Ni vigumu kuwavumilia Junior Lokosa na Fiston

Friday February 19 2021
fiston pic
By Charles Abel

WASHAMBULIAJI Junior Lokosa na Fiston Abdulrazack hawajaanza vizuri katika zao za Simba na Yanga ambazo ziliwasajili katika dirisha dogo la usajili msimu huu.

Abdulrazack ambaye alisajiliwa na Yanga baada ya kuvunja mkataba wake na timu ya ENPPI ya Misri, alikuwa ameicheza timu yake mpya katika mechi mbili tofauti bila kufunga bao au kupiga pasi iliyozaa bao.

Alianzishwa katika kikosi cha kwanza cha Yanga ambacho kilifungwa kwa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya African Sports lakini pia akaja kupangwa katika kikosi cha timu yake kilichotoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City huko Mbeya lakini katika mechi ya juzi ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar hakuwekwa hata benchi.

Presha inaonekana kuwa kubwa kwa upande wake kutoka kwa mashabiki wa Yanga ambao walitegemea makubwa kutoka kwake mara baada ya kusajiliwa kutokana na uzoefu wa kucheza katika ligi mbalimbali barani Afrika lakini pamoja na kuwa na takwimu nzuri za ufungaji.

Kabla ya ENPPI ambayo baada ya kuachana nayo ndio amejiunga na Yanga, Fiston amewahi kuzichezea timu za JS Kabylie, Al Zawra’a, 1º de Agosto, Mamelodi Sundowns, Blomfontein Celtic, Sofapaka, Rayon Sports, Diables Noirs na LLB Academic.

Kwa upande wa Junior Lokosa naye hajawa na mwanzo mzuri ndani ya kikosi cha Simba ambacho kilimsajili kwa ajili ya mahitaji ya mechi za kimataifa baada ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Advertisement

Aliingizwa katika dakika za lala salama la mechi ya mashindano ya Simba Super Cup dhidi ya Al Hilal na baada ya hapo alijikuta akikaa benchi katika mchezo uliofuata dhidi ya TP Mazembe na akaja kuwekwa nje pindi waliposhinda kwa bao 1-0 dhidi ya AS Vita Club, ugenini huko Congo.

Ifahamike kwamba Lokosa atakitumikia kikosi cha Simba katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tu na sio vinginevyo kutokana na timu hiyo kuwa tayari ina wachezaji 10 katika kikosi chake ambao ni raia wa kigeni wanaoruhusiwa kusajiliwa na kila timu ya Ligi Kuu.

Wasifu wa Lokosa nao unasisimua kwani kabla ya kujiunga Simba akiwa mchezaji huru, aliwa kuchezea timu ya Esperance ya Tunisia na pia timu za Kano Pillars na First Bank.

Amewahi kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria mara kadhaa na katika baadhi ya nyakati alifanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa barani Ulaya katika timu za Ludogorets na Brann lakini pia ameshawahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Nigeria.

Wawili hawa, Lokosa na Fiston walisajiliwa kwa mikataba ya muda mfupi wa miezi sita ambayo ndani yake kuna kipengele cha kuongezwa ikiwa wachezaji hao wataweza kufanya vizuri ndani ya vikosi hivyo.

Hata hivyo rekodi na mafanikio ambayo Lokosa na Fiston wamewahi kuyapata huko nyuma walikokuwa wanacheza hazitoshi kuwabeba katika kipindi hiki ambacho Simba na Yanga zinahitaji zaidi huduma zao na sio nini walikifanya kabla ya kujiunga na timu hizo mbili kongwe nchni.

Mchezaji anaposajiliwa katika kipindi cha usajili wa dirisha dogo anapaswa kuingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza kwani usajili wa nyakati hizo hulenga zaidi wachezaji waliokamilika kwa ajili ya mahitaji ya muda mfupi.

Sio rahisi kumvumilia mchezaji aliyesajiliwa na timu katika dirisha dogo kwani tofauti na usajili wa dirisha kubwa kwani siku na idadi ya mechi kabla ya msimu kumalizika huwa chache kulinganisha na kabla ya kuanza kwa msimu ambapo mchezaji hupata nafasi ya kuzoea mazingira, wachezaji wenzake na falsafa ya timu kwa sababu anakuwa na muda wa kutosha.

Kwa bahati mbaya, Fiston Abdulrazack na Junior Lokosa kila mmoja amesajiliwa kwa mkataba wa miezi sita ambayo leo hii imebakiza miezi minne tu kumalizka. Wanahitajika kufanya vizuri kama njia pekee ya kuendelea kubaki katika timu hizo au kupata malisho bora zaidi kwingineko lakini wakiendelea kutofanya vizuri, uwezekano wa kuzitumikia timu hizo za Yanga na Simba kwa muda mrefu ni finyu.

Advertisement