UCHAMBUZI: Simba isijidanganye kwa Kaizer ikaumia!

Muktasari:

SOKA la Bongo linamanjengeka mengi. Linajitofautisha sana na soka tunalolisikia ama kuliona likichezwa na kuongozwa kwenye mataifa mengine. Hata ukiwasikiliza mashabiki, wachezaji hadi viongozi wanavyozungumza kwenye mahojiano yao, unabaini tumeachwa mbali sana.

SOKA la Bongo linamanjengeka mengi. Linajitofautisha sana na soka tunalolisikia ama kuliona likichezwa na kuongozwa kwenye mataifa mengine. Hata ukiwasikiliza mashabiki, wachezaji hadi viongozi wanavyozungumza kwenye mahojiano yao, unabaini tumeachwa mbali sana.

Kuna wakati unaweza kudhani pengine soka linalochezwa na kuendeshwa nchini sio lile lililopo kwa wenzetu hasa Ulaya.

Makocha na wachezaji wote ni kama wamekaririshwa maneno ya kuzungumza kwenye mahojiano mara baada ya mechi zao. ‘Kwanza tunamshukuru Mungu, mchezo umeisha salama na tumepata matokeo.... Katika soka kuna matokeo matatu, kushinda, kushindwa na kutoka sare na leo tumepoteza na tunaenda kujipanga kwa mchezo ujao...”

Wakati mwingine wanaongea na jazba kubwa kama ilivyokuwa juzi wakati nahodha wa Tanzania Prisons, Benjamin Asukile alivyopayuka...Naam amepayuka, kwa vile mchezaji anayejitambua na kujua anapaswa kuzungumza nini, asingeweza kuyasema aliyoyasema hewani...!

Ni wachache wanaojua wazungumze nini, wakati na mahali gani?

Achana na hao, sikiliza baadhi ya viongozi wanachozungumza au kuandika kwenye akaunti zao na zile za taasisi walizopo. Majuzi kabla ya mechi ya Yanga na Azam, kuna jumbe iliandikwa kwenye ukurasa wa klabu ya Azam juu ya kutaka wakomae dhidi ya Yanga na kweli walishinda bao 1-0.

Mmoja wa viongozi wa klabu hiyo alilalamikia juu ya kilichofanywa na Simba, ila naye akazingua tena kwa kuzungumza mambo siyo kabisa, pengine kwa furaha ya ushindi na kujikuta akiingia matatani na wenye mamlaka ya soka. Sio yeye tu, kuna viongozi wengine kibao wamejikuta msambweni kwa sababu ya kushindwa kuzuia hisia na mihemko yao na kulifanya soka letu liwe kichekesho. Zaidi NI mamlaka zinavyotafsiri kauli na makosa na hukumu zake.

Utabisha nini? Juzi kati mmesikia na kuona adhabu mbalimbali zilizotolewa na ile ya Kamati ya Bodi ya Ligi? Adhabu zimekaa kimtego mtego...! Kabla ya adhabu hizo kutangazwa, tayari zilishaenea Bernard Morrison asingeguswa kwa tukio lake la kuonekana kumshika pabaya mshika kibendera. Waliovujisha na kula kiapo HATAFUNGIWA, walidai ni kwa sababu ya Kariakoo Derby na walisisitiza Ibrahim Ame angetolewa kafara, kusudi watu waone adhabu zimetendeka. Kama utani kweli adhabu zikaja kama zilivyo. Ame kala kibano, BM3 kapewa onyo!

Hii sio mara ya kwanza kwa kuenea kwa tetesi juu ya jambo fulani hususan linalozihusu klabu kubwa nchini na mamlaka ya soka nchini na mwishowe kuja vile vile! Sijui huwa ni bahati mbaya au makusudi, lakini haya ni mambo yanayoonyesha bado tunasafari ndefu kwenye soka letu. Fikiria mwamuzi anafungiwa maisha au mwaka mzima kwa sababu ya kujichanganya uwanjani kwenye mechi flani, lakini kosa lilelile likifanywa kwenye pambano lisilohusu timu vigogo, linachukuliwa poa pengine kupewa onyo.

