegas mwezi Septemba, ambapo atarejea rasmi kwenye ndondi za kulipwa.

Na katika kusherehesha kukubaliana na Mayweather, Zambidis, mkongwe huyo wa K-1 kutoka Ugiriki, alichapisha bango la pambano likimuonyesha wawili hao wamethibitishwa kuzichapa Juni 27. Na tangu wakati huo Mayweather ameeleza mara kibao kwamba anakwenda kuuthibitishia ulimwengu wa masumbwi kuwa yeye ndiye “mfalme” wa mabondia wote - kauli ambayo amekuwa akiitoa hadharani mara kwa mara.

Hivi karibuni bondia huyo aliandika kwenye Instagram: “2026 tayari unaonekana kuwa mwaka wa kusisimua kwangu. Niko njiani kuja kuburudisha!! Athens, Ugiriki. Jiandaeni kwa pambano la maonyesho lisilo na kifani. Majira haya ya kiangazi yatakuwa ya mapambano ya kihistoria. Juni ni mwezi ambao historia itaandikwa. Nguvu tofauti. Viwango tofauti.”

Zambidis sasa ana umri wa miaka 45 na kama ilivyo kwa Mayweather, tayari amevuka kilele chake cha ubora na uhimilivu wa kimwili katika misukosuko ya mapigano ulingoni. Hajapigana tangu 2015, ambapo pambano lake la mwisho katika kickboxing lilimalizika kwa ushindi wa pointi dhidi ya Steve Moxon katika tukio la kuaga.

Hivyo basi, dhidi ya Mayweather litakuwa pambano lake la kwanza ndani ya miaka 11 na linaweza kufanyika katika ndondi za kulipwa chini ya sheria za kawaida za mchezo huo.


VS TYSON NA PAC MAN

Bila shaka Mayweather anaonekana kuzichapa na Tyson, jambo ambalo tayari linaonekana kuwa la ajabu kutokana na mpinzani wake huyo kupotezwa vibaya na Jake Paul mwaka jana.

Kurejea rasmi kwa Mr Money kwenye ndondi za kulipwa akiwa na umri wa miaka 49 kutafanyika atakapozichapa na Pac Man. Inaelezwa kwamba mwaka huu huenda ukawa na mauzo makubwa ya haki za matangazo na tiketi za mchezo huo kutokana na mapambano hayo, ikizingatiwa kwamba kila mara anapokuwa anazichapa Mayweather mzunguko wa fedha huongezeka.

Mayweather atakuwa na matumaini ya kulinda rekodi yake isiyo na doa akilenga kupata ushindi wake wa 51. Hata hivyo, Pacquiao ameonya kuwa anapaswa kuwa na hofu, kutokana na hamu yake ya kuwa mtu wa kwanza kumpa kipigo kitakachotia doa kwenye wasifu wake.

Pac Man anasema: “Nataka Floyd aishi na kumbukumbu ya kupoteza mara moja katika rekodi yake ya kulipwa na daima akumbuke ni nani aliyempa kipigo hicho.”

Mayweather na Pacquiao wanapangwa kurudiana katika pambano hilo la kushtua litakaloonyeshwa moja kwa moja na Netflix katika ukumbi wa Dola 2.3 bilioni.

Wawili hao waliwahi kuzichapa katika pambano lililoitwa “Fight of the Century” mwaka 2015, na mpaka sasa pambano hilo ndilo linaloongoza kwa mauzo ya malipo ya moja kwa moja (pay-per-view) katika historia ya ndondi, likifuatiwa na lile la Mayweather 2017 dhidi ya Conor McGregor.

Mwezi Oktoba, Pacquiao alithibitisha kuwa mazungumzo yalikuwa yakiendelea kati yake na Mayweather kuhusu marudiano mwaka huu, na sasa makubaliano yamekamilika.

Pambano hilo, ambalo limewafanya mabondia hao kuanza mapema maandalizi, litakuwa rasmi la kulipwa, jambo linalomaanisha kuwa rekodi ya Mayweather ya ushindi mara 50 bila kupoteza iko hatarini. Hata hivyo, Mmarekani huyo ameahidi kwa wafuasi wake “matokeo ni yaleyale” katika marudiano.

“Floyd na mimi tuliipa dunia pambano ambalo bado ndilo kubwa zaidi katika historia ya ndondi,” anasema Pacquiao.

“Mashabiki wamesubiri muda wa kutosha, wanastahili kuona marudiano haya, na sasa yatakuwa makubwa zaidi kwa kuwa yataonyeshwa moja kwa moja duniani kote.

“Kama ilivyo kawaida, nalitoa pambano hili kwa Wafilipino wenzangu kote duniani na kwa kuiletea heshima Ufilipino.”

Mayweather anasema: “Tayari nilishapigana na Manny na kumshinda mara moja. Safari hii matokeo yatakuwa yale yale.”

Pambano lao la kwanza katika ukumbi wa MGM Grand Garden Arena liliuza malipo ya moja kwa moja milioni 4.6 yenye mabilioni ya dola, huku mapato ya tiketi yakifikia Dola 72.2 milioni, nayo ikiwa ni rekodi.

Mr Money aliishi kulingana na jina lake la utani katika pambano hilo, akiripotiwa kuingiza takribani Dola 250 milioni wakati Pacquiao aliingiza Dola 150 milioni.

KABLA YA KUZICHAPA

Wawili hao wanatarajiwa kupigana katika mapambano mawili tofauti kabla ya kukutana, ambapo Pacquiao ataanza mapema kuzichapa na Ruslan Provodnikov, Aprili 18, huku Mayweather akikutana na Tyson wiki inayofuata.

Pacquiao ameshapigana mapambano saba ya kulipwa kati ya 2016 na 2021 baada ya kuzichapa na Mayweather mwaka 2015, na ilionekana kana kwamba safari yake ilikuwa imefikia mwisho aliposhindwa kwa pointi na Yordenis Ugas, Agosti 2021.

Kwa upande mwingine, Mayweather alipigana mapambano mawili ya kulipwa baada ya ushindi wake dhidi ya Pacquiao, akimshinda Andre Berto miezi minne baadaye na kuifanya rekodi yake kuwa 49-0, na alifikisha 50-0 alipomsimamisha bingwa wa zamani wa UFC, Conor McGregor, katika pambano kubwa miaka tisa iliyopita.

Kama ilivyo kwa Pacquiao, Mayweather tangu wakati huo ameshiriki katika mapambano kadhaa ya maonyesho dhidi ya wapinzani kama Logan Paul, kaka wa KSI, Deji Olatunji na Aaron Chalmers.