UCHAMBUZI: Lionel Andres Messi mambo hufika mwisho

Saturday February 20 2021
messi pic
By Edo Kumwembe

LIONEL Andres Messi mambo hufika mwisho. Tangu alipotua Catalunya akiwa na miaka 13 kwa ajili ya kuchomwa sindano ambayo ingemuwezesha kukua vyema. Hatukuwahi kumuona na sura hii. Sura ambayo tulimuona nayo Jumanne usiku. Haikuwahi kutokea.

Tabasamu limeondoka katika sura ya Lionel ambaye wenzake wanapendelea kumuita Leo. Ulikuwa ni mwendelezo wa kushuhudia kile ambacho kimekuwa kikitokea kwa miaka mitatu iliyopita katika hatua kama hii miezi kama hii. Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kila wakati anausukuma moyo wake na kuunong’oneza kwa sauti hafifu akisema, “huu unaweza kuwa msimu mwingine, msimu tofauti, msimu wenye nuru mpya.” Hata hivyo mambo hayawi kama anavyodhani. Anashindwa kuamini kwamba mambo hufika mwisho. Hakuna kurasa nyingine unayoweza kufungua. Labda anakaribia kuamini.

 Julai, mwaka jana alijaribu kuhama. Alipambana na nafasi yake. Alijaribu kupambana kuondoka katika jiji ambalo limemlea kabla hajabalehe. Alipambana sana, lakini inaonekana kwamba ile sauti ilimjia ikamnong’onenza. Kwamba, “huu unaweza kuwa msimu mwingine, msimu tofauti, msimu wenye nuru mpya.”

Alighairi kuhama na kuamua kukipigania kikosi cha Ronald Koeman. Kikosi cha timu iliyomlea akiwa mtoto. Maisha haya yalianza tangu Barcelona ilipoanza kudorora. Marafiki zake Andres Iniesta na Xavi Hernandes waliondoka akaendelea kupambana. Neymar akaondoka akaendelea kupambana. Luis Suarez akaondoka lakini akaendelea kupambana.

Ni maisha yaliyojaa mashaka. Barcelona hii ya miaka mitatu ni mzigo wa kinyesi ambao Messi ameendelea

Advertisement

 kuubeba kwa huzuni kubwa. Ilianzia wakati AS Roma walipopindua matokeo pale Uwanja wa Olimpiki baada ya kufungwa mabao mengi Nou Camp. Ilionekana kama bahati mbaya fulani hivi ingawa tunaofahamu soka tulijua kwamba Barcelona ilikuwa imegota mwisho.

 Ikaja pale wakati Liverpool walipobadili matokeo Anfield baada ya kufungwa mabao mengi Nou Camp. Liverpool walilazimika kushinda 4-0 dhidi ya Barcelona na kweli wakafanya hivyo huku Leo akiwa uwanjani. Na kinachotia huzuni zaidi ni kwamba Liverpool haikuwa na wachezaji muhimu uwanjani.

 Na sasa inatokea tena dhidi ya PSG. Subiri kwanza, hizi mara mbili za kwanza Barcelona walianza kushinda halafu wapinzani wakabadilisha kibao. Safari hii wameanza kufungwa tena wakiwa kwao na haionekani kama PSG wanaweza kushusha moto wao.

 Kumbuka wameyafanya haya bila ya Neymar. Watakaporudiana madhara yanaweza kuwa makubwa zaidi. Leo analijua hili. Barcelona wanalijua hili. Kufikia hapo sidhani kama Leo atajidanganya kwamba kuna kitu amebakiza Nou Camp. Hapana. Mambo ufika mwisho.

Ni kama hadithi nzuri ambayo mwandishi wake anaandika sentensi ya mwisho. Leo akiendelea kubakia Catalunya ataaibika zaidi.

 Nadhani hakuna jinsi. Kama alikuwa na wasiwasi na maamuzi yake katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka jana, basi pambano la PSG Jumanne usiku lilikuwa likimthibitishia kwamba dunia itaungana na maamuzi yake. Hata baadhi ya watu wa Barcelona watatazama nyuma na kumpa ruhusa ya mioyo yao kuondoka Nou Camp. Mambo hufika mwisho. Messi ameshinda kila kitu na Barcelona. Kila kitu. Ameshinda mataji ya klabu na ameshinda matuzo yake binafsi. Hakuna alichobakiza. Ameuza jezi nyingi pia na amesababisha watu wengi tukate tiketi za ndege na za kuingia Nou Camp kwa ajili ya kumuona akicheza.

