UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Umejifunza nini kwa Simba ya msimu huu Afrika?

SIMBA ya msimu wa 2018/19, ilifika pia hatua ya robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika Kocha Patrick Aussems.
Ilikuwa Simba ya moto sana kwenye washambuliaji, Emmanuel Okwi alikuwa hashikiki, Meddie Kagere alikuwa wa moto, John Bocco alikuwa mtu na nusu.
Pamoja na kuwa timu ilikuwa moto mno kwenye dimba la Mkapa lakini, ilipigwa kiulaini sana ugenini, ilipigwa tano pale Kinshasa na As Vita kama wamesima, ilipigwa tano pale Cairo dhidi ya Al Ahly kama wamelowana, masaa hayarudi nyuma, Simba imetinga tena kwenye hatua ya Robo fainali Afrika na imekuja na somo jipya. Kuna chochote umejifunza kwa Simba hii ya Didier Gomes Da Rosa? Niandikie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu, Simba ya Gomes imekuwa moto mno kwa viungo mashambuliaji.
Luis Miquissone ni kama Lionel Messi wa Simba msimu huu, amekuwa anafanya kila kitu pale juu, akitaka anafunga mwenyewe, asipotaka anatoa pasi ya kuzalisha bao, Clatous Chota Chama ni kama Andres Iniesta wa Simba, amekuwa mtu wa kuamua ni muda gani timu ikimbie na muda gani timu itembee.

Bernard Morrison ni mtu na nusu, yule levo nyingine, yuko Dunia ya peke yake, huu ndiye utofauti wa kwanza ninaouona, huu ndiye ubora wa Simba msimu huu. Larry Bwalya ni kama Mesut Ozil wa Simba, ana mechi zake, ana utamu wake, ana udambwi dambwi wake miguuni.
Ni kama hana nguvu sawa sawa lakini huwezi kuutoa mpira ukiwa kwenye miguu yake, ni fundi kweli kweli, moja kati ya eneo ambalo Simba wanapaswa kuongeza ubora na pengine kuleta mchezaji wa nje ni eneo la ushambuliaji.
Najua yupo nahodha Bocco, yupo Kagere, pia kama yupo Chris Mugalu. Kagere ameendelea kuwa bora Ligi Kuu Bara lakini hajatumika sana Kimataifa. Bocco bado ni mchezaji mzuri lakini amekuwa nje ya Dimba kwa muda mrefu na Simba imekosa huduma yake. Mugalu amepewa nafasi lakini amerukaruka tu, Perfect Chikwende kwa muda aliopata, sina matumaini, anaweza akawa ni mchezaji mzuri lakini sio akiwa Simba, labda anahitaji kwenda timu nyingine, labda malengo ya Simba ni viatu vikubwa kwake. Simba wanahitaji walau kufanya maamuzi magumu. Washambuliaji wawili wanapaswa kuachwa na wengine wawili kusajiliwa na hasa wa kigeni, ni washambuliaji gani wawili ungependa waachwe? Niandikie maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.
Ukiitazama Simba hii kwenye kiungo wa chini, bado unaona kuna haja kabisa ya kuongeza Ng’olo Kante mmoja, yupo Mzamiru Yassini pale kati, yupo Jonas Mkude, kipenzi wa Wanasimba, yupo pia mpiganaji, Tadeo Lwanga mtaalamu wa Software lakini, bado naona haja ya kumeleta kiungo mwingine hapo chini.
Mkude bado ni msaada mkubwa kwa timu lakini, nadhani tangu amalize adhabu yake bado hajarejea kwenye ubora wake, Lwanga ni mchezaji mzuri lakini, anatumia sana nguvu, ni nadra sana kumaliza mechi bila kadi kuonyeshwa kadi.
Mpira wa kisasa umebadilika, kucheza kiungo wa chini haina maana ndiyo uwe mtu wa vurugu, haina maana ni lazima uwachanie watu viatu ndiyo uonekana fundi. Lwanga ni mzuri lakini, anatumia sana miguu kuliko kichwa kwenye maamuzi yake mengi ambayo inaigharimu sana Simba.
