UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umeuona mtihani wa Nabi?

KAMA unayasoma makala haya siku yaliyotoka, namaanisha Jumatano ya Septemba 8, 2021, basi utakuwa umebakiza siku nne kabla ya kuishuhudia timu ya wananchi Yanga ikicheza mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Wiki moja baadae utaishuhudia mechi hiyo hiyo ikipigwa Nigeria kujua kama Yanga watakuwa wamefanikiwa kusonga mbele kwenda katika hatua ya pili.

Wiki moja mbele tena, utawashuhudia Yanga wakiwa Dar es Salaam kuwakabili watani wao wa jadi Simba katika mchezo wa kufungua msimu wa Ngao ya Jamii.

Kama bado hesabu yako haijaenda likizo utakuwa umegundua ndani ya siku 14 Yanga watacheza mechi tatu ngumu na muhimu.

Matokeo yao yatakuwaje? Hakuna anayeweza kutabiri kirahisi. Kama unaweza kutabiri matokeo ya hizo mechi tatu, niandikie kupitia namba zangu hapo juu.

Mechi hizi zinakuja katika wakati ambao zaidi ya nusu ya kikosi cha kwanza cha Yanga ni kipya. Usishangae!

Kama kikosi cha kwanza ataanza Djuma Shaban, Yanick Bangala, Khalid Aucho, Jesus Moloko, Heritier Makambo na golini asimame ‘golikipa mwenye uwezo wa kudaka hadi mishale’ Djigui Diarra, inamaanisha Yanga itakuwa na wachezaji wapya sita ndani ya uwanja, ni zaidi ya nusu.

Je kuna tatizo kuwa na wachezaji wengi wapya kikosini? Hapana. Hakuna tatizo lolote.

Tatizo pekee linaloweza kujitokeza ni kuchelewa kupata muunganiko, kitu wazungu wanakiita ‘team chemistry’.

Kutengeneza muunganiko kunahitaji muda mrefu kidogo.

Tatizo lingine linaibuka hapo, Yanga wamekaa pamoja kwa muda gani? Walienda Morocco kwa ajili ya ‘pre-season’ wakarejea nchini kabla hawajamaliza wiki, wakajiandaa kwa ajili ya Wiki ya Mwananchi kisha wakagawanyika tena, baadhi walirejea kambini kuendelea kujifua, wengine walielekea katika timu zao za taifa kwa ajili ya mechi za kufuzu Kombe la Dunia la Qatar.

Kwa maana hiyo, kikosi kizima cha Yanga hakijakaa pamoja kwa zaidi ya wiki tatu, zaidi ya ile mechi ya Wiki ya Mwananchi dhidi ya Zanaco, hakuna mechi nyingine yoyote waliyocheza wakiwa pamoja.

Majuzi hapa walicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Friends Rangers, ni mpango mzuri waliofanya Yanga katika kutafuta kutengeneza muunganiko ila unakata tamaa unapokumbuka kundi la wachezaji muhimu hawakuwepo kwa sababu ya majukumu ya timu ya taifa.

Ukimaliza yote hayo, unageuka upande mwingine na kuwatazama wapinzani wa Yanga ambao hawafahamiki sana.

Hatuujui uimara wa Rivers United, labda wanaweza kuwa wapinzani dhaifu ambao Yanga watajipigia kirahisi na kusonga mbele kama wengi tunavyotamani.

Tatizo hatuna uhakika na hili ukizingatia hii ni timu ngeni iliyoanzishwa miaka sita tu iliyopita, mara nyingi hizi timu zilizoanzishwa miaka ya karibuni zinakuwa zimefanya uwekezaji mkubwa, huwezi kutegemea wawe dhaifu.

Kama ndani ya miaka sita tu wamemaliza nafasi ya pili Ligi Kuu Nigeria, lazima watakuwa timu imara, lakini hapo hapo tukumbuke namna Plateau United walivyoisumbua Simba mwaka jana.

Huwezi kutegemea mpinzani dhaifu kutoka Nigeria, unapokaa chini na watu wa Yanga kuwasikiliza, wengi wao wanajiamini.

Wanaamini wana timu bora inayoweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kufika hatua za mbali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hili la ligi kuu tuliweke kiporo, ligi ni mbio ndefu zinazohitaji mipango mingi, kuhusu mechi ya ngao ya hisani dhidi ya Simba tuiweke kapuni pia, ‘mechi ya Simba na Yanga haijawahi kueleweka tangu kuumbwa kwa ulimwengu.’

Tabu ipo hapa kwa Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga atachomoka? Hakuna mwenye jibu la uhakika.

Mwisho kabisa nimalizie kwa kuikumbuka kazi ngumu iliyopo mbele ya kocha wa Yanga Nasreddine Nabi, ana kibarua cha kuivusha Yanga kwenda hatua inayofuata Afrika halafu ana kibarua cha kuifunga Simba mechi ya ngao ya jamii, vipi kama atafeli kazi zote mbili?

Yanga wana kifua cha kumvumilia ilihali wanaamini wametengeneza kikosi imara cha kutishia Afrika? Sina hakika na jibu langu, kitu ambacho nina uhakika nacho ni kuwa, Nabi anahitaji dua zetu kuliko kitu kingine chochote. Tumwombee.