UCHAMBUZI: Moyes si bomu, mafanikio ya Ferguson yamemwelemea
Muktasari:
- Ndio maana hata kocha wa Swansea, Michael Laudrup alisema kabla ya mechi kati ya timu yake na Man United katika mechi ya Kombe la FA
DAVID Moyes si kocha mdogo, si kocha asiye na uzoefu wa kufundisha timu kubwa kama Manchester United, si kocha aliyechaguliwa kimakosa kumrithi Sir Alex Ferguson.
Ni kocha aliyeifundisha Everton akaiwezesha kuwepo katika nafasi nane za juu kwa miaka saba mfululizo huku akifanikiwa kuwa kocha bora wa mwaka kwa misimu mitatu kati ya misimu 10 aliyofundisha timu hiyo, anatosha kuaminiwa, anastahili kuifundisha timu kubwa kama Man United. Bahati mbaya amerithi mikoba ya Ferguson huku akiwa na mzigo wa kuwa bingwa mtetezi Ligi Kuu England na sasa anakutana na wakati mgumu akiwa ameshapoteza mechi zaidi ya nne katika uwanja wa nyumbani wanaouita ‘Theatre of dreams’.
Kwa miongo miwili iliyopita ilikuwa si kitu cha kawaida sana Man United kupoteza mechi nyumbani mara kwa mara.
Ndiyo maana hata kocha wa Swansea, Michael Laudrup alisema kabla ya mechi yake ya Kombe la FA na Man United kuwa Uwanja wa Old Trafford anauheshimu kwa historia yake dhidi ya timu pinzani lakini si uwanja maalum kama Bernabeu, Camp Nou. Kwa moyo na mtazamo huo huo, Swansea walifanikiwa kuilaza Man United mabao 2-1 mbele ya mashabiki wake zaidi ya 60,000.
Moyes kwa sasa yupo katika wakati mgumu, mashabiki wa Man United wanalinganisha mafanikio ya mtangulizi wake na kile anachotaka kujianzishia yeye ili kutengeneza historia yake kwenye timu hiyo.
Mbaya zaidi ni baada ya kutolewa katika Kombe la FA wiki iliyopita kwa kuchapwa na Swansea kwani ndani ya saa 48 timu yake ilichapwa tena na Sunderland katika mechi ya nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Ligi maarufu Capital One pale ilipocharazwa mabao 2-1.
Hii ni hali mbaya kwa Moyes kwani mashabiki wanaamini Ferguson aliondoka na kumkabidhi timu ikiwa na kiwango cha juu. Kwa hiyo mafanikio ya mtangulizi wake ndio mzigo anaotwishwa na mashabiki.
Kwa kawada timu kubwa inapokuwa katika hali kama hii, huwa kuna njia mbili kuu wanazotumia walimu kuiondoa hapo ilipo na kurejesha matumaini ambayo mashabiki wameanza kuyapoteza. Kwanza ni kutumia wachezaji wale wale waliotumika mwaka jana lakini kubadilisha kabisa mbinu kwani kwa kutumia mbinu zile zile wachezaji huona hakuna jipya hivyo kukosa kujitolea katika kiwango walichojitolea kwa mtangulizi wake na kufanikisha kutwaa ubingwa.
Kama uwezekano wa kuleta mbinu mpya na utaratibu mpya wa kuendesha timu haupo njia pekee iliyobaki ni kutambulisha wachezaji wapya kisha ukatumia mbinu zile zile zilizozoeleka katika viwanja vya mazoezi na katika mechi ambazo zilifanikisha timu hiyo kuchukua ubingwa msimu uliopita .
Wachezaji kama wanaadamu wengine katika sehemu za kazi, mara nyingi huhamasika wanapofundishwa mbinu mpya au kucheza timu mpya na mazingira mapya, hivyo kwa Moyes kutumia wachezaji wale wale na mbinu zile zile za mtangulizi wake hukosa umakini na kusababisha timu kukosa matokeo inayoyataka.