Mzamiru ni mtu na nusu msimu huu, amekuwa alifanya kazi zote chafu kwenye kiungo, kama angekuwa ni Raia wa kigeni lakini ndiyo watu wangempa heshima kubwa, huyu mwamba anahitaji msaidizi pale dimbani.
Bado naiona haja ya Simba kuleta chuma kingine kwenye eneo hili, wote tumeitazama Simba, wote tumeona walivyoimarika msimu huu, wote tumeona walivyofanya vizuri ugenini msimu huu. Unadhani ni kweli wanahitaji mtu mwingine kwenye eneo ya kiungo?
Msimu wa 2018/2019, Simba ilikuwa na ukuta wa Biscuits sana, ni ukuta ambao ulivunjika kirahisi kila mechi, walioigwa 5-0 na As Vita, walipigwa 5-0 na Al Ahly.
Msimu huu mambo hamekuwa tofauti, ukiachilia mbali kichapo kimoja kizito kutoka kwa Kaizer Chiefs ugenini, Simba imekuwa imara sana, Joash Onyango ni mwanamume na nusu pale nyuma. Pascal Wawa ni Sultan kamili pale kwenye idara ya ulinzi lakini, jua linaelekea kuzama, bado ni mchezaji mwenye msaada lakini yuko maji ya jioni, giza limeanza kuingia, Kennedy Juma ni beki bedui.
Beki kisiki. beki anayejua kucheza na mapungufu yake, sio mzuri sana kwenye kupiga pasi lakini, mipira ya juu yote anaruka juu, anafanya vizuri sana lakini ni vigumu kuamimi kama anaweza kucheza msimu mzima kwenye kikosi cha kwanza kwa ubora ule ule.
Ame Ibrahimu hakupata sana nafasi msimu huu, Erasto ni moja kati ya wachezaji wanaooaswa kupewa heshima kubwa sana, ni mchezaji wa muda mrefu anayeweza kucheza kwenye nafasi zaidi ya sita uwanjani kwa ubora ule ule lakini, Simba inahitaji mwanamume mwingine wa idara ya ulinzi.
Sultan Wawa ni mchezaji mzuri lakini muda unamkataa, ni vema kupata damu changa na bora kuja kuanza ujenzi upya wa eneo hilo. Najua wewe pia mi mfuatiliaji wa idara ya ulinzi ya Simba, nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu, kama wataacha kuongeza mtu, msimu ujao ukuta wa Simba unaweza kugeuka uchochoro pale Kwa Mkapa.
Simba wanaweza kuwa Wanyonge kwa sababu malengo yao yalikuwa kwenda hatua ya nusu fainali ya Ligi Mabingwa Afrika lakini, nadhani kufika robo fainali kwa mara nyingine sio jambo dogo pia.
Simba wamekomaa, Simba wanazidi kupiga hatua kubwa, ni muda wa kuongeza nguvu tena, ni muda wa kuwekeza tena, ubora wa uwekezaji huu wa awali, inaonekana mwisho wake ni robo fainali.
Kuna wanaume wanapaswa kuletwa pale Msimbazi, kuna watu wapya wanahitajika pale kuleta matokeo mapya, nikitazama kulia na kushoto, namuona Shomary Kapombe na Mohammed Hussein lakini, sioni mbadala wa kila mmoja kwenye benchi la Simba. Mnyama anahitaji kusajili walinzi pia wa pembeni kulia na kushoto, hakuna njia ya mkato kwneye kutaka mafanikio. utengenezaji wa timu ya kutwaa ubingwa wa Afrika, haufanyiki kwa simu moja.
Siku Kapombe na Tshabalala wakipata dharura, Simba inaweza kupotea, Simba unaweza kuwa uchochoro, najua na wewe umepata nafasi ya kuwatazama, tafadhali nipe maoni yako kupitia namba ya simu hapo juu.
IMEANDIKWA NA OSCAR OSCAR