Prime
UBWELA: Wanasoka maarufu waliochukiana wakiwa wanakipiga kwenye timu moja
Muktasari:
- Lakini, hilo halijawahi kuwa geni kwenye klabu kama za Manchester United, Arsenal, Real Madrid na nyingine nyingi kutokea wachezaji ambao wanachukiana kama paka na chui.
LONDON, ENGLAND: KATI ya mambo magumu kwa shabiki wa soka, ni kuona wachezaji wa timu yako unayoshabikia, hawapendani, wanachukiana.
Lakini, hilo halijawahi kuwa geni kwenye klabu kama za Manchester United, Arsenal, Real Madrid na nyingine nyingi kutokea wachezaji ambao wanachukiana kama paka na chui.
Kwenye kikosi cha Newcastle United kuliwahi kutokea wachezaji wawili, Kieron Dyer na Lee Bowyer walizichapa wenyewe uwanjani kwenye mechi mwaka 2005.
Hawa hapa mastaa ambao walikuwa wakifanya mazoezi pamoja kila siku, lakini walikuwa wakichukiana kwelikweli bila ya kujali wanacheza timu moja.
El Hadji-Diouf & Jamie Carragher (Liverpool)
Ni rahisi kuhesabu ni watu wangapi kwenye soka hawajawahi kuwa maadui wa Diouf, lakini bifu lake la mchezaji mwenzake wa timu moja, Carragher lilikuwa la aina yake. Wawili hao hawakuwa na uhusiano mzuri tangu walipokutana kwa mara ya kwanza tu kwenye mazoezi ya timu ya Liverpool. Beki Carragher alisema kwamba kitu ambacho alikuwa akitamani kwenye mazoezi ya timu yake ya Liverpool ni kupangwa timu tofauti na Diouf ili tu amchezee rafu. Kila mmoja amekuwa akimshambulia mwenzake kwa maneno hata baada ya wote kustaafu mchezo wa soka. Bifu lisiloisha. Carragher anaamini Diouf hajui boli, wakati Diouf anamnanga Carragher kuwa hamna alichofanya katika soka ilhali yeye Diouf alikuwa staa wa fainali za Kombe la Dunia 2002 akiwa na timu yake ya taifa ya Senegal aliyoipeleka hadi robo fainali kule Korea na Japan.
Emmanuel Frimpong & Samir Nasri (Arsenal)
Unamkumbuka kiungo Emmanuel Frimpong? Mchezaji huyo wa zamani wa Arsenal aliwahi kuweka wazi kwamba hakuwa na uhusiano mzuri kabisa na mchezaji mwenzake kwa wakati huo, Samir Nasri. Frimpong alisema hampendi Nasri na kamwe hatakuja kumpenda hata kama atapewa Dola 5 bilioni. Kauli hiyo inaonyesha jinsi bifu lilivyokuwa kubwa baina ya wawili hao. Ugomvi wa wawili hao ulianzia kwenye mechi ya kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Liverpool, ambapo wakiwa kwenye vyumba vya kubadilishia, Nasri alisimama na kusema Arsenal imepoteza mechi kwa uzembe wa Frimpong.
Teddy Sheringham & Andy Cole (Man United)
Kwenye mechi ambazo wote walikuwa uwanjani wanacheza, washambuliaji hao walikuwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 84.8. Lakini, wawili hao waliokipiga kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi cha Manchester United wakati huo chini ya kocha Sir Alex Ferguson, chuki yao ilianzia kwenye mechi ya kimataifa ya timu ya taifa ya England, katika mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwa Cole kuchezea kikosi cha Three Lions. Cole aliingia kuchukua nafasi ya Sheringham, ambaye aligoma kumpa mkono na hapo ikazuka chuki baina yao na kuchukiana kuliko kawaida.
Lothar Matthaus & tefan Effenberg (Bayern Munich)
Wawili hao walicheza kwa mafanikio makubwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ujerumani pamoja na klabu ya Bayern Munich. Lakini, nyuma ya mafanikio hao, wawili hao walikuwa na chuki kubwa, walichukiana kwelikweli. Kinachovutia kwa wanasoka hao ni kwamba bifu na chuki zao walizoweka kando linapokuja suala la kuzisaidia timu zao ndani ya uwanja na Effenberg alieleza chuki yake kwa Matthaus katika kitabu chake, akimwelezea kwenye ukurasa mzima, ambapo kichwa cha habari kiliandikwa hivi ‘Nini anachojua Lothar Matthaus kuhusu soka’ kisha hakukuwa na maandishi yoyote katika ukurasa huo. Ina maana hajui kitu.
Craig Bellamy & John Arne Riise (Liverpool)
Katika mtoko wa wachezaji wa Liverpool walipokuwa huko jijini Barcelona walikwenda kumenyana na miamba hiyo ya Nou Camp kwenye kipute cha Ligi ya Mabingwa Ulaya, beki wa pembeni Riise alikataa ombi la Bellamy la kumtaka aimbe kwenye karaoke. Na matokeo yake, Bellamy aliporudi hotelini, alikwenda kwenye chumba cha Riise na kumpiga staa huyo wa Norway na mbao la kuchezea mpira wa gofu. Na kuonyesha kwamba kuna chuki baina yao, Bellamy alikwenda kulielezea hilo kwenye kitabu chake. Wawili hao wote walifunga katika mechi hiyo ya Camp Nou, huku Bellamy akishangilia kama anacheza gofu.