 Hata akiondoka Barcelona wengine tutatazama nyuma na kujiambia kwamba,

 “Mwanasoka Bora zaidi kuwahi kucheza soka duniani alicheza Barcelona pale Hispania.” Tunaweza kubishana hapa na pale kwa sababu katika dunia hiihii wamewahi kucheza Pele, Diego Maradona, Johan Cruyff, Cristiano Ronaldo na wengineo  lakini sisi wengine tunaamini hakuna kama Messi.

 Kwa sasa mambo yamefika mwisho. Mwisho wa kusikitisha. Tulitamani kuuona mwisho wa Messi vinginevyo. Labda akiwa amevaa medali ya ubingwa wa Ulaya au La Liga akiwa anashangilia pale Nou Camp.

 Lakini kwa Barcelona hii nadhani haitawezekana. Kila kocha anayekuja huwa anaiacha Barcelona ikiwa mbovu zaidi.

Inaonekana hakuna mwenye tiba ya Barcelona kwa sasa na naamini Leo hawezi kusubiri zaidi. Anahitaji kwenda kwingineko kwa ajili ya kupata timu ambayo itampumzisha. Hasimu wake, Ronaldo amekwenda katika ligi ambayo imempumzisha lakini Messi anahitaji kwenda katika timu ambayo itampumzisha zaidi. Zinatajwa timu mbili. Manchester City na PSG. Sina uhakika Leo atakwenda wapi lakini ni bora aende zake City.

 Kule kuna kocha ambaye anamjulia zaidi duniani, Pep Guardiola. Nadhani atajua ni namna gani anaweza kumpumzisha Messi wa miaka 34 baada ya kumtumia vyema akiwa kijana.

 Lakini zaidi ya yote kuna mtu anaitwa Kelvin De Bruyne. Pengine ndiye kiungo bora zaidi duniani kwa sasa. Unahitaji kucheza na huyu ili upumzike uwanjani. Atafanya maamuzi yote sasa wakati akikaribia lango la adui na kazi ya Leo itakuwa kufunga au kupewa pasi muhimu halafu afanye maamuzi aliyokuwa anayafanya akiwa na miaka 24.

Kando ya De Bruyne kuna mafundi wengi ambao watampumzisha Leo. Ilkay Gundogan amezidi kuwa mtamu. Phil Foden amekuwa mtamu zaidi. Raheem Sterling bado moto. Na wengineo wengi. Wachezaji wote hawa hauwezi kuwapata Barcelona. Leo akienda atapunguziwa majukumu huku  aking’ara zaidi.

Lakini hata akienda PSG sio mbaya. Kule anaweza kutengeneza utatu wa Leo, Kylian Mbappe na Neymar. Ni utatu mtakatifu kama Mbappe hatakwenda Santiago Bernabeu maana kuna kila dalili akaishia huko mwishoni mwa msimu huu.

Kitu ambacho PSG watapaswa kufanya ni kuongeza nguvu katika eneo la kiungo na maeneo mengine muhimu. Utatu wa kina Messi utawafanya wawe tishio zaidi kiasi kwamba maadui hawatawasogelea kwa urahisi wakihofia kushambuliwa kwa ufasaha. Tusubiri tuone kitakachotokea ndani ya miezi mitatu ijayo lakini nadhani tumeuona mwisho wa Leo pale Camp Nou. Kifua chake hakiwezi kuendelea kubeba fedheha hizi ambazo amezibeba dhidi ya Roma, kisha Liverpool halafu na sasa PSG. Kitu kibaya zaidi ni kwamba watu huwa wanamuangalia yeye pindi timu ikifungwa.

 Lakini pia inatoa nafasi kwa Barcelona wenyewe kujenga timu nje ya Leo. Watapoteza mauzo ya jezi, watapoteza mauzo ya tiketi lakini ukweli ni kwamba mambo ufika mwisho. Hata mwisho ulipofika Ryan Giggs aliondoka Manchester United, Francesco Totti alistaafu Roma, Thierry Henry akaondoka Arsenal. Wachezaji wakubwa waliodumu klabu moja kwa miaka mingi nao ufika mwisho. Kinachobakia huwa ni mnara tu na heshima iliyotukuka. Lionel Andres Messi amefika mwisho Nou Camp.

Labda kwa sababu amekuwa mkubwa zaidi lakini hata akina Iniesta nao walifika mwisho. Huwa inatokea mara moja katika maisha ya mwanadamu kushuhudia mwisho huu. Nilikuwepo!

Advertisement