Ufalme wa Simba SC hauna mwenyewe

Muktasari:

SIMBA kumenoga. Siyo kama zamani ambapo staa mmoja au wawili walikuwa wakijijengea ufalme wao. Haikuwa kazi rahisi kubomoa ngome yao, lakini kwa sasa mambo yamebadilika, kila anayejituma ana nafasi ya kutukuzwa na mashabiki wa klabu hiyo.

SIMBA kumenoga. Siyo kama zamani ambapo staa mmoja au wawili walikuwa wakijijengea ufalme wao. Haikuwa kazi rahisi kubomoa ngome yao, lakini kwa sasa mambo yamebadilika, kila anayejituma ana nafasi ya kutukuzwa na mashabiki wa klabu hiyo.

Kinyang’anyiro hicho kinasaidia kuimarisha ushindani mkali baina yao.

Kocha wa Simba, Didier Gomes anapata urahisi wa kumtumia mchezaji anayemtaka kutokana na ushindani uliopo wa kung’ang’ania ufalme mbele ya mashabiki ambao wakati mwingine wanatoa vibunda vya pesa kumpa anayewakosha baada ya mechi.

Mwanaspoti limefanya utafiti wa jambo hilo ndani ya misimu mitatu na kubaini kuwa hakuna mwenye ufalme wake. Upepo umekuwa ukibadilika kulingana na viwango wanavyovionyesha kwenye mechi tofauti katika Ligi Kuu Bara.

AISHI MANULA

Katika eneo la kipa, Aishi Manula ameonekana tangu ajiunge Simba msimu wa 2017 hadi 2021 akitokea Azam FC. Manula anaonekana kukubalika na makocha waliopita kukinoa kikosi hicho, huku akiwapiga benchi makipa wenzake kama Said Mohamed ‘Nduda’ (waliyesajiliwa msimu mmoja), Deogratius Munishi ‘Dida’ (aliyefuata baada ya Nduda) na Beno Kakolanya.

Mashabiki wa Simba huwaambii kitu kuhusu Manula wanaye-muona ni Tanzania One kwa sasa kutokana na kuanza kikosi cha kwanza kwenye timu yao na Taifa Stars, hivyo ana ufalme wa aina yake.

LUIS MIQUISSONE

Kiungo mshambuliaji, Luis Miquissone, raia wa Msumbuji tangu ajiunge na timu hiyo msimu wa 2019/2020 ameleta mabadiliko ya nyimbo za shangwe alizokuwa anaimbiwa Clatous Chama na sasa zinaelekezwa kwake.

Kila kona anatajwa hasa baada ya kuifungia timu yake bao 1-0 dhidi ya Al Ahly ya Misri.

Mbali na hilo, bado anafanya makubwa kwenye Ligi Kuu akiwa na uchezaji wa kujituma bila kuhofia kuumizwa na mabeki ambapo hadi sasa anamiliki mabao manne, pasi tisa za mabao na anategemewa kikosi cha kwanza huku akikosekana mashabiki wake wanaingiwa hofu. Hata hivyo bado hajajimilikisha ufalme kwani kwa muda mrefu upepo unabadilika badilika.

JOASH ONYANGO

Kile kicheko cha kejeli cha kuiona kamati ya usajili ya Simba imesajili beki wa kati ‘babu’ ambaye ni Joash Onyango kutoka Kenya kimefutika na eneo la ulinzi akikosekana mashabiki wanakuwa na wasiwasi na kukuna vichwa. Jamaa anaonekana kucheza kikosi cha kwanza na anamudu kucheza na kila beki. Kuna wakati anapangwa na Kennedy Juma, Pascal Wawa na wakati mwingine Erasto Nyoni anayecheza nafasi nyingi zaidi lakini bado anaonyesha makali yaleyale. Hadi sasa anamiliki bao moja alilofunga dhidi ya Yanga - timu yake ilipotoka sare ya bao 1 - 1 katika mzunguko wa kwanza.

CLATOUS CHAMA

Msimu wa 2019/20, Chama alikuwa na ufalme wake. Alitajwa hadi na timu pinzani kwa ufanisi wake wa kazi. Ndiye aliyeibuka mchezaji bora wa mwaka akiweka rekodi ya kutoa pasi 10 za mabao na kufunga mabao mawili. Ukiachana na Ligi Kuu aliisaidia Simba kutinga hatua ya makundi michuano ya CAF akifunga bao la tatu dhidi ya Nkana ya Zambia.

Msimu huu upepo wa ufalme bado unazunguka kuna wakati akifanya vizuri jina lake linakuwa juu na kila shabiki anamzungumzia, lakini wakati mwingine anatibuliwa na Luis anayeonekana kujituma na kupambana hadi timu za nje kutamani huduma yake.

MEDDIE KAGERE

Alitamba ndani ya misimu miwili mfululizo aliyoibuka mfungaji bora (2018/19 - mabao 23) na (2019/20 - mabao 22). Jina lake lilikuwa na thamani kubwa kwani kila shabiki alitamani kupiga picha naye. Simba imeimarisha eneo la mbele kwa kumchukua Chriss Mugalu ambaye ndiye anaonekana anapangwa zaidi kikosi cha kwanza.

Kagere ambaye kwa sasa anamiliki mabao tisa ndiye aliyefuta ufalme wa Emmanuel Okwi ambaye alionekana mkombozi wa safu ya ushambuliaji ya Simba ambapo msimu wa 2017/18 alimaliza na mabao 19.

Lakini, baada ya kutua Mnyarwanda huyo upepo ulihamia kwake, huku staili ya ushangiliaji wake ikitamba ya kama kufumba jicho moja.

JOHN BOCCO

Aina ya upambanaji wa nahodha John Bocco ambaye ameipa Simba ubingwa mara tatu mfululizo tangu ajiunge nayo msimu wa 2017/18 akitokea Azam FC inawakosha Msimbazi. Akiwa fiti ni kati ya mastaa ambao wana kibali kikubwa mbele ya mashabiki wa timu hiyo ambapo ana mabao tisa.

Wachezaji wengine ambao nyota zao hung’ara kutokana na kujipambanua katika majukumu yao ni Shomary Kapombe na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wakati mwingine ni Benard Morrison ikitokea akafunga nyakati ngumu ambazo timu inatoka jasho kupata matokeo.