UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umeliona tatizo la mkataba wa GSM pale Yanga?

Yanga wamefanya maboresho ya Mkataba wa kutengeneza Jezi na kuziuza na Kampuni ya GSM kwa Kipindi cha Miaka mitano Mkataba wenye Thamani ya Bilioni 10. Hii ni hatua kuwa sana lakini kumekuwa na Maswali mengi sana na hasa kwenye Mitandao ya Kijamii. Wapo wanaosema kilichofanyika ni sawa na kutoa Pesa mfuko wa Shati na kuzipeleka mfuko wa Suruali. Wapo wanaosema hakukuwa na Nguvu yoyote kwenye majadiliano kwa Sababu Kiongozi Mkuu wa Yanga, ndiyo Kiongozi Mkuu wa GSM. Kuna uwezekano mkubwa sana mitazamo hii ikawa na hoja zenye mashiko. Kuna uwezekano mkubwa kukawa na mgongano wa Maslahi ndani yake ndiyo maaana mimi na wewe nataka tuzungumze hapa leo. Rais wa sasa wa Yanga, Eng Hersi Said ndiye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM. Kwa namna yoyote ile, Uwekezaji wowote wa GSM ni lazima atahusika. Kuna kuwa na ugumu sana kwenye majadiliano ya Mkataba mpya upande mmoja akiwa Rais wa Yanga na upande mwingine akiwa Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM. Lakini naomba tujiulize Maswali ya ndani kidogo. Yanga imeanzishwa Mwaka 1935. Kipindi hicho GSM hajafikiriwa hata kuanzishwa. Hata Mmiliki wake hajazaliwa. Yanga imewahi kupata Mkataba Mnono wa Kutengeneza Jezi na kuzisambaza zaidi ya huu wa GSM? Jibu ni hapana. Kuna muda watu tunaishi kwa hisia sana. Kuna muda watu tunaishi kwa hesabau za kudhania! Bilioni 10 kwa miaka mitano ni sawa na Bilioni 2 kila Mwaka. Yanga hawajawahi katika Historia ya Klabu yao kupata kiasi kikubwa cha fedha ya Jezi kama ilivyo kwa sasa.

Kuna watu wana maoni kuwa kama Yanga wangempata Mdhamini mwingine angeweza kuweka Pesa nyingi zaidi kuliko Bilioni 10 za GSM. Labda hoja yao ina mashiko. Tuipe muda wa kuitafakali wakati tukijiuliza Maswali. Kuna Klabu yoyote hapa Nchini ina Mkataba wenye Thamani kubwa wa Jezi kuliko wa GSM? JIBU ni hakuna. Kuna Kampuni yotote imetoa Ofa kubwa zaidi ya Ile ya GSM pale Yanga? Jibu ni hapana. Kuna muda watu tunaishi kwa hisia sana kwenye hizi timu zetu. Kuna muda tunadhani timu zetu zina thamani kubwa kama Manchester United! Kifupi ni kwamba, hakuna timu yoyote Tanzania imewahi kuwa na mkataba wa Jezi wengÈ Thamani kubwa zaidi ya huu wa GSM na Yanga. Ni kweli kunaonekana kuwa na Mgongoni wa Kimaslahi kati ya Yanga na GSM na hasa uwepo wa Eng Hersi Said pande zote mbili lakini bado Yanga imeendelea kuwa Klabu yenye Udhamini Mnono wa Jezi Nchini. Tatizo kubwa la Mgongano wa Kimaslahi huja pale Klabu inapolaliwa au kuingia Mikataba ya Kimagumashi. Kama Yanga wangeingia Mkataba wenye fedha kidogo kwa sababu tu ya uwepo wa Eng Hersi, kungekuwa na tatizo. Timu zetu kuna muda zimekuwa haziheshimu sana Wawekezaji. Kuna muda watu wanadhani hizi timu zinanyonywa tu na Matajiri. Kiukweli ni kwamba, hizi timu zetu kubwa hazikuwa kabisa na Miundombinu ya kufanya Biashara. Wapo Matajiri wengi sana ambao mpaka leo wanatumia Pesa zao bila hata kupata chochote kwenye Klabu hizi. Gharama za uendeshaji wa hizi timu kwa zama hizi sio za Kitoto. Klabu zetu za Simba na Yanga zina Nguvu kubwa sana Nchini lakini bado hazina Miundombinu mizuri ya kujiendesha zenyewe Kiuchumi. Hawa kina Mohammed Dewji MO na Ghalib Said Mohammed, taratibu wanaanza kutengeneza mifumo. Baada ya miaka 10 au 20, tunaweza kuanza kuona Michoro ya Taasisi.

