UCHAMBUZI: Usajili mkopo usiwakomoe wachezaji

Saturday January 02 2021
usajili pic
By Charles Abel

ZIMEBAKI siku 13 kabla ya dirisha dogo la usajili kwa klabu za soka nchini zile za Ligi Kuu, Ligi Daraja la Kwanza, la Pili na Ligi Kuu ya Wanawake lililofunguliwa Desemba 16 mwaka jana halijafungwa rasmi.

Tumeona klabu mbalimbali zikisajili wachezaji kutoka kwingine au wale waliokuwa huru kwa lengo la kuimarisha vikosi vyao kulingana na tathmini ya mapungufu ya kiufundi ya vikosi vyao yaliyoonekana katika mechi ambazo zimeshacheza msimu huu.

Tofauti na usajili wa kipindi cha dirisha kubwa, ule unaofanyika kipindi kama hiki huwa unalenga wachezaji ambao wanakwenda moja kwa moja kucheza katika kikosi cha kwanza cha timu inayomsajili.

Kwa dirisha hili tu iko mifano ya kuthibitisha hilo mmojawapo ukiwa ni ule wa mshambuliaji Saido Ntibazonkiza kutoka Burundi ambaye amesajiliwa na Yanga na baada ya kunaswa tu ameshakuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza akicheza mechi mbili za Ligi Kuu za timu hiyo ilizocheza na timu za Dodoma Jiji na Ihefu ambazo alihusika katika mabao manne akifunga moja na kupiga pasi tatu zilizozaa mabao.

Pia kuna wachezaji kama Deogratias Munishi ‘Dida’ na Juma Mahadh ambao wenyewe tangu waliposajiliwa na Ihefu SC ya Mbeya, wamekuwa tegemeo katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Lakini pia zipo timu ambazo kipindi kama hiki cha usajili wa dirisha dogo, hukitumia kuwatoa kwa mkopo baadhi ya nyota wake kwenda katika timu nyingine.

Advertisement

Mara nyingi wachezaji ambao wamekuwa wakitolewa kwa mkopo ni wale ambao huwa hawapati nafasi ya kutosha ya kucheza katika vikosi vya timu hivyo ili kwa lengo la kulinda vipaji vyao, hupelekwa kwingine ambako kunakuwa na mahitaji nao. Na kwa nchi zilizoendelea kisoka, wachezaji wengi wanaotolewa kwa mkopo huwa ni wenye umri mdogo ambao klabu zinaamini wakienda kwingine na wakapata nafasi za kucheza, wataimarika zaidi na kuwa tegemeo kwa timu hapo baadaye.

Hata hivyo utamaduni wa usajili wa mkopo hapa Tanzania umekuwa tofauti na maeneo mengine duniani kwani hapa klabu huamua kutumia hiyo kama njia ya kuanza kuachana na wachezaji ambao inaona viwango vyao haviridhishi vya kutosha benchi la ufundi la timu husika.

Kwa hapa Tanzania, wachezaji wengi wanaotolewa kwa mkopo ni nadra kurejeshwa katika timu iliyowatoa na wengi wao huwa ni wale ambao mikataba yao inaelekea ukingoni hivyo kipindi cha mkopo kinapomalizika, ndio huachwa rasmi.

Tunaweza kuzishauri timu zetu kubadilika na kuachana na dhana kwamba uhamisho wa mkopo ni fursa ya kuanza kuonyesha mkono wa kwaheri wachezaji na badala yake utumike kama njia ya kulinda na kuimarisha vipaji vya wachezaji ambao baadaye wanaweza kuwa na msaada na umuhimu kwa timu husika.

Hata hivyo ingawa unabakia kuwa utashi wa klabu katika hili, njia au utaratibu ambao timu zetu zimekuwa zikiutumia katika utoaji wachezaji kwa mkopo umekuwa sio mzuri na unakwenda kinyume na kanuni na muongozo wa usajili na hadhi za wachezaji uliotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA). Muongozo huo unazilazimisha klabu kuwashirikisha wachezaji husika pindi inapotaka kuwatoa kwa mkopo na iwapo muhusika ataridhia ndipo uhamisho unapaswa kufanyika.

Kabla usajili wa mkopo haujafanyika, ni lazima pia mchezaji afahamu na awe na uhakika wa namna atakavyolipwa stahiki zake mfano posho na mishahara au matibabu kama mkataba baina yake na klabu inayomtoa kwa mkopo unavyoainisha.

Lakini hiyo imekuwa kinyume chake hapa nchini ambapo klabu zimekuwa zikitumia ubabe katika uhamisho wa mkopo ambapo zimekuwa hazitoi mwanya wa kujadiliana na mchezaji husika na zenyewe ndio zinalazimisha wachezaji waende katika timu ambazo viongozi wanazitaka.

Mbaya zaidi, pindi wachezaji wanapokuwa kwa mkopo, hukumbana na changamoto ya kutolipwa stahiki zao na mwisho wa siku hujikuta wakitelekezwa jambo ambalo huchangia kuporomosha viwango vyao.

Hili linaweza kuepukika ikiwa mamlaka za soka hapa nchini zitaanza kuwa na usimamizi thabiti wa mikataba baina ya wachezaji na klabu na tofauti na sasa ambapo zimekuwa haziwajibiki ipasavyo katika kusimamia haki na wajibu wa kimikataba baina ya pande hizo mbili.

Ni wakati wa kubadilika sasa na kuwa na fikra chanya juu ya uhamisho wa mkopo badala ya kuugeuza kama jalala la kutupa na kutelekeza wachezaji.

Advertisement