UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Simu ya Aziz Ki inavyoita pesa kutoka Tanzania

NIKASIKIA kiungo hatari wa Asec Mimosas, raia wa Burkina Faso, Stephen Aziz Ki amekaribia kumalizana na Yanga.

Kabla msimulizi wangu hajamaliza kunisimulia ghafla nikasikia Simba wameingilia kati dili na wametuma donge nono kwa Ki na muda wowote atasaini mkataba na Simba. Kabla sijamaliza kushangaa ghafla nikaona picha ikimuonyesha Ki akiwa hotelini na ‘rais mtarajiwa wa Yanga’ Injinia Hersi Said.

Wakati nimepigwa na butwaa ghafla tena nikasikia ile ni picha tu na Aziz Ki mwenyewe bado hajakubali kusaini upande wowote.

Hadi naandika makala haya bado nilikuwa katikati ya kizungumkuti sielewi ukweli kuhusu kituo kipya cha Aziz Ki.

Kitu pekee ninachoelewa ni kwamba Aziz anahitajika na wababe wawili wa Kariakoo kwa ajili msimu ujao.

Inawezekana amekwishamwaga wino Jangwani kama wanavyoamini Yanga au labda Simba watafanikiwa kumshawishi na kumshusha Msimbazi, lakini ukweli ni kwamba wote wanaihitaji miguu yake katikati ya uwanja.

Vyovyote vile itakavyokuwa hivi ni vita vya panzi wawili vinavyomfurahisha kunguru mmoja. Kunguru ni mchezaji mwenyewe halafu panzi ni hawa wababe wanaohitaji saini yake. Usidhani Ki ni shabiki wa timu yoyote ile ya Tanzania.

Pengine Simba na Yanga amezifuatilia baada ya wao kuonyesha kwamba wanamhitaji. Labda alikuwa anazifahamu tu kwa kuzisikia kama anavyousikia mlima Kilimanjaro.

Ndiyo, alicheza na Simba lakini hiyo haimfanyi kuifuatilia Simba.

Jiulize hadi sasa Ki amecheza dhidi ya klabu ngapi? Je anazifuatilia zote?

Anachofanya Aziz Ki ni kukaa kando na kuangalia ofa zote wanazozituma Simba na Yanga kisha mwisho wa siku atachagua waliokuja na ofa nzuri zaidi. Anachofanya sasa hivi ni kukaa karibu na simu yake ili ahakikishe kwamba simu yoyote kutoka Tanzania haimpiti.

Atapokea simu ya Yanga kusikiliza ofa yao kisha atapokea simu ya Simba na kuwaambia Yanga wamefika kiasi fulani. Atakapokata atapokea tena simu Yanga na kuwaambia Simba wamepanda hadi dau fulani. Ataendelea na huo mchezo hadi mmoja atakapokubali kunyoosha mikono, kisha yeye atamwaga wino upande mwingine.

Watakaofanikiwa kumpata watatamba kwamba hawawezi kumtaka mchezaji yeyote yule wamkose. Watakaomkosa watahamishia nguvu zao katika kumuombea dua mbaya asifanikiwe ili wapate cha kusema. Kufeli kwa Aziz Ki katika klabu nyingine itakuwa mafanikio kwao. Hata kama wachezaji watakaowasajili wao hawatafanya vizuri sana, lakini kufeli kwa mchezaji waliyemtaka wakamkosa kwao ni mafanikio. Ndiyo maana tuna ile kauli ya ‘soka letu kivyetu-vyetu’

Ndiyo maana hata usajili wa Aziz Ki bado utafanyika ‘ki-vyetu-vyetu.’ Waulize Simba na Yanga walimfahamu vipi Aziz Ki? Najua watakupa lile jibu la siku zote watakuambia walianza kumfuatilia siku nyingi na walimhitaji kwa muda mrefu.

Lakini ukweli unabaki kwamba wote walimfahamu Aziz Ki baada ya kuwashughulisha Simba kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho. Kwa hiyo kama Simba wangemng’oa Jwaneng Galaxy siku ile na kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika labda Aziz Ki asingefahamika nchini na hizi vurugu zisingekuwepo.

Labda Asec wasingetinga makundi Shirikisho, pengine Aziz Ki asingefahamika nchini na hizi vurugu tunazozishuhudia sasa zisingekuwepo.

Lakini hapo unakaa chini na kujiuliza kwani nani aliwaaminisha Simba na Yanga kwamba hakuna kiungo mwingine barani Afrika anayeweza kuwapa wanachokitafuta kwa Aziz Ki? Tatizo kubwa ni kwamba, Simba na Yanga wamekuwa wavivu wa kusaka vipaji ndiyo maana wamekuwa wakishindana kusajili wachezaji wanaowafahamu.

Lakini kuna hili lingine, labda Simba na Yanga wanawafahamu viungo wanaoweza kuwapa wanachokitafuta kwa Aziz Ki sehemu fulani barani Afrika, lakini wanafahamu wakienda kuwasajili watalazimika kulipa kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya kuvunja mikataba waliyosaini na klabu zao.

Hata huyu Aziz Ki wanamgombania kwa sababu wanajua mkataba wake unafika mwishoni na ili kumsajili watahitaji tu kulipa pesa ya usajili kwa mchezaji mwenyewe bila kuihusisha klabu.

Vipi kama Aziz Ki angekuwa na mkataba wa miaka miwili? Nadhani wasingethubutu hata kutuma ofa.

Lakini vipi kama Ki angekuwa anahitajika na wababe Kaskazini? Nafikiri pia wababe wa Kariakoo wasingethubutu kumsogelea. Kwani zimepoteaje hadithi za Victorien Adebayor?