Pamoja na kutumia Pesa nyingi sana na kuleta Mafanikio pale Simba lakini kuna hisia za watu wengi tu pale Simba wanaona ni kama MO anaitumia Klabu kupata Faida kubwa sana. Ni hisia tu. Watu hawaoni hata mchango wake mkubwa alioutoa kwenye kuisimamisha Simba hii imara. Leo hii MO ameamua kukaa tu kimya, kwa mbali unaanza kuona kuna vitu vinayumba pale Simba. Tuwaheshimu sana hawa Matajiri wanaoingia kwenye Klabu zetu. Kabla yao tulikuwa na Klabu hizi wenyewe kwa zaidi ya miaka 80 lakini hatukuwahi kutajirika. Kabla ya GSM kwenda Yanga, Klabu ilikuwepo na hakuwi kupata Pesa kama wanazopata sasa. Kabla ya MO kwenda Simba, Klabu ilikuwepo na haikuweza kutajirika. Tuache hisia za kudhani Simba inathamani Kama ya Real Madrid. Tuache hisia kudhani Yanga inathamani kama Bayern Munich. Ni kweli Eng Hersi ni Mfanyakazi wa GSM na Yanga lakini sijaona Athari za moja kwa moja kwenye Mkataba. Pengine tumetawaliwa zaidi na hisia kuliko uhalisia. Hii ni Biashara ambayo ni lazima GSM wapate na Yanga wapate. Hakuna Msaada hapa. Kama Yanga angeingia Mkataba wenye Thamani ndogo kuliko ule uliopita, ungeleta Maswali mengi. Kama Yanga wangeingia Mkataba unaozidiwa thamani na Vilabu vingine hapa Nchini, Maswali yangekuwa mengi. Kama Yanga ingekuwa imewahi kuwa na Mkataba Mnono zaidi kuliko huu wa GSM, napo kungekuwa na Hoja.

Kuna uwezekano mkubwa Klabu zetu zikitengenezwa vizuri zinaweza kuzalisha Pesa nyingi zaidi lakini kwa sasa, bado sana. Tunaishi kwa hisia zaidi. Tunadhani Vilabu vyetu ni Tajiri kama Bayern Munich. Tunadhani Vilabu vyetu vina thamani kubwa kama FC Barcelona. Watu wengi wanadhani Thamani ni timu ni kuwa tu na Mashabiki wengi! Hili ni tatizo lingine. Kila wakati tunahisi Viongozi wa juu wa Klabu zetu, wanaiba Pesa nyingi sana. Hili nalo ni tatizo kubwa. Kuna muda tunahisi kama Simba ni sawa na Juventus, hili nalo ni tatizo. Bado Klabu zetu zina safari ndefu sana kwenye kujiendesha zenyewe. Bado Klabu zetu zina safari ndefu sana kwenye kuongeza thamani. Mashabiki Peke yake hakuifanyi Klabu kuwa na thamani kubwa. Thamani ya Klabu ni dhana pana sana. Labda Yanga wangeweza kupata Pesa nyingi zaidi lakini kwa sasa bado hawana thamani hiyo. Kuna kazi kubwa sana inapawa kufanyika. Mkataba wa GSM na Yanga ndiyo mkubwa zaidi wa Jezi hapa Nchini. Labda huko mbeleni thamani itaongezeka. Ni kweli kuna Mgongano wa Kimaslahi baina ya GSM na Yanga kuwa na Kiongozi Mmoja, lakini bado nadhani Mkate wa Yanga amebakia pale pale . Hii ni Biashara , sio Fadhila. GSM apate, na Yanga ipate. Sijaona Athari za moja kwa moja kwenye Mkataba huu. Kama Una maoni tofauti, nitumie ujumbe wa meseji kupitia namba yangu ya simu hapo juu nimekaa paleeee!