Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UBISHI WA MZEE WA KALIUA: Ni kweli tuna ligi bora Tanzania kwa sasa?

Muktasari:

UWANJA uko wazi, kila mtu ana maoni yake, kila mtu ana vipimo vyake.

UWANJA uko wazi, kila mtu ana maoni yake, kila mtu ana vipimo vyake.

Je, baada ya kupata nafasi nne za uwakilishi kimataifa ni kipimo tayari tuna ligi bora?

Nipe maoni yake kwa kuniandikia ujumbe kwenye namba yangu ya simu hapo juu.

Ukitazama namna tulivyokusanya pointi za kupata timu nne kwenye michuano ya Afrika, utagundua Taifa limebebwa na Simba maana zaidi ya asilimia 90 ya pointi zetu, zimetokana na matokeo mazuri ya Simba katika kipindi cha miaka mitano ya hivi karibuni.

Simba ndiyo Baba lao, Simba ndiyo Kidume cha Mbegu, kuna tofauti kubwa sana kati ya Simba na timu nyingine kwa sasa nchini, Simba wako mbali sana, tusijidanganye tumefanikiwa kuwa na timu bora.

Tusijidanganye ligi yetu imeimarika, Simba ndiyo wameimarika, Simba ndiyo msingi wa kupata nafasi hizo nne kimataifa, ukitaka kujua ubora wa ligi yetu uwanjani, tazama matokeo ya mwisho ya Yanga, Azam FC, KMC na Mtibwa Sugar, wote walitolewa hatua za awali, wote walichakazwa.

Hakukuwa na mwenye afadhali, Namungo FC nimewaweka kando kwa sababu, wao ushiriki wao ulisaidiwa na mambo tofauti, janga la COVID -19, liliwabeba mechi nyingi wakacheza nyumbani.

Nawapongeza kwa kutinga hatua ya makundi lakini, hawakufika kwa nguvu zao pekee uwanjani, siamini kama wangemtoa De Agosto ya Angola.

Unadhani ligi yetu imekuwa kwa kupata nafasi nne Kimataifa? Niandikie maoni yako kwa namba yangu ya simu hapo juu .

Kama mpira wetu ungekuwa unachezeshwa kwa usawa, kama mpira wetu ungekuwa unachezeshwa kwa haki, ukitoa Simba, timu nyingine zote zilizobaki hazina utofauti mkubwa wa ubora.

Hazizidiani pakubwa, hazipishani sana, wote ni wale wale, hakuna hata mmoja mwenyewe uhakika wa kushinda mechi tano mfululizo, ndugu zangu tusijidanganye, bado tuna kazi kubwa ya kuimarisha ligi yetu.

Pengine pesa zinazoingia ndani ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuanzia msimu ujao za matangazo ya runinga zinaweza kuja kuokoa jahazi, kuna mechi chache sana za ushindani ndani ya ligi yetu.

Sidhani kama zinafika hata 10 kwa kila msimu, ushindani ni wa kawaida sana, mechi bila kuhusisha Simba, Yanga na Azam, mvuto ni kidogo sana, mechi bila wakubwa wa ligi, ni za kawaida mno, tunahitaji kutengeneza Azam FC nyingine, tunahitaji kuongeza washindani zaidi na sio washiriki.

Ukitazama timu zetu zinazopanda daraja, hakuna mtata, hatuoni tena ushindani kama walioleta Mbeya City mwaka waliopanda daraja la Ligi Kuu.

Hizi nafasi nne zisitudanganye ndugu zangu, unadhani ligi yetu imepanda kwa kupata timu nne za kucheza kwenye michuano ya Afrika msimu ujao? Naomba maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Kuna eneo moja ambalo nadhani tumeimarika zaidi, ni eneo la udhamini wa Sh225.6 bilioni za Azam Media, sio mchezo.

Hapa tumepiga bao, kama pesa hizi zitatumika vizuri, tunaweza kupata kina Cloatus Chota Chama wengi, tunaweza kupata kina Prince Dube wengi.

Tunahitaji hawa watu kuimarisha ushindani, tunahitaji makocha wa kigeni wenye kiwango kama Didier Gomes Da Rosa, tunahitaji watu kama kina Hans van dar Pluim, tusijidanganye kwamba Tanzania tuna ligi bora, hakuna kitu, tuna Simba tu kwa sasa ambayo tunaweza kujivunia zilizobaki zote zinafanana tu.

Wote ndiyo wale wale.

Kuna kazi kubwa ambayo timu zetu zinatakiwa kufanya ili kulinda idadi ya timu hizi nne kimataifa, kama walau timu mbili mwakani zitakwenda mpaka robo fainali ya Afrika, itakuwa jambo jema sana, tayari tunaweza kuwa na uhakika na Simba ni timu gani nyingine unadhani inaweza kutupeleka Robo Fainali mwakani?

Nitumie maoni yako kwenye namba ya simu hapo juu.

Sio mara ya kwanza kupata nafasi nne za Kimataifa lakini, huwa hazidumu, mwaka juzi tulipata pia lakini mambo yalikuwa yale yale, Kichwa cha Mwendawazimu.

Hatuhitaji kurudi tena huko, tunahitaji kupata timu ambazo zitakwenda kushindana na sio kushiriki tu, ukiambiwa utaje timu Bora kutoka Ligi Kuu Bara, utaishia kutaja Simba, Yanga na Azam.

Hata hao Azam na Yanga kwa sasa ni kama wanatembelea zaidi historia, nyingine zote zilizobaki ni Pipa na Mfuniko, tunahitaji kuona Mtibwa Sugar ukirudisha ubabe, Coastal Union ile ya mwishoni mwa miaka ya 1980 ikijirudia, tunahitaji kuona timu kama Pamba ya Mwanza ya miaka ile lakini kwa sasa tusijidanganye kama tuna ligi bora Tanzania bado tuna kazi kubwa ya kufanya.

Tusione tatizo kujifunza kwa Simba, wachezaji bora, Kocha Bora na viongozi bora, tunahitaji kuona timu zetu zikifanya vyema kimataifa, matokeo kama ya KMC Kimataifa, Azam FC, Mtibwa Sugar na Yanga hivi karibuni hatuyataki.

Kama hatutofanya vizuri msimu ujao, nafasi nne zitaondoka, mataifa mengine yatazichukuwa na tukiendelea kujiaminisha tuna timu bora, tutatolewa wote mapema.

Walau muda unatosha kwa timu kama Azam na Yanga ambao wana uhakika wa kucheza Kimataifa mwakani ila hatutaki aibu, hatutaki visingizio.

Tunataka ushindi ili kulinda nafasi zetu zote nne. Je, tuna ligi Bora Tanzania? Nipe maoni yako kupitia namba yangu ya simu hapo juu.

Imeamdokwa na OSCAR OSCAR-O658376417