Arjen Robben & Robert Lewandowski (Bayern Munich)
Kwa baadhi ya watu hawakuwa wakipendezwa na staili ya uchezaji ya Robben, kwamba hakuwa mchezaji anayewavutia kumtazama au kuwa naye kwenye timu moja na hilo linaweza kuthibitishwa na straika Lewandowski. Baada ya kuwasili Bayern, straika wa kimataifa wa Poland, Lewandowski mara kadhaa alionekana kukasirishwa na ubinafsi wa Robben na hilo liliibua chuki kubwa baina ya wawili hao ndani na nje ya uwanja. Wakicheza sambamba kwenye fowadi ya Bayern, mambo hayakuwa mazuri kwa wawili hao, lakini kubwa ni Robben kutaka kufunga mwenyewe badala ya kumpasia mshambuliaji wakati wakati yeye ni winga.
Jens Lehmann & Manuel Almunia (Arsenal)
Kwa kawaida kabisa, Lehmann hakupenda kuwa chaguo la pili kwenye nafasi ya kipa na ndio maana alitibuana na Oliver Kahn kwenye timu ya taifa ya Ujerumani, wakati walipokuwa wakigombea nafasi ya kuwa kipa namba moja wa timu hiyo. Na kipa Almunia, ambaye alitazamwa kama kipa sahihi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwenye kikosi cha Arsenal, naye alikuwa kwenye balaa la kutibuana na Lehmann na hakuwa akifahamu kwanini. Na Lehmann aliwahi kumpiga kijembe Almunia aliposema: “Kuwekwa kwenye benchi na mtu aliyeanza kucheza mpira baada ya kufika umri wa miaka 30, haifurahishi.”
Romario & Edmundo (Vasco Da Gama)
Romario alisajiliwa kurudi kuichezea Vasco Da Gama mwaka 1999 kwenda kuunda safu matata ya ushambuliaji sambamba na Edmundo, lakini kumbe wawili hao tayari hawakuwa na uhusiano mzuri. Baada ya Edmundo kumbadili rafiki yake huyo wa zamani kwenye kikosi cha Brazil cha Kombe la Dunia 1998, Romario alibandika picha ya katuni kubwa ya Edmundo kwenye mlango wa choo kimoja katika baa moja huko Rio de Janeiro, utani ambao haukuwa na mwisho mzuri. Jambo hilo lilikuwa kubwa kwenye vyombo vya habari na kudaiwa wawili hao upinzani wao ulikuwa hadi kwenye kugombea wanawake kwenye kumbi za starehe.
William Gallas & Kolo Toure (Arsenal)
Bifu la Toure na Gallas lilifikia hatua ya kwamba wawili hao hata ndani ya uwanja hawakuwa wakiwasiliana katika mechi walizocheza pamoja. Kilichoripotiwa ni kwamba tatizo lilianzia kwa Gallas kukaa kitako golini mwishoni mwa mchezo wa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Birmingham City, kama vile ni mgomo wa kukasirishwa na matokeo kitu ambacho kilimkera Toure, akidhani kwamba beki mwenzake huyo amemlenga yeye kwamba kuna makosa yalifanyika kwenye mabao yaliyofungwa na Birmingham, Toure alisema: “Ukianza kuzungumzia hilo basi habari itakuwa kubwa sana.”
Zlatan Ibrahimovic & Rafael Van Der Vaart (Ajax)
Ni kazi ngumu kumweka Zlatan kwenye orodha hii baada ya ugomvi wake na Van Der Vaart ambao umedumu kwa muda mrefu. Wawili hao walikuwa pamoja kwenye kikosi cha Ajax na walikabiliana kwenye soka la kimataifa katika mechi ya kirafiki, ambapo Van Der Vaart alidai Ibrahimovic alimchezea rafu ya makusudi ili kumuumiza. Hata hivyo, Ibra alikana kumchezea rafu ya makusudi mchezaji mwenzake huyo. Wawili hao waliporudi Ajax waliwekwa kikao na kocha wao Ronald Koeman na ndipo hapo Ibrahimovic alipomtisha Van Der Vaart kwamba atamvunja miguu kama hataomba radhi.
Maxi Lopez & MAURO Icardi (Sampdoria)
Achana na ile ya John Terry na Wayne Bridge waliochukiana kwa kiasi kikubwa baada ya wawili hao kuibiana mwanamke, kali ni hii ya marafiki wawili, Maxi Lopez na Mauro Icardi walipogeuka kuwa maadui wakubwa. Bifu la wawili hao lilianza baada ya Icardi kumchukua mrembo Wanda Nara, ambaye alikuwa mke wa rafiki yake huyo, ambaye ni Lopez muda mfupi baada ya wawili hao kutangaza kupeana talaka. Icardi akabeba ubini wa watoto watatu wa Lopez huku akimchora tattoo mrembo Wanda Nara kwenye mkono wake, kitu ambacho Lopez hakupenda kabisa kwa sababu anahisi alikuwa akisalitiwa muda mrefu.
Lakini kunguru hafugiki, Wanda Nara keshamkimbia na Icardi pia.