Hapa ndiko kwenye tatizo! Leo sio mada yangu, ila nilitaka kusisitiza, wadau wa soka wana kazi kubwa ya kulibadilisha soka letu lifanane na lile linalochezwa ama kuendeshwa na wenzetu.

Kubwa nililotaka kulizungumza kwa leo ni juu ya droo iliyofanyika juzi ya mechi za robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Simba kupangwa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini. Hii ni mara ya kwanza kwa Simba kukutana na timu hiyo tena zikiwa kwenye viwango na ubora tofauti.

Kwa sasa Simba inaaonekana bora kuliko Wasauzi na hilo tayari limeanza kuwaoa kiburi wanachama na mashabiki wa Msimbazi, wanaoamini timu yao ina kazi nyepesi dhidi ya Kaizer.

Soka halipo hivyo. Ni kweli Simba wapo moto kwa sasa kulinganisha na wapinzani wao, lakini soka ni mchezo wa ajabu sana. Ni lazima Simba ijipange na isithubutu kuwadharau wapinzani wao. Dharau yoyote ambayo Simba dhidi ya Kaizer kwa kuangalia matokeo ya mechi zao za makundi msimu huu na rekodi zao kwa ujumla Afrika zinaweza kuwaponza.

Simba irejee matokeo ya mechi zao za nyuma dhidi ya timu walizoziona dhaifu, kwa mfano miaka miwili mitatu iliyopita iling’olewa michuanoni na UD Songo ya Msumbiji.

Simba iliamini UD ingekuwa mchekea kwao, lakini ikatoka suluhu ugenini na kupata sare ya 1-1 nyumbani na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini lililoibeba wapinzani wao.

Sio mechi hiyo tu, kuna mechi kadhaa za kimataifa Simba na wawakilishi wengine wa Tanzania walizichukulia poa na kuondolewa kizembe.

Naamini kama Simba itajipanga vizuri na kuhakikisha inapata matokeo mazuri ugenini, itawarahisishia kazi ya kutaka kurejea rekodi yao ya mwaka 1974 walipotinga nusu fainali ya michuano hiyo ya Afrika.

Ni kweli rekodi zinaonyesha Simba haisumbuliwi sana inapokutana na timu za Kusini mwa Afrika, lakini bado imewahi kupata aibu dhidi ya timu hizo za Kusini ikiwamo ile ya mwaka 2013 walipopigwa nje ndani na kutolewa kwa jumla ya mabao 5-0 na Recretivo do Libolo ya Angola.

Hivyo hizi amsha amsha za mashabiki kwa sasa zikisisitiza Simba wana kazi nyepesi ni kutaka kuitingisha Simba.

Lazima wachezaji wa Simba waandaliwe kisaikolojia, huku wenyewe wakifahamu hizi ni mechi za mtoano ambazo ukifanya kosa dogo tu, timu inatolewa tofauti na kucheza mechi za ligi ya makundi ambapo kama unapoteza mechi moja, unakuwa na nafasi ya kurekebisha makosa kwa mechi zijazo.

Binafsi naamini Simba ina nafasi kubwa ya kutoboa, lakini haiwezi kuwa rahisi kama timu haitajitoa na kupambana kwelikweli kwenye mechi zao mbili hata kama itaanzia ugenini na kumalizia nyumbani.

Ukiangalia kwenye safari yake kutinga robo fainali, Kaizer imepambana kwelikweli, sio timu ya kubezwa, lakini inafungika kwa udhaifu iliyonayo ya kuwa na ngome nyepesi na safu butu ya ushambuliaji kulinganisha na Simba, hata hivyo ni lazima Wekundu wajipange vilivyo.

Kiu ya wanasimba ni kuona chama lao likirejea mafanikio ya 1974 na hata ikiwezekana kurudia ilichokifanya mwaka 1993 walipotinga Fainali za Kombe la CAF na kulikosa taji kizembe!

Lakini kama Wekundu wa Msimbazi hao wataichukulia poa Kaizer na kuamini wataitoa kilaini, basi wakae na kujiandae kufanyiwa sapraizi kwani soka la kisasa limebadilika sana na huwa lina matokeo ya kustaajabisha sana iwe timu inacheza nyumbani ama ugenini. Kila la heri Simba, kazi iendelee!

Imeandikwa na BADRU KIMWAGA